Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii njema jioni ya leo ili niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika kujadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kama ilivyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niungane na Watanzania wote kuendelea kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa namna ambavyo ameendelea kutujalia afya Watanzania wote wakiwemo viongozi wetu na kiongozi wetu mkuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, niendelee kumwombea sana Mheshimiwa Rais aendelee kuongoza Taifa letu kwa busara hiyo aliyonayo, lakini akisaidiwa na Makamu wake wa Rais, akisaidiwa na Waziri wake Mkuu, lakini pia na Mawaziri wote pamoja na watendaji wote wa Serikali; kuanzia ngazi ya Taifa mpaka kwenye vijiji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia, kuendelea kuwashukuru sana wananchi wa Chato Kaskazini. Wananchi hawa wa Chato Kaskazini ni watu wema sana, walinipigia kura kwa mahaba makubwa kwamba nije niwe mwakilishi wao katika Bunge lako Tukufu hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa na mimi siku zote, toka uchaguzi umekwisha, tumekuja Bungeni tumeapishwa, wamekuwa na mimi katika changamoto zote ambazo Mbunge wao nimekuwa nikizipitia na mazuri yote na mema yote tumekuwa bega kwa bega nao. Ninawashukuru sana wananchi wa Chato Kaskazini kwa kuendelea kuniunga mkono na ahadi yangu kwao ni kwamba sitawaangusha katika uwakilishi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye kuchangia hotuba ya Waziri. Katika hotuba ile ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, yapo mambo mengi na mazuri ambayo Serikali imeyaweka mbele yetu kuonesha ina mpango mzuri wa kwenda kutekeleza kwa ajili ya Watanzania. Pamoja na mipango ambayo imewekwa yapo mambo mazuri na makubwa ambayo yametengwa kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Chato Kaskazini, ninatumia nafasi hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali yake, lakini ikiwemo chama change, Chama cha Mapinduzi kwa makubwa na mazuri na mengi yaliyoletwa kwa wananchi wa Chato katika kipindi cha miaka minne ya utangulizi wa utawala wake. Tunamshukuru sana sisi watu wa Chato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yetu ya Chato, ipo miradi mingi ya kimkakati ambayo ililetwa, ambayo nikianza kuitaja hapa nadhani, muda hautatosha lakini itoshe kusema tu kwamba mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi, kwa ajili ya Watanzania waliopo Chato, kwa kweli sisi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na fedha zile ambazo zimeletwa kwa wingi, nilitamani niseme mambo haya. Zipo fedha ambazo zimeletwa kwenye miradi mingi kwenye maeneo yetu, lakini inapokwenda kukamilika miradi ile haisimamiwi sawasawa kwa ajili ya kuleta tija ambayo ilikusudiwa na Serikali yetu. Kwa mfano, leo tukitembea kwenye miji mingi ikiwemo Mji wa Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na miji mingine, wako Wabunge wenzetu hapa wanaomba kujengewa stendi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Chato ni moja ya mji ambao tulipata bahati ya kupata mradi mkubwa wa kujengewa stendi ya kisasa, kama zilivyo stendi nyingine kama Dodoma na kwingineko. Serikali ikifanya intervention ya kwenda kuona yale ambayo yanaendelea kwenye stendi zile utagundua kwamba fedha nyingi zimekwenda kule lakini tija iliyokusudiwa haiendi sawasawa kama ambavyo ilitarajiwa na Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ile stendi ukienda kuna maeneo mengine ambayo hayafanyi kazi kama ambavyo ilitarajiwa kwenda kutumika. Vilevile hata ukienda kwenye stendi yetu ya Chato ambayo imetengewa mabilioni ya fedha mpaka leo, haijakamilika katika ubora ambao unatakiwa na haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, fedha zile zilizokwenda pale zinaishia huko bila kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Kumbe, pengine tusingejenga ule mradi mkubwa unaoonekana sasa upo, ilhali umetumia fedha nyingi, lakini haufanyi kazi ipasavyo; badala yake, tungelielekeza fedha hizo katika kujenga vyoo kwenye shule zetu ili watoto wetu wapate kusoma katika mazingira bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye hii miradi: nimemwona Mheshimiwa Waziri Mkuu amepita huko kwenye mikoa yetu, anapofika kwenye mikoa yetu na maeneo yetu, nimwombe sana aende akashughulike na miradi mikubwa ya kimkakati aone kama tija yake iliyokusudiwa inakwenda kufanya kazi, hilo ndilo lililokuwa ombi langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hiyo kwetu pale Chato kuna uwanja mkubwa wa ndege, ulitumia mabilioni ya fedha na uwanja ule ukaanza kutumika na wananchi wa kule Chato na maeneo mengine ya jirani mpaka na nchi