MHE. EDIFONSI J. KANONI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ardhi ya kilimo kwa wananchi wa Kata ya Mkoe na Mbuluma kutoka katika eneo la NARCO?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo wa Uvuvi ninaomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Edifonsi Joackim Kanoni, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ranchi ya Kalambo ni moja kati ya ranchi 15 zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa, yaani NARCO. Ranchi hii inapatikana katika Wilaya za Nkasi na Kalambo, Mkoani Rukwa. Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, ranchi imepakana na Kata za Mkoe na Mbuluma, ambapo kuna Kijiji cha Katapulo (Kata ya Mkoe) na vijiji vya Mbuluma na Lolesha (Kata ya Mbuluma).
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha ufugaji wa kisasa kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika uchumi wa Ttaifa, Serikali kwa kuzingatia maelekezo ya Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kufungua rasmi Bunge hili la Kumi na Tatu, ya tarehe 14 Novemba, 2025, pamoja na maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025/2030, Serikali inaendelea kutekeleza maelekezo hayo kwa kutenga, kupima na kumilikisha kwa wafugaji maeneo ya shughuli za ufugaji kutoka hekta milioni 3.46 hadi hekta milioni sita pamoja na kuyaboresha maeneo hayo kwa kuyapatia huduma muhimu zikiwemo maji, majosho, malisho na huduma za ugani.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Ranchi ya Kalambo haina eneo la ziada na la kutosha kwa ajili ya kuwezesha shughuli nyingine kwa wahitaji kutoka katika Kata za Mkoe na Mbuluma kwa ajili ya kilimo, kwa kuwa maeneo yote yaliyotengwa kwa sasa yana matumizi mahsusi yanayoendelea.
Mheshimiwa Spika, ninatoa rai kwa halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha kuwa zinatenga, zinapima, kumilikisha, kulinda na kuhifadhi maeneo yote ya kimkakati yaliyotengwa kwa shughuli za mifugo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mifugo ili kukuza uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.