Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John Stephano Luhende (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipa ili niweze kutoa mchango wangu katika Sekta ya Madini. Kwanza ninaanza kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa sana alioonesha katika Sekta ya Madini kwa kuendelea kulisaidia Shirika la STAMICO kuendelea kununua mitambo ya kuchoronga na kusaidia wachimbaji wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Antony Mavunde, Naibu Waziri wa Madini, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Madini kwa kuendelea kufanya kazi ya kusaidia Watanzania kujiendeleza kupitia Sekta ya Madini. Pongezi za mwisho ninamalizia kwa kumpongeza Rais wa Wachimbaji Wadogo, Ndugu John Wambura Bina, leo yuko hapa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo na kuwasaidia kupata exposure ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa ninapitia mitandao ya kijamii, nimeona baadhi ya wachimbaji wadogo wameelekea Canada kwa ajili ya kujifunza uchimbaji wa madini ili waweze kuleta tija ndani ya Taifa letu. Hongera sana ndugu Rais wa Wachimbaji Wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku ya leo nitachangia jambo moja tu kuhusiana na Sekta ya Madini na jambo hili linahusu shughuli za utafiti katika Sekta ya Madini. Shughuli za utafiti katika Sekta ya Madini ni sawa na kupanda mbegu kwa wale wakulima. Kadri unavyoongeza utafiti, ndivyo tunavyopanda mbegu ya uvunaji wa madini na kuleta maendeleo yenye tija ndani ya Taifa letu. Hata hivyo, Sekta ya Utafiti ina changamoto kubwa. Sekta ya Utafiti inakabiliwa na ukosefu wa Bodi ya Wajiolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi hii tumeanza kuipigania tangu 2017, Waheshimiwa Mawaziri wengi tumewaalika kwenye TGS, Mheshimiwa Waziri Mkuu pia amefika na kila Mheshimiwa Waziri aliyefika pale aliahidi kwamba jambo hili la msingi kwa maslahi mapana ya Taifa na watahakikisha linasajiliwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami Januari mwaka huu swali langu mojawapo la kwanza kuuliza ndani ya Bunge hili, lilikuwa ni lini Serikali itaweza kusajili Bodi hii ya Wajiolojia. Majibu yaliyotoka ni kwamba Bodi hii inatarajiwa kusajiliwa na bado Wizara inaendelea kukusanya maoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hivi, Wizara tunawaomba sana muda wa kukusanya maoni umekwisha na maoni waliyonayo yanatosha, huko mtaani hali si shwari. Sasa hivi huwezi kutofautisha Mjiolojia na vishoka walioko huko, wananchi wanatapeliwa sana. Wapo watu wanaojiita wao ni wataalam wa utafiti wa madini, wananchi wanatumia fedha kubwa kuwalipa, wanaandaa ripoti feki, wanakula fedha ya utafiti na wananchi wale wanawekeza fedha nyingi kwenye maeneo ambayo yamefanyiwa utafiti feki, hivyo wanakula hasara kubwa sana na kupelekea kufilisika kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mifano hai ya watu wengi ambao wameandikiwa taarifa feki za kiutafiti na wakawekeza fedha nyingi na wengine wamekopa. Ukitembelea kwa mfano Mkoa wa Geita maeneo ya Nyarugusu, kuna mradi mkubwa sana ulianzishwa na mchimbaji mdogo, lakini ulikufa kwa sababu wataalam walimwandalia taarifa feki za kiutafiti. Ukienda maeneo mengine ya Bukombe kule, kuna mradi ulikufa kwa sababu wataalam walimwandalia taarifa feki ya kiutafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, taaluma hii ya Wanajiolojia inasaidia sana katika nyanja zifuatazo:- Utafiti wa maji; sasa hivi ukiangalia kwenye majimbo yetu, tunachimba visima vingi vya kuchoronga lakini visima vingi pia tunapata maji na vingine hatupati maji. Hii ni kutokana na kwamba taarifa za kijiolojia zinazofanyika pale zinakuwa hazina uhalisia. Hivyo Serikali inaingia gharama kubwa ya kuchoronga visima visivyotoa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo takwimu mbalimbali za uwepo wa mafuta, gesi na kadhalika. Kazi hizo zinafanywa na hawa Wajiolojia, lakini bahati mbaya sasa ukosefu wa hii Bodi umepelekea wale Wajiolojia ambao ni halisi wanaojua kazi, wanakuwa siyo waadilifu, kuna wakati wanafoji data.