Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Charles Muguta Kajege (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami naomba niende moja kwa moja kwenye hoja zangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nilipata bahati ya kuwa katika Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa tukapitia baadhi ya gharama katika baadhi ya mikoa. Kitu cha kwanza nilichogundua ni kuwa kuna ugawaji wa rasilimali ambao hauendani na hali halisi ya wananchi. Kwa mfano, kuna ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu gharama yake itakuwa 1.5 billion, lakini ukiangalia gharama hizi zinazidi mara tatu ujenzi wa vituo vya afya ambavyo vimekubaliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka nijielekeze katika Jimbo langu la Mwibara kwa sababu muda ni mfupi. Naomba katika Jimbo la Mwibara tupate maji kwa sababu licha ya kuzungukwa na robo tatu ya Ziwa Viktoria lakini maeneo mengi bado hayana maji ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, vituo vya afya vilevile ni tatizo kubwa. Katika Kata za Nasimo, Kibara, Chitengule, Igundu, Nampindi, Kwilamba, Namuhula, Butimba na Nyamiholo bado hakuna huduma nzuri za afya. Katika maeneo hayo wananchi wamejitahidi sana kujenga maboma ya zahanati. Serikali iliahidi kwamba ingemalizia, naomba Serikali itekeleze na yenyewe wajibu wake.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni katika barabara. Barabara nyingi za Mwibara hazipitiki lakini hasa nitazungumzia barabara moja ambayo inatoka katika Kijiji cha Buguma - Chigondo haipitiki kabisa kwa sababu mkondo wa maji umekatisha katikati ya barabara. Kama leo nikiongozana na Waziri wa TAMISEMI akienda kuona jinsi ambavyo wanawake wanavuka pale sidhani kama atafurahi. Kwa hiyo, naomba barabara hii na yenyewe ipewe umuhimu katika kujengwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni elimu. Tuna matatizo ya vyumba vya madarasa, maabara, maktaba na nyumba za walimu. Vilevile maboma mengine ambayo wananchi wamejenga hajayakamilika, naomba Serikali itusaidie.

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ni kivuko kati ya Nasimo na Kisiwa cha Nafuba. Naomba Serikali itufikirie kutusaidia katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, lakini tatizo lingine ni fidia kwa wananchi ambao walipisha mradi wa barabara ya kutoka Bulamba - Kisorya. Hawa nao bado hawajalipwa, naomba vilevile tufikiriwe.

Mheshimiwa Spika, lingine ni wakulima wa pamba. Hawa ni karibu mwaka wa tatu sasa hivi hawajalipwa pesa zao. Nafikiri Wizara husika inaweza kuangalia namna ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu ajira ziko katika maeneo makubwa mawili, kwanza ni kilimo. Bahati nzuri tunazungukwa na Ziwa Viktoria, naomba tupewe skimu za umwagiliaji maji na vilevile tupate mikopo ya matrekta.

Mheshimiwa Spika, lakini sekta nyingine ni uvuvi. Sasa hivi samaki wamekuwa wajanja huwezi ukawavua kwa kutumia zana za kizamani. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie namna ya kutusaidia kupata zana za kisasa kuliko Maafisa Samaki au Maafisa Uvuvi kuendelea kuwakamata wavuvi wetu kwa kutumia zana za zamani.

