Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila na shukrani kama sitamshukuru kwa dhati Mwenyezi Mungu aliyenipa uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, ambaye aliongoza vikao vikubwa na jina langu likawa miongoni mwa wagombea na mwishowe nawashukuru wapigakura wa Jimbo la Tandahimba kwa kunirejesha tena kwa kipindi cha tatu. Mungu awabariki sana Wanatandahimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo ya kuzungumza kwenye Bajeti ya Wizara hii ya Waziri Mkuu. Kwenye jambo la barabara, mimi napongeza sana, nafurahi sana kazi inayofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, anafanya kazi kubwa sana. Nilitamani wakati anafanya ziara yake, basi angepata ziara moja ya Mkoa wa Mtwara, hasa kipindi hiki cha masika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunayo barabara ambayo fedha zake zimetoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, maana yake ni fedha ambazo hazina mashaka. Tunaye mkandarasi anayetengeneza Barabara ya Mtwara – Mnivata – Tandahimba – Nanyamba – Masasi. Barabara hii kama Mheshimiwa Waziri Mkuu angefika kipindi hiki cha masika, nadhani kuna hatua zingechukuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi huyu amekuwa mtu ambaye haoneshi dhamira njema ya kuwafanya watu wa Tandahimba, Nanyamba, Newala mpaka Masasi kupita kwa kiwango cha lami. Kutoka Mnivata kwenda Tandahimba ni kilometa 46, lakini leo ikinyesha mvua unatembea saa tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana mkandarasi huyu tumeingianaye mkataba, na mwezi wa 10 mwaka huu ilitakiwa akabidhi barabara ile. Kwa hiyo, matamanio yangu kama itampendeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kama atapata nafasi, twende Mtwara aone namna anavyoweza kusaidia watu wa Mtwara, ili barabara hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunao Mradi wa Maji wa Makonde ambao mpaka sasa umekamilika kwa 32%. Ninayo mashaka makubwa ya mradi huu kutokamilika kwa wakati. Sasa kwa sababu tuko kwenye bajeti, na hili siyo jambo dogo, Mradi wa Maji wa Makonde unakwenda kuwasaidia wananchi zaidi ya milioni moja wa Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mradi ambao, kama mtaweka macho, tunakwenda kuzungumza tatizo la maji likiwa limepungua kwa kiasi kikubwa sana. Sasa kama utapata fursa ya kuja kwenye mradi wa barabara, nadhani miongoni kwa kero kubwa tutakazosikia Mkoa wa Mtwara ni ujenzi wa barabara na Mradi wa Maji wa Makonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye hoja ya fedha ya Mfuko wa Vijana, ile shilingi bilioni 200 ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa kwa dhamira njema. Ile fedha imeenda Wizara tofauti tofauti, dhamira ni njema, lakini kwa sababu tunayo Wizara yenye dhamana ya vijana, na ina full instruments, nadhani ni busara fedha ile ingesimamiwa na Wizara ya Vijana yenyewe kwa sababu, fedha yenyewe inaeleweka, ni shilingi bilioni 200, na tunazo wilaya hapa zaidi ya mia moja themanini na kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingekuwa jambo la busara Serikali ikasema tu, kwenye hizi fedha za vijana, basi kila wilaya itenge shilingi bilioni moja na fedha kidogo, ili kila wilaya iguswe. Otherwise, kuna watu watalalamika fedha iliyoenda kwenye mifugo inaweza ikawa nyingi wakati tuna Sera ya Viwanda ambayo kila wilaya watajenga viwanda. Kama fedha hii ingeenda kwenye Wizara ya Vijana tafsiri yake ingewagusa vijana moja kwa moja maeneo walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingekuwa jambo jepesi sana, tunao Wakuu wa Wilaya wazuri, tunao Wakurugenzi wazuri na tunao maafisa vijana kila wilaya. Ushauri wangu ni kwa sababu, michakato bado inaendelea, Serikali ione kama kuna uwezekano fedha hii irejeshwe kwenye Wizara ya Vijana, ili Waziri mwenye dhamana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana wawe na nguvu ya kuisimamia