Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dougras Didas Massaburi (1 total)

MHE. DOUGRAS D. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali ya kaka yangu Mheshimiwa Naibu Waziri. Pia nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii ya TAMISEMI na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kaka yangu Mheshimiwa Chalamila na DC wetu wa Ilala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Mei, niliuliza swali linalohusu Barabara ya Banana – Kitunda mpaka Msongola na hatua za haraka zikachukuliwa. Ninaipongeza Serikali yangu, zaidi ya shilingi bilioni nane zimelipwa na sasa mkandarasi yuko kazini kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami, lakini pamoja na pongezi hizo sasa ninayo heshima kubwa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kivule, niulize maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; tunayo barabara inayotoka Kampala University kupita Majohe mpaka Chuo Rada, kilometa 6.35. Swali la pili, ni barabara inayotoka Njia Nne kupita Buyuni – PSSSF mpaka Taliani, inaunganisha Jimbo la Kivule na Jimbo la zamani la Ukonga; na kwa kuwa Serikali yetu sikivu ilitupatia jimbo hili jipya la Kivule, changamoto kubwa ni miundombinu ya barabara na nyakati hizi za mvua kumekuwa na changamoto kubwa ya kupitika kwa barabara hizo. Basi angalau siku ya leo tupate majibu ya Serikali kwenye maswali yangu mawili ya nyongeza katika Wizara yetu ya TAMISEMI. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Dougras Didas Massaburi, Mbunge wa Jimbo la Kivule kwa uchapakazi wake na kwa kweli anawawakilisha ipasavyo wananchi wa Jimbo la Kivule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napokea pongezi zake kwa Serikali yetu na kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli, kwa hakika Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya barabara na katika Jimbo la Kivule, Mheshimiwa Mbunge ameshuhudia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Barabara ya kutoka Kampala University – Magohe – Rada, kilometa 6.35 na Barabara ya Njia Nne - Buyuni, ni barabara muhimu sana ambayo inaunganisha wananchi wa Taliani – Magohe. Ni barabara ambazo kwanza kwa kutambua umuhimu wake Serikali imeshaziweka kwenye Mpango wa DMDP II, inakwenda kujengwa kwa ile 70%. Hivi sasa wanaendelea na taratibu za manunuzi ili kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara hizi, Serikali imefanya maamuzi na sasa zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa mfano katika mwaka huu wa fedha wakati tunajiandaa na ujenzi wa lami, imekwishatengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya matengenezo madogo madogo. Mwaka wa fedha 2026/2027 imetengwa shilingi milioni 950 kwa ajili ya ujenzi kiwango cha lami kilometa 0.6. Pia imetengwa shilingi milioni 100 kwa ajili ya matengenezo madogo madogo (periodic maintenance), na imetengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi. Barabara hii yote jumla yake ni kilometa 5.26 na zote zitajengwa kiwango cha lami kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Kivule kwamba Serikali iko kazini, itahakikisha barabara hizi zinajengwa na zinapitika vizuri kwa manufaa ya wananchi.