Mheshimiwa Spika, kitu kingine naiomba Serikali kuangalia ulipaji wa madeni kwa wale waliotoa huduma Serikalini. Kwa mfano, nina kampuni mbili za jimboni kwangu; moja ni Swahili Ceramics, hawa wanaidai TBA zaidi ya milioni 139 kuanzia mwaka 2017 hawajalipwa, naomba Serikali ichukue hatua. Kampuni nyingine ni Wajenzi Enterprises ambao wanaidai Halmashauri ya Gairo milioni 10.5. Hawa nao wanasumbuliwa, naomba nao waangaliwe.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia halmashauri ya kwetu ambayo ni ya Majimbo mawili ya Mwibara na Bunda Vijijini; ili uweze kwenda katika Jimbo la Bunda Vijijini inabidi uvuke Jimbo la Bunda Mjini. Ushauri wangu naomba Bunda Vijijini na Bunda Mjini wawe katika halmashauri, moja sisi Mwibara tubaki peke yetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda huu, naomba na mimi niunge mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, kwa kunipa nafasi hii. Ninaomba nitumie fursa hii kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu kwa kuendelea kuweka pesa nyingi sana katika sekta hii ya ujenzi wa barabara zetu, hakika Mama yupo juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nitumie fursa hii kumpongeza Waziri Mheshimiwa Bashungwa na timu yake nzima ya Wizara kwa kazi nzuri. Vilevile, ninampongeza Mhandisi Malibe, ambaye ni RM wa Mkoa wangu, kwa kazi nzuri anayofanya na pia kwa ushirikiano wake mzuri sisi Waheshimiwa Wabunge. Hakika tumempata mtumishi mzuri katika Mkoa wa Mara, apate maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jimbo langu naishukuru Serikali kwa kukubali kuanza kutafuta pesa kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kati ya Kisorya na Ukerewe. Pia, kwa kuanza mchakato wa kuipandisha barabara ya Busambara kwenda Mugara kwa kuiweka katika TANROAD ili baadaye iweze kujengwa katika kiwango cha lami. Ahsante sana Mama, ahsante sana Mheshimiwa Bashungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali ianze kuangalia upya ujenzi wa barabara kipande cha Nyanguge kwenda Bunda, hiki kipande kimechakaa sana, kuna viraka vingi sana. Vilevile, barabara hii imekuwa ni nyembamba sana ilijengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita. Naona sasa muda umefika wa kuweza kuibadilisha barabara hii iweze kuendana na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, ujenzi wa barabara inayopita nje ya Mji wa Dodoma, sasa hivi utaangalia, jana mimi nimeshindwa nimechelewa hata kuuliza swali langu, kwa sababu ya msongamano kati ya round about ya Shabiby na hapa Bungeni, kuna malori mengi sana, kuna mabasi mengi sana pia yanapita pale, sasa kuna msongamano umekuwa mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naiomba Serikali yetu imalizie kipande kile ili yale mabasi na malori yaweze kupitia kule nje ya Mji. Vilevile, ninaomba Serikali ikamilishe ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma, huu wa Msalato, mahitaji ya usafiri wa ndege ni makubwa sana kama ambavyo watani wangu Wahaya wamezungumza nao wanapenda sana kutumia ndege. Sasa wanashindwa kutumia ndege, kwa sababu ndege hazifiki hapa. Kwa hiyo, ninaomba sana uwanja huu ukamilike ili uweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine kuna tatizo la malipo ya wakandarasi, mimi ingawa nipo katika sekta hii, lakini sipo katika ujenzi wa barabara. Wakandarasi wengi sana wamefilisika na wengi sana sasa hivi wanaumwa magonjwa ya moyo, kwa sababu ya madeni waliyonayo. Kila siku Serikali inasema kwamba, itawalipa, sasa Serikali ituambie ni lini italipa haya madeni? Kama haiwezi kulipa madeni, kwa nini inaendelea kutoa hizi tender wakati inajua kabisa kwamba, haiwezi kulipa haya madeni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninampenda sana Mheshimiwa Bashungwa, lakini katika hili nafikiri leo shilingi yake itabakia kwangu mpaka aje na mpango maalum wa kuweza kulipa haya madeni. Kwa kusema hayo machache.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, mara kadhaa nimeiomba Serikali kupitia upya madai ya wananchi waliopisha ujenzi wa Barabara ya Bunda kwenda Kisorya, kwani baadhi ya wananchi wanadai kuwa bado hawajalipwa fidia zao. Naiomba Serikali kupitia bajeti ya mwaka huu wa 2025 iwalipe wananchi hao stahili zao.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ya usafiri kati ya Visiwa vya Nafuba, Sozia, Nyamuguma, Machwela na Buyanza ni changamoto kubwa sana kwa wananchi. Naiomba Serikali ivipatie kivuko visiwa hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Vilevile nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mwibara sasa hivi limeanza kung’ara, namshukuru sana. Pia, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Waziri wa TAMISEMI na wasaidizi wake pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI kwa kazi kubwa na jukumu kubwa sana walilonalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika maeneo yafuatayo: Kwanza ni katika sekta ya afya. Huduma za afya katika Jimbo langu la Mwibara bado haziridhishi. Tunavyo tu vituo vitatu vya afya vya Kasahunga, Kisorya na Kasuguti, lakini bado huduma zinazotolewa siyo za kiwango cha vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza ni kwamba, hivi vituo vimejengwa kwa muda mrefu sana. Kwa mfano, Kituo cha Kasahunga kina zaidi ya miaka 20, lakini bado hakijakamilika. Kituo cha Kasuguti kina zaidi ya miaka 15 bado hakijakamilika na Kituo cha Kisorya kina zaidi ya miaka saba bado hakijakamilika. Naiomba Serikali yangu sasa hivi iweze kutufikiria vizuri sana na kutupa kipaumbele iweze kukamilisha vituo hivyo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusia na Mfuko wa Jimbo. Naipongeza sana Serikali kwa kuongeza fedha katika mfuko huu, lakini nataka niishauri Serikali, pesa hizi naomba zigawanywe sawa sawa katika kila Jimbo.

