Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Moses Ludovico Kaegele (2 total)

MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kijiji cha Tundu ni kijiji chenye wakazi zaidi ya 3000 na kijiji hicho kipo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, namna pekee ya kufikia pale kijijini ni njia ya maji. Tokea ziwa limechafuka wakazi wa pale hawafikiki. Je, ni lini serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufungua Barabara kutoka Kala kwenda Tundu na kujenga madaraja mawili ili wananchi hawa waweze kupata huduma za msingi kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninaomba nikiri kuwa Mheshimiwa Mbunge alikwishakuja ofisini kwenye ofisi zetu za TAMISEMI. Tumekwishakaa na watalam, tumeangalia umuhimu wa barabara hii ambayo ipo pembezoni kabisa, lakini inaenda kwenye kata yenye wakazi zaidi ya 3000. Kupitia mradi wetu wa Mheshimiwa RISE tunaangalia uwezekano wa kuweka madaraja; ambapo yanahitajika madaraja takribani matatu; ili tuweze kufungua uchumi kwa eneo lile na kusaidia wananchi wetu wa eneo lile.
MHE. MOSES L. KAEGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu ambayo yana matumaini, lakini nina swali moja la nyongeza. Katika vijiji hivyo yapo maeneo ambayo yapo nje ya Hifadhi ya Loasi ya mipaka ya Hifadhi ya Loasi halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado maeneo hayo yanaendelea kulindwa na watu wa hifadhi; na kwa kuwa wananchi wanaongezeka, lakini ardhi haiongezeki, je, Serikali haioni ni muda mwafaka basi wa kwenda kuangalia hiyo mipaka ili yale maeneo ambayo yapo nje ya hifadhi yaweze kurejeshwa kwa wananchi waweze kujiandaa na msimu wa kilimo ujao kwa ajili ya kuwaepusha na migogoro mingine ambayo inaweza kutokea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la Ndugu yangu Mheshimiwa Kaegele, kwanza ninampongeza sana kwa namna anavyowapambania wananchi wake hasa katika suala hili. Ni mara kadhaa anakuja ofisini, tunakaa kuzungumzia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali imepokea ushauri wake na ipo tayari kupeleka wataalamu wake kushirikiana na Halmashauri pamoja na Ofisi ya Mbunge ili kwenda kuhakiki mipaka hii na kutoa ufafanuzi unaofaa kwa maendeleo na maslahi ya wananchi.