Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Cornel Lucas Magembe (5 total)

MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja la nyongeza. Kuna vijiji takribani vitano katika Jimbo la Chato Kaskazini, ambavyo ni Vijiji vya Mkungo, Nyakato, Buzirayombo, Itale na sehemu kubwa ya Ilyamchele. Vijiji hivi havipati mawasiliano kwa sababu hakuna mtandao na hii husababisha utoaji wa elimu hasa kwenye shule za msingi na Sekondari ambako sasa wanatumia TEHAMA wanafunzi wanashindwa kupata haki yao kama wanafunzi wengine. Je, Wizara ina mpango gani wa kwenda kuweka mtandao katika maeneo hayo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la ndugu Mheshimiwa Magembe, Mbunge wa Chato Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la swali la msingi, tunatambua changamoto ya mawasiliano nchi nzima na ninaamini kila Mbunge aliyemo katika jengo hili ana changamoto ya mawasiliano katika Jimbo lake kwenye sehemu moja au nyingine. Ndiyo maana sisi kama Wizara tunaandaa mkakati wa miaka mitano wa kuyafikia maeneo yote yenye changamo ya mawasiliano na tunaamini katika kipindi hiki cha miaka mitano, tutafika kila eneo kule ambako hakuna minara, tutajenga minara mipya, kule ambako minara imezidiwa, tutaiongezea nguvu ili kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 changamoto ya mawasiliano katika Majimbo mbalimbali na hapa nchini iwe imepungua kwa kiasi kikubwa au tumeimaliza kabisa. (Makofi)
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ninapenda kujua Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini atapanga safari ya kwenda na mimi jimboni ili akajionee hali halisi ya Kata ya Nyamirembe ambayo ni makao makuu ya tarafa ambayo ina wakazi zaidi ya 23,000 na vijiji vinne ambao wanahitaji kwa haraka utekelezaji wa ujenzi wa kituo hiki cha afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile tayari Serikali imeshapeleka fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasenga, lakini Kasenga ni moja ya kata zilizoko kwenye Tarafa ya Kachwamba, ambapo kuna kata nne ambazo mpaka sasa hawana gari la wagonjwa (ambulance). Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapata ambulance ambayo itawasaidia katika kuwaharakisha kuwapeleka katika hospitali nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya kaka yangu Mheshimiwa Cornel Lucas Magembe, kule tumezoea kumwita mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Magembe kwa kuendelea kuwapambania Wananchi wa Jimbo la Chato Kaskazini. Nianze kwa kujibu swali la kwanza kwamba lini tutafanya ziara katika kata hii yenye wakazi zaidi ya 23,000 ili kujionea hali halisi na kuboresha miundombinu? Nimwambie tu kaka yangu, kwamba Jimbo la Chato Kaskazini liko katika Mkoa wa Geita, na mimi ninatokea Mkoa wa Geita, Jimbo la Busanda. Kwa hiyo, huyu ni jirani yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatenga muda mimi na yeye tuweze kwenda kuwaona wananchi hao na kuwaambia nini Serikali inaendelea kufanya kwa ajili ya maendeleo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshawasiliana na wenzetu Wizara ya Afya, zile ambulance ambazo zimeshafika tuweze kuzitoa na tumalizie taratibu za Kiserikali ili tuweze kuwapatia hasa wahitaji, na hasa zile kata ambazo hazikupata na zile halmashauri ambazo hazikupata waweze kupata ambulance hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Spika, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza lenye sehemu (a) na (b). Kwanza ninapenda kujua Barabara ya kutoka Nyamirembe – Ichwankima – Kasenga – Biharamulo yenye zaidi ya kilometa 50, itaanza kujengwa lini, kwa sababu imekuwa ikiwekwa kwenye mpango wa ujenzi, lakini utekelezaji wake umekuwa haufanyiki?

Mheshimiwa Spika, la pili, ...

SPIKA: Ah, ah, swali ni moja tu.

MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari ameshafika ofisini kwa ajili ya kuulizia hiyo barabara. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulishafanya usanifu, na katika mwaka wa fedha uliopita ilikuwepo kwenye bajeti. Nimhakikishie kwamba barabara hii tutaiweka kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami, kwa sababu tayari pia wenzetu wa uchukuzi wameshajenga bandari pale Nyamirembe ambayo sasa bila hiyo barabara itakuwa haina maana.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninapenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mradi mkubwa wa maji uliojengwa kwenye Mji wa Chato ambao ni miongoni mwa miradi ya maji katika miji 28 sasa umekaribia kukamilika kwa 90%, lakini mpaka sasa sijaona kama hatua ya upelekaji maji imeanza. Katika vile vijiji 23 ambavyo mradi mkubwa umepita, vinavyotoka katika kata za Vikome, Ijamchele, Katende na Muungano, je, kauli ya Serikali ni nini juu ya mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa miji 28 katika Mji wa Chato, na kweli uko katika hatua nzuri kabisa, lakini sera yetu ya maji ni kuhakikisha kwamba pale ambapo chanzo cha maji kinatoka, wananchi wa eneo hilo wanakuwa wanufaika namba moja. Hilo la kwanza; pili, pale ambapo bomba kuu (transmission line) inapopita, wananchi left and right kilometa 12 wawe wanufaika wa maji ambayo yanachukuliwa kutoka kwenye chanzo; na tatu, kule sasa kulikokusudiwa kupeleka maji ndipo sasa watakuwa walengwa namba tatu.

Mheshimiwa Spika, hili tutaendelea kulisimamia isipokuwa kuna miradi ambayo tunaanza kwanza kwa kujenga bomba kuu, na baadaye zinaanza kupatikana offtake kulingana na vijiji sasa ambavyo vimepitiwa katika lile bomba kuu.

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu kwamba vijiji vyake tutahakikisha tunafanya usanifu na kufanya ile needs assessment ili kuhakikisha wananchi wa vijiji na kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, zinapitiwa na kunufaika na mradi huo wa maji kutoka miji 28.
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kupeleka kwenye Halmashauri ya Chato kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye shule hizi ambazo nimemuuliza Naibu Waziri, hasa Shule ya Nyamirembe, Shule ya Nyabugera, Shule Magiri na Shule ya Msingi Katende na Shule ya Msingi Rutunguru, ni shule ambazo kwa sasa ukifika ni hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi zina zaidi ya watoto 2,000 kwa kila shule, lakini unakuta kuna madarasa matatu ambayo yanafanya kazi na madarasa mengine ni chakavu kabisa. Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia njia za haraka ili kuhakikisha kwamba watoto hawa wanawanusuru hali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba shule hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge wa Chato Kaskazini amezitaja ni shule kongwe na chakavu na ndio maana Serikali imeendelea kupeleka fedha kwa awamu kuhakikisha kwamba shule hizi ninakarabatiwa na katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imepeleka zaidi ya shilingi bilioni tatu na milioni tisini kwa ajili ya ukarabati wa shule hizi chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 mwaka ujao Serikali imetenga shilingi 150,000,000 kwa ajili ya shule hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja ili zikarabatiwe na ziwe na viwango vizuri kwa ajili ya kutoa huduma ya elimu kwa wanafunzi. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Magembe, kwamba Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa shule zetu na ndio maana tumeendelea kutenga fedha kwa awamu na fedha hizo zitapelekwa mwaka ujao wa fedha ili kukarabati shule hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia hapo, Serikali imefanya tathmini ya uchakavu wa shule za msingi kote nchini na kutambua jumla ya shule 10,595 kongwe na chakavu ambayo tathmini ya awali inaonesha tunahitaji takribani shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuandaa mipango ya ukarabati wa shule hizo kwa awamu ili ziwe na ubora unaotakiwa kwa ajili kutoa huduma hapo shuleni. Ahsante. (Makofi)