Hakuna formula ambayo tutatumia hapa ambayo itafanya Jimbo lingine liweze kupata inavyostahili. Hakuna formula nakwambia! Fedha hizi zigawanywe kama ambavyo zimegawiwa pesa za TARURA, kila Jimbo lipate pesa sawa sawa. Tukishagaiwa hivyo sasa, kila Mbunge atakwenda kupambana na mambo yake huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo letu la Mwibara lina ardhi ya kutosha na lina maji ya kutosha, tunachohitaji ni elimu sahihi na mafunzo sahihi ili tuweze kutumia fursa zilizopo katika sekta hizo za uvuvi na kilimo. Jimbo letu tumeshaenda hatua moja mbele katika kutafuta Chuo cha VETA. Kata yetu ya Butimba imetoa ekari 57 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hiyo. Naomba Serikali sasa itufikirie katika mgawo wa VETA katika kipindi hiki ambacho kinakuja nasi tuweze kupata Chuo cha VETA katika Jimbo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule kama tatu kongwe za msingi ambazo majengo yake yameshachakaa na baadhi ya viongozi wa elimu wamekuja na wamesema kwamba, hayo majengo sasa hivi hayastahili kutumiwa tena. Naomba Serikali yetu sasa iweze kufikiria namna ya kujenga shule hizi kongwe za zamani ili ziweze kuwa salama na ziweze kuendelea kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la posho za Madiwani limezungumzwa na wenzangu wengi waliotangulia. Wakati wa kampeni tunasema tunakwenda na mafiga matatu, yaani Rais, Mbunge na Diwani, lakini baada ya uchaguzi sisi wengine tunawafungia nje hawa Madiwani, tunakuwa tena hatuwatendei haki. Pamoja na mapendekezo ambayo yametolewa kwamba posho zao ziongezwe angalau ziwe shilingi 800,000/= kwa mwezi, mimi naona kama bado hazitoshi. Nashauri angalau wapate shilingi milioni moja kila mwezi ili waweze kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao Madiwani ndio first responders wetu. Ndio wanaotatua matatizo ya wananchi sisi tukiwa huku Bungeni. Vilevile tusisahau kwamba na wao wanatumika kama ATM huko majimboni mwetu. Kwa hiyo, naomba nasi tuweze kuwafikiria waweze kupata posho ya kutosha waweze kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zaidi ya miaka 13 sasa hivi tangu mradi wa ujenzi wa barabara ya Bulamba hadi Kisorya ufanyike. Kuna wananchi ambao walitoa nyumba zao zikabomolewa kwa ajili ya kupisha mradi huu, lakini bado mpaka sasa hivi hawajalipwa.

Naomba Serikali yetu sasa iharakishe malipo ya hawa wazee ambao wengi wao sasa hivi maisha yao yamekuwa magumu; wengine walipoteza nyumba zao na kwa hiyo, wameshindwa kujenga nyumba zao upya.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na kaka yangu kwa mchango wake mzuri. Ni kweli, hiyo barabara ni ya muda mrefu na ni kweli kwamba sio wananchi tu wa upande wa Jimbo la Mwibara, hata wa Bunda Mjini mpaka kwenda kule Nyamuswa na wenyewe mpaka sasa hivi hawajapisha na wametenga maeneo yao kwa sababu Wilaya ya Bunda wanahitaji barabara ya lami ambayo itaenda kuunganika na Arusha. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kajege, unapokea Taarifa?

