MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Msongola – Mbande hadi Chamazi kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dougras Didas Massaburi, Mbunge wa Kivule, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Msongola – Mbande (kilometa 7.4) ni sehemu ya Barabara ya Chanika – Mbagala Rangitatu yenye jumla ya kilometa 29.2 ambapo jumla ya kilometa 25.4 zimejengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, ujenzi wa kilometa 3.8 zilizobaki katika sehemu ya Msongola – Mbande unaendelea ambapo kwa sasa jumla ya kilometa 1.6 zimewekwa tabaka la lami, kilometa 1.1 zipo kwenye tabaka la kokoto (CRR) na kilometa 1.1 zipo kwenye hatua za matabaka ya udongo. Ujenzi wa barabara hii unatarajia ukamilike mwezi Juni, 2026.
MHE. DOUGRAS D. MASSABURI aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa madaraja na Barabara ya Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dougras Didas Massaburi, Mbunge wa Jimbo la Kivule, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kibeberu kwenda Magole ina urefu wa kilometa 2.89 na ni kiungo muhimu kwa wananchi wa Kata ya Mzinga na Kitunda. Katika mwaka wa fedha 2026/2027 barabara hii imejengwa kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 127.13. Serikali imekuwa ikitenga bajeti kuhakikisha Barabara za Kitunda – Nyangasa – Kibeberu hadi Magole zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imejikita katika ujenzi wa Barabara ya Kitunda – Mwangati – Kwa Mpalange ambapo katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kiasi cha shilingi milioni 950 kimetengwa. Ujenzi wa Madaraja na Barabara za Nyangasa – Kibeberu na Magole itawekwa kwenye bajeti baada ya kukamilika kwa Barabara ya Kitunda – Mwangati - Kwa Mpalange. Ahsante.