Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ali Khalil Mirza (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ALI KHALIL MIRZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu ili kuchangia, ninapenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima nikaweza kufanikisha shughuli hii. Aidha, ninachukua nafasi hii pia kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kukiwakilisha chama chetu katika Jimbo la Kiembe Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwendelezo huo huo ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni hii. Kwanza ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye maono, yenye maelekeo, inayotia moyo na inayoonekana inaelekea wapi katika kuliendeleza Taifa letu, hasa katika sekta hii ya nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna maendeleo ya uchumi au ya jamii yanayoweza kuendelea bila nishati iliyokuwa ya uhakika na nishati ambayo itakuwa na bei nafuu. Tumeona mipango yetu ya Dira 2025 – 2030 na 2030 – 2050, imeelekeza kwamba kwanza kuwe na uchumi utakaokuwa kutoka asilimia 5.7 kwenda asilimia saba na pia kuelekea katika uchumi wa shilingi trilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo hayo ambayo yanatarajiwa yote yanategemea nishati ya umeme. Hakuna maendeleo, hakuna uwekezaji na hakuna ukuaji wowote wa biashara na uchumi utakaoweza kufanikiwa bila umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeziona juhudi ambazo zimechukuliwa chini ya uongozi wa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuongeza umeme kutoka uliokuwa megawati 1,400 hadi leo megawati 2,500. Hayo ni maendeleo makubwa ambayo yataweza kubeba matumaini ya sisi kuendelea kama uchumi wetu ulivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uendelezaji wa nishati ya umeme, sera ya nishati ya umeme imeeleza kwamba tunaweza kuwa na umeme mbadala na vyanzo mbalimbali. Hilo ni moja ambalo limezungumzwa tangu asubuhi, kwa hivyo ninapenda kulisisitiza kwamba tuingie katika umeme mbadala katika nyanja mbalimbali; umeme wa jua, umeme wa upepo, umeme wa bahari na kadhalika. Hiyo itatupa uhakika zaidi, umahiri zaidi wa upatikanaji umeme uliokuwa wa uhakika na umeme ambao utakuwa wa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia suala la umeme ninapenda kuzungumzia kidogo suala la gesi. Tuna mazungumzo yanayoendelea ya gesi ya shilingi bilioni 42; na hii ndiyo game changer katika nchi yetu. Mazungumzo hayo tunaomba yaendelee vizuri na yatakapokamilika ninategemea kwamba nchi yetu itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo, lakini pia mapato ya nchi yatazidi kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sisi tunaendelea katika mazungumzo hayo, ningeshauri taasisi inayosimamia masuala ya gesi na petroli ikajitayarisha katika eneo la elimu. Tunahitaji kuwafunza vijana wetu, tunahitaji kuwapeleka katika vyuo mbalimbali ili tujitayarishe kabisa katika hizo technicalities za eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu kwa upande wa technically, hata kwa upande wa wale watakaoingia katika mazungumzo (negotiations), sisi tunahitaji ku-develop katika negotiation skills zetu ili tuweze kuwa sawasawa na wale ambao sisi tutakuwa tunazungumza nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hayo, ninapenda kuunga mkono moja kwa moja Wizara hii. Ahsante sana. (Makofi)