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naichukua kabisa na kuikubali hiyo Taarifa. Nami nasisitiza tena kwamba, haya malipo yafanyike mapema sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo. Naunga mkono hoja hii ya TAMISEMI. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja hii ya Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vilevile nataka niwapongeze Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Hawa wamekuwa ni kiunganishi kizuri sana kati yetu na Serikali na hakika hakuna hata siku moja ambayo nimekwenda kuwaona, na wakashindwa kunisaidia katika kutatua changamoto yangu. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imefanya kazi kubwa sana katika kipindi cha hii miaka minne. Miradi mingi imetekelezwa. Sasa nitaigawa katika maeneo mawili, kwanza Kitaifa na lingine katika jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kwanza ni wa Bandari ya Dar es Salaam. Baada ya DP kupewa hii Bandari ya Dar es Salaam imekuwa na mafanikio makubwa. Katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2024 mpaka Machi mwaka huu, jumla ya makasha 686,515 yameingia, ukilinganisha na makasha 670,724 katika kipindi hicho hicho katika mwaka uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni moja. Vilevile muda wa meli kutia nanga kusubiri kuingia bandarini umepungua kutoka siku 30 hadi kufikia siku tatu. Hii ni improvement kubwa sana katika upande wa bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere ambao thamani yake ni shilingi trilioni 6.6. Mpaka kufikia Machi mwaka huu, jumla ya megawati 2,115 zimeingia katika Gridi ya Taifa na huu umeme umeweza kuingia katika vijiji vyote 12,318, lakini vilevile na vitongoji 33,657 ikiwa ni asilimia 52.3 ya vitongoji vyote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi jimboni kwangu nataka nikiri kwamba, kama kuna jimbo ambalo limepata miradi mingi, ni pamoja na Jimbo langu la Mwibara. Kwa upande wa elimu katika kipindi cha miaka minne, tumeweza kujenga shule nane mpya za sekondari ikiwa ni pamoja na shule moja ya wasichana ya special, Mara Girls, ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 4.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumepata VETA ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 3.3. Pamoja na hiyo, tumeweza kupata madarasa mengine mapya 315, ambayo kama ingekuwa ni shule za msingi, ukigawa katika madarasa ambayo hayana mkondo, maana yake ni kwamba, tumepata shule nyingine mpya za msingi 45 na matundu 260 ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya. Jimbo langu limeweza kupata vituo vingine viwili vipya vya afya; Kituo cha Isanju na Kituo cha Kisolya. Pamoja na hivyo, huduma zime-improve ikiwa ni pamoja na kupata x-ray na ultrasound.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna zahanati mpya zimejengwa, ambazo ni Zahanati ya Mranda, Nambaza, Lagata, Mwiseni na Sozia, lakini kuna zahanati nyingine ambazo zitakamilika hivi karibuni. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara. Mwaka 2021 wakati tunaingia madarakani, Jimbo la Mwibara lilikuwa halipitiki kabisa, barabara zote zilikuwa kama zimekufa, madaraja yalikuwa yamepasuka hayapitiki na baadhi yalikuwa yanabeba wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtangulizi wangu aliyekuwa ametangulia, aliwahi kusema kwenye mkutano wa hadhara kwamba, hizi barabara au haya madaraja hayataweza kujengwa labda mpaka Yesu atakapokuja, lakini kupitia Serikali ya Dkt. Mama Samia haya madaraja na barabara zimeweza kujengwa katika mwaka mmoja. Nampongeza sana mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara tumeweza kujenga tena barabara nyingine kuunganisha maeneo mengine. Kwa mfano, barabara ya kutoka Bugala – Sikilo, Barabara ya kutoka Nambaza – Igundu na barabara nyingine ambayo itajengwa kutoka Kalukekere – Musoma Vijijini. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba, maeneo yote yanafikika kwa uhakika, lakini vilevile barabara nyingine zote sasa hivi zinapitika kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu hakuna sehemu ambayo barabara haipitiki, sasa hivi unaweza ukaenda hata na IST wakati kufikia mwaka 2020 ulikuwa hauwezi kwenda hata na Land Cruser. Kwa hiyo, hali ya barabara jimboni kwangu imekuwa nzuri sana na huduma zimekuwa nzuri zaidi. Naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maji, vilevile tumepata miradi mikubwa ya maji ikiwa ni pamoja na mradi wa kutoka Buzimbwe – Lagata na Kabainja. Mradi huu unategemewa kukamilika hivi karibuni. Vilevile kuna mradi wa Isanju – Nyalugoma ambao umeshakamilika na vilevile kuna mradi mkubwa ambao umemaliziwa kusanifiwa, mradi ambao utapitia katika vijiji 33 ambao vilevile ukiwa katika kata sita ambazo ni Kata Kisolya, Nampindi, Igundu, Nansimo, Chitengule na Kibara. Mradi huu utakapokamilika utakuwa ni game changer kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji katika Jimbo la Mwibara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, bado jimbo langu lina changamoto. Changamoto ya kwanza ni maji. Kama nilivyozungumza, kuna mradi wa maji ambao umekamilika kusanifiwa, lakini bado haujakamilika. Kwa hiyo, maeneo yote ambayo bado mradi haujaanza, maana yake ni kwamba yana matatizo ya maji. Naiomba sana Serikali ifanye kila iwezalo ili mradi huu uweze kujengwa na kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kwenye kilimo. Kilimo ni sekta muhimu sana katika jimbo langu ambayo inasaidia wananchi wengi katika kupata kipato chao. Pamoja na kwamba jimbo langu kila kata imegusa kwenye maji, lakini bado tuna tatizo la maji sehemu nyingine nyingi. Hivyo, naomba Serikali itusaidie kujenga scheme za maji; na hii nimeshaongea na Mheshimiwa Waziri Bashe, tupate scheme za maji katika maeneo ya Kisorya, Mwitende, Kigaga, kuna Bulamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishapata hizi schemes nina imani kwamba hatutakuwa na haja tena ya kuomba vyakula Serikalini. Kwa hiyo, naomba Serikali itusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu umeme. Ni kweli kwamba vijiji vyote 12 vimepata umeme, lakini bado kuna vitongoji havijapata umeme. Kama ujuavyo umeme ni kila kitu sasa hivi katika maisha, tunaomba Serikali itusaidie umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika umeme, nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu, na hii ni Wizara yake. Aliahidi mwaka 2020 wakati akiwa anafanya ziara jimboni kwangu kwamba ataipatia Nafuba umeme wa sola. Kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu naye yupo hapa, nafikiri atasikia na nina imani kwamba tutapata umeme hivi karibuni katika hilo eneo la Nafuba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mawasiliano. Jimbo langu vile vile lina visiwa vingi ikiwa ni pamoja na Nafuba, Buguma, Sozya na sehemu nyingine. Kutoka kwenye hivi visiwa kuja nchi kavu, kuna tatizo kubwa la usafiri. Serikali imeniahidi mara kadhaa kuhusu kunipatia vivuko. Naomba sasa Serikali itekeleze ahadi zake ili tupate vivuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja tena katika upande wa elimu. Pamoja na kwamba tumepata shule mpya nyingine nane, lakini bado tunahitaji. Upande wa elimu, bado haijakaa vizuri. Kuna shule kongwe ambazo madarasa yake yamechakaa sana, naomba Serikali ianze kutusaidia kurekebisha madarasa hayo katika shule za Chitengule, Nansimo, Namibo A, Kinkombyo, Namhula Stoo, Kabainja, Ragata na Buzimbwe. Ukienda katika shule hizi, hali yake siyo nzuri, madarasa kabisa ni kama hayatakiwi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umeisha, malizia.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itusaidie katika kuboresha haya madarasa kwenye hizi shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunahitaji minara ya simu. Bado mawasiliano siyo mazuri katika jimbo langu. Kwa hiyo, tunahitaji minara mingine mingi ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya, bado tuna upungufu wa madaktari, wauguzi na vifaatiba. Tunahitaji tena bado tupewe vituo vingine vya afya. Kuna ahadi za Serikali mwaka 2024 wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika jimbo langu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kajege...

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie dakika moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jimboni kwangu aliahidi kwamba kutajengwa kituo cha afya katika sehemu za Bulamba. Kituo hicho bado hakijajengwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atekeleze ahadi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na hivyo naunga mkono hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika hotuba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Kama walivyofanya watangulizi wangu na mimi napenda nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ambayo amefanya katika kipindi hiki kifupi. Katika kipindi hiki kifupi tumeona miradi yote mikubwa inaendelea kutekelezwa kawa kasi kubwa na kwa ubora wa hali ya juu, mahusiano yetu na nchi zingine za nje yamepanuka