Supplementary Questions from Hon. Ado Shaibu Ado (11 total)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona. Kwa vile tatizo hili la tembo kuvamia vijiji na kuharibu mazao, kuuwa binadamu ni tatizo kubwa sana katika Jimbo la Tunduru Kaskazini na Wilaya ya Tunduru kwa ujumla wake. Ambapo kwa msimu wa kilimo wa 2025/2026 peke yake jumla ya waathirika 1791 wameharibiwa mazao yao na askari wa vijiji mpaka sasa wako 23 tu. Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa waathirika wote na kuongeza idadi ya askari wanyamapori wa vijiji (VGS)?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshaweka fedha na zimeshaingia na sasa tunafanya utaratibu wa kulipa kupitia mfumo. Kilichochelewesha ilikuwa tunalipa manual, unaenda kijijini unaenda kulipa, pengine unaenda kulipa milioni tano unatumia gharama ya milioni nne, lakini kwa sasa tunatumia mfumo na mfumo huu umetuwezesha. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira hawa watu wetu watapata malipo yao.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niulize swali dogo la nyongeza. Mbunge wa Tunduru Kusini Mhandisi Fadhili Chilombe, ninafahamu kwamba ameleta hoja na kufuatilia mara nyingi Wizara ya TAMISEMI juu ya haja ya kuigawanya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kupata Halmashauri mbili na mchakato wetu ulifika mpaka RCC, tuna watu zaidi 400,000 na tuna kilometa za mraba 18,000.
Mheshimiwa Spika, tunataka kauli ya TAMISEMI ili Watanzania wanaoishi Tunduru wapate kauli ya Serikali ndani ya Bunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi, uanzishwaji wa mamlaka za kiutawala ikiwemo hili analoliongelea Mheshimiwa Mbunge, Ado Shaibu, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya LAAC unazingatia Sheria ile ya Uanzishwaji ya Mamlaka za Wilaya, Sura Na. 287 pamoja na Sheria ya Uanzishwaji wa Mamlaka za Miji, Sura 288.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa maelekezo na ushauri kwa Halmashauri ya Kibaha, vivyo hivyo wananchi wa Tunduru wafuate utaratibu huo na TAMISEMI kazi yetu ni moja tu kufanya tathmini na mapitio kama vigezo vimezingatiwa. (Makofi)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kaskazini ni moja kati ya majimbo ambayo hayana kituo cha afya kwa kila tarafa, na kwa kuwa Tarafa ya Nampungu ni tarafa pekee ambayo haina kituo cha afya na haijapata bajeti ya kutosha katika ukamilishaji wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mpungu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pia Jimbo la Tunduru Kaskazini lipo katika mpango wa kupata kituo cha afya cha kimkakati; na kwenye yale maombi tuliyowasilisha Hazina kimo kituo hiki cha afya cha Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kukamilisha baadhi ya majengo katika vituo vya afya ambavyo bado havijakamilika ili kuendelea kutoa huduma kwa watu wetu wa Jimbo la Tunduru kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa, Kituo Kikukuu cha Polisi cha Wilaya ya Tunduru ni kikongwe na kidogo, katika mazingira ambayo yanalazimisha sisi akina Ado ambao huitwa mara kwa mara pale kuhojiwa, tumewashuhudia makamanda wetu wakiwa wanaendesha mahojiano ndani ya chumba kimoja kwa watuhumiwa zaidi ya mmoja, hali ambayo inaondoa kabisa weledi, je, ni lini, Serikali itafikiria kujenga kituo kipya cha Wilaya ya Tunduru ili makamanda wetu wafanye kazi kwa weledi na utaratibu unaohitajika, ikiwemo faragha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpomgeza sana Mheshimiwa Ado Shaibu, lakini ninaomba nimkumbushe tu kwamba kituo cha Polisi alichokitaja na vituo vyote vya Polisi nchini, uwepo wake siyo kwa ajili ya akina Ado Shaibu, ni kwa ajili ya wale wote ambao watakuwa wanahalifu sheria za nchi hii. kwa hiyo, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vituo vya Polisi vya ngazi ya wilaya, ambavyo kwa taarifa yetu ya awali tulisema kwamba tuna vituo vya Polisi 75 vya ngazi ya wilaya, ambavyo ama vinahitaji ukarabati au vinahitaji kujengwa upya kwa lengo la kufikisha hadhi ya daraja B, kwa maana ya kituo cha wilaya, kwa hiyo, na kituo cha wilaya ambayo Mheshimiwa Ado Shaibu amekitamka, nacho kipo kwenye mpango huo. Kadiri ya hali ya upatikanaji wa fedha tutaendelea kujenga vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Tunduru, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa Mahakama ya kisasa ya ngazi ya wilaya. Kwa miezi mitano hivi sasa ujenzi ule umesimama. Swali langu ni kutaka kujua, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mahakama ile ili tuweze kupata huduma inayokusudiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ado Shaibu Ado, Wakili Msomi, kwa swali lake zuri lenye lengo la kufuatilia upatikanaji wa haki katika jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niendelee tu kumsisitiza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza mradi wa kimkakati kabisa ambao unatokana na mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama na kwa sasa Mahakama inatekeleza mpango huu wa pili na imetumia wastani wa shilingi bilioni 524.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mahakama kuanzia katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo mpaka Makao Makuu ya Mahakama kama tunavyoliona jengo letu la Judiciary Square.