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sekta ya Utafiti pia kuna fraud kubwa sana huwa inaendelea. Kwa mfano, ili uweze kupata taarifa sahihi, kuna namna ambayo unatakiwa ufanye katika kupata taarifa hizo iwe geophysics, iwe kwenye ku-drill na kadhalika. Kwa hiyo, kuna wakati mtu anakuja anakuletea ripoti amechoronga mashimo 20, lakini kiuhalisia mtu yule amechoronga mashimo 10. Mashimo 10 mengine ameandika data feki na bado analipwa fedha ya mashimo 20. Madhara yake ni kwamba utakapoenda kutekeleza mradi huo, lazima utafeli kwa sababu utakuwa ni mradi ambao hauna taarifa za kujitosheleza kuweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uwepo wa hii Bodi ambayo Wizara ya Madini wakiweza kuisajili, itahakikisha kwamba Wajiolojia wote ama wataalam wa Sekta ya Utafiti ndani ya Sekta ya Madini wanakuwa waadilifu. Wale ambao hawatakuwa waadilifu, bodi hii itawajibika kuhakikisha kwamba inawafutia leseni za utafiti kwa sababu tutakapokuwa na hii Bodi, ili uweze kutafiti katika nchi hii tutaweka utaratibu wa kwamba mradi wowote lazima usajiliwe na ukisajiliwa mradi ule, ni lazima utalipiwa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ile itatumika katika uendeshaji wa Bodi hii lakini kuna baadhi ya fedha itaingia Serikalini kama vyanzo vya mapato, ili mteja aliyefanyiwa utafiti atakapoleta malalamiko ya kwamba utafiti ule aliambiwa hapa kuna dhahabu kilo 10 akachimba shimo lake pale akakuta hakuna dhahabu mfano, anayo fursa sasa ya kulalamika kwenye hiyo Bodi na yule mtu aliyemfanyia utafiti wa kumdanganya akachukuliwa hatua za kisheria na kulipa gharama alizotumia mchimbaji huyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuchangia katika Fungu la Utafiti wa Madini kupitia GST, STAMICO na TPDC. Ninashauri Serikali kupitia Wizara ya Madini, waweke utaratibu kama ambavyo tumeweka utaratibu kwenye Mifuko mingine kama Road Fund kwamba kila lita ya mafuta yanayoingia hapa nchini kuna shilingi 100 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, waweke pia utaratibu kwamba kila gramu moja inayouzwa ya dhahabu ama ya madini yoyote yale, kiasi fulani cha fedha kiingie kwenye Mfuko wa Utafiti wa Madini ndani ya Taifa letu. Kwa kufanya hivyo tutahakikisha kwamba tunapata fungu la kutosha wakati wote wa uzalishaji wa madini yetu ambalo fungu hilo litatumika sasa katika kuziwezesha taasisi zinazohusika na masuala ya utafiti ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kuchangia suala la CSR, kumekuwa na changamoto kubwa katika jamii yetu. Unakuta eneo hilo linazalisha madini mengi sana, hata hivyo, mazingira ya eneo hilo ikiwemo barabara, shule, hospitali zinatia huruma sana na wawekezaji hawawajibiki kusaidia maendeleo ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, ninapendekeza Wizara ya Madini ije na mkakati, waje na sheria na sisi Waheshimiwa Wabunge tutaunga mkono sheria hiyo, waweke kwamba, CSR kuanzia sasa tuanze kulipa kwa asilimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tujue kwamba kwa kila kiwango fulani cha madini unachozalisha, kuna asilimia fulani ya CSR ambayo italipwa moja kwa moja kwenye masoko yetu ya madini na fedha ile itaweza kuingia kwenye Mfuko huo ili iweze kusaidia wananchi wetu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOHN S. LUHENDE Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo mengine, lakini kutokana na uchache wa muda, nitayachangia kwa njia ya maandishi. Hata hivyo, ninakushukuru sana na niwapongeze Wizara ya Madini kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kutoa niliyonayo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nianze kwa shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa leo nikiwa salama salimini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pili zielekee kwa Serikali yote ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Shukrani za tatu zielekee jimboni kwangu kwa wananchi wote wa Jimbo la Bukene kwa kunichagua kwa kura za kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imefanya ndani ya Jimbo