Primary Questions from Hon. Eng. Amosy William Maganga (3 total)
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Ipole – Rungwa na Sikonge – Kipili kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Amos William Maganga, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Ipole – Rungwa inayounganisha Mikoa ya Tabora na Mbeya umekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Sikonge – Kipili Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Baada ya Usanifu kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: -
Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Amosy William Maganga, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria kutoka Tabora kwenda katika Wilaya za Sikonge, Urambo na Kaliua mkoani Tabora kwa gharama ya shilingi bilioni 143.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 253 sambamba na ujenzi wa matanki tano yenye jumla ya ujazo wa lita milioni nane yakiwemo matanki mawili yenye ujazo wa lita milioni tatu yaliyojengwa katika maeneo ya Tumbili na Misheni, wilayani Sikonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo umefikia wastani wa 76.5% za utekelezaji na umeanza kutoa huduma kwenye baadhi ya maeneo ya Mji wa Sikonge wakati utekelezaji ukiendelea. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2026 ambapo Serikali itafanya usanifu wa kufikisha huduma ya maji kupitia mradi huo kwenye maeneo ya pembezoni umbali wa kilometa 12 kutoka bomba kuu ikiwemo Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha SGR katika eneo la Nyahuwa ili kuboresha usafiri na usafirishaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Amosy Maganga kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza (kilometa 1,219), Tabora hadi Kigoma (kilometa 506) na Uvinza hadi Musongati (kilometa 282). Aidha, ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Makutupora hadi Tabora (SGR Lot 3) unaendelea kutekelezwa ambapo eneo la Nyahuwa linapatikana katika kipande hiki cha ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tathmini na usanifu uliofanyika, kipande cha tatu cha kutoka Makutupora hadi Tabora kitakuwa na Kituo Kikuu kwa ajili ya abiria na mizigo katika Mji wa Tabora. Vituo vya kati katika Mji wa Manyoni na Itigi na vituo vidogo kwa ajili ya abiria pekee kwenye Mji wa Tura, Malongwe, Goweko na Igalula. Aidha, Katika Mji wa Nyahuwa, itajengwa njia ya kuchepushia treni (passing loop). Wakazi wa Mji wa Nyahuwa wataendelea kupata huduma za SGR katika vituo vilivyo karibu, yaani Malongwe na Goweko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya maeneo ya kuwekwa kwa vituo vya abiria na mizigo vya aina mbalimbali hufanywa kupitia upembuzi yakinifu uliofanywa kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi, biashara na kijamii kwa miji na vijiji vyote vilivyopo pembezoni mwa reli, pamoja na kuzingatia umbali baina ya kituo cha mwendokasi kwa treni ya SGR ili kuweza kuendeshwa kwa tija na ufanisi.