Primary Questions from Hon. Bakari Bakari Shingo (3 total)
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja kukemea vitendo vya kutoza gharama za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inayoelekeza kutoa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum ikiwemo akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 wasio na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatangaza rasmi kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote awamu ya kwanza itakayohusisha makundi ya wananchi ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito, walemavu na wazee wasio na uwezo, ambapo kundi hili litagharamiwa na Serikali. Kukamilika kwa hatua hii kutawezesha wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma za afya kwa kugharamiwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha kuwa wanatekeleza maelekezo ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za afya kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara kwa sehemu ya Mombasa hadi Gongo la Mboto kupitia mradi wa mabasi yaendeayo haraka awamu ya tatu (DRT 3). Aidha, kwa barabara ya inayopita maeneo ya makaburi ya Kiltex, tayari kuna mkandarasi anaendelea kuifanyia matengenezo kwa kuchonga tuta na kuweka tabaka la changarawe ili kuwezesha barabara kupitika majira yote ya mwaka. Kazi za matengenezo zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Barabara ya Pugu – Mnadani – Bangulo hadi Ulongoni B utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Pugu – Mnadani – Bangulo hadi Ulongoni B ina urefu wa jumla ya kilometa 4.36 ambapo imetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.017 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami urefu wa kilometa 1.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa ujenzi huu unafanyika kwa awamu mbili; awamu ya kwanza ni urefu wa kilometa 0.3 kwa gharama ya shilingi milioni 575.526 kupitia chanzo cha mapato ya ndani ya halmashauri na ujenzi wa awamu ya pili una urefu wa kilometa 0.9 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.442 kupitia fedha za jimbo na tozo za mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa awamu ya kwanza umekamilika, kwa sasa mkandarasi anaendelea na Ujenzi wa awamu ya pili, ambapo utekelezaji wake umefikia 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhudumia mtandao wa barabara wa Jimbo la Ukonga kwa kujenga, kufanya ukarabati na Matengenezo kulingana na upatikanaji wa fedha, ninaomba kuwasilisha.