fedha hii kuhakikisha kwamba, imewafikia vijana wenyewe kwa uzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenzangu amezungumza hapa, TAMISEMI ni katika Wizara ambazo zinagusa uti wa mgongo wa Taifa letu. Mimi ukiniuliza bajeti tuliyonayo, natamani kabisa tuongeze fedha kwenye Wizara hii ya TAMISEMI, ili itusaidie sisi wakulima wa korosho, wakulima wa miwa, wakulima wa mbaazi, na wakulima wa choroko. Taifa hili 76% ni wakulima. Barabara zetu vijijini ni mbovu kuliko unavyofikiria. Leo ukienda, mvua zinavyonyesha kwenye Taifa hili hali ya barabara za vijijini ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami, tuongeze fedha kwenye Wizara ya TAMISEMI, hususan kwenye TARURA kwa sababu, ndiyo wanalisha Watanzania tulionao. Leo ukienda kwenye Jimbo langu la Tandahimba, barabara zake haziko sawasawa kabisa, na tunazo barabara ambazo ndiyo zinatoa korosho vijijini kupeleka mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama zinapanda, barabara ni mbovu, wenye magari wanataka gharama kubwa kwa sababu, wanatengeneza vipuli kila uchao. Kama Wabunge wenzangu wataridhia, tuone namna ya kuongeza bajeti kwenye Wizara hii ya TAMISEMI, ili wapeleke fedha za TARURA tukatengeneze barabara zetu vijijini kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukibaki hapo TAMISEMI, wenzangu wamezungumza vizuri suala la Waheshimiwa Madiwani. Fedha wanayopewa Waheshimiwa Madiwani, haikidhi mahitaji ya Tanzania ya leo. Kumpa posho Mheshimiwa Diwani ya shilingi 350,000/= siyo sawasawa. Kwa kuwa Wizara hii iko chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, aone namna ya kuongeza posho ya Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itawapendeza Serikali, Waheshimiwa Madiwani wanafanya kazi kubwa. Sisi tukiwa Bungeni hapa wapate vipando, japo pikipiki. Kila Mheshimiwa Diwani apate pikipiki ya kufanyia kazi kwenye eneo lake, na jambo hili linawezekana. Mheshimiwa Waziri Mkuu akisema, zipo halmashauri ambazo zina fedha, ni kutoa maelekezo tu, Wakurugenzi wanunue pikipiki, Waheshimiwa Madiwani wapewe vitendeakazi, wakimaliza muda wao wataweza kuziacha au zinaweza kutumika kwa namna nyingine kwa sababu, zitakuwa ni vipando vya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanafanya kazi kubwa. Kuna kata kama yangu, Kata ya Ngunja yenye vijiji saba, ukienda kuangalia utoke Mangombya uende Ngunja, utoke Ngunja uende Namindondi Chini au Namindondi Juu, ni zaidi ya kilometa 10 au 12. Mheshimiwa Diwani hana pikipiki, anatembeaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kuona namna wanavyoweza kuwasaidia wenzetu, Waheshimiwa Madiwani, ambao wakati wote ndio wapo na wananchi na wanasimama badala yetu kuisemea Serikali, ndio wanaosimama kutafuta kura za Rais, na ndio wanaosimama kutafuta kura za Waheshimiwa Wabunge. Hawa waweze kuongezewa posho na wenyewe wajione kwamba wapo kwenye base moja ya kusimamia maendeleo ya wananchi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Wenyeviti wa Serikali za Vijiji. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuchukua mihuri. Ile migogoro ilikuwa mingi, lakini na wenyewe kama Serikali itaona inafaa na wenyewe wanapaswa kupewa posho. Serikali ione ni namna gani Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji kwa sababu, wakati wote wanafanya kazi kubwa, inawezekana kuliko hata watumishi wa Serikali. Wao ndio wako na wananchi wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Afisa Mtendaji amepata dharura, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji ndio anasimama pale kutatua matatizo, lakini migogoro yote ya jamii tuliyoizungumza usiku na mchana wenzetu Wenyeviti ndiyo wanafanya kazi kubwa. Serikali ione namna ya kuwapa posho hawa Waheshimiwa Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji na wenyewe wafanye kazi zao kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)