Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuleta maendeleo; na sisi watu wa Mkoa wa Katavi tumenufaika sana baada ya fedha nyingi zilizoletwa kwenye mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, kwenye halmashauri yangu tu tumepata shilingi bilioni 558 ambazo zimekwenda kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ya Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo na nyinginezo. Tunamshukruu sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kusukuma maendeleo. Ziara ambazo anazifanya zina mafanikio makubwa sana ndani ya nchi yetu, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite sana kwenye suala la miundombinu. Tumebahatika kupata mvua nyingi kwenye nchi yetu ambayo kimsingi imekuja kuharibu suala la miundombinu ya barabara za vijijini, mijini na barabara kuu. Eneo hili tunahitaji kupata fedha za kutosha ili tuweze kukarabati miundombinu iliyokufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti tulizonazo za TARURA za barabara kuu, hazitaweza kumudu kukarabati barabara ambazo zimeharibika. Nina ushauri kwa Serikali; ninaomba sisi Wabunge tuchukue dhamana zetu kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumsaidia Mheshimiwa Rais ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo tutaishauri Serikali kuweza kwenda kuvifanyia kazi. Ninaamini kuwa Serikali ikikubali mawazo ya Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukatoka mahali ambapo kwa sasa tupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri, kama tukikubaliana, la kwanza, Serikali iendelee kudhibiti Mfuko wa Barabara ambao tumekuwa tukichangia kupitia tozo mbalimbali. Ile Mifuko ambayo imewekewa ring fence lazima iheshimiwe. Tunaomba tuweze kuanzisha chanzo kipya cha mapato. Tukianzisha kwenye Mfuko wa Mawasiliano ambao utakwenda kusaidia kupata fedha za kukarabati miundombinu iliyoharibika, tuna nafasi ya kuweza kwenda kukarabati barabara zilizoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kuwa wataalam wetu wakikubali tunaweza tukapata fedha takriban shilingi trilioni moja kwa shilingi mia moja tu, ambayo tukikubaliana tuiweke kwenye muda wa maongezi inaweza kwenda kusaidia kupunguza tatizo tulilonalo kwa sasa la uharibifu wa miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi trilioni moja ikipatikana igawanywe iende kwenye barabara za TANROADS na iende kwenye zile barabara zinazomilikiwa na TARURA. Itatusaidia sana kutatua kero ambayo ipo takriban kila mkoa, takriban kila wilaya na kwenye vijiji na kata zetu ambazo zimeathirika sana baada ya mvua nyingi zilizonyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa yetu ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni mikoa ambayo inapata mvua nyingi sana. Mvua zilipozidi sisi Mikoa ya Katavi na Kigoma ilijifunga kwa sababu madaraja yaliathirika kwa kiwango kikubwa sana. Ninaomba hili tulifanyie kazi; na sisi Wabunge tuchukue dhamana zetu kwa kuishauri Serikali tuisimamie ili waweze kupata fedha ambazo zitaenda kukarabati miundombinu ya barabara zilizoharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninapenda kuipongeza Serikali ni kwenye suala la uvuvi haramu kwenye Ziwa Tanganyika. Ninaipongeza Serikali wameanza juhudi za kwenda kutafuta nyavu zile ambazo zina uharibifu mkubwa kwenye eneo la Ziwa Tanganyika. Maisha ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma, maisha ya wananchi wa Mkoa wa Katavi na Rukwa wanaoishi pembezoni na Ziwa Tanganyika yanategemea shughuli za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo lipo ni wananchi wanaovua kwa kutumia nyavu zile ambazo zimepigwa marufuku. Zipo nyavu maarufu zinazoitwa filimayaya