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru aliyoitaja tayari imeshafikiwa na mpango huu wa pili, na tayari mkandarasi yupo site anaendelea na ujenzi wa Mahakama hiyo, nimhakikishie kwamba ni dhamira ya Mahakama kuhakikisha wananchi wanapata majengo bora ya kisasa kwa ajili ya upatikanaji wa haki. Kwa hiyo, jengo hilo litajengwa na litakamilishwa ili wananchi wake waweze kupata huduma bora kabisa za upatikanaji wa haki katika jimbo lake.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Tunduru ni moja kati ya Wilaya ambazo hazina Vyuo vya VETA, na kwa kuwa ujenzi wa awamu ya kwanza wa Chuo cha VETA, Tunduru unaohusisha majengo tisa mpaka sasa bado unasuasua, kwani ulipaswa kukamilika mwaka 2024 lakini mpaka sasa haujakamilika, ni ipi kauli ya Serikali juu ya kukamilishwa kwa Chuo cha VETA Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu kwenye swali la msingi, tunatarajia vyuo hivi kukamilika Septemba, 2026. Hata hivyo, ahadi ya Serikali ni kwamba baada ya Bunge hili nitafanya ziara mahususi ya kupitia Vyuo hivi na kuona maendeleo ya vyuo hivi ili tuone wapi tunakwamua, pale vyuo hivi vilipokwama. (Makofi)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Ninaomba niseme, ingawa mara kadhaa huwa tunaingia kwenye anga za vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa sababu nilitoa ahadi ya kwamba nitakuwa sauti yao ndani ya Bunge hili kupigania maslahi yao na haki yao, siyo Tunduru tu, na nchi nzima, ninaomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa Serikali iko katika kufanya tathmini na kutafuta fedha, na kwa sababu hali ya gereza lile ni chakavu, na inasikitisha sana kwa kiwango ambacho Askari wale wanakosa hata ofisi za uhakika za utawala; na wameanzisha mpango kwa fedha ndogo za utawala wanazopewa kujenga ofisi ndogo nje ya magereza, je, ni kwa nini Serikali katika hatua ya dharura isiwapige jeki Askari wale kuhakikisha kwamba wanapata ofisi ndogo ya utawala wakati mipango mikubwa ya Serikali ikiwa inasubiriwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hali ya Askari Magereza Wilayani Tunduru katika eneo la nyumba za makazi imekuwa ni duni sana, hali ambayo ni ya nchi nzima kwa Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Jeshi la Zimamoto, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Askari wetu nchini wanapata makazi bora ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kuliko hali ilivyo hivi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninampongeza sana Mheshimiwa Ado Shaibu kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Amesema, kwa kuwa wamekuwa wakiingia kwenye anga za vyombo vya ulinzi mara kwa mara, kwanza nimsihi kwamba wasiingie kwenye hizo anga pale isipohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo hivi vya ulinzi na usalama uwepo wake siyo kwa sababu ya kumwonea mtu, ni kwa sababu ya kufuata sheria tulizozitunga sisi Wabunge humu kwa ajili ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuwapiga jeki Gereza la Tunduru, nataka kumhakikishia kwamba Serikali kupitia Jeshi la Magereza itahakikisha kwamba inawapa fedha Gereza la Tunduru ili kuweza kukamilisha ofisi zao kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile hali ya upanuzi kama nilivyoeleza, tutaendelea kutenga fedha kwenye bajeti na fedha hizi nilizozieleza sasa ni zile zitakazotokana na vyanzo vya ndani vya Jeshi la Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali la pili la nyumba za Askari, nikiwa najibu maswali ya msingi jana, nilitoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na nyumba za Askari kwa upande wa Serikali. Mpango uliopo ni wa muda mrefu wa kujenga nyumba 6,368 kwa nchi nzima kwa ajili ya Askari Magereza. Ninamhakikishia kwamba tutaendelea kuutekeleza mpango huo kadri ya hali ya fedha zitakavyopatikana. (Makofi)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ilitoa ahadi katika Bunge hili, kupitia swali la msingi nililoliuliza kwamba inao mpango wa kuhakikisha Kiwanda cha Kubangua Korosho Tunduru maarufu kama Kiwanda cha Bias, kitaanza kufanya kazi katika msimu wa mavuno ya korosho wa mwaka huu; na kwa kuwa imebaki miezi michache kwa msimu wa mavuno ya korosho kuanza, ni ipi kauli ya Serikali juu ya hatua iliyofikiwa ili kuhakikisha kwamba ahadi hii inatekelezwa kwa vitendo? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwa na ahadi ya huyu mwekezaji kuanza uzalishaji wa kubangua korosho katika msimu huu. Tumemwita Wizarani ili atuambie amefikia wapi? Kwa sababu kuna commitment ambayo tumeweka na wananchi wanasubiria kule kuona kwamba uzalishaji wa korosho unaendelea, na pia commitment yake inaheshimiwa. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri kwamba siku chache zilizopita baada ya kuhoji hapa juu ya malipo ya mkandarasi Tunduru Mjini katika mradi wa usambazaji wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 3.4, naomba nikiri kwamba Serikali promptly imetekeleza na imemlipa mkandarasi yule. Kwa hiyo napenda kutambua jitihada hizo na kuipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kufahamu ni lini mradi ule wa usambazaji wa maji Tunduru Mjini utakamilika? Ahsante.
