Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Wilson Charles Mahera (2 total)

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza maji Kata za Bisumwa, Bukabwa, Nyankanga, Butuguri, Bwiregi, Buruma, Kyanyari, Buhemba, Mirwa na Kikirango?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Wilson Mahera Charles, Mbunge wa Jimbo la Butiama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Mradi mkubwa wa Maji ya Ziwa Victoria wa Mugango – Kiabakari - Butiama uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 70 na unanufaisha wananchi kwenye Kata za Wilaya za Butiama na baadhi ya maeneo ya Wilaya za Bunda pamoja na Musoma Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mradi huo umeanza kutoa huduma kwenye vijiji 22 vinavyopatikana kwenye kata saba za Wilaya za Butiama na Musoma Vijijini. Aidha, kazi ya upanuzi wa mradi huo inaendelea kwa awamu kadiri fedha zinavyopatikana ili kuweza kufikisha huduma ya majisafi na salama kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ikiwemo baadhi ya vijiji vya Kata za Bisumwa, Bukabwa, Nyankanga, Butuguri, Bwiregi, Buruma, Kyanyari, Buhemba, Mirwa pamoja na Kikirango.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa majengo muhimu yanayohitajika katika Hospitali ya Wilaya Butiama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, naomba kumjibu Mheshimiwa Dkt. Wilson Mahera, Mbunge wa Jimbo la Butiama:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Butiama ni moja kati ya hospitali 25 ambazo zimejengwa katika awamu ya tatu ya ujenzi wa hospitali za halmashauri ambao ujenzi ulianza mwaka 2021/2022. Jumla ya majengo tisa yamejengwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Butiama kwa gharama ya shilingi bilioni 3.02.

Mheshimiwa Spika, majengo yaliyokamilika ni pamoja na jengo la OPD, maabara, EMD, jengo jumuishi la uzazi, yaani martenity complex. Aidha, jengo la OPD limekamilika na huduma za wagonjwa wa nje zimeanza kutolewa mwezi Novemba, 2024.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imetengewa shilingi milioni 500, kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo yaliyosalia. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika hospitali za Halmashauri Wilaya ya Butiama.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.