Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ZEYANA ABDALLAH HAMID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nishukuru kwa kupata fursa hii kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Shukrani zangu nizitangulize kwa Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi Watanzania ni waungwana sana na uungwana anaotuonesha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa Kitanzania, inastahili shukurani za kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine yote tuliyoyatamania katika sekta zote hayatafanikiwa, kama hatutafanya kazi nzuri, ambayo Mheshimiwa Rais ametuonesha maono jinsi ya kupita, wapi pa kuwekeza na namna ya kufanikiwa. Niipongeze sana Wizara kwa kutupangia mpango mahususi, mipango endelevu, mipango inayokwenda kumgusa mwanafunzi wa kila rika toka wa chekechea mpaka wa vyuo na vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Wizara kwa kuwa na sisi, katika safari hii ya elimu na hasa tukiangalia mafanikio yaliyofikiwa kwa mwaka uliopita, ambao wametupa summary leo, lakini kutuwekea mipango inayokwenda kutekelezwa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027. Sisi Wabunge wa vyuo na vyuo vikuu, tuna jicho la ukaribu sana kuangalia vipi tutaweza kuwawasilishia wananchi na kuiwasilishia Serikali kwa ambayo yanabidi yafike kwa wananchi na sekta ya elimu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwenye vitabu vya Imani, kwamba hawatakuwa sawa, wanaojua na wasiyojua. Quran inasema: “Qul hal yastawī al-ladhīna yaalamūna wa-al-ladhīna lā yaalamūn.” Kwenye mafunzo haya tunajiambia, Taifa lililoelewa na lisiloelewa halitakuwa sawa. Nimemwelewa sana Profesa pale alivyotupeleka katika tathmini ya nchi tofauti. Tanzania katika awamu hii, nayo pia imejipelekea katika kuhakikisha tunahama katika Taifa lililokuwa halielewi, na nini tunataka tuelewe, wapi tunataka tuwekeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini, ninaunga mkono hoja hii ya Bajeti ya Elimu? Tumeona namna dira ya Wizara imekwenda moja kwa moja, kutoa Taifa lenye skill transformation. Hii nitapita katika vipengele tofauti, ambavyo leo Waziri ametuonesha katika mpango huu. Tunaipongeza Wizara kwa kutuandalia mpango mahsusi wa vyuo viwanda na waajiri, kwa sababu huku ndiko tunakwenda kulijibu lile suala, vijana tunaowasomesha wataajirika vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye huu mpango, wamelenga kwanza moja kwa moja kwenda kuboresha curriculums. Mitaala itakapouliza au itakapohoji, waajiri wanataka nini? Ndiyo tutarudi kuhakikisha tunasomesha kwa malengo na tunawashirikisha vijana wetu, wajitayarishe kujitoa katika vijana wenye malengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu umetuletea mfumo mpya wa usomeshaji ambao ni work based learning. Work base learning, inabinua juu chini, chini juu, elimu kutoka kwenye nadharia kwenda kwenye vitendo na hizi zipo nyingi. Kuna ambazo tutakuja kuziona wakati wanazitekeleza, za problem based learning ambayo inachukua tatizo mahsusi kutoka kwenye sekta, linalileta darasani na vijana wetu wanali-innovate and then linarudi kwa waajiri kulitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna learning based models ambazo zinatestiwa, zinasomesheka vipi na tunachanganya taaluma kutoka nje pia, kuona hizi taasisi zinazoajiri zitawatayarisha vipi vijana wetu. Mpango pia umeona umuhimu wa innovations na hivi vitu ambavyo vinabidi vitengewe fedha, saa nyingine vinakuwa ni vya majaribio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Innovations zinatumia resource kubwa za labs na tumeona vyuo vingi ambavyo vinahitaji laboratory za viwango vya juu, kuweza ku-test hizi kazi za wanafunzi, kuweza kupata data za namna mafanikio haya yanapatikana. Pia, information decisiyon making nazo tumezishuhudia kwenye huu mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha inayohitajika kuweka sustainability ndiyo ambayo Wizara inatuomba leo tuiwekeze. Sababu nyingine za kuunga mkono hoja, ni kuangalia namna vyuo, hasa vya kati, vya amali, vya mafunzo stadi, ambavyo vimekwenda kuwekezwa. Lile ongezeko la vyuo 32, ni sawa na 84% nayo inawekeza katika kuwajengea uwezo vijana kwa vitendo, namna vilivyotawanywa katika mikoa, wilaya na pia halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ujenzi wa vyuo vikubwa vitano vya Polytechnic na tunaishukuru sana Wizara kwa kutuletea chuo kimoja Zanzibar. Vyuo hivi vya ki-polytechnic, siyo tu vinajenga uwezo wa vitendo na elimu stadi kwa ngazi ya kati, lakini kwa hali ya juu ambayo moja kwa moja inaweza kwenda kutumika katika sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatuomba shilingi bilioni 250, kwenda kuwekeza katika vyuo hii vya polytechnic. Ninaunga mkono hoja na kwa kuangalia zaidi miradi, kuna mradi wa educational skill for productive jobs, kuna miradi ambayo tumeiona katika skills and transformation for regional integration na miradi hii nayo inakwenda moja kwa moja kuwekeza skills au study.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudia nasaha ambazo Rais, Mheshimiwa Dkt. Ruto alitupa kuhusu maadui wa nchi mbalimbali. Akatuambia kwamba, adui huyu ni ukosefu wa ajira na tukichanganya haya ambayo tumeyaona, ni wazi kwamba, adui siyo tu ukosefu wa ajira, lakini kukosa kutumia rasilimali zetu za nchini kuchanganya na elimu ambayo tunaisomesha ili kutengeneza ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba niunge mkono hoja, kwa sababu tuna kila uwezo wa kutengeneza ajira. Tuna kila uwezo wa kusomesha. Tuna kila uwezo wa kuwekeza na kuiunga mkono sekta hii kwa sababu ya kubadilisha mindset za elimu, kutoka elimu nadharia kwenda kwenye elimu ya vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)