Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. David Mwakiposa Kihenzile (71 total)

MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza:-

Je, lini Shirika la Ndege Tanzania litaanza safari za Pemba?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia afya njema. Pili, kwa sababu ninasimama kwa mara ya kwanza hapa, nitumie nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi. Kwa unyenyekevu mkubwa nimepokea uteuzi huu na ninaahidi kufanyakazi kwa juhudi, maarifa kwa ajili ya maslahi makubwa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee ninakushukuru wewe kama mlezi na Kiongozi wangu kwa ushirikiano mkubwa ulionipatia nikiwa Msaidizi wako kwa nafasi ya Mwenyeketi wa Bunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Kilimo na Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, ninaomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kujibu swali la Mheshimiwa Salimu Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ATCL itaanza safari za Pemba baada ya kupata ndege za kutosha kuweza kutoa huduma bila kuharibu ratiba za safari za sasa na urukaji kwa wakati. Kwa kuwa mwisho wa Septemba, 2023 ATCL inatarajia kupata ndege mpya moja aina ya Boeing B737-9MAX na ndege ndogo aina ya Dash 8 Q300 matengenezo yake yanatarajiwa kuwa yamekamilika na kurejea katika ratiba zake za utoaji wa huduma. Uwepo wa ndege hizo kutaiwezesha ATCL kuanzisha safari zake katika kituo cha Pemba kwa tija na ufanisi mkubwa.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka Mdaki katika Bandari ya Dar es Salaam kwa meli za abiria na mizigo za Azam Sea Link ili kuondoa usumbufu na kero kwa abiria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TPA imenunua midaki mitatu kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi katika eneo la Azam Link na eneo la kuhifadhi mizigo (Baggage room) ambapo midaki miwili imeshafungwa eneo la kuingia na kutoka katika eneo la kuhifadhi mizigo (Baggage room) na mdaki mmoja utafungwa katika eneo la Azam Link. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitIa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imetenga fedha kwa ajili ya kununua midaki mingine, kwa ajili ya eneo la Lighter Quay na yadi ya magari (RORO Yard), ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya mapitio ya bei ya nauli za Shirika la Ndege Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kawaida nauli za safari za ndege hupangwa na soko kulingana na aina ya huduma inayotolewa. ATCL kama ilivyo kwa mashirika mengine ya ndege yanayotoa huduma zake kibiashara, nauli zake zinapangwa na soko kwa kuzingatia matakwa ya sheria za ushindani ambapo vigezo vinavyotumika katika kupanga nauli hizo ni pamoja na gharama za uendeshaji ili kuhakikisha kuwa mashirika ya ndege yanahimili ushindani wa soko na kujiendesha kwa tija na ufanisi.
MHE. ASYA SHARIF OMAR K.n.y. MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa madarasa na mabweni ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) Mabibo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP), mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, imeanza ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500. Ujenzi wa mabweni hayo umefikia asilimia 28. Aidha, kupitia mradi huo Serikali inajenga jengo lenye Madarasa ya wanafunzi 1,500 pamoja na maabara na karakana yenye kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 30.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Rasilimali Mafunzo (maktaba) chenye madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,653 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo kwa sasa upo kwenye asilimia 85.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Chuo, itaanza ujenzi wa Jengo la Kitaaluma la ghorofa tano litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,700 kwa siku, mara litakapokamilika.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka alama za kuongoza meli katika eneo la kuegesha meli kwenye Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ina mpango wa kujenga miundombinu ya bandari katika Ziwa Nyasa hususani Bandari ya Mbamba Bay. Ujenzi wa bandari hizi utahusisha pia usimikaji wa vifaa vya kuongozea meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TPA ina mpango wa kuweka alama za kuongozea meli katika bandari za maeneo mengine kuanzia mwezi Machi, 2024 kwani kupitia Mradi wa Upanuzi na Maboresho ya Miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Program – DMGP) maboya yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yataondoshwa kwa sababu mradi huo unahusisha pia uwekaji wa maboya mapya katika Bandari ya Dar es Salaam lakini kwa kuwa maboya hayo bado yapo katika matumizi yatasimikwa katika bandari nyingine.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, nini Mkakati wa Serikali wa kuifanya Bandari ya Tanga iwe na ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa Bandari ya Tanga ilikuwa haihudumii meli na shehena ya kutosha kutokana na changamoto ya kasi ndogo ya huduma za meli na shehena hizo ambazo zilipaswa kuhudumiwa nangani umbali wa kilomita 1.7 kutoka gatini. Hali hii ilipunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Bandari ya Tanga na ushindani wa bandari hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali kupitia TPA, inaendelea na maboresho ya bandari hiyo katika maeneo ya miundombinu, mitambo na vifaa ili kuvutia meli na shehena nyingi zaidi kama mkakati mahsusi wa kuifanya bandari hiyo ifanye kazi kwa ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo TPA ina mkakati mahsusi wa kimasoko kwa ajili ya Bandari ya Tanga ambao lengo lake ni kuteka soko la kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DRC. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwashawishi wateja wakubwa kutumia bandari hiyo kwa kutoa punguzo la tozo.
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati na kufufua reli kutoka Kilosa hadi Kidatu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Mbunge wa Kilosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa vipindi tofauti imeendelea kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini. Kuhusu ufufuaji wa reli kutoka Kilosa hadi Kidatu, Serikali kupitia TRC katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya kuanza kazi za awali za marekebisho na ufufuaji wa njia katika kipande hiki chenye urefu wa kilomita 108 ambayo imefungwa kwa muda mrefu zaidi. Reli hii inaunganisha Reli ya Kati na TAZARA eneo la Kidatu. Aidha, kwa sasa TRC imekamilisha tathmini ya kihandisi ikiwemo makadirio ya gharama ya mradi (Engineering estimates) na inaendelea na ukamilishaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumwajiri Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kumuomba Mheshimwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi - Mbunge, pamoja na wananchi wa Kilosa kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na juhudi ya urejeshwaji wa njia hii ambayo ni muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria. Lengo la Serikali ni kuendelea kufanya maboresho katika maeneo yenye mahitaji ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza: -

