Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shaffin Ahmedali Sumar (4 total)

MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri sana kwa majibu mazuri ambayo kwa kweli yanatia moyo. Ninaomba niulize swali la kwanza; Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo ambalo linaweza kutokea ya bei ya tumbaku kushuka na kwa kuzingatia kwamba wakulima tayari walishalima tumbaku yao, walishafulia mabedi na tayari walishaweka mbolea: mbolea ambazo ni NPK, CAN na UREA ambazo mpaka sasa hazijapewa ruzuku?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali itaweka lini mpango mzuri wa utaratibu rasmi wa ushirikishi na kuruhusu kampuni za tumbaku kwenda kujinadi kwa wakulima ili mkulima awe na haki ya kuchagua kampuni ambayo ana maslahi nayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Shaffin Ahmedali Sumar, Mbunge wa Uyui, ni moja ya Wabunge makini sana, ambaye anafanya kazi nzuri katika jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu kwamba, moja, sisi kama Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakabiliana na anguko la bei katika mazao yote nchini ikiwemo tumbaku. Moja ya jambo kubwa ambalo tunalifanya ili kutoa ruzuku ya pembejeo, maana yake ni kumpunguzia mkulima gharama ili azalishe kwa gharama ya chini na akishazalisha aweze kuuza katika bei inayohusika, hata panapotokea anguko la bei maana yake walau mkulima anaweza akapata faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunaendelea kujenga viwanda vya kuchakata haya mazao vikiwemo viwanda vya kuchakata tumbaku. Yote ile ni kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama. Tuna viwanda ambavyo, AMCOS zinakaribia kujenga vile viwanda vya vifungashio. Lengo lote lile ni kutaka kumpunguzia mkulima bei ya zao lake. Kwa hiyo, kitu ambacho nikuthibitishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba moja ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mazao yote yanaingia katika mpango wa ruzuku, lakini kwa awamu na kwa kuzingatia mahitaji ya kila wakati, ikiwemo hili eneo ambalo ameliaininisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa kampuni kwenda kujinadi, kwa sababu tumekuwa na kila mwaka tuna mkutano wa wadau wa tumbaku na jambo hili lilishakuwa linafanyika hapo nyuma kabla ya kubadilishwa mfumo wake, basi sisi kama Serikali tumelipokea na katika kikao kinachokuja kwa wadau tutalifikisha pale. Wadau watalijadili na yale watakayokubaliana, sisi Serikali tutakuwa tayari kuyatekeleza.
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Kwa kuwa tatizo la mawasiliano ni la nchi nzima na katika Jimbo langu la Uyui tatizo kama hili lipo na linasumbua sana katika Kata ya Ibili, Ibelamirundi, Ndono, Makazi na Bukumbi. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam ili waangalie maeneo ambayo yanafaa kuweka mnara waweze kuweka haraka iwezekanavyo ili wananchi waache kupanda miti kutafuta mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Uyui kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumwelekeza tena Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma timu ya wataalam katika Jimbo la Uyui kuweza kufanya tathmini na kutambua changamoto zilizopo za mawasiliano katika jimbo hilo.
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Ninaomba kuuliza swali. Je, ni lini barabara inayounganisha barabara tatu, kwa maana ya Tabora Mjini – Ulyankulu na Jimbo la Uyui, itajengwa kwa kiwango cha lami ambapo wananchi wengi wanahitaji lami ili waweze kunufaika na huduma hiyo?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sijamsikia, amesema Tabora Mjini hadi...

MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayoounganisha wilaya tatu za Tabora Mjini, Ulyankulu na Uyui ambapo kuna kata zangu za Idiri na Usagai.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tumeshaifanyia usanifu, na kwa kweli Serikali inatafuta fedha ili iweze kuijenga kwa sababu ni kweli ni barabara muhimu na inapita kwenye maeneo mengi na hasa ikiwa inaunganisha hizo wilaya alizozitaja Mheshimiwa Mbunge. Tumeshakamilisha usanifu, kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, na ninaishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, huu upembuzi sasa unaelekea kutekelezwa na muda siyo mrefu, mradi utakuwa umekamilika. Je, nini mpango wa Serikali kusaidia zile kata ambazo zipo jirani na mradi huu, ambazo ni Kata ya Bukumbi na Igulungu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana nia njema sana ya kuwasambazia maji Watanzania mpaka kwenye vitongoji, na Kwa kuwa, sisi Mkoa wa Tabora tayari tuna Mradi wa Ziwa Victoria, na kwa kuwa, mradi huu umefika katika wilaya mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Tabora Manispaa ambapo kuna Bwawa la Igombe, je, nini mpango wa Serikali kuangalia vile vijiji vilivyopo jirani na Bwawa la Igombe ambapo kuna vijiji vya Kata yangu ya Ibiri na Usagala kuweza kupatiwa maji kwa sababu, bado mpango huo haujawafikia maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza kwa kusimamia vyema ajenda hii ya maji kwa ajili ya wananchi wake wa Uyui. Pia, ajenda hii inaenda sambamba kabisa na Sera ya Maji ya kuhakikisha kwamba, Watanzania wanapata huduma ya majisafi na salama. Bwawa hili la Shitage litaweza kuwafikia wananchi wa Bukumbi na Igulungu ambao Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu, tutafanya usanifu wa kina. Baada ya hapo, tutafanya usanifu mwingine, kwa ajili ya miundombinu. Katika usanifu wa miundombinu hii sasa tutahakikisha Bukumbi pamoja na Igulungu wanakuwemo katika mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la pili kama ambavyo nimesema, linaendana na sera yetu ya maji. Pale ambapo bomba kuu linapita kushoto na kulia kilometa 12, sisi tunahakikisha vijiji husika vinapata huduma ya majisafi na salama. Tunatambua Serikali imeweka uwekezaji mkubwa wa kuleta maji ya Ziwa Victoria, ambayo yanapokelewa katika Bwawa la Igombe, yanaenda katika Wilaya ya Kaliua na Urambo. Tutahakikisha vijiji vilivyopo katika maeneo yaliyozunguka Bwawa la Igombe vinapata huduma ya majisafi na salama. Nakushukuru sana.