Supplementary Questions from Hon. Zainab Rashid Kawawa (8 total)
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Katika Mkoa wa Lindi, Halmashauri za Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Mtama pamoja na Kilwa, hazina masoko ya kisasa. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri hizi zinajengwa masoko ya kisasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, utaratibu wa masoko ya kimkakati huwa yanaanza na andiko kutoka kwenye Halmashauri husika. Andiko hilo huwasilishwa TAMISEMI, nasi kwenye Wizara yetu hufanya mapitio na baadaye kulipeleka kwenye Wizara ya Mipango ambao wakiridhia hulifikisha Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupatiwa fedha na kuanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, hivyo, kwa uhitaji alioutaja Mheshimiwa Mbunge wa Mkoa wa Lindi, ninawaelekeza Wakurugenzi wa maeneo yote yaliyotajwa kuwa na ushirikiano na wawakilishi wa wananchi ili kufuata hatua hizo na hatimaye Serikali iweze kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi wanatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha za ujenzi wa barabara ya kilometa 10 kwa Barabara ya Liwale – Nangurukuru. Barabara hii ina jumla ya kilometa 231. Pia barabra hii ndiyo kitega uchumi kikubwa sana kwa wanachi wa Liwale pamoja na wa Wilaya ya Kilwa...
SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais sifa moja kubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya 100%, je, ni lini sasa tutafuta kilio cha wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kutukamilishia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ili sasa Wilaya ya Liwale iweze kuunganishwa na wilaya nyingine kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Lengo la Wizara, na kama alivyosema Awamu ya Sita ni kujenga barabara zote na hasa zinazounganisha barabara kuu na makao makuu ya wilaya ama makao makuu ya wilaya na makao makuu ya mkoa, ikiwepo hiyo Barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 231.
Mheshimiwa Spika, tumeshaanza kutoa hizo kilometa 10, lakini kikubwa zaidi katika hiyo barabara Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami, kulikuwa na changamoto kubwa sana za madaraja. Sasa tumejenga madaraja mengi sana katika huu mpango wa dharura ambao unaendelea kukamilisha ili kuhakikisha kwamba wakati tunatafuta fedha ya kujenga barabara yote wananchi hawa wawe na uwezo wa kupita kipindi chote cha mwaka.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale katika Mkoa wa Lindi haina kituo rasmi cha Polisi na wilaya hiyo ilishatenga eneo kubwa na zuri kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, ni lini sasa Serikali itatujengea kituo cha Polisi cha daraja A?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Zainab kwa swali lake la msingi la kuomba Kituo cha Polisi cha Wilaya ambapo kwa sasa hakipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuweke vizuri kumbukumbu; kwa kuwa ni Kituo cha Polisi cha Wilaya, maana yake hakitakuwa daraja A, kitakuwa ni daraja B. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachukua hoja yake, na kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba katika vituo 75 vya wilaya na cha kwake kipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutatoa umuhimu kwenye maeneo ambayo hayana kabisa vituo vya Polisi vya wilaya ili kusudi naye tuweze kumjengea.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bwawa la Mto Rufiji ni lini Serikali itaanza ujenzi wake kwa kuwa tumesubiri kwa muda mrefu ahadi hiyo mpaka sasa hatujaona utekelezaji wake? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vyanzo vya uhakika ambavyo tunavitegemea ni Bonde la Mto Rufiji, kwani litatatua changamoto kwa ukubwa wake katika utoaji wa huduma katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Vilevile tunatamani baada ya kuchukua haya maji kuyapeleka Dar es Salaam, tuyachukue pia tuyapeleke mikoa ya Lindi. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali tayari imeshaanza mchakato wa kumpata mshauri ili aanze kufanya upembuzi yakinifu na baada ya hapo, tuweze kufanya usanifu wa kina, ili kupata gharama ya utekelezaji wa mradi huo. Tukishapata gharama, ndipo sasa Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kuutekeleza mradi huo. Ninakushukuru sana.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Ninaipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi Mmoja mpaka Masasi. Sasa kuna hii barabara inayotoka Masasi mpaka Nachingwea, Nachingwea mpaka Liwale, kilometa 175. Pale tumeambiwa tutajengewa kilometa 75 kuanzia Liwale mpaka Kiangara. Mkandarasi amepatikana, lakini bado hajalipwa fedha na hajaanza kazi. Ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili mkandarasi huyu aanze kazi kutoka Liwale kuelekea kiangara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea hela katika bajeti inayokuja. Tumepanga bajeti, ikipitishwa tutamlipa huyo mkandarasi advance ili aanze kujenga hiyo barabara, ahsante.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaomba nianze kwa kuipongeza Wizara ya Maji kwa jitihada za kutumia maji ya Mto Rufiji kama Mradi wa suluhisho la kudumu la kutuletea maji katika Mkoa wetu wa Lindi ambapo sehemu nyingi zitanufaika. Mradi huu ni mpango wa muda mrefu, lakini bado haujaanza nadhani, kwa hiyo, unatupa tu matumaini.
