Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuongea katika Bunge lako hili Tukufu. Vilevile, mimi ninaamini upinzani siyo kusema hapana kwa kila kitu. Kilicho kizuri lazima kipongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa mimi nikiwa mkazi wa Wilaya ya Nkasi ambayo kipindi cha nyuma ilikuwa ni giza, tulikuwa kweli kwenye peripheral na sasa hivi ni tofauti kabisa. Wilaya yetu ya Nkasi sasa hivi inaweza kuwa inafahamika hata kwa watu wengi waliopo hapa. Ninasema ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ningependa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hasa kwa ziara yake ya mwezi Machi ambapo alikuja Jimboni kwangu Nkasi Kaskazini. Ninaomba nitoe shukrani za wananchi wa Nkasi kwa maana kweli ziara hii imekuwa ni ya win-win kwa maana kwamba wananchi wenye kero zao hata wale wa shilingi 200,000 ziliweza kutatuliwa na papo kwa hapo wakaweza kulipwa fedha zao. Wananchi wanashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani hata Waziri Mkuu naye atakuwa amefaidi kuujua ukweli kwamba katika ngazi hizo kuna viongozi wengi hawatimizi wajibu kwa maana kwamba kesi ya shilingi 200,000 inamsubiri Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo limesaidia, na ninaamini katika ile timu yake iliyopo ya monitoring and evaluation itakuwa imeliona hilo, kwa sababu tuliambiwa tayari inazo indicator za kutosha. Kwa hiyo, itaweza kuona ni kwa namna gani hali hiyo iweze kuboreshwa kwa safari yake Mheshimiwa Waziri Mkuu asihangaike tena na kesi hizo bali ziweze kutatuliwa na viongozi waliopo katika ngazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ninatokea wilaya ambayo uti wake wa mgongo ni kilimo, ninaomba vilevile niishukuru sana Serikali kwa kutuwezesha sisi wakulima wa Wilaya ya Nkasi pembejeo za ruzuku. Ninaomba nikwambie kwamba kwa msimu huu, Jimbo la Nkasi Kaskazini litavuna sana. Tegemea mavuno ya kutosha, zile warehouse ziandaliwe za kutosha kwani mavuno hasa ya mahindi yatakuwa ni mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wilaya yetu, kilimo bado kina vikwazo ambavyo ninataka niishauri Serikali ikiondokana na hivyo, tunaweza tukavuna zaidi, tija ikaongezeka. Tatizo la kwanza ni hilo la wanyama; tembo. Kwa kweli limekuwa ni kero kubwa kweli kweli. Mimi na viongozi wa TAWA tunakesha kuwasiliana namna ya kuwafukuza tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi jana tu Kijiji cha Chongokatete kimevamiwa na kundi kubwa la tembo. Ninaishukuru TAWA, Wilaya ya Nkasi inafanya kazi vizuri sana. Sasa, ninaomba kuhusu tembo, uharibifu ule isiwe fidia. Ningeomba sana kushauri, iwe ni malipo sawa na uharibifu mwingine wowote. Kuna mifugo iko kule huwa inaharibu mimea ya wananchi, mabwana shamba wanafanya tathmini na fidia halisi inafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa nao ni mifugo. Wale ni wafugaji, hawa wengine ni wetu Serikali, ninaomba sana unapotokea uharibifu, tathmini ifanyike na malipo yasiwe fidia, bali yawe kwa kiwango cha uharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani suluhisho la kudumu katika kadhia hii ni kuweka fensi tu. Ingependeza kama tungeweka fensi maeneo yetu yote. Kwa Jimbo langu la Nkasi Kaskazini, ianzie Kalila ije hadi Masolo. Tukiweka fensi tutakuwa tumekamilisha, tatizo hili tunaweza kuwa tumeliondoa kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, maono ya Mheshimiwa Rais wetu kuhusu kukuza kilimo nchini ni kwamba by 2030 Tanzania itakuwa imejitegemea kwa suala la mbolea kwa 100%. Sasa, nina wasiwasi na kasi tuliyonayo kama kweli inaweza ikayafikia haya maono ya Mheshimiwa Rais. Ninaomba kutoa rai kwamba