Je, Mkandarasi wa SGR kipande cha Seke-Malampaka hadi Malya ameajiri wananchi wangapi wanaotoka maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imeendelea kumuelekeza mkandarasi wa ujenzi wa reli ya SGR, kuendelea kutoa ajira kwa wananchi wanaopitiwa na mradi, sambamba na kufuata taratibu na sheria za ajira nchini. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa SGR kipande cha Mwanza - Isaka (kilometa 341), kinachojumuisha kipande cha Seke - Malampaka hadi Malya kama sehemu ya mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ajira; hadi kufikia mwishoni mwezi Agosti 2023, mkandarasi ameajiri jumla ya wananchi 6,793. Kati ya hao, wananchi 1,639 kutoka Mkoa wa Shinyanga, wananchi 1,973 kutoka Mkoa wa Mwanza, wananchi 525 kutoka Mkoa wa Simiyu, wananchi 352 kutoka mkoa wa Tabora na wanachi 2,304 kutoka mikoa mingine.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kumsimamia Mkandarasi kuhakikisha kuwa anaajiri kwa kutoa kipaumbele kwanza kwa wananchi wa maeneo husika kabla ya kutafuta ujuzi stahiki kutoka maeneo mengine.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka alama za kuongoza meli katika eneo la kuegesha meli kwenye Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ina mpango wa kujenga miundombinu ya bandari katika Ziwa Nyasa hususani Bandari ya Mbamba Bay. Ujenzi wa bandari hizi utahusisha pia usimikaji wa vifaa vya kuongozea meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TPA ina mpango wa kuweka alama za kuongozea meli katika bandari za maeneo mengine kuanzia mwezi Machi, 2024 kwani kupitia Mradi wa Upanuzi na Maboresho ya Miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Program – DMGP) maboya yaliyopo Bandari ya Dar es Salaam yataondoshwa kwa sababu mradi huo unahusisha pia uwekaji wa maboya mapya katika Bandari ya Dar es Salaam lakini kwa kuwa maboya hayo bado yapo katika matumizi yatasimikwa katika bandari nyingine.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi 438 Waliofanyiwa uthamini kupisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege Kilwa – Masoko?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilikamilisha zoezi la Uwekaji Wazi Daftari la Fidia (valuation report disclosure) kwa wananchi 438 waliofanyiwa uthamini ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hiyo, mnamo mwezi Agosti, 2023 Wizara ya Fedha ikishirikiana na Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Lindi, walifanya na kukamilisha zoezi la uhakiki wa daftari la fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua hizi, zoezi la ulipaji wa fidia litaanza mara baada ya Wizara ya Fedha kukamilisha taratibu zote za kifedha.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Ghati la Kisasa la Abiria kwenye Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. DAVID M. KIHENZILE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha huduma kwa wananchi wake katika maeneo mbalimbali ya nchi, likiwemo Jiji la Dar es Salaam. Ili kuendeleza juhudi hizo, Serikali kupitia TPA inakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa gati la kisasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambao hadi sasa upo katika hatua za mwisho na unatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Ramadhan Suleimani Ramadhan na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwa kuendelea kufuatilia kero za wananchi katika maeneo yao. Serikali itaendelea kuboresha huduma hizo ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao bila kikwazo chochote.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia ajira ya kudumu vijana ambao wanatumika kama vibarua kwenye ujenzi wa Reli nchini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu inaonyesha kuwa, toka kuanza kwa ujenzi wa mradi wa Standard Gauge mwaka 2017 hadi kufikia Desemba 2023 jumla ya vijana wa Kitanzania 51,153 wameshiriki katika ujenzi wa mradi wa SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998, ajira katika Utumishi wa Umma uzingatia sifa na weledi (merits) na hutolewa kwa ushindani wa wazi. Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa vijana wanaoshiriki katika mradi wa ujenzi wa SGR wanapata ujuzi mahsusi katika teknolojia ya reli ya kisasa ambayo itahitajika katika kuhakikisha uendelevu wa reli tunayoijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumtaarifu Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge, kuwa kwa kuzingatia mahitaji ya uendeshaji wa reli, vijana hawa watapewa kipaumbele kwa kuwa na sifa za ziada (added advantage) zinazohusiana na ujuzi waliopata kwa kushiriki katika ujenzi wa reli pindi ajira hizo zitakapotangazwa.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani kumaliza migogoro kati ya bajaji na daladala katika miji mingi nchini inayotokana na routes kugongana?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajaji ni miongoni mwa vyombo vya kukodi vinavyodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kupitia Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (magari ya kukodi) za mwaka 2020 (TS 78). Daladala ni miongoni mwa vyombo vinavyodhibitiwa na LATRA kupitia Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020 (TS 76).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa vyombo vingine vinavyodhibitiwa chini ya Kanuni za magari ya kukodi, bajaji huwa hazipangiwi njia (route) ya kutoa huduma kama daladala. Badala yake, hupangiwa vituo vya maegesho kwa ajili ya kusubiri abiria ili wakodi na kupelekwa maeneo mbalimbali na kurejea kwenye vituo hivyo kusubiri abiria wengine. Aidha, kanuni ya 15 (h) ya Kanuni za magari ya kukodi inakataza vyombo vinavyodhibitiwa chini ya Kanuni za Magari ya Kukodi, kuingilia huduma za daladala au mabasi ya masafa marefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia LATRA imekuwa ikitoa elimu na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha migogoro hii inakoma. Aidha, kwa sasa LATRA inahimiza madereva wa bajaji na pikipiki kuungana kupitia SACCOS kwa lengo la kuongeza elimu na usimamizi wa kundi hili. Tayari SACCOS inayojulikana kama KIBOBAT SACCOS imesajiliwa mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kufanya majiribio ya mpango huu kuanzia mwezi Februari, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu, napenda kuchukua nafasi hii kuiagiza LATRA kuongeza udhibiti wa vyombo hivi kwa kuharakisha jitihada za kuwaunganisha madereva wa pikipiki na bajaji kupitia SACCOS kwa lengo la kuongeza udhibiti wao. Aidha, niwaombe viongozi wa Serikali kwenye maeneo mbalimbali nchini kuungana na LATRA kuhakikisha bajaji zinatoa huduma kwa mujibu wa sheria ili kuepusha madhara ya kiuchumi na kijamii tunayoyashuhudia sasa.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, Serikali imefikia hatua gani kuwalipa fidia wananchi 438 waliofanyiwa uthamini ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushughulikia na kufuatilia kwa ukaribu suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege, Kilwa Masoko linakamilika. Hatua ya awali ya kutambua wafidiwa na mali zao imekamilika na kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Sambamba na hilo maombi hayo yamewasilishwa Serikalini kwa ajili ya malipo. Hivyo, Serikali itahakikisha kuwa wananchi wote wanaopisha maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja hicho wanalipwa fidia zao stahiki.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, lini Serikali itanunua meli za abiria zitakazorahisisha usafiri kwa wananchi kati ya Pemba, Tanga, Mtwara na Unguja?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) imetenga kiasi cha fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya upembuzi yakinifu ili kujua aina ya meli zitakazojengwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi wa mikoa ya Tanga, Mtwara, Lindi, Pemba na Unguja ambapo zitatoa huduma kwa njia ya maji katika mwambao wa Bahari ya Hindi kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi katika ukanda huo. Matokeo ya utafiti huo ndiyo yatakayobainisha aina na ukubwa wa meli itakayojengwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko Mikoa ya Pemba, Tanga, Mtwara na Unguja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mikakati ya Serikali ya kununua meli kwa ajili kutoa huduma katika mwambao wa Bahari ya Hindi, hata hivyo kutokana na fursa za kibiashara zilizopo katika mikoa ya Tanga, Unguja, Mtwara, Lindi na Pemba, Serikali imeendelea kuhamasisha sekta binafsi kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa kununua meli za biashara ili kuhudumia hilo soko ambapo kutachochea ukuaji wa uchumi katika mikoa hiyo na kuongeza pato la Taifa kwa ujumla.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanza ujenzi wa kipande cha Reli ya TAZARA kutoka Tunduma hadi Bandari ya Kasanga?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha reli ya TAZARA na Bandari ya Kasanga ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika ukanda huo hususani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TAZARA inamilikiwa na Serikali mbili; Tanzania na Zambia, tumeanza mazungumzo na wenzetu Zambia ili kutenga fedha katika bajeti ya TAZARA kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa reli hiyo kwa lengo la kubaini gharama za ujenzi wake na manufaa yake kiuchumi.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kutoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilometa 1,000. Aidha, mradi huu ni mmoja wa mradi unaopendekezwa kupatiwa ufadhili wa fedha za maandalizi ya mradi kupitia Mfuko wa Miradi wa Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC-PPDFA) ambapo kwa sasa timu kutoka Benki ya Afrika Kusini (DBSA) ilikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya uthibitisho wa nyaraka (due diligence) za mradi ili kuendelea na hatua zingine za upatikanaji wa ufadhili wa fedha zitakazotumika kumnunua mshauri elekezi atakayekuwa na jukumu la kupitia andiko, kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza: -

