Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. John Stephano Luhende (4 total)

MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha kisasa katika eneo la Kisasiga Jimbo la Bukene?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Tabora ikiwemo Jimbo la Bukene. Kwa mwaka 2025/2026, jumla ya miradi nane ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Jimbo la Bukene inaendelea, ambapo utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni Kahamanhalanga, Mambali, Ikindwa, Malolo, Igombe, Lakuyi, Nindo na Sigili. Kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu, kutaiwezesha Serikali kujua gharama halisi kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji pamoja na kuimarisha miundombinu ya mashambani ili kuwezesha kufanyika kwa kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka 2026/2027 imepanga kufanya tathmini katika eneo la Kisasiga kwa lengo la kubaini mahitaji halisi ya miundombinu ya umwagiliaji. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, mradi huu utaingizwa katika mipango ya Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:-

Je, lini usajili wa Bodi ya Wanajiolojia nchini utakamilika ili kulinda na kuongeza ufanisi katika shughuli za utafiti na uchimbaji madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa John Stephano Luhende, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na hatua za uanzishwaji wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Jiosayansi Tanzania (Tanzania Geoscientists Registration Board), kwa kifupi itajulikana kama (TGRB). Taratibu ambazo zimeshatekelezwa ni pamoja na uandaaji wa rasimu ya Waraka wa Mapendekezo ya Baraza la Mawaziri, kuhusu kuanzishwa kwa bodi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Wizara ya Madini ipo katika hatua ya ukusanyaji wa maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau kuhusu masuala mbalimbali likiwemo suala la kuainishwa kwa vyanzo vya mapato vitakavyohakikisha bodi pendekezwa inaweza kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, baada ya zoezi la ukusanyaji na uchambuzi wa maoni kutoka kwa wadau kukamilika, Wizara itawasilisha waraka huo kwenye ngazi za maamuzi za Serikali ikiwa ni pamoja na ngazi ya kikao cha kitaalamu cha Makatibu Wakuu (IMTC) na kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya kuanzishwa rasmi kwa bodi hiyo kwa mujibu wa sheria. Ahsante sana.
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nzega – Itobo – Igusule hadi Kagongwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa John Stephano Luhende, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Nzega – Itobo – Igusule hadi Kagongwa, kilometa 65, unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Hadi sasa jumla ya kilometa 18.3 kuanzia Kagongwa hadi Igusule zimejengwa mpaka tabaka la tatu la barabara kwa ufadhili wa mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta (EACOP). Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kumalizia ujenzi wa tabaka la lami kwa sehemu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu ya barabara hii iliyobaki kuanzia Igusule hadi Nzega, urefu wa kilometa 46.7 itajengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:-

Je, lini Kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga Mradi wa SGR Bukene italipa fidia ya shilingi 2,666,666,666.64 inazodaiwa na Halmashauri ya Nzega?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Stephano Luhende, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga Mradi wa Reli ya Kisasa kipande cha nne (Tabora hadi Isaka). Imeshaanza utekelezaji wa makubaliano yao ya tozo za madini ujenzi yanayotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha nne hususani kwa madini ujenzi yanayotwaliwa na kutumika kutoka katika machimbo zilizo chini ya usimamizi wa Wilaya Nzega Vijijini kama ifuatavyo; mnamo mwezi Machi, 2026 Kampuni ya Yapi Merkezi imelipa jumla ya fedha za Kitanzania shilingi 66,000,000 ikiwa ni awamu ya kwanza ya malipo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya malipo ya tozo za madini ujenzi kiasi cha fedha za Kitanzania shilingi 136,000,000 inalipwa mwezi Mei, 2026, ikifuatiwa na malipo ya awamu ya tatu ya jumla ya fedha za Kitanzania shilingi 136,000,000 ambayo inalipwa mwezi Julai, 2026; na kisha malipo ya tozo za madini ujenzi yenye thamani ya fedha za Kitanzania shilingi milioni 136.7 yataendelea kufanyika kila mwezi kuanzia mwezi Oktoba, 2026 hadi mwezi Machi, 2028.