Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Chacha Mwita Wambura (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CHACHA M. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia siku hii ya leo katika bajeti hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha sisi sote tuna afya na tumeweza kuwemo ndani ya hili Bunge. Pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anatusimamia na kutuongoza kama Kiongozi wetu Mkuu katika nchi yetu hii ya Tanzania. Pamoja na yeye niwapongeze sana na kuwashukuru wasaidizi wake wa karibu Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali hasa Wizara yetu hii ya Nishati. Kiukweli bila kificho na kila mmoja na kila Mtanzania anaona jinsi gani ambavyo Wizara ya Nishati inafanya kazi nzuri hapa Tanzania. Wizara hii imekuwa ni mojawapo ya Wizara ya mfano katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata umeme. Siyo kupata umeme tu hata katika service pale ambapo kunakuwa kuna changamoto Wizara hii watu wake wamekuwa waki-respond kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana watendaji wote wa TANESCO Tanzania kwa jinsi ambavyo wana-respond kwenye matatizo ya umeme yanavyokuwa yametokea kwa uharaka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee sana ni ushahidi uliotosha kabisa kuona jinsi ambavyo Wizara imeshughulika na suala la mafuta. Nchi zingine jirani tunaona kwamba kuna changamoto kubwa na wengine wamefika sehemu hata vituo havina mafuta lakini kwa Tanzania tunajivunia Wizara yetu, tunajivunia Mheshimiwa Rais wetu kwa jinsi ambavyo amehakikisha masuala ya mafuta kwetu Tanzania hatujapata upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tunavyozungumza, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba, mafuta tunayo na siyo tu kwa taarifa, ukienda kwenye vituo Tanzania nzima utakuta vituo vyote vimefunguliwa na mafuta yanapatikana. Kwa jambo hili ninapenda kuwapongeza sana Wizara ya Nishati ambayo inaongozwa na Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na mambo mazuri hayo, ninapenda kusema jambo moja. Katika maisha changamoto inapotokea inatengeneza fursa. Sasa katika suala zima la changamoto ya mafuta ilivyotokea tumeona kwamba, kuna fursa zingine zimejitokeza ambazo, kama Serikali na kama Wizara na kama Taifa, tunahitaji kuharakisha na kuongeza nguvu kuhakikisha tunaendelea kwenye hivyo vipaumbele vingine, ili pale ambapo mafuta yanaleta changamoto tuweze kupata njia mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hapa tunayo gesi, lakini pia, tunao umeme ambao tunaona kabisa kwamba, tuna mpaka excess. Tunajua kwamba, nchi zingine duniani zinabadilika, zinatoka kwenye kutegemea sana mafuta zinaenda kwenye kutegemea gesi pamoja na umeme. Sisi hapa Tanzania, wale ambao tumefanikiwa kwenda kwenye maonesho ya TANESCO pale, kwenye Wizara ya Nishati tumeona gari ambalo linatumia umeme. Kama leo tungekuwa tunayo magari mengi Tanzania yanayotumia umeme tusingekuwa tunawaza sana mafuta kwa sababu tungekuwa tume-switch na tunatumia umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kuangalia pia, Tanzania hapa tunayo gesi na kuna magari tayari yameanza kutumia gesi. Ombi langu na ushauri wangu sasa kwa Serikali ni kwamba, tuongeze kasi kwa Tanzania nzima kuongeza hizi filling station za gesi, tuongeze hizi sehemu za kuchaji magari, ili tuhamasishe Watanzania wengi zaidi waweze kuagiza haya magari na inapotokea crisis kama hii, basi tuweze kupata alternative ambayo watu wanaweza wakatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia magari ya Dangote yanaweza yakatoka kule Mtwara mpaka Dar es Salaam kwa kutumia gesi, lakini hayo hayo magari ya Dangote hayawezi kuondoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza, kuelekea Kanda ya Ziwa kwa kutumia gesi. Wakifika Dar es Salaam inakuwa ni kituo na huku hivi inakuwa hakuna. Kwa hiyo, tukifanikiwa kuongeza filling stations za gesi na umeme watu hawatanunua magari na tutapunguza tatizo la mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ninaomba pia, niweze kuzungumzia jambo moja lingine ambalo ninatamani niishauri Wizara yetu ya Nishati. Tunajua kabisa miundombinu yote ya umeme inamilikiwa na TANESCO, muundombinu wowote unapokuwa mahali popote huo muundombinu unaanza kumilikiwa na TANESCO. Sasa Wizara imesema kuna Sheria ipo inaruhusu mwekezaji kujiunganishia umeme halafu akawa anarudishiwa kwa asilimia kidogo kidogo, hela kiasi inaenda kwenye Wizara na kiasi anajirudishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tunalifahamu watu wachache sana. Ninaiomba Wizara iende kutangaza jambo hili, iwafahamishe wawekezaji, ili kila mwekezaji anapotaka kuweka umeme, anapokuwa na mradi wake, asisubiri TANESCO mpaka ipate bajeti, asisubiri Wizara mpaka ipate bajeti, aweze kujivutia umeme akiwa na assurance kwamba, ile pesa itarudishwa. Maana kama akiwa na assurance hiyo atapeleka hakika umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, kuna jambo kubwa ambalo ninalichukua kuwapongeza sana REA. REA wamefanya kazi kubwa hapa Tanzania, wamesambaza umeme, umefika sehemu nyingi sana, lakini kuna jambo moja dogo ambalo wakati mwingine linachafua ule uzuri wa jambo lile ambalo limefanyika; kuna sehemu moja unakuta mwananchi mmoja anafanyiwa connection na REA na mwananchi mwingine anafanyiwa connection na TANESCO. Gharama za ku-connet watu hawa ambao wako sehemu moja ni tofauti. Ninaiomba Serikali iende ikafanye tathmini upya kwa jambo hili. Ione jinsi gani inaweza ikasimamia na kuondoa hizi dosari ndogo ambazo mwisho mwisho wa siku zinaweza kuharibu jambo kubwa zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na Mungu awabariki sana. Ahsante sana. (Makofi)