Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kassim Hassan Haji (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia Wizara hii yenye dira na taswira ya wanafunzi wenzetu; wanafunzi ambao tunaamini katika bajeti hii wanakwenda kupata maendeleo makubwa zaidi, hususan katika trilioni ambazo ameziweka Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshauri Mheshimiwa Waziri. Bajeti hii ni kubwa sana na bado katika maeneo ya vijijini tuna majengo ambayo hayajamalizika, majengo ambayo hayana ubora. Kwa hiyo nimwoombe sana Mheshimiwa Waziri, kwamba fedha hizi zitakapoingizwa aende akakamilishe majengo yale ili wanafunzi hawa waweze kusoma katika maeneo ambayo yatakuwa mazuri na maeneo ambayo yatawasaidia hata walimu kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwanza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa nafasi za walimu 12,678, si jambo dogo katika kuboresha mambo ya elimu. Lililobaki sasa kwao Mheshimiwa Waziri ni kwenda kuboresha mambo mazima ya walimu wenyewe. Waende wakawaboreshee posho zao, waende wakawaboreshee angalau na wao wapate motisha ya kwenda kutembea katika maeneo mengine, ili haya mambo yaweze kwenda vizuri na watoto wetu wapate elimu nzuri ili na wao waweze kuwa na nguvu ya kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja leo inabidi hapa nilizungumze kidogo. Mimi na Mheshimiwa Waziri tunakaa jirani pale, hebu kesho au kesho kutwa, atoke saa kumi na mbili. Sisi tunaokwenda mazoezi huwa tunawaona watoto wale wa kindergarten, wanatolewa majumbani na mabasi saa kumi na mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukaangalie hii sera kwa kweli. Hawa watoto wadogo ambao wako KG 1, KG 2 kutoka saa 12.00, hata kama ndiyo tunatengeneza watu wazuri, lakini kwa wao ninaona bado. Twende tukaangalie hii sera ya kuona wao angalau waweze kutoka saa 4.00 kwenda shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaomba nigusie suala dogo tu; ninaomba twende tukaangalie sana, twende tukawashauri wenzetu wa Zanzibar, katika sera nzima ya kwao ya elimu ya amali iweze kuungana na VETA. Kuna tatizo, bado watoto ambao wanamaliza katika vyuo vya amali Zanzibar, wanapokuja kufanya application katika sehemu za kazi bado ni tatizo katika vyeti vyao. Vyeti havisomani na mifumo ya vyeti bado haijawa sawa. Nimwombe sana Mheshimiwa, wafanye kama memorandum au jambo lingine lolote ambalo linaweza likawasaidia na wao waendane na elimu hii elimu ya VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha vyuo vya amali. Vyuo vya amali hivi kwetu tunaona ni taswira nzuri, vilevile vitaleta tija kwa sababu wengi wao ambao wanamaliza katika vyuo hivi wanaenda kujiajiri wenyewe bila kupitia katika ajira za Serikali. Nimwombe sana Mheshimiwa wavisaidie vyuo hivi. Wamezungumza hapa, hapa, na wamesema kwamba wanakwenda kuvijenga, na wanakwenda kuvimalizia. Siyo kuvijenga na kuvimalizia, tuviwekee na vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi dunia iko katika utandawazi, watu wanaenda katika TEHAMA; twende tukawasaidie hawa, angalau wanapomaliza katika vyuo hivi basi na wao waweze kujiajiri bila kutegemea Serikali hizi ziwape ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la msingi kabisa; kuna watoto ambao wanafanya michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA. Tumezungumza hapa, kwamba tunatengeneza shule nyingi za vipaji, shule nyingi za mikoa, na shule nyingi za wilaya; Mheshimiwa Waziri hebu akajikite sasa kuweka shule hizi za vipaji maalum kwa watoto hawa ambao tunawategemea katika michezo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano imeanzishwa shule ya Malya, kuna watoto ambao wanakwenda katika michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA wako ambao tunawapa zawadi kwa sababu wao ni watoto waliofanya vizuri. Watoto hawa tuwachukue, kutokana na vipaji vyao tutengeneze kanda ambazo zitakwenda kusaidia vipaji hivyo ili na wao waweze kujiajiri baada ya kumaliza katika shule hizo na waendeleze vipaji vyao. Kama tunavyojua sasa hivi vipaji ni ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, kwa kuzingatia hoja hizi ninaomba bajeti hii, Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ipewe kipaumbele cha kutosha ili kwenda kuweka mfumo mzima wa elimu katika ubora. Vilevile, tumsaidie Mheshimiwa Rais ili maono, dhamira na matakwa yake ya kusema kwamba, sasa hivi tunakwenda kulifungua Taifa letu na kwamba elimu ndiyo iwe kila kitu, basi twende tukaipitishe bajeti hii kwa nguvu zote na kwa umoja wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)