Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zena Maulidi Katambo (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa na mimi kuchangia leo katika hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa kuwa leo ni mara yangu ya kwanza, ninaomba nitumie fursa hii kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Lindi ambao wameniwezesha kunifikisha hapa leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia jukwaa hili kuwaeleza kwamba nitawapa uwakilishi ambao umetukuka na nipo tayari kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, kwa dhati ya moyo wangu ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kujitolea kwake kwa hali na mali kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, ninamshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, tumemwona katika kipindi ambacho yupo kwenye nafasi hii amezunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kufanya ziara ambapo katika ziara hizo amefanya shughuli mbalimbali na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumtia moyo Waziri Mkuu, nimweleze kwamba wananchi tunafurahishwa na kasi yake ya utendaji kazi na kwamba aendelee hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, mchango wangu kwa siku ya leo katika Wizara hii ninauelekeza kwenye barabara. Mkoa wa Lindi tunazo changamoto kubwa sana za miundombinu ya barabara. Barabara hizi changamoto inaanzia barabara kuu ambayo inaunganisha Mkoa wa Lindi na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara hii tumepitia changamoto mbalimbali ambapo katika msimu wa mvua wa mwaka 2024 ambao nchi yetu tulikumbwa na Kimbunga Hidaya, Mkoa wa Lindi, barabara hii iliathirika kwa kiasi kikubwa na kuharibika kwa madaraja, na pia sehemu kubwa ya barabara kuharibika vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, ninaipongeza Serikali kwa jitihada zake ambazo imefanya kwa kurekebisha yale madaraja makubwa ambayo yalikuwa yanaathiri matumizi ya barabara ile ambapo kwa kipindi cha mwaka 2025 wananchi wa Mkoa wa Lindi ni mashahidi kwamba baadhi ya nyakati tulilazimika kukaa kusubiri kungojea maji yapungue ili tuendelee na safari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imemaliza changamoto ile ya upande wa madaraja na kwamba sasa angalau tuna uhakika wa kusafiri moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Lindi. Hata hivyo, tunayo changamoto nyingine katika barabara hiyo ambapo ile athari ya mvua iliharibu maeneo mengi ambapo barabara ile ina mashimo mengi, kwa kweli haipitiki vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika changamoto hii Serikali imejitahidi kuziba viraka katika barabara ile ili angalau wananchi waendelee kuitumia. Kutokana na uharibifu ule mkubwa, ninaiomba Serikali, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi suluhisho la kudumu tunaomba tujengewe barabara mpya ili kusudi iendane na mahitaji ya sasa tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba barabara hii mpya kwa sababu tunafahamu kwamba Mkoa wa Lindi kwa sasa kuna miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inafanyika. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na bandari ya uvuvi iliyopo Wilayani Kilwa. Bandari hii Serikali imewekeza shilingi bilioni 280.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwekezaji huo, tunaiomba Serikali itutengenezee hii barabara kuu ili jitihada ambazo zimetumika kuwekeza kwenye mradi ule ziendane na miundombinu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunazo changamoto za barabara za ndani ya mkoa. Mkoa wa Lindi hauna wilaya ambazo zimeunganishwa kwa lami kati ya wilaya na wilaya. Hivi hapa tunavyozungumza, wananchi wa Wilaya ya Liwale ambao wanapitia barabara ya Nangurukuru kwenda Dar es Salaam hawawezi kusafiri siku ya leo, tangu jana barabara zimeharibiwa na mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Nachingwea, wananchi wa Kilimalondo - Mbondo, wananchi wa Kilimalondo - Kiegei - Namapwia - Nero Mission hawawezi kusafiri kati ya maeneo hayo kwa sababu mvua hizi zinazoendelea zimekata madaraja katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Kilwa tunazo kata za Kandawale, Njinjo, Kipatimu, Kibata ambapo katika kata hizi wananchi hawawezi kuingia wala kutoka nje ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya ya Ruangwa tunazo changamoto katika kata ya Matambalale, Chunyu, Nambilanje na Mandawa. Kwa ujumla tunaomba Serikali itusaidie kupitia TARURA kujenga madaraja na kwa awamu ya kwanza ituletee madaraja katika barabara hizi kwa sababu kiujumla hizi changamoto zimekuwa ni zile ambazo zinaendelea. Hizi changamoto ni zile ambazo zinatokea kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika harakati za kutibu tatizo hili, tunaomba Serikali itujengee madaraja ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni umeme. Utakubaliana na mimi, Mkoa wa Lindi huenda ndiyo mkoa pekee au labda imebaki mikoa miwili mitatu ambayo bado haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kutokuunganishwa na gridi ya Taifa mkoa wetu una changamoto kubwa ya ukosefu wa umeme wa uhakika. Kwa Mkoa wa Lindi, umeme kukatika mara 10 mpaka 20 kwa siku ni jambo la kawaida. Hali hii inatuathiri sana wananchi wa Mkoa wa Lindi, lakini pia tunapata athari za kiuchumi ambapo tunakosa wawekezaji ambao wapo serious kwa ajili ya kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, kwa kuwa sasa hivi nchi yetu tunazalisha umeme zaidi ya mahitaji yetu, ninaiomba Serikali ituunganishe na sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi ili kusudi na sisi tuweze kunufaika na hii keki ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nimalizie kwa kuipongeza Serikali katika mradi wa LNG. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa hivi ipo kwenye hatua za mwisho za kusaini makubaliano ya utekelezaji wa uzalishaji wa gesi ya asilia kupitia mradi wa LNG Mkoani Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una thamani ya shilingi trilioni 100. Huu ni mradi mkubwa kuliko mradi wowote ambao nchi yetu ya Tanzania imewahi kuutekeleza. Mradi huu unasubiriwa sana na wananchi wa Mkoa wa Lindi, kwa sababu hii ilikuwa ni ahadi tangu Serikali ya Awamu ya Nne; ilituahidi kutekeleza mradi huu, lakini hatukufanikiwa, Serikali ya Awamu ya Tano na mpaka sasa ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa kweli tumeusubiri sana mradi huu, tunatamani na tunaiomba sana Serikali iharakishe zoezi la usajili na kusaini documents za makubaliano ili kusudi mradi uanze kazi, na pia uweze kuchangia kwenye Taifa na dunia kwa ujumla kwa sababu unalenga kuuza gesi ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mapendekezo ya Bajeti ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Lindi, hususan wakina mama, ninapenda kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa katika ujenzi wa bandari ya uvuvi, bandari ya Kilwa. Serikali ya Awamu ya Sita sasa hivi katika Mkoa wetu wa Lindi katika Wilaya ya Kilwa imejenga mradi wa bandari ambayo inahusiana na uvuvi yenye thamani ya shilingi bilioni 280. Mradi huu hadi sasa umefikia 98% ya utekelezaji wake, na muda wowote Mheshimiwa Rais anatarajiwa kwenda kuuzindua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi tunashukuru sana na tunaiomba Serikali kupitia mradi huu, kuna miradi mingine midogo midogo ambayo inaenda kutekelezwa inayoambatana na mradi huu wa bandari ya uvuvi. Miradi hiyo ni pamoja na kiwanda cha kuchakata samaki, soko la kisasa la samaki, karakana za matengenezo kwa ajili ya miundombinu hii ambayo itatumika kwenye uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mradi huu pia unahusiana na ujenzi wa ghala kwa ajili ya zao la mwani. Tunafahamu kwamba zao la mwani nchi hii lilikuwa lipo nyuma kidogo na wakulima ambao wanahusiana na zao la mwani mara nyingi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili linajumuisha wanawake wengi katika maandalizi yake, lakini pia wanawake wengi ndio wanajihusisha katika sekta ya uzalishaji wa zao la mwani. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali kwa kitendo cha kuleta hili ghala ambalo tunaenda kupeleka zao la mwani katika mfumo wa soko la Stakabadhi Ghalani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kulipeleka hili zao katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani unaenda kuwahakikishia wakulima moja kwa moja uhakika wa soko na kuuza mazao yao hali ambayo inaenda kuinua kipato chao cha uchumi. Bandari hii pia tunatarajia kutoa ajira za moja kwa moja za vijana, wananchi 3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi, tunatarajia kunufaika na huu utekelezaji wa huu mradi moja kwa moja ambapo wananchi ambao wanahusika na zoezi la uvuvi wanatarajiwa kwenda kuwezesha kwenda kuvua katika bandari kuu ambapo hapo awali kabla ya utekelezaji wa mradi huu haujatekelezwa wananchi walikuwa wanashindwa kufika kwenye yale maji makubwa, hivyo kushindwa kupata samaki wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu wa bandari ya uvuvi tunakwenda kuboresha kipato cha Mtanzania moja kwa moja, kwa Mtanzania mmoja mmoja, pia kuinua zile familia ambazo zinahusika na shughuli za uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Lindi wanaendelea na maandalizi ya kuhakikisha kwamba wananufaika na uwepo wa bandari hii na hawaishii tu kuwa watazamaji. Katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Lindi wananufaika, tarehe 12 mwezi wa Tano, Wilaya ya Kilwa imefanya kongamano kubwa la kuhamasisha wananchi kuwa tayari kutumia fursa ya uwekezaji katika bandari hii pale itakapoanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, kwa sababu mradi huu unavipengele vingi, tuiombe Serikali kwamba muda utakapofika miradi hii itekelezwe kwa wakati, pia ikamilike ili kusudi zile gharama kubwa, hii shilingi bilioni 280 ambayo imeshatolewa na Serikali iende kuleta tija ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mifugo. Kwa asili wananchi wa Mkoa wa Lindi sisi siyo wafugaji, lakini Serikali kati ya mwaka 2015/2020 ilikuja na mpango wa kuwahamasisha wafugaji kutoka sehemu mbalimbali za nchi kuhamia Mkoa wa Lindi kwa sababu Mkoa wa Lindi ulikuwa na eneo kubwa ambalo lipo wazi kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wafugaji wale waliitikia wito na wamekuja kwa wingi. Hata hivyo, licha ya kwamba wafugaji wale wamekuja na kutuletea baraka ya uwepo wa chakula kama nyama na maziwa, tumekutana na changamoto ambayo sasa imeanza kuibuka, ya uwepo wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa baadhi ya maeneo, almost Wilaya zote...