Je, lini mgogoro kati ya wananchi wa Kiwanja cha Ndege Mwanza na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege – Mwanza utatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali Kuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa ina nia ya dhati na imeendelea na jitihada mbalimbali katika kushughulikia mgogoro huu ili kuhakikisha unaisha. Aidha, taratibu za utwaaji ardhi zinaendelea kwa kufanya uthamini wa mali za wananchi, pindi uthamini utakapokamilika taratibu nyingine zitaendelea kulingana na Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Uthamini.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua usafiri wa Reli kutoka Dodoma kwenda Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) ina mpango wa ufufuaji na ukarabati wa miundombinu ya Reli ya Kati yenye kiwango cha Meter Gauge. Aidha, TRC inaendelea na ukarabati na uboreshaji wa Njia Kuu kutoka Dar es Salaam - Isaka ambapo kwa awamu ya kwanza uboreshaji umefanyika kutoka Dar es Salaam hadi Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa awamu ya pili, Serikali ina mpango wa kuboresha kipande cha Tabora – Isaka ikiwemo kukarabati kipande cha Dodoma – Manyoni kwa maeneo yaliyobaki wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza. Vilevile, Serikali inafanya tathmini ya ukarabati wa njia ya reli ya Manyoni – Singida ili kuimarisha shughuli za kiuchumi kupitia usafiri wa reli kwa kuunganisha ukanda huo.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Bandari Kavu utaanza katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na taratibu za utwaaji ardhi katika eneo lililotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduma la takribani ekari 1,600 kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu. Aidha, taratibu za utwaaji ardhi zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na pindi zitakapokamilika, taratibu za ulipaji fidia unatarajia kufanyika katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, ujenzi wa bandari kavu utaanza baada ya kufanya usanifu wa miundombinu ya bandari pamoja na taratibu za ununuzi wa mkandarasi atakayetekeleza ujenzi huo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA K.n.y. MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza:-

Je, lini mgogoro kati ya wananchi wa Kiwanja cha Ndege Mwanza na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege - Mwanza utatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Angeline Sylvester Mabula, Mbunge wa Ilemela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali Kuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa ina nia ya dhati na imeendelea na jitihada mbalimbali katika kushughulikia mgogoro huu ili kuhakikisha unaisha. Aidha, taratibu za utwaaji ardhi zinaendelea kwa kufanya uthamini wa mali za wananchi. Pindi uthamini utakapokamilika, taratibu nyingine zitaendelea kulingana na Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Uthamini.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-

Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushughulikia na kufuatilia kwa ukaribu suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea. Hatua ya awali ya kutambua wafidiwa na mali zao imekamilika na kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Aidha, maombi hayo yamewasilishwa Serikalini kwa ajili ya malipo. Pia Serikali itahakikisha kuwa wananchi wote wanaopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa miradi mbalimbali wanalipwa fidia zao stahiki.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA auliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mabasi yanayokwepa kuingia stendi na kushusha abiria barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabasi yote ya masafa marefu hupangiwa ratiba na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambazo huonyesha stendi za kupakia na kushushia abiria pamoja na muda wa kusimama kwenye stendi hizo. Aidha, mabasi ya masafa marefu yamepangiwa kusimama katika stendi moja tu kwa kila Mkoa isipokuwa pale ambapo basi hilo lina abiria anayeshuka katika stendi ya wilaya. Utaratibu huo umepangwa ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji wa abiria wa masafa marefu kwa kuwalazimisha kuingia kwenye stendi hata kama hawana abiria wa kupanda au kushuka. Hivyo Basi hailazimiki kuingia katika stendi ya Wilaya iwapo hakuna abiria wanaoshuka au kupanda basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa madereva wanaokaidi kuingia stendi za mikoa na kushushia abiria nje ya stendi hususan barabarani, madereva hao wanakiuka maelekezo ya kifungu cha 50(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 kinachomzuia mtu yeyote kuegesha au kusimamisha gari barabarani bila kujali watumiaji wengine wa barabara, hivyo wanavunja sheria.
MHE. KILUMBE S. NG`ENDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ukarabati wa Reli ya Kati kwa kuwa miundombinu yake ni chakavu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TRC inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya njia ya reli iliyopo ambapo hadi sasa imekamilisha ukarabati wa njia ya reli kipande cha Dar es Salaam – Isaka ya Kilometa 970 kupitia mradi wa Tanzania Intermodal Rail Project (TIRP). Halikadhalika, TRC imesaini mkataba wa ukarabati wa njia ya reli ya kati kwa kipande cha Tabora – Kigoma yenye urefu ya kilometa 411 tarehe 23 Juni, 2023 na Kaliua – Mpanda ya kilometa 210 tarehe 26 Novemba, 2022. Kazi ya ukarabati inaendelea, na kwa upande wa Tabora – Kigoma ya kilometa 411 inatarajia kukamilika baada ya miezi 54 na Kaliua – Mpanda inatarajia kukamilika mwezi Mei, 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo TRC imesaini mkataba wa ununuzi wa malighafi za ukarabati wa reli (mataruma na vifungio) kwa ajili ya ukarabati wa njia ya reli ya Kaskazini ikijumuisha kipande cha Ruvu – Mruazi Junction.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga upya Uwanja wa Ndege wa Newala ambao umeharibika kwa kiasi kikubwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Newala ipo katika hatua za kufanya tathmini ya uchaguzi wa eneo jipya kufuatia eneo la sasa kutofaa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege. Baada ya kukamilika kwa tathmini ya eneo hilo ambalo tayari limeshajumuishwa kwenye Ramani ya Mipango Miji Na.03/NEW/31/04/2021, taratibu za utwaaji na umilikishwaji wa ardhi zitafanyika. Taratibu za utwaaji na ukamilishaji zitakapokamilika, fedha za ujenzi wa kiwanja cha ndege zitatengwa kwa ajili ya bajeti husika.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi 447 wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi 447 wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko. Taratibu za maandalizi ya malipo haya zinaendelea na pindi zitakapokamilika malipo haya yataanza kulipwa mara moja.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kushughulikia huduma za abiria wenye mahitaji maalum na wagonjwa kwenye viwanja vya ndege?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa inaweka miundombinu na vifaa wezeshi ili kuhakikisha huduma kwa abiria wenye mahitaji maalum na wagonjwa wanapata huduma stahiki katika viwanja vya ndege. Hii ni pamoja na kusanifu na kujenga majengo ya abiria sambasamba na miundombinu wezeshi kama vile maliwato maalum (disabled toilet), ngazi za mjongeo (ramp), usimikaji wa ngazi za umeme (lift escalators) na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na vifaa maalum vya kuwahudumia abiria wenye mahitaji maalum pamoja na wagonjwa katika viwanja vya ndege kama vile viti vya magurudumu (wheelchair); pia, katika kuhakikisha uwepo wa watoa huduma wanaowahudumia watu wenye mahitaji maalum na wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na wagonjwa katika foleni za ukaguzi wa abiria (screening) na foleni za kuingia ndani ya ndege (boarding) kuufanya usafiri wa anga kuwa rafiki kwao.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mpanda Mjini kwenda Bandari ya Karema, Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam – Mwanza kilometa 1,219 kwa awamu ya kwanza na kutoka Tabora – Kigoma kilometa 506 na Uvinza Musongati kilometa 282 kwa awamu ya pili. Ujenzi huu uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo kipande cha Dar es Salaam – Dodoma kilometa 444 kimeanza uendeshaji kwa safari za abiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaendelea na maandalizi ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Kaliua – Mpanda – Bandari ya Karema ambapo upembuzi yakinifu umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kaliua – Mpanda – Karema yenye urefu wa kilometa 321 kwa kiwango cha standard gauge (SGR). Reli hii inatarajiwa kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Bandari ya Karema kwa upande wa Tanzania na Bandari ya Kalemie kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ujenzi huo utaanza mara baada ya kupatikana kwa rasilimali fedha.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege uliopo Wilaya ya Kahama ili uwe na hadhi ya kutua ndege kubwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, Benki ya Uwekezaji ya Watu wa Ulaya imeendelea na ukarabati pamoja na upanuzi wa miundombinu yote katika Kiwanja cha Ndege Shinyanga ili kiwanja hicho kiweze kutumika wakati wa usiku na mchana. Utekelezaji umefikia 66.8%. Pia Serikali kwa kushirikiana na kampuni binafsi iliyokuwa ikichimba madini Mjini Kahama, imefanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa kujenga jengo jipya ya abiria na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu mingine ili kuendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa, Serikali itakamilisha kwanza Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga na endapo mahitaji ya mkoa yataongezeka, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka taa Uwanja wa Ndege wa Mafia ili kuwezesha ndege kubwa kupeleka watalii kutembelea Kisiwa cha Mafia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025, Serikali ina mpango wa kufunga taa za kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Mafia kwa ajili ya kuwezesha kutolewa kwa huduma za masaa 24 ambapo kutachangamsha uchumi wa Mafia na kukuza utalii nchini.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itahakikisha usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia Meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria ni suala la muda wote na ni kipaumbele namba moja kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) inahakikisha usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia vyombo vyote vya majini, ikiwemo meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria kwa kukagua meli hizo mara kwa mara na kuzipatia vyeti vya ubora, ambapo kwa cheti hicho inamaanisha meli imekidhi vigezo vya usalama kwa abiria na mali zao, ulinzi na utunzaji wa mazingira majini. Aidha, meli zote ikiwemo MV Victoria zinasisitizwa kuwa na vifaa vya uokozi ambapo abiria melini hutangaziwa uwepo wa vifaa hivyo na jinsi ya kuvitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, TASAC inaendelea na mikutano ya uelewa na kufanya kaguzi za kushtukiza kwa meli na kuhakikisha manahodha na wafanyakazi wengine wote wamepata mafunzo ya umahiri na kuwa na vyeti hai vinavyotolewa na TASAC.
MHE. AGNES E. HOKORORO K.n.y. MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga bandari kavu Nang’omba Wilayani Nanyumbu ili kuhudumia mizigo ya nchi ya Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa Bandari Kavu limepewa kipaumbele katika Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) uliohuishwa wa mwaka (2021 – 2045) ambao umeweka vigezo vya ujenzi wa bandari zote kavu kwa vipaumbele kutokana na matarajio ya ukuaji wa shehena katika maeneo yanayopakana na nchi za jirani. Aidha, utafiti ulifanyika katika Bandari Kavu ya Nang’omba katika Wilaya ya Nanyumbu na kubaini kuwa bandari hiyo haijakidhi vigezo vya ujenzi wa bandari kavu vilivyotajwa hapo awali na hivyo kutobainishwa katika mpango wa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, Serikali inachukua wazo la Mheshimiwa Mbunge ili kulifanyia kazi kwa siku zijazo baada ya kufanya utafiti wa ukuaji wa shehena ambao ni moja kati ya vigezo vya kujenga bandari kavu.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kujenga reli ya mwendokasi ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli ya Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye kilometa 1000. Aidha kwa sasa Serikali inaendelea na utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kiasi cha shilingi 702,625,000 kimetegwa kwa ajili ya kumwajiri mshauri elekezi (transaction advisor) atakayekuwa na jukumu la kuandaa andiko, makabrasha ya zabuni na kutusaidia kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumuomba Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, pamoja na wananchi wa Mtwara, Ruvuma na Lindi na Mikoa ya Kusini na Watanzania kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya kuanza ujenzi wa njia hii kwa kiwango cha Standard Gauge.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kutoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilometa 1,000. Aidha, mradi huu ni mmoja wa mradi unaopendekezwa kupatiwa ufadhili wa fedha za maandalizi ya mradi kupitia Mfuko wa Miradi wa Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC-PPDFA) ambapo kwa sasa timu kutoka Benki ya Afrika Kusini (DBSA) ilikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya uthibitisho wa nyaraka (due diligence) za mradi ili kuendelea na hatua zingine za upatikanaji wa ufadhili wa fedha zitakazotumika kumnunua mshauri elekezi atakayekuwa na jukumu la kupitia andiko, kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupunguza vifo vinavyotokana na mabadiliko ya hali ya hewa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuwezesha miundombinu ya ukusanyaji, uchakataji na ufungashaji wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini. TMA imeendelea kufanya usambazaji wa taarifa hizo za hali ya hewa kwa umma kupitia vyombo vya habari mbalimbali na kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutatua changamoto ya msongamano wa abiria na mizigo Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPA inafanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kufanya maboresho ya ujenzi wa miundombinu ya kuhudumia abiria na shehena za mwambao pamoja na meli za utalii zikiwemo zile ziendazo Zanzibar. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali inategemea kukamilika mwezi Mei, 2024. Kazi hizi zinafanyika ili kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya msongamano wa abiria na mizigo.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendeleza miundombinu hiyo kwa ubia na sekta binafsi ili kuikamilisha kwa wakati na viwango vyenye ubora wa usalama ambapo kutapunguza gharama kwa Serikali. Kukamilika kwa miundombinu ya kuhudumia meli na mizigo na abiria kutakuwa ni suluhisho la kudumu ambapo kutavutia meli nyingi za utalii kutumia Bandari ya Dar es Salaam.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza: -

Je, lini Halmashauri ya Wilaya ya Maswa itapewa CSR inayotokana na uwepo wa Mradi wa SGR?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mikataba ya ujenzi inayoingiwa kati ya TRC na mkandarasi imeendelea kuzingatia suala la uwajibikaji kwa jamii yaani Corporate Social Responsibility (CSR) kwa kutenga fedha. Aidha, Mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR umeendelea kutoa CSR katika maeneo ambapo mradi unapita na mpaka sasa mradi umefadhili miradi mbalimbali yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 9.5. Kwa upande wa Wilaya ya Maswa, kwa kuanzia Mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR kwa kipande cha Isaka-Mwanza umeshatoa CSR yenye thamani ya shilingi milioni 28.4 ambazo kwa kuanzia zimeelekezwa kwenye mradi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari ya Wasichana Mataba, Mwasalage na ujenzi wa Shule ya Sekondari Mashimba.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN K.n.y. MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza:-

