MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Tumekuwa na ahadi ya muda mrefu sana ya Uwanja wa Ndege wa Musoma, na sasa tumeambiwa kwamba miezi michache iliyopita kwamba utamalizika.
Je, ni lini uwanja huo sasa utamalizika ili wananchi wa Musoma wapate haki ya kupanda ndege?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Getere kwa kuuliza swali katika wa Uwanja wa Musoma ambao kimsingi wote tunafahamu, kihistoria huo ni Mkoa ambao Baba wa Taifa alikuwa anatokea ni Mkoa wenye madini, ni Mkoa wenye utalii.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua uzito na umuhimu wa uwanja huu ulikwishafanya uamuzi wa kutenga fedha na ujenzi ulishaanza na hivi ninavyozungumza tupo asilimia 58.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wetu wa Mkoa wa Mara kwamba tunaendelea na taratibu za ndani mara tu tutakapokamilisha taratibu za kifedha tutaukamilisha uwanja huo ili uanze kutumika na wananchi kwa sababu imekuwa ni kilio cha muda mrefu.