Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu mpendwa aliyoitoa jana ambayo kimsingi iliakisi na kuonesha wazi nia na dhamira ya wazi kabisa ya Serikali yetu ya kutatua matatizo yanayoikabili nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda kuchangia katika suala zima la ukombozi wa kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu. Binafsi pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa, lakini bado ninaendelea kuamini kwamba ukombozi wa kiuchumi wa nchi hii na kuwafanya wananchi wetu kuacha kuendelea kumiminika kutoka vijijini kuhamia mijini; ni kuendeleza kwa juhudi kubwa mambo ya msingi ya kimaendeleo katika maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna yoyote ile, ni lazima tuje na jibu la kimsingi sana la kuwakomboa wakulima wetu, wanapolima kuhakikisha wanapata masoko, tunawasaidia wanalipwa kwa wakati, lakini pia tuwe na majibu ya zile taasisi mbalimbali zilizoundwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wao kimaisha kama tunavyoongelea vitu kama COPRA, Bodi za Kahawa, Bodi za Mbolea na kadhalika. Serikali lazima ihakikishe kwamba hizi zinafanya kazi vizuri na kwa uadilifu mkubwa ili kuwafanya wakulima wetu waweze kuwa na uhakika wa kwamba wanachokilima kinarudi kwao na kuwapatia faida ili waweze kuendesha maisha yao na familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunakabiliwa na matatizo makubwa katika maeneo ya vijijini. Mambo mengi yamjadiliwa, lakini kwa kuwa hii ni hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na huenda nisipate nafasi nyingine ya kuchangia kwa kina kama leo. Hivyo ninaomba sana, pamoja na yote yaliyosemwa, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa, bado tunalo tatizo kubwa sana hasa maeneo ya vijijini, miradi ya maji kule imekwama kwelikweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo sehemu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini yeye kama msimamizi mkuu wa Serikali, kwa kweli ninaomba aliangalie kwa jicho la pekee sana eneo hili. Mathalani katika wilaya yangu, Vijiji vya Mbanga, Lituhi, Puru, Nangombo, Ngendere, Ngumbo, Malungu, Lihuli, kote kuna miradi ya maji iliyowekwa, lakini miradi hii yote hakuna hata mradi mmoja unaoendelea mpaka sasa imesimama na hivyo kuwapatia maisha magumu sana wananchi wa vijijini ambao wengi wao wanatamani waje mijini kupata huduma bora wakati wangebaki kule na kulisaidia Taifa letu katika ukuzaji wa uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuzunguka na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama katika mikoa mbalimbali na wilaya mbalimbali. Mheshimiwa Waziri Mkuu anafanya kazi kubwa sana kwa niaba ya Serikali. Hata hivyo, ninaendelea kutoa rai kwamba kazi hii anayoifanya ni lazima iendane na kuunda controls, kuunda miundombinu ya Serikali itakayoweza kusimamia huko chini wanapoondoka na miradi inapokwenda iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, controls hizi zitafanya kwamba si lazima kiongozi apite mwenyewe physically ili kupata taarifa ya maovu yaliyokuwa huko chini, ubovu na utekelezaji wa kazi huko chini uwe na muundo rasmi unaoweza kufanya Serikali Kuu kufahamu kila mahali nini kinafanyika, nini kinaendelea na matokeo yake yakaja huku kwa ajili ya utekelezaji. Sasa hivi hapa tukiongea karibu kila Mheshimiwa Mbunge atakwambia kuna miradi iliyokwama kwake na Serikali Kuu kwa muda mrefu haina taarifa na haijachukuliwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukiendelea kujenga Serikali ambayo itasubiri mpaka Viongozi Wakuu wafike kule ndiyo waweze kutatua yale matatizo na kuyaona, itatuchelewesha kama nchi. Tujenge controls, Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inakuwa