letu la Bukene. Tunashukuru sana kwa hilo, lakini kulingana na uchache wa muda ninaomba nielekeze kwa mambo ambayo ni changamoto kubwa sana ndani ya Jimbo letu la Bukene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Bukene hatuna stendi ya abiria. Wananchi wa Jimbo la Bukene walioko huko hawana usafiri kwa sababu hatuna stendi hata moja ndani ya jimbo letu la Bukene. Kwa hiyo, ninaomba Serikali kwenye mipango ya bajeti hususan Ofisi ya Waziri Mkuu uwekwe mpango wa stendi ndani ya Jimbo letu la Bukene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, miundombinu ya barabara ndani ya Jimbo la Bukene ni mibaya, hairidhishi, ina changamoto kubwa na kwa kipindi hiki cha masika ni barabara nyingi sana hazipitiki. Baadhi ya mifano ya barabara ambazo ni changamoto kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI wanatakiwa wazishughulikie ni Barabara ya Sigiri - Bulende, barabara ya Itobo - Kalitu, barabara ya Mwamala - Ikindwa hadi Uduka, barabara ya Ngwatu hadi Gulyambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia mpaka mahali wananchi wanalazimika kukusanya magogo ili waweze kutengeneza daraja la dharura ili waweze kuwa wanapita kutoka maeneo ya Ngwatu kuelekea Gulyambi ambako ndiko kuna zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Bukene tuna changamoto katika idara ya afya, kwa mujibu wa Sera ya Afya tuliyonayo ya nchi hii kwamba kila kata angalau iweze kuwa na kituo cha afya. Jimbo la Bukene tuna kata 17, lakini tuna vituo viwili vya afya: Itobo na Bukene. Vituo hivi vya afya vimeelemewa sana na mbaya zaidi kwa sasa hivi tunatumia control namba kulipia ili tuweze kupata huduma za kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye hivyo vituo hatuna uhakika wa huduma ya kifedha. Mawakala hawapo pale na wananchi hawatibiwi pasipo kuwa wamelipa ile fedha ambayo wanatakiwa walipe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Serikali kupitia TAMISEMI ihakikishe kwamba mnaweka mawakala pale wafanye kazi masaa 24 ili wananchi wa Jimbo la Bukene waweze kupata huduma za kifedha kwenye vituo hivyo vya afya. Pia, tunazo kata mbalimbali ikiwemo Kata ya Mambali, Kata ya Semembela. Kata ya Mambali peke yake ina wakazi takribani 30,000, na Kata ya Semembela ina wakazi takribani 23,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata nilizozitaja zote mbili hazina hata kituo kimoja cha afya. Wanatumia zahanati na zahanati hizo zilizoko kule zimezidiwa. Kwa hiyo, ninaomba kuishauri Serikali kupitia TAMISEMI wahakikishe kuwa katika mipango yao ya bajeti wanaweka kipaumbele kwenye hizo kata mbili za ndani ya Jimbo la Bukene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu ndani ya Jimbo la Bukene tunazo changamoto nyingi. Jimbo letu la Bukene hatuna shule ya sekondari ya kidato cha tano na cha sita. Zilizopo ni mbili tu ambazo zimeanzishwa hivi karibuni; na zina-accommodate wasichana, kwa maana ya wanafunzi wa kike, iko moja pale Mwangoye na nyingine ipo Kili pale Uduka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watoto wa kiume, ndani ya Jimbo la Bukene hawana shule ya kwenda kusoma kidato cha tano na cha sita. Elimu hiyo ya kidato cha tano na sita ndiyo daraja pekee la kuwawezesha wanafunzi wetu waweze kuelekea chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kuishauri Serikali iweze kuliangalia hilo na ihakikishe kwamba angalau tuanze kwa shule mbili. Jimbo langu lina tarafa mbili. Kuna Tarafa ya Bukene na Tarafa ya Mwakalundi, angalau shule moja kila tarafa tuweze kuwasaidia watoto wa kiume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninataka kuzungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Nzega. Shughuli zetu nyingi tumejikita kwenye kilimo, ufugaji na biashara kidogo, lakini kwa sasa hivi kuna shughuli ambayo inaajiri vijana wengi sana, shughuli ya uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli ya uchimbaji wa madini imeingia dosari katika Wilaya ya Nzega. Eneo ambalo tunajishughulisha kwa uchimbaji huo ni eneo la Lusu, Nata na Mwangoye. Eneo la Lusu zamani kulikuwepo na mgodi mkubwa wa Resolute. Waliweza kuachia eneo hilo na wananchi wakawa wanaendelea kujishughulisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa limekuja jeshi, wanataka kuchukua hilo eneo kwa ajili ya mambo yao ya kijeshi. Hata hivyo, ukiangalia sisi kama Mkoa wa Tabora, ndio mkoa mkubwa kuliko yote nchini nzima na tuna kambi nyingi sana za kijeshi. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Serikali tuwape fursa mikoa mingine kuweka kambi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kambi tulizonazo za kijeshi ndani ya Mkoa wa Tabora zinatutosha. Eneo hilo sasa libaki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za wananchi ikiwemo kilimo, ufugaji pamoja na uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya milima ambayo jeshi wanachukua ni ile milima ya dhahabu. Kwa hiyo, wananchi hatuna sehemu nyingine ya kufanya kazi hiyo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa sababu ndiyo eneo pekee tunalotegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wakati wizara wanakuja kutoa mrejesho wa majibu, waje na majibu ya kuhusiana na hili suala la jeshi kuchukua eneo la uchimbaji wa madini ambalo wananchi wa Wilaya ya Nzega wanaendelea kulitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nijikite kwenye kuishauri Serikali kwenye hoja mbalimbali za Kitaifa. Ninaomba kushauri kuhusu uendeshaji wa Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa akihutubia mkutano, alizungumza kwamba anaagiza ma-RAS ili wawe wanatoa taarifa ya fedha zinazokuja kwenye miradi ya maendeleo ndani ya majimbo yetu, wawe wanatuandikia barua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitu kimoja. Tunatakiwa twende na wakati tulionao sasa hivi. Wanatakiwa wa-digitalize mfumo mzima wa uendeshaji wa Serikali, hasa kwenye masuala ya kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye halmashauri ama kwenye wilaya, tuna watu kama wafuatao: Mkuu wa Wilaya, DAS, OCD, DSO, Mkuu wa TAKUKURU, Magereza, Mwenyekiti wa Halmashauri, na Mbunge. Utengenezwe mfumo ambao fedha ikingia kwenye halmashauri kwa ajili maybe ujenzi wa kituo cha afya katika Jimbo la Bukene, message hiyo i-click iingie notification kwa watu wote hao; iingie kwa OCD, iingie notification kwa TAKUKURU, kwa Mbunge, kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na wengine wote wakubwa wakubwa ambao wanahusika na masuala haya ili kuongeza uwazi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo tutapunguza speed ya ubadhilifu uliopo ndani ya Serikali na muda mwingi sasa tunaotumia kuzijadili taarifa ya CAG, tutatumia kufanya mambo mengine kwa sababu mkiwa wengi ambao mna taarifa juu ya hilo suala, tutaweza kuu-control wizi kwa urahisi zaidi, kwa sababu watu 10, watu nane hawataweza kuelewana kucheza dili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mifumo ya ulipaji kwa mkandarasi, inaifanyika kama kuwa siri. Unakuta mkandarasi amelipwa 100%, mradi uko 20%. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba, mkiweka uwazi siku ambayo mkandarasi analipwa 100% ya mradi mzima, watu wote hao wanapata notification. Kwa hiyo, walio na uwezo sasa wanaweza ku-intervene na ku-control fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, juzi hapa tumekumbwa na tatizo la uhaba wa mafuta. Ninaishauri Serikali tutafute suluhisho la kudumu, tuanzishe benki ya mafuta hapa nchini, yaani the Petroleum Bank. Ili wananchi tunapofanya shughuli zetu za kiuchumi, tunapoamua kuhifadhi mapato yetu, unaweza ukahifadhi katika mfumo wa mafuta.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie, hoja yangu nataka kumaanisha kwamba, kwa mfano, sasa hivi tuna maghala ya mahindi, tuna maghala ya mpunga na kadhalika. Kwa hiyo, Serikali ijenge underground storage facilities kwa ajili ya mafuta na wananchi tutawekeza katika kununua mafuta, tutaweka kama akiba yetu, na Serikali ikipata dharura ya mafuta, wananchi tutawauzia mafuta hayo na kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mmheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)