MHE. PROF. JOYCE L. NDALICHAKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujua je, ni lini Serikali itakamilisha kazi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo nguzo za umeme zilichimbwa tangu mwezi Agosti, 2025 lakini hakuna kinachoendelea kama vile eneo la Kidiama, Kumulama, Kumuhama, Mrufiti Mpya pamoja na maeneo yote?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kupata majibu ya Serikali kwa sababu wananchi wanatamani sana kupata umeme na hasa wakizingatia Serikali imefanya kazi kubwa, imekamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere na uzinduzi umefanyika lakini wao bado umeme haujawafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini kwa kufuatilia kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati. Kumbukumbu zangu nilipofanya ziara katika Mkoa wa Kigoma upande wa Kasulu Mjini kulikuwa na changamoto ya mkandarasi ambaye tayari alikuwa ameshalipwa advance payment lakini alikuwa anasuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hatua za kisheria zimeshachukuliwa na mwezi Septemba mwaka huu tutaleta mkandarasi mwingine ili aweze kuendelea na kazi ya kupeleka umeme na atalipwa. Yule alikuwa amelipwa advance payment lakini anasuasua huyu mwingine atakayeletwa atalipwa fedha na ninakuhakikishia kabla ya mwaka 2030 vitongoji vyako vyote vitakuwa vimepata umeme. Ahsante sana.