Mheshimiwa Spika, swali langu sasa, kwa kuwa tunavyo vyanzo vingine vya mito ama vya maji ambavyo vinaweza vikatumika wakati tunasubiria mradi huu uje kuanza, kwa mfano katika taarifa…
SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali…
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: … Kijiji cha Nahama ambacho kina uhaba mkubwa wa maji, tuna vyanzo vya mapango ya Nang’ole katika Kijiji cha Nandete ambavyo vina maji ya kutosha. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kutumia chanzo hiki kama suluhisho la muda, wakati tunaendelea kusubiria mradi mkubwa ambao unakuja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali na umekuwa utaratibu wa Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kulingana na uhitaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini. Ombi la Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kupitia sekta ya maji tunalipokea badala ya kusubiria suluhisho la kudumu. Wananchi wa eneo lake wanahitaji kupata huduma ya maji na sisi tutaenda kufanya hivyo ili waweze kupata maji wakati tukiwa tunasubiri utekelezaji wa mradi mkubwa.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari ya Anna
Magowa iliyopo Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi, ni shule ya watoto wa kike, lakini haina ukuta, ni shule ya bweni na ina watoto wa kike. Je, ni lini Serikali, itajenga ukuta kwa ajili ya kusaidia watoto wale wa kike wasome kwa usalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika shule zetu tunahitaji kuboresha sana usalama na hususani kwa kujenga uzio ili wanafunzi wetu wawe katika mazingira bora na salama zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa
Zainab Kawawa, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Lindi
kwamba hivyo ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali na
tutahakikisha kwenye bajeti zetu za mapato ya ndani ya
halmashauri, lakini fedha Serikali kuu tunazipa kipaumbele shule kama hiyo ili tuhakikishe tunajenga fence na kuboresha usalama kwa wanafunzi wetu.
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Ukisoma ile investment guide inaonesha namna gani Mkoa wetu wa Lindi ni mkoa wa kimkakati hasa kiuchumi, lakini pia una historia nzuri ya kutafuta kupambania uhuru wa nchi mbalimbali za Kiafrika, ina vivutio vya bahari, ina ardhi nzuri ya uwekezaji, inavutia kwenye kilimo pamoja na vivutio vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba Sera ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kujenga viwanja vikubwa katika kila mkoa wa nchi yetu ya Tanzania.
Sasa je, kwa vivutio hivi ambavyo vipo katika mkoa wetu wa Lindi; ni lini Serikali itajenga kiwanja kikubwa cha ndege katika Mkoa wa Lindi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi napenda kumjibu Mheshimiwa Zainab Kawawa ambaye anataka kufahamu ni lini Uwanja wa Ndege wa Lindi utajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana naye na kumpongeza Uwanja wa Ndege wa Lindi ni uwanja umuhimu kiuchumi kama alivyosema kutokana na uzalishaji wa mazao ya kibiashara kama vile korosho, mazao ya chakula na kadhalika, lakini pia pale Lindi Serikali inayo ajenda ya Mradi wa LNG. Hivyo uwanja huu ni muhimu sana acha utalii pamoja na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuujenga uwanja huu na hatua zifuatazo zimekamilika; kwanza kukamilisha usanifu, lakini pili tulikwishatangaza na kumpata mkandarasi lengo ni kujenga uwanja mkubwa wenye hadhi na wa kisasa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 120 na kwa sasa tunachokizungumza ni kutafuta fedha za malipo ya awali ili mkandarasi alipwe na aanze kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kipindi ambacho michakato ya ndani inakamilika na hatimaye tuweze kuanza ujenzi wa uwanja huu.