Je, ni kiasi gani Serikali inahakikisha vyombo vya usafiri majini vinatimiza takwa la kuwa na vifaa vya uokozi kwa abiria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TASAC inachukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha vyombo vya usafiri majini vinatimiza takwa la kuwa na vifaa vya uokozi kwa abiria. Hatua hizo ni kama ifuatavyo:-

(i) Ukaguzi wa vyombo vyote vya usafiri majini na utoaji wa vyeti vya ubora. Ukaguzi huu unahakikisha vyombo vina vifaa vya uokozi kama maboya ya kujiokoa kwa abiria wote;

(ii) Kutoa elimu kwa jamii na kampeni maalum kwa jamii zinazoishi maeneo yanayozungukwa na maji. Lengo ni kuwafundisha wamiliki wa vyombo na abiria umuhimu wa vifaa vya uokozi na taratibu za usalama; na

(iii) Kampeni za usalama wakati wa sikukuu ili kuhakikisha havizidishi idadi ya abiria iliyoainishwa kwenye vyeti vyao. Vyombo vinavyoshindwa kufuata sheria hupigwa faini hadi shilingi milioni 6.25 kwa vyombo vikubwa (zaidi ya mita 24) na shilingi laki nne kwa vyombo vidogo (chini ya mita 24).

Mheshimiwa Spika, vilevile Tanzania kupitia TASAC inatekeleza mikataba ya Shirika la Bahari Duniani yaani International Maritime Organization (IMO) kama SOLAS (Safety of Life at Sea Convention). Mkataba huo wa lazima kwa nchi mwanachama pamoja na mambo mengine unalazimisha vyombo vya usafiri majini kuwa na vifaa vya uokozi ambavyo vinakidhi viwango vya kimataifa.
Kukarabati Meli Zilizopo Ziwa Tanganyika

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati meli katika Ziwa Tangayika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeanza ukarabati wa meli zilizopo Ziwa Tanganyika. Taarifa za ukarabati huo ni kama ifuatavyo:-

(i) Ukarabati wa meli ya MV Liemba; mradi huu ulianza rasmi tarehe 13 Julai, 2024 baada ya mkandarasi kulipwa malipo ya awali kiasi cha dola za Kimarekani 1,890,405.31. Mradi huo unaogharimu kiasi cha dola za Kimarekani 13,192,850.00 na unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi 24 kwa mujibu wa mkataba husika hivyo utakamilika tarehe 13 Julai, 2026.

(ii) Ukarabati wa meli ya MV Mwongozo; mchakato wa kumpata mkandarasi wa kuikarabati meli ya MV Mwongozo uko katika hatua za mwisho ambapo tayari mkandarasi M/S Songoro Marine ameshapatikana na kwa sasa taratibu za kuandaa mkataba zinaendelea. Mradi huo ambao utagharimu dola za Kimarekani 4,000,000 umepangwa kutekelezwa ndani ya miezi sita .

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa meli ya MT Sangara; mradi huu sasa umefikia 98% na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2025. Mradi huo umegharimu dola za Kimarekani 3,606,595.00.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa utaanza Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Njombe ni muhimu kimkakati hususan kwenye kukuza uchukuzi katika usafiri wa anga kijamii, kiuchumi na kibiashara ikiwemo biashara ya mazao ya misitu, mbogamboga, matunda (maparachichi) ambayo yote hayo huzalishwa na kusafirishwa nje ya nchi. Aidha, kufuatia uboreshwaji wa Shirika la Ndege la ATCL uliopelekea manunuzi ya ndege kubwa ya mizigo aina ya Boeing 767-300 F, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kushirikiana na Mkoa wa Njombe imekamilisha uchambuzi wa eneo jipya la TANWAT kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege na sasa Serikali inaendelea na taratibu za utwaaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali imeidhinisha taarifa za awali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo kiasi cha shilingi milioni 804 zimetengwa kwa mwaka 2024/2025 huku Mtaalamu Elekezi akiendelea na utayarishaji wa rasimu ya mwisho ya nyaraka zitakazotumika kwa ajili ya ununuzi ya mkandarasi atakayetekeleza mkataba wa ujenzi. Mara baada ya kazi hii kukamilika, ujenzi utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa mwaka 2025/2026 Serikali inatarajia kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya Kiwanja hicho.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha za ujenzi wa kilometa chache za Barabara ya Lupiro, Malinyi, Kilosa kwa Mpepo na Namtumbo ambayo ni ya Ilani ya CCM?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga kwa sehemu ya Ifakara – Lupiro – Mtimbira yenye urefu wa kilometa 112 ikiwa ni sehemu ya barabara kutoka Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo hadi Lumecha Mkoa wa Ruvuma ambapo hiyo barabara yote kwa ujumla wake ina kilometa 435.8 kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA aliuliza:-

Je, lini ATCL itaanzisha usafiri wa Ndege kutoka Dodoma – Mwanza - Mbeya na Arusha ili kupunguza gharama kwa wasafiri wanaokwenda mikoa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ATCL inaendelea kupanua mtandao wa safari kwa kuzingatia mpango mkakati wake na mahitaji ya soko. Kwa sasa, ATCL inahudumia vituo 26 kutokea Dar es Salaam vikiwemo vituo 14 vya ndani ya nchi. Safari za Dodoma – Mwanza zinatarajiwa kuanza Desemba 2025, huku tathmini ikiendelea kwa safari za Dodoma – Mbeya na Dodoma – Arusha.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kusafisha na kuweka uzio Uwanja wa Ndege Urambo kwa kuwa ni muhimu kwa Biashara ya Tumbaku na ni Uwanja wa dharura?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na pendekezo la ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama katika Kiwanja cha Ndege Urambo na tayari suala hili limejumuishwa katika Rasimu ya Mpangomkakati wa TAA wa miaka mitano ijayo ili kutoa wigo wa matumizi ya rasimalifedha inayotengwa katika bajeti ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya ukarabati na upanuzi wa viwanja vya Ndege ikiwemo Ujenzi wa Jengo Jipya la Abiria katika Kiwanja cha ndege cha Tabora ambalo ujenzi wake umefikia 94.1%.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uhakikishaji wa Kiwanja cha Ndege cha Urambo kipo salama, TAA inaendelea na utekelezaji wa maagizo ya kitaifa kuhusiana na ulinzi na usalama, ikiwemo na ushirikishwaji wa wananchi ili kulinda mipaka kupitia uhamasishaji wa ulinzi shirikishi. Hali kadhalika, kiwanja hiki kina hati miliki ili kuepuka uvamizi wa ardhi unaoweza kufanyika kutokana na idadi ndogo ya shughuli za kiuendeshaji zinazofanyika kiwanjani hapo.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO K.n.y. MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali kuendeleza Bandari ya Kyamkwikwi na kujenga barabara ya kuunganisha Bandari na Barabara Kuu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPA imekamilisha kazi ya kuhuisha Mpango Kabambe wa Mwaka 2021 - 2045 wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Bandari Nchini.

