MHE. DKT. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulipa shilingi milioni 5.9 kwa wananchi 26 wa Kata za Kisongo, Musa na Mwandet ambao wameathiriwa na wanyamapori wakali sana.
Mheshimiwa Spika, wanyama hawa wamebadili tabia, wakawa wanashambulia watu na wahifadhi. Pia kuna majangili wanatumia silaha za kisasa, wanawashambulia wananchi na wahifadhi wa maliasili. Je, lini Serikali itawapatia wahifadhi wa maliasili waliopo Jimbo la Arumeru Magharibi silaha sitahiki aina ya SMG au AK-47 ili wahifadhi waweze kuokoa maisha ya wananchi na mali zao; pia wahifadhi wawalinde wanyamapori wetu ili wasiendelee kuuawa na hawa majangiri?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini watapewa silaha hizo? Kwa mujibu wa sheria na kanuni zetu, wahifadhi wetu wana viwango maalumu vya umiliki wa silaha. Siyo kila aina ya silaha wanaweza kutumia.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kumhakikishia ni kwamba, Askari wetu wa hifadhi wataendelea kupewa silaha zinazostahiki kwao ili kuhami wanyamapori wetu na kupamba na majangili.
MHE. JOHANNES L. LUKUMAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Arumeru Magharibi lina wakulima wazuri sana wa mazao ya mboga mboga. Wakulima hawa wanapoteza mazao yao ya mboga mboga baada ya kuvuna.
Je, Serikali itasaidia ujenzi wa vyumba vya kutunza baridi yaani cold rooms Kata ya Bangata na Kata ya Ilkiding’a ili wakulima hawa wasiendelee kupata hasara?
Mheshimiwa Naibu Spika, la nyongeza kidogo, ningemwomba Naibu Waziri kama atakubaliana na mimi kuongozana kwenda Jimbo la Arumeru Magharibi akashuhudie hao wakulima wazuri wanavyopoteza mazao yao ya mboga mboga. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimthibitishie tu Mheshimiwa Dkt. Johannes, Mbunge wa Arumeru Magharibi kwamba moja, niko tayari tutaongozana mara baada ya Bunge la bajeti nitafika maeneo mengi nchini, lakini la pili ni kwamba Serikali moja ya mpango tulionao ya kupunguza hii post-harvest loss ni kujenga cold rooms katika maeneo yote yanayofanya kilimo cha mboga mboga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lipo katika mipango ya Serikali, kwa hiyo, nitakuja kujionea na baada ya hapo tutafanya maamuzi. Ahsante sana.