ambazo asili yake zinatoka Nchi ya Burundi, Congo na Rwanda; ndiyo wanaoziingiza zile nyavu na zile nyavu zinahatarisha maisha yote ya viumbe hai vilivyopo kwenye Ziwa Tanganyika. Hata yale ambayo Mheshimiwa Chipando, Mbunge wa Kigoma alikuwa anayazungumzia wala si ya uongo, ni ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maisha ya Watanzania wa ukanda wa ziwa yanategemea uvuvi. Niiombe Serikali, juhudi ambazo imeanzisha kwa sasa za kupiga marufuku na kufanya ile operation inayofanyika kwa sasa ndizo zifanyiwe kazi kuliko yale mawazo ya kufunga ziwa. Unapofunga ziwa hujapata suluhu, suluhu ni kwenda kufanya operations ambazo zitawafanya wale wamiliki waweze kuacha uvuvi haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua tu iliyofanyika juzi, operation ambayo imefanywa ndani ya Mkoa wa Kigoma na mpakani mwa Mkoa wa Katavi imewafanya wale wavuvi haramu na wengi wao ni watu wanaotoka DRC Congo na wanaotoka Burundi wamekimbia. Wengine wanasubiri sasa hali itakapokuwa imepoa warudi tena kwenye yale maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, katika hiki kipindi ndipo ambapo wafanye operation ya bila kikomo ili kutoa tatizo la uvuvi haramu. Suala la kufunga Ziwa, sisi ndiyo tunaowanyanyasa wananchi wetu. Burundi hawafungi Ziwa na Congo hawafungi Ziwa; tunaofunga ni sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki hawana mipaka. Inapokuwa huku kumekuwa na hali ya unafuu, wale Wakongo ndiyo wanaokuja kuvuna rasilimali ambazo tumejiwekea sisi wenyewe. Ninaomba hili wakalifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwenye eneo la miradi iliyoletwa na Serikali. Mkoani kwangu nimepokea fedha za maendeleo, nimepata fedha za kujenga kituo cha afya, tumepata fedha za kujenga zahanati na miradi ya elimu. Tatizo lililopo kwenye Ofisi ya TAMISEMI, vibali kwa ajili ya miradi hiyo kufanyika hawatoi. Wanapeleka fedha, zinafika zinakaa. matokeo yake zile fedha zitatolewa kipindi cha mwishoni. Unapoziruhusu mwezi Mei, haziwezi kufanya kazi, mwezi Juni mwishoni zinarudi tena Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali waharakishe kutoa vibali ili waweze kufanya ile miradi ikamilike kwa sababu malengo ambayo wameyafanya ni kwenda kutekeleza ile miradi ya maendeleo. Hili ni la muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwa kuishauri Serikali kwenye eneo la hewa ukaa. Serikali tumekuwa tukiishauri mara kwa mara, kwenye eneo hili lazima tuweke mkakati wa uvunaji wa hewa ukaa ili tuweze kupata fedha za ziada ambazo zitaisaidia Serikali kwenye miradi ya maendeleo. Kwa bahati mbaya sana kumekuwa na urasimu mkubwa sana kwenye eneo hili. Mkoani kwangu tuna msitu ambao umekaa zaidi ya miaka mitatu, tunataka uwekezaji uwekezwe lakini maamuzi ya kutoka Serikalini yanachukua muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hili walifanyie kazi watoe ule urasimu ambao unafanyika, waondoe vikwazo ili watu waweze kupata haki na stahiki za kwao. Tuna misitu mingi ambayo ipo kwenye halmashauri ikiwemo misitu inayomilikiwa na TANAPA. Huko wakiweka sheria ambazo zinaweza zikaruhusu uvunaji, Taifa litapata fedha nyingi na wanapata chanzo kipya cha mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya. Tunaishukuru Serikali kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kuipongeza Serikali kwa kutenga fedha shilingi bilioni sita kwa ajili ya upembuzi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kuyaleta Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi. Mradi huu kwetu sisi ni mradi muhimu ambao utakuja kutatua kero ya maji ndani ya Mkoa wa Katavi kwenye eneo langu takribani vijiji 20 watanufaika