Mheshimiwa Spika, Mpango huo umeainisha mahitaji ya uendelezaji wa Bandari nchini ikiwa ni pamoja na Bandari ya Kyamkwikwi katika Ziwa Victoria. Mpango Kabambe huo unatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano mitano ambapo kwa sasa TPA imeanza na ujenzi wa Gati la kuhudumia shehena na abiria katika maeneo hayo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege Omukajunguti utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto za usalama wa Ndege na abiria katika Mkoa wa Kagera, Serikali imeanza utekelezaji wa mpango wa kudumu unaohusisha mjenzi wa kiwanja kipya kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa ambapo mnamo mwezi Januari, 2025, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi iliteua timu ya wataalam kwa lengo la kufanya tathmini ya uchaguzi wa eneo la ujenzi wa kiwanja kipya kikubwa cha Ndege ya Daraja 4C ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za abiria zinazoweza kubeba hadi abiria 220 kwa wakati mmoja. Pamoja na majukumu mengine, lengo la Kamati hiyo lilikuwa ni kufanya tathmini na kushauri eneo linalofaa kwa ujenzi wa kiwanja hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya eneo pendekezwa ambalo ni eneo la Kihabajwa lililopo eneo la Wilaya ya Misenyi imeridhiwa na Serikali na kwa sasa inaendelea na taratibu za utoaji ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya, tayari imeanza kushauriana na Serikali ya Mkoa, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Baada ya zoezi la utoaji ardhi kukamilika taratibu za ujenzi zitaanza mara moja. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, lini Bandari ya Kwala itaanza kutumika kwa uhakika Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala. Miradi mbalimbali imetekelezwa na kukamilika ikiwemo ujenzi wa reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka eneo la Kwala hadi Barabara Kuu ya Morogoro, ujenzi wa uzio wa eneo lenye ukubwa wa hekta 60, ambapo kati ya hizo hekta tano zimewekwa sakafu ngumu (pavements), kwa ajili ya kuweza kupokea makasha 3,500 kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi wa Bandari Kavu ya Kwala, kumeiwezesha bandari hii kuanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Agosti 2023, ambapo hadi mwezi Disemba, 2024 jumla ya makasha 684 yamepokelewa. Kati ya hayo, makasha 406 yamekwishakabidhiwa kwa wateja.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini mnara wa mawasiliano wa kuongozea ndege utajengwa katika Uwanja wa Ndege Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili Kiwanja cha Ndege kiwe na mnara wa kuongozea ndege kinahitaji kukidhi matakwa makubwa manne ambayo ni kuwa na ndege za ratiba maalum, kuwa na idadi kubwa ya miruko na mituo ya ndege, kuwa katika eneo lenye hali mbaya ya hewa hasa ambayo inaleta uono hafifu kwa rubani na sababu nyingine za msingi kama itakavyoonekana inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa Kiwanja cha Ndege Mpanda hakijaweza kukidhi matakwa yaliyoainishwa na hivyo huduma za kuongoza ndege zinazotua katika kiwanja hicho hutolewa kutokea mnara uliopo katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora kama ilivyokasimiwa na kituo kikuu cha kuongozea ndege kilichopo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je, lini ahadi ya ujenzi wa Reli ya Kusini itaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa Njia ya Reli ya Mtwara - Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye urefu wa kilomita 1,000. Kwa sasa, Serikali inaendelea na taratibu za kutafuta mwekezaji atakayejenga reli hiyo kwa kiwango cha Standard Gauge (SGR) kwa utaratibu wa Ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya kuanza ujenzi wa reli hiyo.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali iliamua kujenga bandari Karema wakati upande wa DRC bado hawajajenga?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilisaini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha miundombinu ikiwemo bandari ili kuchochea shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutimiza azma hiyo, Serikali kupitia TPA ilianza maboresho ya Bandari za Kigoma pamoja na ujenzi wa Bandari mpya ya Karema katika Ziwa Tanganyika. Kwa sasa TPA inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kuendeleza Bandari za Moba na kwa upande wa Kalemie ujenzi umeanza kwa kushirikiana na mwekezaji. (Makofi)
MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga uzio wa umeme kwenye Reli ya SGR kutoka Ngerengere hadi Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi wa uzio katika mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha Morogoro hadi Dodoma. Hivi sasa, ujenzi wa uzio huo umefikia 95.12%. TRC inaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-

Je, lini Uwanja wa Ndege Mafia utaboreshwa ili ndege kubwa ziweze kutua?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kutokana na umuhimu wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia katika kuhudumia watalii na wananchi kwa ujumla kiwanja hiki kina barabara nzuri ya kuruka na kutua, barabara ya kiungio na eneo la maegesho kwa kiwango cha lami. Miundombinu hiyo inawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba takribani abiria 50 kwa wakati mmoja kama ATR 42 na fokker 50 kutumia kiwanja hiki kwa ufanisi majira yote ya mwaka (kiangazi na masika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 Serikali imepanga kusimika mfumo wa taa za kuongozea ndege ili kuwezesha ndege kutua na kuruka nyakati za usiku. Mipango ya Serikali kwa miaka ya fedha ijayo ni kurefusha barabara ya kuruka na kutua pamoja na kujenga jengo jipya la abiria.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha Meli katika Vijiji vya Nsele na Lifuma ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari 2023, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilikamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kuendeleleza Bandari za Mbamba Bay, Itungi, Kiwira, Ndumbi, Manda, Matema, Liuli and Lupingu. TPA ilianza utekelezaji wa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi ambayo imekamilika. Kwa sasa TPA inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa Bandari zingine katika Ziwa Nyasa vikiwemo Vijiji vya Nsele na Lifuma utaendelea kufanyika kadri rasilimali fedha itakavyopatikana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini Taa za kuongozea Ndege zitafungwa katika Uwanja wa Ndege Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu gharama za usimikaji na uendeshaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege ni kubwa na hivyo Serikali imekuwa ikitekeleza miradi hiyo katika Viwanja vya ndege vyenye miruko na mituo mingi ambayo inapelekea hitaji la mashirika ya ndege kuja nyakati za usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Mpanda kina miundombinu ya barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio na eneo la maegesho katika kiwango cha lami na jengo jipya la kisasa la abiria na idadi ya ndege zinazotumia Kiwanja cha Ndege cha Mpanda kwa ratiba maalum ni kutoka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) pekee ambayo inakuja na mara tatu kwa wiki Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, serikali inatoa wito kwa wadau mbalimbali ikiwemo mashirika ya ndege yaweze kuanzisha safari za ratiba maalum katika kiwanja hiki na Shirika la Ndege la ATCL kuongeza idadi ya miruko na mituo ili kuwezesha Serikali kusimika mfumo wa taa za kuongozea ndege.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -

Je, lini Uwanja wa Ndege Urambo utawekwa uzio ili kuimarisha usalama?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na pendekezo la ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama katika Kiwanja cha Ndege Urambo na tayari suala hili limejumuishwa katika rasimu ya Mpango Mkakati wa TAA wa miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mpango huo, TAA inaendelea na utekelezaji wa maagizo ya Kitaifa kuhusiana na ulinzi na usalama, ikiwemo ushirikishwaji wa wananchi kulinda mipaka kupitia uhamasishaji wa ulinzi shirikishi.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, kwa nini Kampuni za CCECC na YAPI MARKEZI zinazojenga SGR Bukene zinatoa ajira zisizohitaji ujuzi kwa Vijana wanaotoka nje ya Bukene? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) inaendela na ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza (Km 1,219), Tabora – Kigoma (Km 506) na Uvinza – Msongati (Km 282) ambao ni chachu katika uchumi wa Taifa. Utekelezaji wa mradi huu umetoa fursa za ajira kwa wenye ujuzi (skilled) na wasio na ujuzi (unskilled).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajira za wasio na ujuzi, mradi huu umetoa kipaumbele kwa wazawa katika maeneo ambayo yamepitiwa na mradi kwa kupewa ajira hizo kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi (local content).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumtoa hofu Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene kuwa Serikali imekuwa ikizingatia ajira kwa wazawa ambao wamepitiwa na mradi katika maeneo yote ikiwemo Bukene.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi hususan Wafugaji wanaolisha mifugo maeneo ya hifadhi ya reli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeandaa mpango maalum wa kuhakikisha masuala ya mazingira na jamii yanatekelezwa kwa kuzingatia sheria za Kitaifa na Kimataifa. Aidha, TRC imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafugaji kupitia mpango maalum wa ushirikishwaji wa wadau yaani “Stakeholders Engagement Plan”.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu hii inatolewa katika shughuli za mradi za kila siku na kupitia kampeni maalum zinazofanyika kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo usalama wa miundombinu ya reli kwa wadau.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ulinzi ni jukumu la kila mwananchi. Hivyo naomba kutumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuungana Serikali na TRC katika kutoa elimu ya usalama wa miundombinu ikiwemo ya reli kwa wananchi wa maeneo yao.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, mafunzo gani yanatolewa na Serikali kwa Wanawake kuhusu usimamizi wa biashara za uchukuzi na mbinu bora za usafirishaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara mbalimbali na taasisi zake imeendelea kutoa mafunzo kwa wanawake wajasiliamali kuhusu biashara za uchukuzi na mbinu bora za usafirishaji. Mafunzo haya yanatolewa kwa lengo la kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta ya uchukuzi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya ujasiliamali yameendelea kutolewa kupitia taasisi zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Small Industries and Development Organization (SIDO), Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) na National Economic Empowerment Council (NEEC, ambapo wanawake hupewa elimu ya namna ya kuanzisha, kuendesha, kukuza biashara za uchukuzi kama usafirishaji wa abiria, mizigo na usambazaji wa bidhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mafunzo haya ya udereva wa magari ya biashara yameendelea kutolewa kupitia taasisi zifuatazo: National Institute of Transport (NIT) na Vocational Education and Training Authority (VETA) ambapo wanawake wameendelea kufundishwa kuendesha magari makubwa (mabasi, malori, magari ya abiria, magari ya mizigo) pamoja na usalama barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, hivi karibuni LATRA kupitia Vyuo vya NIT na CBE, wameanzisha mafunzo ya wahudumu wa mabasi ambao wengi wao ni wanawake. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga reli ya kisasa kutoka Kituo Kikuu cha SGR Dodoma hadi Uwanja wa Ndege Msalato?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa katika Jiji la Dodoma (Dodoma Commuter Train). Ujenzi wa Reli hiyo unalenga kuimarisha usafiri katika Jiji la Dodoma kwa kuunganisha Jiji na viunga vyake ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali ipo katika hatua za utafutaji wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli hiyo.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza: -

Je, kwa nini Shirika la Ndege la Tanzania lisianzishe safari za ndege za moja kwa moja toka Zanzibar mpaka Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba nisimame na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kwa nafasi ya Naibu Waziri wa Uchukuzi. Ahadi yangu kwake ni kuendelea kufanya kazi hii kwa uaminifu, uzalendo na uadilifu mkubwa huku nikiwaahidi Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa hili ni Bunge letu ni la kwanza tangu nchi yetu ifanye tukio kubwa la kihistoria kule Mwanza, ninatumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuzindua rasmi meli ya MV Mwanza, meli kubwa ya kwanza katika nchi yetu ambayo inabeba abiria 1,200, tani 400 na magari makubwa na madogo ya kutosha, itakayokuwa inaunganisha nchi yetu pamoja na nchi jirani. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuzindua meli hii kubwa kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ndege Tanzania kwa sasa inafanya safari za ndege kutoka Zanzibar mpaka Dodoma kupitia Dar es Salaam. Uamuzi wa kupitia Dar es Salaam ni wa kibiashara ili kuhakikisha ndege inakuwa na ujazo wa kutosha. ATCL inaendelea kuangalia fursa ya kuanzisha safari za Zanzibar na Dodoma punde idadi ya abiria itapoongezeka na kuwezesha ndege kuwa na ujazo wa kutosha angalau wa 80%.
MHE. NAPE M. NNAUYE aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuanza upembuzi wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kusini kufuatia maandalizi ya Mradi wa LNG?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TRC imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya standard gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilometa 1,000. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea na utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kutumia utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Kwa upande wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara, Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Mpango Kabambe wa East African Railway Master Plan imetambua umuhimu wa kipande hiki cha reli kitakachounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Mtwara kutokana na umuhimu wake kiuchumi, kijamii na utengamano wa Kikanda. Hata hivyo, kwa sasa reli hiyo bado haijawekwa katika mipango ya Serikali kwa kutumia fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kufafanua kuwa, kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR na miradi mbalimbali ya kimkakati nchini; na miradi hiyo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo inatekelezwa kwa awamu kutokana na uhitaji wa fedha nyingi kwa wakati mmoja. Hivyo, nitoe rai kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi na kampuni za fedha kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya reli ikiwemo reli ya kusini kwa kuanza na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli hiyo.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mwanza utakamilika ili uwe na hadhi ya Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa kufanya maboresho makubwa ya Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ili kuwa cha kimataifa umeanza. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaohusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, upanuzi wa eneo la maegesho ya ndege na ujenzi wa barabara za kiungio unaendelea.

Mheshimiwa Spika, ujenzi utaanza mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza gati katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuhudumia meli nyingi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Vitu Maalum Vijana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia utekelezaji wa Mradi wa DMGP (Dar es Salaam Maritime Gate Project) katika Bandari ya Dar es Salaam unaoendelea ambao umehusisha uboreshaji wa gati nane kuanzia gati namba sifuri hadi gati namba saba, ikiwa ni pamoja na uongezaji wa kina cha lango la kuingilia meli (Entrance Channel) hadi kufikia meta 14.5 na lango la kugeuzia meli (Turning Basin), mradi huu umechangia kuongeza ufanisi na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi kuliko hapo awali na hivyo kuongeza idadi ya meli na kiasi cha shehena inayohudumiwa na Bandari hiyo kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaratibu mpango wa ujenzi wa gati mpya zipatazo 10 ili kuhudumia meli nyingi zaidi kwa wakati mmoja.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha wanawake wanashiriki katika miradi mikubwa ya uchukuzi, ikiwemo Mradi wa SGR?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka sera, sheria na miongozo mbalimbali inayolenga kuhimiza na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika ajira. Katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa SGR, wakandarasi na washauri wanawajibika kuzingatia masharti ya mikataba, pamoja na sera za Kitaifa ambazo zinataka utoaji wa fursa sawa za ajira kwa wanawake na wanaume katika kada mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa masharti ya mikataba ya ujenzi inayotumika katika Ujenzi wa SGR, mkandarasi na mshauri, wanatakiwa kufuata sheria zote za nchi, zikiwemo zile zinazohusu ajira, kazi na usawa wa kijinsia. Hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza utekelezaji wa matakwa haya ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia, inaendelea kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara ya utekelezaji wa sera na miongozo hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa, malengo ya usawa wa kijinsia yanafikiwa na wanawake wanapata fursa stahiki za kushiriki katika miradi mikubwa ya kimaendeleo nchini.
MHE. MWINYI JAMAL RAMADHAN aliuliza:-

