MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:-
Je, lini Meli za Liemba na Mwongozo zitaanza tena kutoa huduma ndani ya Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Bazilio Kapunda Mbwilo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Meli za MV Liemba na MV Mwongozo zitaanza kutoa huduma za usafiri katika Ziwa Tanganyika baada ya ukarabati kukamilika. Kwa sasa ukarabati wa MV Liemba unaendelea na upo katika hatua ya ufungwaji wa vifaa muhimu baada ya kupokelewa na inatarajiwa matengenezo hayo kukamilika mwezi Juni, 2026 na kukabidhiwa kwa TASHICO mwezi Julai, 2026, kwa ajili kuendelea kutoa huduma za usafirishaji ndani ya Ziwa Tanganyika. Aidha, taratibu za kuanza ukarabati mkubwa wa MV Mwongozo unaendelea kukamilishwa ili kuanza matengenezo hayo hivi karibuni.
MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:-
Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Bazilio Mbwilo Kapunda, Mbunge wa Nkasi kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Namanyere – Kipili ni sehemu ya Barabara ya Msangama – Namanyere – Katongoro – New Kipili Port, yenye urefu wa kilometa 64.8. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mradi huu umeingizwa katika mpango wa bajeti, kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa kuanza na sehemu ya Namanyere – Mfili II Bridge yenye urefu wa kilometa 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha, kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.