na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kasi uliyonayo na ukizingatia wewe ndiye tulienda pamoja kuangalia kile chanzo cha maji kwenye Ziwa Tanganyika, ni vizuri sasa mkaelekeza nguvu ili kutatua kero ya maji kwenye eneo hilo la Mkoa wa Katavi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana kwenye Mradi wa Kalema – Kapalamsenga, Kijiji cha Itetemia na Itunya huu mradi ni mradi wa muda mrefu takribani shilingi bilioni 1.3 zilitengwa, hatua ya awali ilishafanyika utandazaji wa mabomba ulishakamilika umebaki hatua ya kujenga tenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana mkandarasi aliyepewa mradi huu alipolipwa shilingi milioni 181 aliondoka jumla, ameutelekeza ule mradi. Niiombe Serikali imfuatilie mkandarasi ili aweze kujenga lile tenki wananchi waweze kunufaika. Mradi huu umechukua muda mrefu, sasa ni mwaka wa tatu haujakamilika. Niombe sana Mheshimiwa Waziri hili ni jambo ambalo ukilitekeleza utakuwa umetusaidia sana wananchi wa Wilaya ya Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni mradi wa Kijiji cha Katobo, mradi ambao una thamani ya shilingi bilioni 1.7. Mradi huu unategemea kuhudumia Vijiji vya Kambanga, Igalula na Ifukutwa. Mradi huu ulishatengewa fedha, lakini bado fedha hazijafika kwa wakati, tunaomba mradi huu uwekee maanani na utenge mazingira ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Mji wa Majalila; Mji wa Majalila ni mji ambao unakua chanzo chake cha maji kilishazidiwa kwa kuwa tuna idadi zaidi ya watu 10,000 wanategemea kupata huduma ya mradi wa maji. Niombe sana Mheshimiwa Waziri mahitaji ya mradi huu tunahitaji ujenzi wa tenki ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua lita milioni moja ili uweze ku-supply kwenye maeneo yale ambayo wananchi wanahitaji kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utahitaji fedha takribani shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuchimba kisima kipya na kujenga tenki ambalo litasaidia kupeleka huduma kwa wananchi na kutatua kero ya wananchi kwenye maeneo hayo. Eneo hili ni muhimu ndiyo Makao Makuu ya Wilaya, Hospitali ya Wilaya wanakosa maji, wananchi wanakosa huduma kwa sababu maji yaliyopo sasa hivi hayatoshelezi kulingana na idadi na taasisi za Serikali kuwa nyingi kwenye maeneo hayo. Niombe sana hili ulifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kuishauri Serikali, naungana mkono na namuunga mkono ndugu yangu Mheshimiwa Mnzava, Mheshimiwa lazima tujenge msingi wa kuvuna maji. Mheshimiwa Rais wa Kwanza, Mwalimu Nyerere alijenga mabwawa karibu kila kona ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwangu kwenye Kijiji cha Majalila kulikuwa na Bwawa la maji ambalo lilikuwepo na lilitoa huduma kubwa sana, lakini sasa hivi tuna majengo mengi ya Serikali ambayo yanajengwa mkishirikiana na Wizara ya TAMISEMI mnauwezo kabisa kila nyumba ya Serikali inayojengwa iwekewe mazingira ya uvunaji wa maji itasaidia sana kutatua kero ya maji katika maeneo mengi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili halijafanyiwa kazi ipasavyo, ni vyema tukatunza vyanzo vya maji, lakini tukajenga msingi ambao kupitia fedha zile zinazoidhinishwa kwenye Wizara mbalimbali, kwenye majengo ya Serikali yanaweza kabisa yakatufanya sisi nchi yetu tukatatua tatizo la maji ambalo lipo karibu kila kona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nasisitiza tunahitaji Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika uweze kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Rukwa ambao kimsingi hawajanufaika na upatikanaji wa maji kutokana na resource ya maji zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono. (Makofi)