Je, kwa nini Bandari ya Dar es Salaam inashindwa kupokea meli nyingi kwa wakati mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upokeaji wa meli katika gati za bandari zote duniani hutegemea mambo kadhaa yakiwemo urefu wa gati kwa meli husika, ukubwa wa yadi ya kuhudumia shehena, kina cha lango la kuingilia meli, vifaa vya kuhudumia shehena, mifumo ya kuhudumia meli na shehena iliyo fungamanishi, aina na ubora wa barabara na reli zinazoingia na kutoka Bandarini, kasi ya ongezeko la shehena na mahitaji ya meli, pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inazo gati 13 zenye uwezo kuhudumia meli za aina ya Post Panamax ambazo ni kubwa katika ukanda unaohudumiwa na Bandari za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Hata hivyo, idadi hii ya gati bado ni ndogo ukilinganisha na kasi ya ongezeko la meli na shehena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kutokana na ongezeko la meli na shehena kwa ujumla, Bandari ya Dar es Salaam inaendelea na mipango kuongeza idadi ya gati, vifaa na mifumo stahiki ili kukabiliana na hali hiyo. Kwa kuanzia, ujenzi wa gati la meta 500 katika Bandari ya Dar es Salaam umeanza sambamba na maandalizi ya ujenzi wa gati nyingine nne (gati namba 12-15) ambapo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na TPA imeanza mazungumzo ya awali na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata mkopo nafuu kugharamia ujenzi wa gati hizo.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza: -

Je, Serikali imechukua hatua gani za kurejesha Bandari za Kibirizi na Ujiji zilizokumbwa na madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi na kujaa maji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TPA imefanya tathmini ya madhara yaliyosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan kuongezeka kwa vina vya maji katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa ambapo baadhi ya Bandari kama Ujiji na Kibirizi zimeathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa TPA imeanza kazi za ukarabati na kuweka miundombinu mbadala, ili Bandari hizo za Kibirizi na Ujiji zirejee kufanya kazi kama ilivyokuwa awali. Aidha, kazi zinazoendelea zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Juni, 2026.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, lini Uwanja wa Ndege wa Kyabajwa utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza Mradi wa Kiwanja Kipya cha Mkoa wa Kagera kwa kuingia mkataba na mtaalamu elekezi, ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kiwanja hicho kinachotarajiwa kujengwa katika Eneo la Kyabajwa. Mtaalamu elekezi anatarajiwa kukabidhiwa eneo la kazi na kuanza kazi ndani ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Januari – Machi, 2026).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026. Baada ya hapo, hatua za utekelezaji wa mradi huo zitaanza.
MHE. SIGRADA W. MLIGO K.n.y. MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa bandari ndogo ya Kagunga na Soko la Kagunga utakamilika ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamimzi wa Bandari Tanzania (TPA) mnamo mwaka 2015 ilitekeleza mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kagunga wenye thamani ya shilingi bilioni 3.8, uliohusisha ujenzi wa gati, ghala la mizigo, jengo la abiria, nyumba ya wafanyakazi, vyoo, uzio na kibanda cha mlinzi. Mradi huu ulikamilika mwezi Januari, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali pia kupitia TPA iliingia Mkataba na Mkandarasi ESSAU Construction Ltd. wenye thamani ya shilingi milioni 190.2 kwa mfumo wa Kurudisha kwa Jamii au Corporate Social Responsibility (CSR) kwa Halmashauri ya Kigoma Vijijini kwa ajili ya ujenzi wa soko ambao nao umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyopelekea maji kujaa, bandari hii kwa sasa haitumiki. Serikali kupitia TPA inaendelea na mpango wa kufanya maboresho ya bandari hiyo na hatua iliyofikiwa ni kufanya utafiti wa namna bora ya kutatua changamoto ya kujaa kwa maji na maboresho jumla ya bandari hiyo.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa hoteli katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uandaaji wa pembuzi yakinifu ya ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro. Kwa sasa taratibu za kutafuta mwekezaji wa ujenzi wa hoteli zinaendelea.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga uzio wa Uwanja wa Ndege Urambo ili kuutunza vema Uwanja huo na kuwa salama?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama katika Kiwanja cha Ndege cha Urambo na hivyo inakubaliana na pendekezo la ujenzi wa uzio katika kiwanja hicho. Katika hatua za utekelezaji, suala hili tayari limejumuishwa katika rasimu ya Mpango Mkakati wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wa miaka mitano ijayo, ili kuwezesha upangaji na upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia bajeti ya maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ukarabati, uboreshaji na upanuzi wa viwanja vya ndege nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia TAA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa Kiwanja cha Ndege cha Urambo kinaendelea kuwa salama. Hatua hizo ni pamoja na utekelezaji wa maelekezo ya kitaifa kuhusu ulinzi na usalama wa viwanja vya ndege, pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi wanaozunguka eneo la kiwanja kupitia dhana ya ulinzi shirikishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kiwanja hicho kinamiliki hati ya ardhi, jambo linalosaidia kulinda mipaka yake dhidi ya uvamizi na matumizi yasiyoidhinishwa, hususan katika mazingira ambayo kiwango cha shughuli za kiuendeshaji bado ni cha chini. Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kadri itakavyohitajika ili kuhakikisha usalama na maendeleo endelevu ya miundombinu hiyo muhimu.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Bandari ya Tanga - Kilimanjaro - Arusha - Singida hadi Musoma (kilometa 1108) utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kuunganisha reli ya Bandari ya Tanga na Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida hadi Musoma. Kwa sasa hatua inayoendelea ni kuhuisha yaani review tafiti hizo, ili kuendana na mahitaji ya sasa ikiwemo ushirikishwaji wa makampuni ya madini yanayowekeza kwenye ushoroba huo. Aidha, Serikali inaendelea na kufanya majadiliano na kampuni mbalimbali ili kufanya uwekezaji wa reli hii ya kimkakati.
MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia wapi kuhusu mwekezaji aliyeonesha nia ya kuwekeza Hoteli ya New Musoma ambayo ni alama ya Mji na Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika la Reli linaendelea kuboresha nyumba na majengo ya biashara pamoja na hoteli zinazomilikiwa na shirika ikiwemo Hoteli ya Musoma. Aidha, TRC imejidhatiti katika kuhakikisha kwamba inashirikisha sekta binafsi katika kufanya uwekezaji wa hoteli hii ili kuleta tija na kuongeza mapato ya shirika.

Mheshimiwa Spika, TRC ilipokea mwekezaji ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika Hoteli ya Musoma. Aidha, shirika limemtaka mwekezaji kuwasilisha andiko la mradi, pamoja na michoro ya maboresho anayotaraji kuyafanya. Pindi atakapokamilisha uwasilishaji wa nyaraka hizo hatua za kuendelea na majadiliano zitaanza.