Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suleiman Mohamed Rashid (4 total)

MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pamoja na majibu hayo nina swali la nyongeza. Serikali haioni haja kuandaa mwongozo wa dharura wa uboreshaji ambao utaweza kuzingatia kulipwa kwa posho ya kujikimu pamoja na posho maalum kwa walimu ambao wanasahihisha mitihani hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya walimu wanaosahihisha mitihani kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo pamoja na posho wanazolipwa Serikali pia hulipa malazi, chakula, matibabu wakati wote wa kazi. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tumeupokea. (Makofi)
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kipekee nimpongeze yeye pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Rais kwenye hili suala la elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na mahitaji ya taaluma ya akili unde, Serikali imejipangaje ili taaluma hii kuweza kusomeshwa katika maskuli (shule)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa ruhusa yako ninaomba nimjibu Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Jimbo la Mwera, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile ambavyo Serikali imejipanga katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, ndivyo ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba kwa upande wa elimu ya akili unde, mikakati mbalimbali imeendelea kuchukuliwa. Kwa mfano, matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine miongozo mbalimbali imetolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miongozo imetolewa katika kutekeleza teknolojia za kidijitali katika elimu msingi, vyuo vikuu na vyuo vya ualimu. Pia kuna utekelezaji wa AI katika masomo, lakini pia Serikali imekuwa ikitoa ufadhili wa fursa za masomo ya nje ya nchi, lakini pia tumeendelea kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu ili kuona kwamba mazingira ya watoto wetu ya kujifunzia yanaendana na mahitaji halisi ya teknolojia ikiwemo elimu ya akili unde. (Makofi)
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu gari hizi, mwaka wa fedha 2024/2025 kituo chetu tulipatiwa gari moja lakini baada ya hapo ilihamishwa na ikaenda Mkoa ili aweze kutumia RTO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini kauli yake juu ya gari hizo mbili ambazo mpaka sasa hivi ninazungumza hazijafika ndani ya Kituo hicho cha Mwera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, gari hizi mbili nilizozitaja ni katika mpango wetu wa Jeshi la Polisi wa kugawa magari nchi nzima kila Wilaya, kila OCD na kila OCCID anapatiwa gari moja. Na haya ndiyo magari mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Kituo cha Polisi cha Mwera ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Magharibi A. Ninafahamu kwamba shaka au wasiwasi wa Mheshimiwa Mbunge unatokana na kwamba kwa sasa kituo hicho cha polisi kipo katika hatua za mwisho za ujenzi kwa maana ya Kituo cha Daraja B.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo shughuli nyingi za magari hayo zimekuwa zikionekana zinafanyika kupitia Kituo cha Polisi cha Bububu. Kwa hiyo ndio maana Mheshimiwa Mbunge amekuwa na hofu kwamba magari hayo hayapo kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini magari haya ni kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Daraja B kiliopo Mwera. Kwa hiyo, mara baada ya kukamilika ujunzi ule magari yale yatatoka kule Bububu anapoona yana-park yatakuja ku-park pale Mwera na huduma zitaweza kuendelea kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa hatua ambayo imefikia. Pia ninampongeza pia Naibu Waziri kwa majibu ambayo ameweza kutupatia. Nina maswali mawili ya nyongeza.

(a) Je, ni faida gani ambayo imepatikana baada ya utatuzi wa hoja 15 kati ya hoja 18?

(b) Je, ni mikakati gani ya Wizara ambayo imejipangia kuhakikisha hoja tatu ambazo zimebakia tunazitatua kabla 2030?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala haya ya Muungano, yeye pamoja na Wabunge kutoka Zanzibar pamoja na Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 aliyekuwa Rais wetu, Mzee wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa maelekezo ya kubadilisha namna ya kufanya majadiliano kuhusu hoja za Muungano. Hivyo, ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya pamoja ambapo Kamati hii imeleta ufanisi mkubwa sana katika kushughulikia hoja za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 hadi leo Kamati hii imepokea hoja 25, na katika hizo imeshashughulikia hoja 23 na kuzibakiza hoja mbili. Kwa hiyo, huo ulikuwa ni mkakakati mkubwa ndani ya Serikali wa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuondoa hoja hizi kwenye hoja za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndani ya Serikali tumeendelea kupitia timu mbalimbali za wataalamu kufanya mapitio ya sheria, mapitio ya kisera pamoja na kuandaa nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kuiwezesha Kamati hii ya pamoja kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati hii ya pamoja kiutaratibu ambao tumeuweka inaongozwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka pia kufahamu faida ambazo zimepatikana kwa kuondosha hoja hizi za muungano ambazo zimekwisha fanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazitaja chache kwa sababu ni nyingi. Kwanza, ushiriki wa Zanzibar kwenye masuala ya Kimataifa na kikanda umekuwa bayana. Nafasi ya Zanzibar inaonekana kwa dhahiri katika ushiriki huo, katika kuandaa hoja na kuandaa msimamo wa pamoja kama nchi kwenye makubaliano ya Kimataifa tunapokuwa tumewasilisha hoja au kuhudhuria mikutano hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeweka utaratibu mzuri wa shughuli za uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu. Tumeweka miongozo ambayo inaondoa migongano isiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wafanyabiashara kutoka Zanzibar wameondolewa mzigo wa kulipa kodi mara mbili. Kodi ya mapato (Pay as You Earn) pamoja na Kodi ya Zuio (Withholding Tax).

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, kupitia kamati hii ya pamoja tumepelekea kuondoa hoja iliyokuwa ikitupa mkanganyiko katika mikopo ya Kimataifa inayohitaji dhamana na ile isiyohitaji dhamana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaomba kuwasilisha.