(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ado Shaibu, Mbunge, na kwa hakika Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeshajipambanua na kuhakikisha kwamba maendeleo hayana chama na ndiyo maana tunashuhudia kwamba Mheshimiwa Mbunge kaomba na Serikali imechukua hatua. Maana yake wananchi wa Mheshimiwa Ado Shaibu wanaendelea kushuhudia utekelezaji mzuri kabisa wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha
Mapinduzi ukiwa unatekelezwa na Mheshimiwa Ado Shaibu katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba yeye kama sauti ya wananchi wake tutaendelea kumpatia ushirikiano hasa katika jambo ambalo amelisema la kusogeza huduma zaidi kwenye makazi ya wananchi kupitia usambazaji wa mabomba.
Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo siku ile nilikujibu na Serikali imetenda, hili nalo nakujibu nikiwa nakupatia
matumaini ya kutosha kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kumtua mama ndio kichwani hana mchezo.
Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto hii ya maeneo ya kulimia inayowakabili wananchi wa Malinyi inafanana kabisa na changamoto ambayo inawakabili wananchi wa Vijiji vya Twendembele na Naluwale Wilayani Tunduru ambapo maeneo yao pia yalitwaliwa kutokana na masuala ya uhifadhi; na kwa kuwa viongozi mbalimbali waandamizi wamekuwa wakiwapa ahadi, especially kwa wenzetu wa Twendembele, kwamba maeneo yataongezwa, nini kauli ya Serikali sasa katika kutekeleza ahadi hizi za viongozi ili wananchi wa vijiji hivyo vya Twendembele na Naluwale wapate maeneo ya kulima, kwa sababu pressure ya kuongezeka kwa watu imekuwa kubwa na maeneo ya kulima ni madogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile ndugu yangu Mheshimiwa Ado Shaibu kwa swali lake la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu nimwambie Mheshimiwa Ado, kauli ya Serikali ni kwamba, Serikali inachokiahidi lazima itakitekeleza, na maana yake huwa tunafanya tathmini na kuna vikao ambavyo kila hatua huwa tunavifanya. Tukishamaliza hatua zote za vikao ambavyo tumevifanya, maana yake tutakuja kuwaonyesha wananchi ni eneo gani wanapaswa sasa walilime hususan katika eneo hilo la Twendembele, Tunduru ambako ameliainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwathibitishie tu kwamba ahadi ya Serikali iko palepale na itatekelezwa mara baada ya kumaliza hatua zote za kiutaratibu.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali langu la nyongeza; kwa kuwa, kwenye Mkutano wa Bunge uliopita niliomba Mwongozo wa Kiti cha Spika juu ya hatma ya vituo vya kimkakati. Na kwa sababu, sasa Mheshimiwa Waziri amesema msimamo wa Serikali ni kwamba, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha wanafanya kazi kwa Pamoja, kuhakikisha fedha zinapatikana, ili kuwezesha kumalizika kwa vituo vile vyote vya kimkakati. Ninaomba kwanza niondoe sasa lile ombi langu la mwongozo kwa sababu, nimeupata vizuri kupitia kauli ya Waziri. Nawashukuru kwamba, kwenye kituo chetu nilichokiombea wakati ule, cha Nampungu, kimepelekewa fedha zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu. Mwaka 2010 Mheshimiwa Rais Magufuli, wakati wa kampeni, alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kata ya Namiungo, ambayo ina vijiji saba na ni kata kubwa sana yenye wakazi wengi...
NAIBU SPIKA: Ngoja kwanza Mheshimiwa. Mheshimiwa Ado.
MHE. ADO S. ADO: ...ninauliza swali sasa. Ni lini ahadi hii itatekelezwa?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge samahani. Umesema mwaka gani?
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Naibu Spika, 2015.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ado Shaibu, kwanza kwa kuondoa mwongozo ule ambao alikuwa ameuleta Bungeni. Hii inaonesha ni namna gani Mheshimiwa Ado amekuwa mwenye busara sana kuona kwamba, hakuna haja ya kuendelea kujadili jambo hili kwa sababu, limepata ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kata hii anayoitaja Mheshimiwa Ado ni moja ya kata ambazo zinatakiwa kupelekewa fedha, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pale. Ni kweli tunafahamu kwamba, kata ile ina vijiji saba ambavyo vinategemea kupata huduma, kama tutajenga kituo cha afya pale. Kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Ado, na ninafahamu anafahamu uchapakazi tulionao kwenye Wizara yetu, tutahakikisha tunampelekea kituo hicho cha afya pindi tutakapopata fedha. Ninakushukuru.