Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mecktridis Fratern Mdaku (4 total)

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina Miradi ya Maji katika Kijiji cha Misegese – Ihowanja na Mtimbira na miradi hii imekaa muda mrefu zaidi ya miaka mitatu sasa bila kukamilika. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha miradi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, ni Mbunge mahiri, na pia ni Mjumbe katika Kamati yetu ya Maji na Mazingira, tunaendelea kutambua mchango wake mkubwa sana katika kuishauri Serikali na kuisimamia. Katika kuwatetea wananchi wake, sisi tutaendelea kumpa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo madai ya wakandarasi ndani ya Jimbo lake, na tayari yameshaletwa na yameshafika kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu, wanayafanyia kazi. Tunaamini kabisa kwamba ndani ya kipindi cha miezi miwili mitatu hii, tutapeleka fedha ili wakandarasi hawa walipwe ili miradi hii ambayo imekaa kwa muda mrefu iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali, siyo hiyo miradi pekee, miradi yote inayoendelea kutekelezwa nchini tunayo maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba tunakamilisha kwanza hii miradi ambayo imeishaanza badala ya kuanza miradi mipya ili kuhakikisha kwamba tunaanza kupata matokeo kabla ya kuanzisha miradi mingine mipya. Ninakushukuru sana.
MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina mtandao wa mita chache za lami. Je, ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuongeza kupitia programu ya kuboresha Halmashauri za Wilaya au Makao Makuu ya Wilaya kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, Mheshimiwa Mecktridis amelifuatilia suala la Barabara za Malinyi mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tunaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe na pale inapowezekana kuendelea kujenga barabara kiwango cha lami na tutahakikisha kadri fedha zinapopatikana tunatoa kipaumbele cha juu kabisa kwa ajili ya Mji wa Malinyi.
MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano katika maeneo ya Jimbo la Malinyi hususan katika Kata za Usangule, Mtimbira, Biro pamoja na Ngoeranga.

Je, ni lini Serikali itakwenda kujenga minara katika maeneo yao hayo ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatekeleza mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa minara katika maeneo yote yenye changamoto ya minara hapa nchini. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu huu, tutayafikia maeneo yote yenye changamoto ya umeme yakiwemo maeneo aliyoyataja hayo. Kwa hiyo, mpango wetu huu wa miaka mitano unakusudia kutatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya mawasiliano nchini kama sio kuyamaliza kabisa. Nakushukuru.
MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia ninaipongeza Serikali kwa jitihada zake inazozifanya katika Jimbo la Malinyi kwa kuboresha na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kuwa siyo vizuri kuchukua maeneo ya wananchi na kuyaingiza kwenye Hifadhi za Taifa kabla ya kuwapa maeneo mbadala kwa ajili ya kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Mheshimiwa Mecktridis Fratern Mdaku, Mbunge wa Jimbo la Malinyi kwa swali lake zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia concern yake kuhusu wananchi wake, lakini moja nimhakikishie, Serikali inapokuwa inachukua eneo lolote, ni lazima inakuwa imeshafanya utaratibu wa kuhakikisha tumewashirikisha wananchi, lakini nia kubwa inakuwa ni kuwasaidia wananchi wenyewe. Kwa hiyo, hata ukiangalia kwenye hili bonde, lengo kubwa ni kuhakikisha tunahifadhi kwa ajili ya kupata vyanzo vya maji vya mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Hilo ndilo lengo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa cha kumkuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliunda Kamati ya Mawaziri nane, ambayo moja ya jukumu alilotupatia ni kuhakikisha tunapotengeneza mradi wowote, Wizara zote za kisekta zinazohusika katika eneo husika, yaani kwa mfano kwenye hilo bonde, kuna Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na zile Wizara zote za kisekta zinakuwa zinahusika katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba sisi kama Wizara za kisekta tutakaa pamoja na kuangalia yale maeneo ambayo tunapaswa kuwasaidia zaidi wananchi ili kuhakikisha tunapata tija ambayo inaleta matokeo kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.