Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Wilson Charles Mahera (5 total)

MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Bwilegi ni miongoni mwa kata ambazo vijiji vyake vipo mbalimbali sana katika Wilaya ya Butiama, lakini Kijiji cha Lyamsanga sasa hivi kwa muda wa miaka miwili, wananchi wameshakusanya mawe na mchanga trip 50 na kokoto trip 16. Je, lini Serikali itapeleka fedha ili wananchi wa Kijiji cha Lyamsanga waweze kupata shule ya sekondari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Butiama na ninawapongeza sana wananchi kwa kutoa nguvu zao kukusanya mawe na mchanga, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ya sekondari. Ninaomba kutumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama, walete taarifa rasmi ya maandalizi kwanza, kama eneo linakidhi vigezo vya kuwa na shule hiyo ya sekondari. Pili, walete taarifa ya maandalizi kupitia mapato ya ndani na Serikali Kuu iweze kuona namna bora zaidi ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa shule hiyo ya sekondari.
MHE. DKT. CHARLES W. MAHERA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Busegwe – Kitaramanka, yenye urefu wa kilomita 18 inapita katika kata tano za Busegwe – Mliaza – Buhemba na Mirwa, pamoja na Sirorisimba. Barabara hii ni muhimu sana kwenye shughuli za kiuchumi katika Jimbo la Butiama.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipokuja Butiama tulimwomba aweze kuipatia lami barabara hii akaridhia na kwa umuhimu wa barabara hii, ni Barabara ya TARURA, lakini inasimamiwa na TANROAD. Sasa swali la msingi, je, ni lini usanifu utaanza wa barabara hii, ili kusudi tuweze kupata lami katika Jimbo la Butiama?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ahadi za viongozi wetu wakuu wa nchi na hususan Mheshimiwa Rais, ni maelekezo kwetu sisi wasaidizi wake ndani ya Serikali. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge Mahera kwamba, tunaendelea na utaratibu wa kupitia ahadi zote za viongozi wetu wakuu kwa nchi nzima na tumekuwa tukitekeleza kwa kadiri ambavyo fedha zinapatikana.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Butiama ina kata 18, lakini kati ya hizo, kata tisa tu ndiyo zenye vituo vya afya. Pia kuna kata kubwa kama vile Buruma, Buiregi, Bumangi, hazina vituo vya afya. Je, Serikali ina mpango gani kujenga kituo cha afya angalau kwenye kata ya Buruma yenye vijiji sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Serikali inapongeza kwa maana ya kwamba tayari ana vituo tisa ndani ya kata 18, wakati huo kuna baadhi ya kata 14 ina vituo viwili. Kwa hiyo, ni juhudi kubwa ambayo imefanyika na tunaendelea kushirikia na Mheshimiwa Mbunge kuona ya kwamba tunazidi kuongeza vituo vya afya katika jimbo hilo.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuletea mradi mkubwa wa maji wenye uwezo mkubwa sana wa kuweza kuzalisha lita milioni 35 kwa siku, lakini kwa sasa ni lita milioni 17. 5 kwa siku, ila mradi huo kwa sasa unatoa lita milioni tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuweza kusambaza maji katika vijiji ambavyo vinausubiri kwa hamu kubwa, kuna miradi miwili ambayo iko Wizarani ya 4.8 billion na 3.5 billion. Je, ni lini Wizara itatoa kibali ili miradi hiyo iweze kutangazwa wakandarasi wapatikane? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa vile mradi huu ni mkubwa sana na utafika kwenye Kata ya Mirwa, tunayo Kata ya jirani ya Sirorisimba ambayo iko karibu na Wilaya ya Serengeti na Kijiji cha Baranga Kata ya Buswahili hawana mradi wa maji. Je, Wizara ina mkakati gani wa kuanza kuandaa mradi ili vijiji hivyo navyo vipate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, nilipata ziara katika Jimbo lake na alikuwa kwenye safari zake, lakini aliamua kuahirisha na kurudi jimboni kwake ili tuweze kufanya ziara kwa pamoja. Ninampongeza sana kwa namna ambavyo anaendelea kuguswa na changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo lake ni 78%, lakini tunayo miradi miwili inayoendelea yenye gharama ya shilingi bilioni tano lakini vilevile, mradi huu ambao Mheshimiwa ameongelea, ni mradi ambao unatokana na ahadi za Viongozi wa Kitaifa. Ni mradi ambao sisi kama Serikali na sekta ya maji ni lazima mradi huu utekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mradi huu ninaufahamu vizuri kwa sababu nina picha nzima ya Butiama. Kikubwa tu ni kwamba ile taarifa ambayo amesema, ilishafika Wizarani, ninaomba nimhakikishie kwamba haijafika mpaka sasa, lakini tumeshawasiliana na watu wetu ili waweze kuileta kwa haraka ili tuhakikishe kwamba tunachukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu wa Buhemba utakapotangazwa, utafika mpaka katika eneo la Sirorisimba ambapo utaenda mpaka kwenye Kata ya Mirwa kule. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aondoe shaka, Serikali itakapotoa kibali na mradi ukatekelezwa maeneo yote hayo yatapata huduma ya majisafi na salama. Ninakushukuru sana.
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kuchukua nafasi hii kwanza kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo saba, ambayo yanaendelea kujengwa kwa sasa. Uhakika ni kwamba, majengo ambayo yamekamilika ni manne. Sasa majengo tisa ambayo bado yanahitajika, kwa mfano jengo la huduma ya macho, jengo la kuhifadhia maiti, majengo ya huduma ya kinywa na meno, pamoja na karakana ya hospitali na jiko, haya ni majengo muhimu sana ambayo yanahitajika.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani kuongeza kasi kuhakikisha kwamba majengo haya yanakamilika ili wananchi wa Butiama waweze kupata huduma nzuri ya afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri ikiwezekana mwezi wa Saba tuambatane naye aende kuangalia hali halisi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunaendelea kusisitiza ukamilishaji wa majengo haya na tunawaelekeza wataalamu wetu kuwa waadilifu katika kazi hii. Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, imetuma baadhi ya timu yetu kwenda kuangalia ujenzi wa mejengo haya ili yakamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la pili, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tuko tayari muda wowote kufanya ziara. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge lako hili Tukufu la Bajeti tutaongozana naye kwenda Butiama kujionea miundombinu hii, ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)