tuongeze kasi ya kujenga viwanda. Gharama tunayoitumia sasa hivi kuagiza mbolea kutoka nje ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutengeneze mbolea zetu by kipindi hicho kweli tuwe nayo. Sasa, ningetegemea nione kuanzia bajeti hii Waziri anasema nini kuhusu kuwa na viwanda vyetu vya mbolea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ruzuku za pembejeo, Waheshimiwa wenzangu wameongea, nami ningependekeza kwamba isiwepo namna yoyote ya kuondoa ruzuku katika awamu hii. Hii ruzuku iendelee, wakulima wetu bado ni wachanga, tukimwambia Mfuko wa DAP aununue kwa shilingi 120,000 uzalishaji utashuka sana. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara husika, habari ya ruzuku ya pembejeo iendelee kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninadhani ni wakati sahihi sasa hivi katika kukuza kilimo, tuwavutie vijana. Tunasema wanatoka vyuo vikuu hawana ajira, ajira wanapaswa kuwa nayo. Tunayo maeneo mengi sana yanayofaa kwa kilimo hasa Jimboni kwangu na wilaya kwa ujumla, lakini sidhani kwamba vijana watavutiwa na kutumia jembe la mkono, hilo sitarajii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa nini sasa hivi kutengeneza viwanda vyetu hata kutengeneza power tiller au hata trekta? Tunazo taasisi zetu za majeshi, Nyumbu wanashindwa kweli kutengeneza power tiller au trekta? Ninaomba sana kwamba sasa tuwekeze zaidi kwenye kutengeneza viwanda kwa ajili ya zana za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee suala la barabara. Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka 2025 kwenye ziara yake ya kampeni alituahidi sisi Watu wa Nkasi kutupatia barabara mbili kwa kiwango cha lami. Ya kwanza ni ya kutoka Namanyere – Kipili ambako kuna bandari. Barabara ya pili ni kutoka Lyazumbi – Kabwe, napo ni kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo ni muhimu sana. Wakati uchumi wetu unakua kwa asilimia tano nukta tano mpaka asilimia sita, ninaamini ni kwa sababu hatujaweza kulitumia Ziwa Tanganyika. Kama hizi barabara zitawekwa vizuri, na hizi Bandari mbili za Kipili na Kabwe zikaimarishwa, ninaamini tutapata fedha nyingi kwa maana Eastern Congo kuanzia Mji wa Moba kuja Kusini wanategemea bandari hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana Wizara hizi mbili zinazohusika mzione hizi Bandari za Kabwe na Kipili pamoja na barabara zake kama lango muhimu kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nisikie kauli ya Serikali maana ninaona kama vile ina utata. Je, children under five wanatakiwa walipie matibabu? Akina mama wajawazito kwa huduma za kliniki, iwe wazi nao je, walipie? Wazee zaidi ya miaka 60 tunasemaje? Maana kunakuwa na kauli tofauti tofauti. Ningeomba hilo liweze kufafanuliwa vizuri katika kikao chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nkasi bado ina changamoto kubwa ya maji. Inapofika mwezi Septemba lile Bwawa la Likopo hukauka kabisa na water table hushuka kiasi kwamba visima vya wananchi walio wengi huwa vimekauka na hivyo mama hutumia hadi masaa sita kupata ndoo moja ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mradi wa maji ambao Serikali ilisaini bwawa liweze kujengwa, ulisainiwa Novemba, 2024, ikafika Novemba, 2025 ambapo ndiyo mradi ulitakiwa ukamilike, hilo bwawa likawa bado halijapatiwa fedha. Tukafanya renew ya mkataba kwamba sasa ianzie Novemba, 2025 mpaka Juni, 2026, hadi leo ninaongea hakuna shilingi iliyopelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri alione hili, kwani Wilaya ya Nkasi na hususan Mji wa Namanyere una shida kubwa sana ya maji ya kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)