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, almost wilaya zote wananchi wanapambana. Hivyo ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atueleze mpango wa Serikali kuhakikisha wanapambana na changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii uliyonipatia na mimi niweze kushiriki katika kutoa maoni yangu katika mchango wa mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii ya Afya ya Mwaka 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa. Sisi wote na wananchi kwa ujumla tumeshuhudia katika hiki kipindi kifupi ambacho ameshika Wizara hii, amefanya mambo makubwa, ametekeleza miradi mikubwa na ametuletea dira ambayo inaonesha kwamba nchi yetu kama tutaenda kutekeleza hii miradi ambayo Wizara hii inatuomba fedha leo, tunakwenda kwenye ile nchi ya ahadi kwa upande wa sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Samizi ambaye kwa pamoja na Mheshimiwa Waziri wamekuwa wakishirikiana kuhakikisha kwamba Wizara hii inakwenda vizuri. Mheshimiwa Dkt. Samizi ni mtu mkarimu sana kwa kweli, Mwenyezi Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninapenda kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanywa katika sekta ya afya. Katika sekta hii, wote ni mashahidi kwamba Serikali imejenga miradi mbalimbali ya kutolea huduma za afya kuanzia Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Mikoa, lakini na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huduma hizi za hii miradi ambayo Serikali imetekeleza kwa Mkoa wa Lindi, tunashukuru sana kwa kuletewa ule ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo kwa sasa Mkoa wa Lindi tumepata hospitali ya rufaa na wananchi wanakwenda pale kupata matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunafahamu sera ya nchi hii kwa sekta ya afya ni kuhakikisha kwamba kila Kata inakuwa na kituo cha afya. Kwa upande wa Mkoa wa Lindi hali yetu siyo nzuri kwa upande wa miundombinu ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakutolea mfano wa huduma za vituo vya afya. Kwa mfano kwa Wilaya ya Nachingwea tuna vijiji 129, kati ya vijiji 129 tulivyonavyo, tuna zahanati 49 pekee, lakini pia kwa upande wa vituo vya kutolea huduma za afya Wilaya ya Nachingwea ina Kata 36 ambapo kata hizi zote kama ile sera ya kituo cha afya katika kila Kata ingetekelezwa, tungekuwa na vituo vya afya 36. Kwa sasa ninasikitika kusema kwamba, Wilaya ya Nachingwea inavyo vituo vya afya viwili ambavyo vinafanya kazi effectively, vituo vingine vya afya viwili vinaendelea kujengwa, lakini vinajengwa kwa mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba hizi Halmashauri zetu hali ya uchumi siyo nzuri. Kwa hiyo, utekelezaji wa ile miradi unasuasua. Kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Lindi tunamwomba Mheshimiwa Waziri atuangalie kwa jicho la pekee tuongezewe vituo vya afya, tuongezewe zahanati ili na sisi tuweze kuhudumiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la miundombinu ya huduma za afya nina ushauri kidogo. Ninaishauri Serikali ibadilishe sera yake ya majengo hasa ya vituo vya afya. Zile labour ambazo akina mama tunazitumia tukiwa katika kipindi cha kujifungua, zipo kama ma-hall yaani kwamba ni ukumbi, kila mtu anaingia. Ni vitanda tu vimepangwa, tunakosa staha wakati tukiwa tunajifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la kuboresha ile miundombinu ni suala rahisi, halihitaji gharama kubwa. Kwa kupitia Wizara tunaweza tukaelekeza kwa kushirikiana na TAMISEMI angalau vile vituo ambavyo tayari vipo, tukaenda kuboresha ile miundombinu ili ituwezeshe katika kile kipindi cha kujifungua, tujifungue kwa staha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaipongeza Serikali kwa sera ya Bima ya Afya kwa Wote. Katika sera hii ya Bima ya Afya kwa Wote, sisi wananchi wa Lindi ambao tunatumia ushirika katika mazao yetu tulikuwa tunaomba, tunavyofanya biashara za mazao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. ZENA M. KATAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyofanya biashara za mazao, kuna ushuru. Kule tunakatwa na zile agency ambazo zinapata ule ushuru. Wale ni watu ambao wanatuhudumia sisi wanachi wa Mkoa wa Lindi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akae nao kwa sababu ni wa kwetu. Kama watakaa pamoja, hawatakataa kuchangia angalau shilingi 15 kwa kilo ili kusudi wakulima wa Mkoa wa Lindi tunufaike na Bima ya Afya moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)