Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edefonce Joackim Canoni (4 total)

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pia ninashukuru kwa kupata mradi wa barabara kutoka Matai – Kashesha ambayo ni ya kilometa 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikikamilika, itachochea uchumi sana katika Wilaya ya Kalambo, na Serikali itakusanya mapato katika Kituo cha Forodha Kashesha. Wananchi wa Kalambo wanataka kupata majibu ya Serikali, je, ni lini barabara hii ambayo inaendelea kusuasua, itakamilika ili waweze kufaidika? Watapata ajira, tutachochea Uchumi, na pia tutapata wawekezaji kwa sababu ipo mpakani mwa Zambia na Tanzania.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba hii barabara ni muhimu sana na hasa kwa kipindi hiki kwa sababu ni moja ya barabara kuu, na pia tuna kituo chetu cha forodha kule. Tunavyoongea barabara hiyo kutoka Matai – Kasese ina kilometa 50. Mheshimiwa Mbunge atakubalina, kwamba, ili kufanya haraka tumeigawa katika vipande viwili, kwa maana ya lots; Matai – Tatanda, Tatanda – Kasesya na tuna Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumechelewa kwa sababu mkandarasi alikuwa anadai. Tumeshamlipa na mkandarasi wa kipande cha pili tunafanya maandalizi ya kumlipa ili barabara hii iweze kukamilika, kwa sababu sasa magari mengi yanayotokea Zambia yanapita huko kwenda mikoa ya Kaskazini na hata kwenda nchi jirani. Kwa hiyo, tunalitambua hilo na tunalipa umuhimu mkubwa sana kuhakikisha kwamba hiyo barabara yote inajengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Kalambo ina bandari ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi, uchumi wa Wilaya ya Kalambo na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bandari Serikali imewekeza shilingi 7,200,000,000 lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, imezama toka mwaka 2023. Nini mpango wa Serikali kuboresha bandari hii ili ianze kufanya kazi iwanufaishe wananchi wa eneo lile pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza kufafanua kidogo. Kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuweza kutambua kazi ambayo Serikali imefanya kwenye upande wa Bandari yetu ya Kalambo, Mkoani Rukwa, ambapo ni moja ya bandari ambazo zilirasimishwa, lakini pamoja na kurasimishwa Serikali iliona umuhimu ikaiendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, pamoja na dhamira njema ya Serikali kuiendeleza tulipata changamoto kubwa ya maji. Kwa hiyo, maji yalijaa na yale maji hayakujaa kwenye Bandari ya Kalambo peke yake, ni karibu maziwa makuu yote. Tayari Serikali inaandaa mkakati, tumetafuta mkandarasi au mshauri mwelekezi, ambaye anatusaidia kutuambia nini tukifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni katika kutatua changamoto ya maji yaliyojaa kwa sasa hivi. Mbili, in long run, ni tufanye nini, ili tatizo kama hili likijitokeza, basi lisiweze kuathiri bandari zetu na hivyo, wananchi wa Kalambo na maeneo mengine wanufaike na bandari ambazo zipo kwenye maeneo yao.
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, ninapongeza sana kwa majibu ya Serikali, lakini pia ninasema katika Wilaya ya Kalambo, Kata za Mbuluma na Mkoe Wananchi wa Kijiji cha Lolesha, Kalemasha, Mbuluma, Mao, Katapulo, Mkoe pamoja na Ilimba wana changamoto kubwa sana ya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuomba Serikali iwasaidie hiyo ardhi kwa ajili ya mifugo. Je, ni utaratibu upi unaotumika ili kuweza kukodi hayo maeneo na hasa kipaumbele katika hayo maeneo ambayo nimeyataja katika vijiji hivyo ambavyo nimevitaja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Waziri, upo tayari kuambatana na mimi Mbunge kwenda mpaka kwenye eneo hilo katika Wilaya ya Kalambo, Kata ya Mbuluma na Mkoe ili wananchi waweze kuwasilisha kero mbele ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kupambania maslahi ya wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, ninaomba niyajibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja. Mheshimiwa Mbunge amehitaji kujua ni utaratibu gani unaotumika kukodi maeneo hayo? Swali lake la awali lilikuwa linahitaji kujua ni namna gani tunaweza tukatenga maeneo hayo ambayo yamepimwa mahususi kwa ajili ya mifugo ili yatumike kwa ajili ya kilimo?

Mheshimiwa Spika, ninarudia tena kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vijiji hivi tayari kuna maeneo 31 ya ranchi ambayo yameshatengwa na kutolewa kwa wananchi. Katika Kijiji cha Mbuluma tumetenga hekta 3,167 na Kijiji cha Lolesha hekta 2,107 ambazo tayari wameshapewa wananchi na wanaendelea kwa shughuli za mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa vile tayari Serikali ina commitment ya kuongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta milioni 3.4 mpaka hekta milioni sita, maana yake tayari katika maeneo yetu hatuna maeneo ya ziada kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge amehitaji kujua kama tuko tayari kuambatana naye kwa ajili ya kwenda kusikiliza kero za wananchi wake. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, hilo ndiyo hasa jukumu letu kubwa. Kwa hiyo, muda na wakati ambao tutapanga kwa pamoja tutaambatana na kwenda kuwasikiliza wananchi wetu hasa wafugaji katika kata hizi ili tuweze kutatua changamoto zao. (Makofi)
MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kalambo katika Kata za Ulumi, Mnamba, Mambwe Nkoswe na Mambwekenya ni wazalishaji wakubwa sana wa mazao. Je, ni lini mpango wa Serikali kujenga maghala katika eneo hilo ili wananchi hawa wanapovuna wawe na sehemu ya kuhifadhi wakati wanasubiri soko? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninaomba tu nijibu kwa ujumla kama nilivyojibu katika maswali ya msingi. Moja ya jukumu kubwa tunalolifanya sasa ni kwamba imeundwa timu ya wataalam kupita na kufanya tathmini katika maeneo yote nchini ikiwemo katika jimbo lako Mheshimiwa Mbunge na baada ya kumaliza ile tathmini jukumu letu litakuwa ni kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kwa hiyo, hata wewe upo katika sehemu ya mpango kwa sababu ndiyo jukumu kubwa tulilonalo sasa hivi. Ahsante sana.