za jirani, uwanja ule ulikuwa unatumika kwa ajili ya kusafirisha watu, lakini mpaka leo ninavyozungumza, mabilioni ya fedha yamepotea katika uwanja ule. Sasa umebaki kwenda kwa Wasukuma kwenda kuanika pale mihogo ili wapate udaga waende wakale chakula badala ya kuweka ndege pale. Sasa shida iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninamwomba sana Waziri anayeshughulika na mambo ya usafirishaji na uchukuzi, wahakikishe kwamba Chato bado tunahitaji tupate ndege kwa sababu fedha ya Serikali ilikufa pale kwa kujenga kiwanja cha ndege katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ziko bandari mbili ambazo zilijengwa kwa fedha kubwa zaidi ya shilingi 6,000,000,000, iko Bandari ya Nyamirembe, iko na bandari ya Bwina. Bandari hizo zilitarajiwa kwamba baada ya kukamilika, meli zingeanza kutia nanga katika maeneo hayo, wananchi wapate huduma ya usafiri na pia kuwezesha upatikanaji wa mizigo kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza miaka minne iliyopita ya bandari zile kuchukuliwa shilingi bilioni sita mpaka sasa hazitumiki na meli zipo kutoka Mwanza kwenda huko kwetu, lakini haziwezi kufika pale zinakwenda kwenye maeneo mengine. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba mahali ambapo Serikali imeamua kuwekeza fedha zake, basi fedha zile zikatutumike kama ambavyo zimekusudiwa kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninaomba niishauri Serikali hasa wakati inapokuwa inatoa miradi kwa wakandarasi, ninaona wakandarasi ambao ni private wanaweza wakafanya vizuri kuliko wakandarasi ambao ni taasisi za Serikali. Nina mfano pale kwangu pale Chato, kuna mkandarasi ambaye alikuwa National Housing alikuwa amepewa kujenga shule... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie tu hili, kwamba wako wakandarasi ambao wamepewa kujenga shule zetu, iko Shule ya Mbuye ya watoto wenye mahitaji maalum. Shule imejengwa kwa fedha nyingi lakini mpaka sasa haijakamilika na mkandarasi ameacha mradi amekwenda na ile shule inahitajika watu wasome pale na fedha zilipelekwa nyingi.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu ya muda, ninaomba niseme ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi, ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya elimu, ambayo tunajadili kupitisha bajeti yake. Kwanza ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kweli, kwa kiwango kikubwa ameifanya Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi ambazo Kimataifa zinaonekana zinakwenda kasi katika hii sekta ya elimu. Tunamshukuru na kumpongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda Pamoja, Naibu Waziri wake, pamoja na watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu. Kwa kweli, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Elimu, Waziri pamoja na wasaidizi wake wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa sana kwetu sisi Kamati, lakini kwa niaba ya Bunge zima ambalo sisi ni wawakilishi wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi yao wanayoifanya, ukienda kupitia mambo ambayo wameyaleta leo hapa Mezani kwa kweli, hata hizi fedha shilingi trilioni 2.3 ambazo wanaomba tuziidhinishe zikawe matumizi katika Wizara hii, mimi binafsi naona bado ni kidogo sana. Kama inawezekana, basi ninaomba Bunge lako hili Tukufu liangalie namna nyingine na kuishauri Serikali itafute fedha nyingine ya kuiongezea Wizara hii kwa sababu, ina mambo makubwa inayokwenda kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Sita ilipoingia madarakani toka mwaka 2021 ukienda kule vijijini mabadiliko ambayo utakutana nayo kwenye vijiji vyetu na kwenye Kata zetu ni mambo ya kupigiwa mfano ambayo hayajawahi kutokea toka tumepata uhuru katika nchi yetu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kuangalia shule za msingi ambazo zimeanzishwa mpya bila involvement ya mwananchi mwenyewe kuchangia fedha yake ni shule nyingi sana huko tunakotoka. Ukienda pia kwenye shule za sekondari kwa maana ya sekondari mpya pamoja na madarasa ambayo yamejengwa na miundombinu mingine kwa kweli Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi ya kutukuka na ya kupigiwa mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi ambacho kimefanyika ni kuja na mpango huu wa kuhakikisha kwamba kila wilaya tunakwenda kupata VETA na ambayo leo hapa tulikuwa tunaambiwa zaidi ya vyuo 64 ambavyo vinajengwa na vinaelekea kwenda kukamilika viko karibu 67%, viko kwenye hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikuhakikishie na kulidhbitishia Bunge lako Tukufu kama Mjumbe wa Kamati ile, tumekwenda tumeona kwa macho kazi nzuri ambayo inafanyika ika katika miradi hiyo na insha Allah inakwenda kukamilika, ninadhani baada ya kupata kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chato ni moja ya Wilaya ambazo zimenufaika na mipango mingi ya Serikali ya Awamu ya Sita. Chato imepata shule nyingi za sekondari, imepata shule nyingi za msingi, lakini tumekwenda mbali zaidi sisi tumepata VETA kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule hizi za sekondari zilizojengwa nitoe ushauri kwa Wizara, ni kwamba tumejenga sekondari nyingi, wananchi maeneo mengine wamehamasika wameanzisha shule za sekondari, lakini katika sekondari hizo ambazo zimejengwa na wananchi pamoja na zilizojengwa na Serikali, sekondari hizi hazina maabara katika shule zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali na Wizara yenyewe kwamba tukitaka kufanya vizuri na kupata vijana ambao watakuwa ni wazuri watakaokwenda kwenye vyuo vyetu vile vya VETA ambavyo vimeanzishwa kwa wingi, tunaomba Wizara ijikite kwenda kukamilisha maabara zinazokosekana katika sekondari zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Jimbo langu la Chato Kaskazini, kwenye Kata 14 ninazo shule zaidi ya shule 19 za sekondari, katika shule 19 zile shule 12 hazina maabara kabisa. Shule zile zimekuwa zikifanya vizuri zimekuwa zimeanza kufanya kazi, leo ni miaka mingine takribani miaka mitano, miaka minne na kadhalika. Sasa ninaiomba Wizara sana kwamba wakati inakwenda kupeleka pesa zile za matumizi kwenye shule hizi, kwenye sehemu ya sekondari. Ninaomba katika shule hizi zifuatazo katika Jimbo langu la Chato wazingatie kuziletea maabara ili watoto wale waweze kupata elimu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya kwanza ambayo ina tatizo kubwa la maabara ni Shule ya Sekondari Mwelani, Shule ya Sekondari Mkungo, Shule ya Sekondari Bukamila, Shule ya Sekondari Nyambiti, Shule ya Sekondari Itale, Shule ya Sekondari Rubambangwe, Shule ya Sekondari Katende, Shule ya Sekondari Ilyamchele, Shule ya Sekondari Buhingo, Shule ya Sekondari Kasenga, Shule ya Sekondari Nyambogo na Shule ya Sekondari Nyamirembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unakwenda kugawa fedha hizi na ninaomba kwenye shule zile tuweze kupata angalau tujenge maabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine kwa Wizara ni kukamilisha ile miradi ambayo imeanzishwa na Wizara. Iko miradi mingi ambayo imeanzishwa imepeleka fedha nyingi. Kwa mfano, pale Chato kulianzishwa shule ya watoto wenye mahitaji maalum, ile shule imepeleka zaidi ya bilioni nne ambazo zimetumika, leo hii ni miaka mitatu shule ile imeshindwa kufunguliwa kwa sababu tu imekosa shilingi 900,000,000 lakini shilingi 400,000,000,000 imekwishatumika, shilingi 900,000,000 ndiyo imekosekana ya kwenda kukamilisha shule ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Waziri kwamba wakati unakwenda ku-wind up utueleze watu wa Chato, shule ile ni ya watoto wenye mahitaji maalum kwa Tanzania kwa sababu ziko shule tatu tu ambazo zilianzishwa katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watoto wanahitaji kusoma, lakini leo ukienda kwenye shule ile majengo yameanza kuchakaa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakwenda ku-wind up ahakikishe kwamba anatueleza hiyo shule ya Chato inakwenda kuanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye miundombinu na kwenye maeneo ambayo ujenzi ulikuwa umeshaanza, Mkoa wa Geita hatuna tawi la chuo kikuu, lakini kulikuwa kumeanzishwa na Wizara kwenda kujenga Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale Chato kwenye eneo la Kasagara, lakini mpaka sasa hivi nikwambie yule mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi hiyo ya kwenda kuanzisha ujenzi wa chuo kikuu kile alishabeba mitambo, alishabeba kila kitu akaondoka, ameacha eneo lile. Eneo lile lilichukuliwa kwa wananchi na wananchi wakapata fidia yao, lile eneo sasa wanataka wananchi kuanza kuvamia na kwenda kuendeleza shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwamba, tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linapaswa lijengwe pale Chato, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi atusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake pia Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba wanakwenda kuanzisha maktaba, Chato kulianzishwa ujenzi mkubwa wa Maktaba ya Taifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja. Maktaba kubwa ya Taifa ilianzishwa pale, ambapo maktaba ile itakapokwisha itasaidia watu wengi na wanafunzi wengi kutoka kwenye shule nyingi ambazo zinazunguka Mji wa Chato na vyuo vikuu ambavyo tunatarajia kuvianzisha pale, kipo Chuo cha IFM, kipo Chuo cha Utumishi wa Umma.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ahsante kwa mchango wako.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)