Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Marirta Gido Kivunge (2 total)

MHE. MARIRTA G. KIVUNGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Miradi ya Maji iliyosimama kwenye Halmashauri za Wilaya ya Meru, Longido na Monduli?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa miradi ya maji yote inayoendelea na ile iliyosimama kote nchini, ikiwemo miradi sita inayoendelea katika Halmashauri za Wilaya za Meru, Longido na Monduli. Miongoni mwa miradi inayoendelea katika wilaya hizo ni pamoja na Mradi wa Maji Kikatiti, Samaria; Mradi wa Maji Kata ya Uwiro iliyopo Wilaya ya Meru; Miradi ya Maji Tingatinga na Ketumbeine, Wilaya ya Longido, sambamba na mradi wa maji unaolenga kunufaisha vijiji 13 vya Wilaya ya Monduli.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hiyo yote kwa pamoja inagharimu zaidi ya shilingi bilioni 38.7, ambapo hadi mwezi Machi, 2026 zaidi ya shilingi bilioni 5.8 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji. Mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa kipaumbele cha kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi hiyo kadiri zinavyopatikana, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
MHE. MARIRTA G. KIVUNGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya cha Mfereji ikizingatiwa kuwa, fedha za ujenzi wake zilitengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali alilolileta Mheshimiwa Marirta Gido Kivunge, Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mfereji ina jumla ya wakazi 8,068 na ina vijiji vinne vya Komesha, Emurua, Idonyonado na Mfereji. Vijiji vya Mfereji na Idonyonado vina zahanati zinazotoa huduma. Aidha, Kijiji cha Emurua, ujenzi wa zahanati upo hatua ya ukamilishaji na Kijiji cha Komesha ujenzi upo hatua ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2024/2025 Serikali imetoa shilingi milioni 250, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, Kata ya Sepeko, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Ujenzi umehusisha jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, choo cha nje na kichomea taka. Aidha, ujenzi umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma kuanzia mwezi Julai, 2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wakazi wa Kata ya Mfereji wanapata huduma za rufaa na dharura katika hospitali ya wilaya wakati Serikali ikiendelea kutenga fedha na kujenga vituo vya afya kwenye kata za kimkakati zitakazokidhi vigezo kote nchini, ikiwemo Kata ya Mfereji katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.