Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Cornel Lucas Magembe (2 total)

MHE. CORNEL L. MAGEMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamirembe ambapo ni Makao Makuu ya Tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe, Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 Serikali imejenga na kuboresha jumla ya vituo vya afya vitano katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa gharama ya jumla shilingi bilioni 2.64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na mwaka 2025/2026 Serikali imetoa jumla shilingi milioni 489 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu katika zahanati ya Kasenga na kuwa kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma za dharura na za upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga jumla shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato kikiwemo Kituo cha Afya Iparamasa kilichotengewa jumla shilingi milioni 108.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati kikiwemo Kituo cha Afya Nyamirembe ili kusogeza huduma za dharura na upasuaji kwa mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya ukarabati wa Shule za Msingi Nyamirembe, Nyabugere, Katende na Magiri ambazo zimechakaa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe, Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu chakavu au ujenzi wa miundombinu mipya katika shule ambazo miundombinu yake haiwezi kukarabatiwa. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026 Serikali imetoa shilingi bilioni 3.09 kwa ajili ya ujenzi shule za msingi 11, madarasa 153 katika shule chakavu 24 na ukamilishaji wa madarasa matatu katika Shule za Msingi Nyamirembe na Magiri Wilayani Chato.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga shilingi 150,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita katika Shule za Msingi Katende na Nyarubugere. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha za ukarabati au ujenzi wa miundombinu mipya katika shule za msingi chakavu nchini ikiwemo Shule za Msingi Nyamirembe, Nyabugere, Katende na Magiri, ahsante.