Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zainab Rashid Kawawa (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya maamuzi ya haraka ya kupunguza matumizi ya mafuta kwa kuanzia na ofisi ya kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri tu kwamba, ni muda muafaka sasa wa kutumia nafasi hii ya changamoto ya upatikanaji wa mafuta kama fursa kwa kuanza kutumia gesi yetu ambayo inatumika kwenye magari. Wataalam wajielekeze kwenye kupanua mradi wa gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo gesi wananchi wanaitumia kwenye magari Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, si vibaya kama wataalam watatushauri vyema kuongeza wigo na kuileta katika mikoa mingine ili tuweze kuitumia hii gesi ambayo pia ni ya gharama nafuu sana kama njia mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye kwa kweli amelivaa joho lake la Uwaziri Mkuu na ameenea kwenye kiti chake sawasawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu amezunguka katika maeneo mbalimbali na katika Mkoa wetu wa Lindi pia amezunguka. Tunaona ambavyo inaleta tija ya uwajibikaji na inaleta funzo la uwajibikaji. Ninataka niwaambie Watanzania, kwamba Taifa hili lina-operate katika mfumo wa decentralization tangu wakati wa Azimio la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, decentralization maana yake ni ugatuaji wa Madaraka; mgawanyo wa majukumu na wa madaraka kuanzia ngazi ya wananchi ambao wanachagua viongozi wao kwenda kwenye ngazi za vitongoji, vijiji, mitaa na mijini. Vilevile kwenda kwenye ngazi za kata ambapo wanawapata Madiwani, kwenda kwenye ngazi za wilaya ambako wanapata Wabunge wa majimbo, kwenda kwenye ngazi za mkoa kwa maana ya upande wa Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri kila mmoja akatambua wajibu wake katika eneo lake, kwa sababu dhumuni la kufanya huu ugatuaji wa madaraka lilikuwa ni kumpunguzia Rais mzigo wa uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi. Hivyo, ni vyema kila mtu kwenye eneo lake akawa tayari kuwahudumia wananchi. Si vyema kusubiri masuala ambayo yanahitaji kuhudumiwa ngazi ya chini kumsubiri mpaka Mheshimiwa Waziri Mkuu aje kumhudumia mwananchi huyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema tujitathmini, ni vyema tutende haki, tuwahudumie wananchi wetu kwa kuwa hiyo ni dhima ambayo Mwenyezi Mungu ametupa. Kesho atakwenda kutuuliza nilikupa nafasi yako uliitumikiajie kwa waja wangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuendelea na jitihada za kukuza ajira katika nchi yetu. Mheshimiwa Rais ametuletea mradi mkubwa sana, Mradi wa Bandari ya Uvuvi; bandari ya kisasa, bandari kubwa ambayo haijawahi kutokea katika nchi za Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari hii inatarajiwa kuzalisha ajira zisizopungua 300, ajira rasmi. Bandari hii kama itafanya kazi ipasavyo upo mnyororo wa thamani wa huduma mbalimbi zitakazofanyika pale zinazohusiana na bandari moja kwa moja; ajira zisizopungua 30,000. Thamani ya bandari hii ni shilingi bilioni 280.5; na mpaka sasa utekelezaji wake umekwishafikia 97%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matumaini makubwa sana na bandari hii, hasa kwenye hili eneo la ajira. Tunaona kuna fursa ya vijana kwenda kufanya shughuli za uvuvi wa samaki, tunaona kuna fursa ya vijana na wanawake, maana wanawake wengi huwa wanafanya biashara za samaki. Kwa hiyo, tunaiona fursa kubwa sana ya ajira katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba, mpaka sasa hali ya umeme katika eneo la bandari bado si ya uhakika. Hali ya umeme kwenye eneo lile ambalo litahitaji kuwa na majokofu ya kuhifadhi tani zisizopungua 60,000 kwa mwaka si ya uhakika. Umeme tunaoambiwa unaohitajika pale si chini ya megawati 300. Mpaka sasa tunaambiwa tunatumia umeme, tunavuta umeme kutoka Songosongo ambao sina uhakika kama unaweza kukidhi haja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, kwa uzito wa mradi huu na kwa gharama ambazo Serikali imekwishaingiza pale, watuletee umeme wa gridi ya Taifa. Pale sisi Wabunge tunapofanya majukumu yetu tunalala Kilwa, tunalala wapi tunahamahama. Ukikaa Kilwa umeme unakatika kwa siku si chini ya mara 10, ndio ukweli wenyewe ‘Haki ya Mungu’. Siyo chini ya mara 10. Sasa, tunawezaje kuleta mradi mkubwa kama huu halafu hatuna umeme wa uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wanahitaji kuhifadhiwa ili wasiharibike, ni perishable; sasa watahifadhiwaje kama hakuna umeme wa uhakika? Kwa hiyo, ninaomba, ili tuweze kuleta matumaini makubwa kwa Taifa letu na kwa vijana wetu na kwa wananchi wetu wanaoitegemea bandari hii, hasa kwenye ajira, basi tunaomba tutekelezewe jambo hili kwa haraka. Kwa sababu, kama tumeshafikia 97% tumebakiza muda mchache wa kumalizia na kuanza, ni vyema basi likatekelezeka hili jambo kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya barabara pia inahitajika. Kutoka Kilwa Masoko hadi kwenda Nangurukuru na kuelekea sehemu nyingine barabara ile ni mbovu. Kwa hiyo, ni vizuri ikatengenezwa ili kusudi usafirishaji wa samaki na vyombo vya moto vitakavyokuwa vinapita pale viweze upita kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena Mheshimiwa Rais kwa kukuza ajira kwenye sekta ya kilimo. Katika Mkoa wetu wa Lindi tumeona jitihada kubwa zimefanyika za kuchochea ajira kwenye eneo hili la kilimo, kwa sababu kitendo cha Mheshimiwa Rais kuendelea kutuletea pembejeo za ruzuku kumechochea vijana wengi kuingia kwenye kilimo na uzalishaji umeongezeka, hasa kwenye mazao ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazao ya ufuta tumezalisha kilogramu milioni sabini na tano laki saba na sitini, ukilinganisha na mwaka uliopita ambapo tulizalisha kilogramu milioni sitini na nane laki mbili na hamsini na nne. Kwenye zao la korosho tumezalisha kilo milioni mia moja arobaini na tatu laki nne na sitini ukilinganisha na kilo milioni 115, kwa msimu uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata zaidi ya shilingi bilioni 360 kwenye korosho na takribani shilingi bilioni 200 kwenye zao la ufuta. Hii ina-reflect namna ambavyo vijana wetu wanahamasika katika ajira na kujiajiri wenyewe kwenye eneo hili la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?

MWENYEKITI: Ndiyo.

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia. Tunaomba tusaidiwe kuondolewa migogoro ya wafugaji kwa sababu kuna wafugaji wengi sana wanahamia kwenye Mikoa yetu ya Lindi, mkoa ambao ni wa wakulima. Tunashindwa kufanya kilimo kizuri kutokana na mashambulizi makubwa ya mifugo.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)