Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mecktridis Fratern Mdaku (2 total)

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA K.n.y. MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Ifakara – Lupilo hadi Malinyi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mecktridis Fratern Mdaku, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Ifakara – Lupilo hadi Malinyi kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu ilikuwa ni kukamilisha ujenzi wa daraja la Magufuli (meta 384) katika Mto Kilombero pamoja na barabara ya maingilio (kilometa 9.143) ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa katika barabara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa sehemu ya Ifakara – Lupilo – Mtimbira yenye urefu wa kilometa 112 ambapo taratibu za malipo ya awali kwa Mkandarasi ili aweze kuanza kazi zinaendelea. Kwa sehemu zilizobaki, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi.
MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea maeneo ya kilimo Wananchi wa Malinyi baada ya maeneo yao kuingizwa kwenye Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali kupitia Tangazo Na. 64 la tarehe 24 Februari, 2023 ilitangaza baadhi ya maeneo ya Wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero kuwa sehemu ya Pori la Akiba la Kilombero kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji vya Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa wakilima mpunga waliathirika baada ya maeneo yao kuingia kwenye Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeweka mkakati wa kupanua na kuboresha skimu za umwagiliaji za Itete hekta 850 na Bonde la Usangule hekta 12,000 ili kutoa maeneo mbadala ya kilimo chenye tija kwa wananchi walioathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi hii ambapo ujenzi wa skimu ya Itete umefikia 64% na upembuzi yakinifu wa bonde la Usangule umefikia zaidi ya 80%. Skimu hizi zikikamilika zinatarajiwa kunufaisha wakulima zaidi ya 9,000. Sambamba na hilo, Wizara itaendelea kutoa elimu ya kilimo bora ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.