Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bazilio Kapunda Mbwilo (4 total)

MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ili hizi meli ziweze kujiendesha kwa faida, zinahitaji abiria wa kutosha na kivutio kimojawapo cha abiria kutumia meli hizi, ni pamoja na bandari. Sasa bandari mbili zilizoko ndani ya jimbo langu, Bandari ya Kipili na Kabwe, zote zimezama. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha bandari hizi zinakuwa nzuri ili zivutie watu wengi zaidi kutumia usafiri huu wa meli?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Watu wengi sana wa mwambao wanafanya biashara na nchi jirani ya Congo na husafirisha mizigo, hasa kwa kutumia maboti ambayo yamesababisha vifo vya mara kwa mara kwa hawa wafanyabiashara. Je, Serikali itaweka ratiba ya walau mara mbili kwa mwezi; moja ya hizo meli iweze kwenda Congo, Mji wa Moba na Kalemie, ili wawe salama zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji na maswali yake ya nyongeza, ambayo ameuliza. La kwanza, ameuliza kuhusiana na upatikanaji wa abiria. Ni kweli, Serikali inatambua kwamba meli hii na nyinginezo ambazo zinajengwa ni kwa ajili ya kusaidia abiria pamoja na mizigo. Kimsingi abiria wapo, na changamoto kubwa, ambayo imeipata nchi yetu kwenye takribani maziwa yote matatu ni kujaa kwa maji.

Mheshimiwa Spika, tayari tupo na mkakati wa muda mfupi ambao tunaendelea nao kupitia TPA. Pamoja na mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba yale maji ambayo yamejaa kwenye Bandari zetu karibu zote kuanzia Kabwe, Kasanga mpaka kule Kigoma zinaweza kuondolewa, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa kwamba, tunalifanyia kazi jambo hilo kwa lengo la kusaidia wananchi wetu ambao baada ya kutokea maji haya, kwa kweli wanashindwa kusafiri kwenye bandari hizo.

Mheshimiwa Spika, hoja yake ya pili, tuichukue kama ni ushauri. Meli itakapokamilika kupitia mpango wa kibiashara, tutatazama, kupitia TASHICO, kuona wapi iende kulingana na uhitaji utakaokuwepo, ikiwa ni pamoja na ushauri wake anaoutoa kwenda kwenye nchi jirani, kupitia Bandari ya Moba, Kalemie, pamoja na maeneo mengine.
MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na neema ya mvua ambayo Wilaya yangu ya Nkasi imepata katika msimu huu imepelekea barabara zote za pale Mjini Namanyere kuharibika sana. Sasa mvua imeisha; je, ni lini Serikali itatuwezesha kujenga hizo barabara zilizoharibika vibaya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa ufuatiliaji wake wa mara kwa mara alishakuja Ofisi za Waziri Mkuu, TAMISEMI mara kadhaa na tumemhakikisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kufuatia mvua hizi nyingi barabara zetu zimaharibika za Jimbo la Nkasi Kaskazini, Wilaya ya Nkasi kwa ujumla lakini pia katika eneo la Namanyere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie kwamba tayari Serikali tumeshatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TARURA kote nchini, TARURA Mkoa na TARURA Wilaya wanaendelea na utangazaji wa zabuni wa 60% ya bajeti kwa ajili ya matengenezo ya haraka na ya dharura kwa barabara zote zilizoathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumsisitiza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Rukwa na Wilaya ya Nkasi kuongeza speed na kufika pia Namanyere na kuona barabara zilizoharibika ili ziweze kupata kipaumbele kwenye bajeti ambayo tayari tumetangaza kwa ajili ya kupata wakandarasi.

MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wakati nchi yetu inasifika kwamba umeme sasa umefika karibu vijiji vyote nchini lakini Kijiji cha Uhuru kilichopo Kata ya Mkinga, Wilaya ya Nkasi hadi leo hii bado hakina umeme na ukizingatia kwamba kijiji hicho kipo kisiwani kina mahitaji maalum.

Je, ni lini sasa Serikali italeta umeme katika kijiji hicho cha Uhuru?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza pia Kaka yangu Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa karibu kuhakikisha tunawaangazia wananchi wa Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vitongoji na vijiji ambavyo vipo maeneo ya visiwani, Serikali imezingatia kwa kupeleka umeme, ambapo kwingine tumepeleka umeme wa nishati ya jua, kwingine tumepeleka umeme kwa kupeleka nyaya. Kwa hiyo ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, lengo la Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kila mtu anapata umeme na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Kijiji hiki cha Uhuru ambacho kipo katika Kata ya Nkasi ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge mikakati inaendelea kuhakikisha tunafikisha nyaya za umeme ili na wao waweze kupata umeme wa Gridi ya Taifa, na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda pamoja kuangalia uwezekano wa kuongeza kasi na kuwanufaisha wananchi wa Kijiji cha Uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.
MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaishukuru Serikali kwamba, sasa barabara hii imefikia hatua nzuri. Kwa kuwa, barabara hii ni muhimu sana, hasa kwa mapato ya Serikali, kutokana na mizigo mingi inayokwenda nje ya nchi inapitia Bandari ya Kipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kitu kimoja katika hizo kilometa 20 au hata ikibidi, pungufu ya hizo zianzie bandarini kwenyewe kwa ajili ya yale malori yanapokuja na mizigo; kwa sasahivi yanahangaika sana kuingia pale bandarini, lakini lami ikianzia bandarini hata kilometa mbili tunaweza kuwa tumevutia wasafirishaji wengi kuendelea kuitumia Bandari hiyo ya Kipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kama Bandari ya Kipili ilivyo muhimu kwa uchumi wa nchi hii, Bandari ya Kabwe nayo ni hivyohivyo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, walau kilometa moja tu tuijenge, ianzie bandarini, ili kuwezesha magari baada ya mihangaiko huko mbugani kwenye matope mengi yanapoingia kwenye gati yaweze kupita kirahisi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, kwa pamoja, ya Mheshimiwa Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakiri kupokea ombi lake, lakini pia, namweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na kupokea huo ushauri, lakini lengo letu hasa ni kuhakikisha zile barabara zinapitika na tunajua barabara zinazotoka bandarini zinakuwa ni zenye uzito mkubwa. Kwa hiyo, pamoja na kupokea ushauri, lakini tutakachoshauriana na wataalamu ni hasa yale maeneo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kwa magari kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linaweza likatoka bandarini, lakini kama litakwama Katikati, hata kama tutakuwa tumeweka lami mwanzoni itakuwa haina maana. Cha msingi ninadhani tutaangalia yale maeneo korofi, ambayo yanaweza yakafanya barabara isipitike tufanye hasa kwa maombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kabwe tumeanza kufanya hivyo, maeneo yenye madaraja membamba na kwa maeneo korofi, tumetoa maelekezo yatengenezwe, ili magari yaweze kupita. Kwa hiyo, tutashauriana, lakini pia, wataalamu watashauri nini cha kufanya, hasa kulingana na ombi lako. Ahsante sana.