MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya cha Igwisi katika Jimbo la Kaliua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kaliua kwamba pamoja na yeye tayari tumeshawasilisha andiko kuhusu hili ombi la fedha kutoka Hazina. Kwa hiyo, kituo cha afya cha kimkakati katika Jimbo la Kaliua, kwa confidence kabisa nimwambie Mheshimiwa Mbunge awaambie wananchi kwamba tunakwenda kukijenga na kianze kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali. Pamoja na kazi nzuri wanazofanya Wizara ya Nishati, ninaomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itawasha umeme kwenye vijiji vya Nsimbo, Mpongolwe, Isunda, Luyembe na Sentaelo katika Jimbo la Kaliua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge letu, hadi sasa vijiji vyote ndani ya nchi yetu vimeshapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Kaliua, kaka yangu, kwa kweli safari hii Kaliua wametuletea Mbunge wa moto sana. Yuko mbio kuhakikisha anapata matokeo. Hii ni kwa sababu tangu ameingia Bungeni mpaka sasa hivi tumefanikiwa kumpelekea vitongoji 22 ambavyo wakandarasi wako site kwa ajili ya kufanya survey na kupeleka umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya mwaka huu wa fedha vitongoji 22 ambavyo tumepeleka, na hivi alivyovitaja, vimo ndani yake vitapatiwa umeme, na hili kwake Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuwasha pamoja vitongoji, ahsante.