decentralized, inashuka chini kwenye halmashauri huko chini kuzisimamia. Ikiendelea kusimamia kutoka pale juu ni ngumu sana kufika na kuelewa nini kinafanyika huko chini na kurekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali inabana matumizi kwa sababu tuliambiwa na Mheshimiwa Rais hapa kwamba masuala yanayoendelea kiuchumi duniani siyo rahisi kupata miradi na fedha nyingi tulikuwa tunapata kwa wafadhili. Sasa katika hili, ninaomba pia kuchangia na kutoa mawazo kwamba moja ya sehemu kubwa sana ambayo Serikali inatumia matumizi makubwa sana ukiangalia kwenye bajeti, ni matumizi ya magari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa rai kwamba, sasa hivi imefika wakati maalum ambapo Serikali ianze kuangalia aina ya magari yanayotumika na kazi anazofanya mtumishi. Unakuta mtumishi yeye ni Mkurugenzi, lakini anafanya kazi Dodoma tu hapa, hatoki nje ya Dodoma, kazi yake iko hapahapa Dodoma na njia zote ni za lami, lakini anatumia V8 ya shilingi 480,000,000/=. Kwa nini asingetumia gari ya kawaida kwa sababu yuko eneo la mjini hapahapa na haendi mbali. Serikali inatumia V8, Land cruiser zaidi ya mia nne na kitu ambacho wengine hata hawakupaswa kuyatumia hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho sasa hivi ninawakumbusha hata hawa ambao wanayatumia hayo magari kwamba sasa hivi tuna tatizo la mafuta. Utakuta sasa hivi bado madereva wetu wanakaa na haya magari asubuhi mpaka jioni wanatusubiri huku yanaunguruma tu, yanakula mafuta tu pale. Sasa unajiuliza haya mafuta wanajua yananunuliwa kwa dola? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni gharama ya Serikali, mtu anamsubiri bosi wake, anaungurumisha gari ya Land Cruiser asubuhi kuanzia saa mbili mpaka saa saba mchana linaunguruma eti lisipate joto, sasa lisipate joto namna gani na mafuta haya ni ya Serikali. Tunapotaka kudhibiti matumizi ya Serikali, tuanze na sisi wenyewe viongozi, tudhibiti matumizi ya aina ya magari tunayotumia lakini pia na matumizi ya mafuta yanayotumika na magari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika kwenye gari lako muulize dereva wako kwa nini unaungurumisha gari toka asubuhi mpaka saa saba, haya mafuta ni kodi ya wananchi. Kwa hiyo, Serikali ina kila sababu sasa hivi ya kuhakikisha inatengeneza controls kuanzia za mtu mmoja mmoja mpaka za Serikali ili tuweze kubana matumizi na kuhakikisha fedha zinazobanwa zinarudi kwa wananchi kwa ajili ya kuleta maendeleo kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia haya, ninaomba kutoa shukrani tena kwa wananchi wangu ambao ninachangia kwa niaba yao na kwamba nitaendelea kuwahudumia na kuwaletea michango yao kadri wanavyonituma na ninashukuru sana kwa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOHN J. NCHIMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipatia. Kwanza kabisa ninaungana na mwenzangu aliyepita kuipongeza na kuitakia kheri kwa mwaka mpya wa fedha unaokuja Wizara ya Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi pia ninapenda kuwapongeza katika maeneo machache. Moja, ni kuendelea kuimarisha kwa utoaji wa huduma kwa umma, hasa kupitia e-Government. e-Government imekuwa ikitatua matatizo mengi sana ya Watanzania na inawapunguzia adha mbalimbali. Pia ninapenda kuwapongeza katika eneo la uwajibikaji, hasa upokeaji wa malalamiko kwa kuanzisha mtandao wa kupokea malalamiko na wananchi wengi wanapeleka malalamiko yao kule na yanachukuliwa hatua zinazostahiki na wanajibiwa kwa wingi inavyowezekana; kwa hili pia nipongeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho pia ninapenda kuwapongeza kwa kuendeleza na kuwezesha kukaribia kufikia hatua ya 50/50 kati ya akina mama na akina baba katika utumishi wa umma. Hili ni jambo kubwa sana na pengine tunaweza tukawa tunaongoza katika Afrika Mashariki katika kuwasogeza akina mama katika nafasi hizo na wamekuwa ni msingi wa utumishi bora katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya, nitakuwa sijatendea haki nafasi yangu kama sitatoa ushauri kidogo ili na wao waone wapi pa kwenda kurekebisha na wapi pa kupaangalia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza ninachopenda kukiongelea hapa, bado kuna changamoto sana ya upungufu wa walimu maeneo ya vijijini na wafanyakazi wengine kama wa afya na kadhalika. Maeneo ya vijijini yana upungufu mkubwa sana na maeneo ya mijini na wizarani wamejaa watumishi wengi sana. Ninaifahamu wizara moja ina watumishi kama 60 lakini maafisa utumishi wapo 14. Nilikuwa nawauliza mnafanyaje kazi? Wanasema kuna wiki unaweza ukawa hujagusa file hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa watu wanatakiwa watawanywe na kutengenezwa usawazishaji ili waweze kwenda vijijini. Sasa, hii ni kazi ya Utumishi kufahamu nani yupo wapi, anafanya kazi gani na anafanya kwa mazingira gani. Hii lazima Utumishi waifanye, ni kazi yao muhimu sana ili kuweza kufanya maeneo ya pembezoni yaweze kupata watumishi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010 tatizo hili lilionekana, kwamba maeneo ya vijijini watumishi hawapendi kukaa kwa sababu mazingira ni magumu, sehemu nyingine hamna nyumba, hamna chochote. Serikali ilianza mchakato wa kutoa mwongozo wa kuwapatia motisha wale walimu na watumishi wengine wa afya na kadhalika, wanaokaa mazingira magumu maeneo mbalimbali. Mwongozo ule ulipita na mpaka leo haujaanza kutekelezwa; lakini wenzetu wa Utumishi wameendelea kuwahamisha watumishi vijijini na kuwaleta mijini badala ya kuwatekelezea mwongozo huu ili wabaki kule kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huu mwongozo ninafikiri umefikia wakati sasa kwa Mawaziri hawa ninaowaona na kasi yao utekelezwe ili kuwapatia motisha watumishi walioko maeneo ya vijijini waweze kukaa, walioko maeneo yenye mazingira magumu waweze kukaa na kufanya kazi na kulitumikia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianzisha utaratibu wa kupima utendaji kazi kwa kutumia PEPMIS; ule utaratibu umeanza kutumika na sasa ninafikiri ni mwaka mmoja na kitu. Ninadhani ni wakati muafaka wa kwenda kuupitia upya. Utaratibu ule kwa sasa na nao umegeuka kuwa kazi, kwa sababu mtumishi anatumia masaa mengi kuujaza ule mfumo; na nchi yetu ina maeneo mengi hayana mtandao, inabidi wapande pikipiki na baiskeli kwenda sehemu za mbali kwenda kujaza ili wasikose vyeo kwenye upandishaji wa vyeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daktari mmoja wa Muhimbili ananiambia alikuwa anafanya surgery ya wagonjwa 14 kwa wiki, imebidi apunguze mpaka 13 ili ajaze mfumo wake wa PEPMIS asije akakosa cheo. Mfumo wa PEPMIS umegeuka kuwa kazi badala ya kitendea kazi cha kupima performance. Waende kwa watumishi watawaeleza haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa rai kwa Utumishi wajipunguzie kazi. Wanafanya kazi nyingi sana ambazo wangeweza kuzifanya zikafanywa kwenye taasisi na kadhalika. Kwa mfano, mashirika ya umma tangu miaka ya 1961, mzee wangu Profesa hapa atatuambia, wamekuwa wana bodi zao, wanaajiri wenyewe, wanatengeneza succession plan, watumishi wanakua. Sasa hivi Utumishi imenyang’anya ile inaajiri kwa niaba yao. Wale waliwekwa ili wawe semi-government autonomies, waweze kushindana na private sector.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukimchukua mwanasheria kutoka kwenye halmashauri yangu mimi, ambaye amezoea kukusanya kodi, unampeleka aende aka-vet mikataba kwa sababu yeye ni senior, hawezi kuwa mwanasheria sawa na yule aliyezoea kupitia mikataba. Hata kama ni mwanasheria, lakini professionally, mme-grow up tofauti, lazima mwende katika yale maeneo yenu. Sasa, Utumishi hawezi kuwa jack of all trades, anataka aende huku aajiri, aende huku aajiri, aende huku ahamishe, atoe huku apeleke huku. Hiyo inawafanya kule kunakuwa kuna weakness kubwa na Utumishi wenyewe wanashindwa kuangalia masuala ya msingi, wanakuwa wote wanagombania kupeleka watumishi maeneo yenye maisha bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barua za watumishi za malalamiko, barua za kupanda vyeo wakiwa wameonewa na kadhalika zikienda Utumishi zinakaa mpaka mwaka mmoja hazijajibiwa. Maafisa utumishi wanaogopa kuyasema haya kwa sababu wanaogopa ni mabosi wao. Sasa, leo tunaona tuwaambie, watengeneze utaratibu wa siri kuwafuata watumishi wakawaoneshe jinsi ambavyo barua zao zinaachwa kujibiwa zaidi ya mwaka ndani ya utumishi. Hili jambo ninadhani likiwa sasa kwa kasi mpya ya Mawaziri wapya ninaamini litakwenda kurekebishwa bila tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahamisha watumishi bila kuangalia weledi wao. Mwaka jana au mwaka juzi, kuna nurse amekwenda India kusoma miezi sita, robotic surgery ambazo nchini kwetu ndiyo zinaingia. Amekaa miezi sita kwa gharama zetu sisi akisoma robotic surgery, amerudi amekaa mwezi mmoja kapata barua ya Utumishi, akahamishiwa damu salama kwenda kukusanya damu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa haya tutanyamaza vipi? Ni kwa sababu Utumishi wanakaa pale mezani wanaanza kuhamisha, peleka huyu, peleka huyu! Hawafanyi consultation na Wizara Mama, hawafanyi consultaion na mashirika, hawafanyi consultation na Wakurugenzi wa Halmashauri kujua yule wanayemuhamisha ana umuhimu gani kule wanakotaka kwenda kumtoa. Sasa hii haiwezi kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji nchi hii kuwa na Salary Board itakayokuwa inasimamia mishahara ya watumishi wa umma. Sasa hivi Wabunge watakuwa ni mashahidi, kila ndugu yake anayemjua anakufuata anamwambia nihamishie shirika fulani, nihamishie shirika fulani kwa sababu lina mishahara bora na yale mashirika bora hata kusikia yanatangaza kazi ni ngumu sana. Mara zote utaona tu kule kuna watumishi wanaingia wapya, wanaingia lakini hata kutangazwa huwa hayatangazwi. Mara moja moja utaliona moja au mawili. Yale yenye mishahara bora sitaki kuyataja nitakuwa siko sawasawa na nitakuwa sijawatendea haki, lakini wanayajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule hata mtumishi akiwa amestaafu, mwezi haupiti vetting imemalizika na mtu mpya kashaingia na ameajiriwa. Ukienda yale mashirika ya mwenzangu na mimi ya Posta, mwaka mmoja, miwili hakuna mtumishi kaenda pale kwa sababu hakuna anayetamani kwenda. Wanakwambia vetting bado, vetting bado, vetting bado, lakini hawa watumishi wanaogombania kwenda kule wana sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtumishi ni mhasibu kama mhasibu mwingine yuko halmashauri, yupo wizarani, yupo wapi akitoka tu akienda e-Government anatoka na mshahara wa milioni mbili mpaka milioni kumi na tano. Nani ataacha kugombania kwenda huko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inawa-demoralize wengine ambao wanaona; hii Serikali ni yetu wote na nchi hii ni yetu wote. Watumishi wote lazima waende kwenye utaratibu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOHN J. NCHIMBI: …waende kwenye utaratibu wa Salary Board itakayokuwa ina-regulate mishahara ya watumishi wote ili kupunguza tofauti iliyokuwepo hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ninaamini haya yatafanyiwa kazi katika bajeti inayokuja. (Makofi)