zaidi na kukua zaidi, biashara yetu ya nje na ya ndani imekua na kupanuka zidi yote hii katika kipindi kifupi hiki cha utawala wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa TAMISEMI na timu yake kwa uongozi mzuri ambao wamefanya katika kipindi hiki kifupi. Kama walivyozungumza wezangu imekuwa ni raisi zaidi kumpata Mheshimiwa Waziri Kairuki, muda wote ukimpigia simu anapokea simu na bado anakuletea mrejesho ambao ni mzuri. Nakupongeza sana Waziri wetu Kairuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Mwibara nitazungumzia baadhi ya changamoto ambazo ndiyo kikwazo kikubwa katika maendeleo yetu. Changamoto ya kwanza ipo katika Sekta ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitembelea katika shule za Mwibara nyingi hasa shule za msingi utakuta kuna upungufu mkubwa sana wa vyumba vya madarasa na hata vile vyumba vya madarasa viliyopo bado vimechakaa sana, wanafunzi katika chumba kimoja utakuta ni zaidi ya mia moja, vilevile vyumba hivi vingi havina sakafu kwa hiyo watoto wanasoma katika vumbi. Shule hizi ni kama Shule ya Msingi Gundu, Chitengule, Nampangala, Igundu, Buyomba, Susi, Bwanza, Shabirizi, Visambu, Bunele, Mlagata, Kinkombe na Kabaija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kutembelea katika hizi shule ni kama hazipo, kwa sababu majengo ni mabovu na mengine sasa hivi hawaruhusiwi hata watoto kuyatumia, kwa hiyo ni kama majengo hayapo. Vilevile upungufu wa madawati madarasa mengi hayana madawati kwa hiyo wanafunzi wanasomea chini. Sasa ukiangalia kwamba madarasa kwanza wanafunzi wako wengi katika darasa moja vilevile ni kwamba hawana madawati plus kwamba hata sakafu hazipo, ni chafu, ni vumbi kwa hiyo mazingira ya kusomea hawa wanafunzi yanakuwa ni magumu sana. Sasa inakuwa ni vigumu kumchukua mwanafunzi anatoka katika madarasa haya aka–compete na wanafunzi wengine ambao wanatoka katika mazingira mazuri sana ya elimu, kwa hiyo lazima naiomba Serikali iweze kuangali hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kingine ni upungufu wa walimu. Katiba hotuba ya TAMISEMI Mheshimiwa Waziri amesema kuna upungufu wa Walimu zaidi ya 89,932 katika shule za msingi wanaokuja kuajiriwa mwaka huu tunaona ni kama 13,000 peke yake ambayo ni sawa sawa na asilimia 14 hawa walimu ni wachache sana hawatoshi. Nilikuwa naomba Serikali yetu ifikilie namna ya kuongeza walimu, kwa sababu kama hatuna walimu hizi shule tunatoa elimu ya namna gani kama hatuna walimu na tulikubaliana kuanzia mwanzo kwamba mojawapo ya maadui wetu ni ujinga sasa hatutoweza kutoa ujinga kama walimu hawatoshi katika mashule yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ina changamoto ni katika sekta ya afya. Kwa sasa hivi ninavyo vituo Vitatu vya Afya Kisolya, Kasaunga, Kasuguti lakini bado havijakamilika, hivi bado havina majengo kutosha, vifaatiba havipo na wauguzi hawatoshi. Ningeomba sana Serikali ifikirie namna ya kuvikamilisha vituo hivi ili viweze kutoa huduma inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna maeneo ambayo sasa huduma ya afya iko mbali sana, kwa mfano Kata ya Igundu na Kata ya Namuhula nilikuwa nasikia kwamba Serikali ifikirie kujenga vituo vya afya katika Kata hizo mbili. Vilevile mwaka jana wakati ziara ya Mheshimiwa Rais katika Wilaya ya Bunda Tarehe Saba Februari, alielekeza kwamba hospitali ya Halmashauri nyingine ijengwe katika Jimbo la Mwibara, hilo agizo bado halijatekelezwa naomba hii Wizara ifikirie namna ya kujenga hiyo hospitali mapema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni michango ya wananchi kusaidia katika miradi ya maendeleo. Sina tatizo na michango, lakini tatizo langu ni kwamba michango mingine imekuwa ya holela. Kwa mfano, juzi nilipokuwa Jimboni, nilipita katika Kijiji kimoja cha Busambara. Hawa wameletewa pesa shilingi 54,824,000 kujenga matundu 20 ya choo. Wananchi wameombwa kuchangia tena shilingi 15,000 katika kila kaya. Nikawauliza, hivi gharama ya choo kimoja, tundu moja ni kiasi gani? Wakasema ni shilingi 1,500,000. Sasa kwa hesabu rahisi ni shilingi milioni 30. Nikawauliza, hizi Shilingi milioni 24 zinazobakia zinakwenda wapi? Hawakuwa na jibu. Nikawaambia wananchi msichange, hizo pesa zinatosha. Nilikuwa naomba, Serikali yetu iangalie vilevile kuhusu uchangishaji holela kutoka kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, bado kuna upotevu wa pesa katika Jimbo langu. Kuna wizi tuseme, kwa mfano, kuna shilingi milioni 300 ambazo zimepelekwa katika Kituo cha Afya cha Kasuguti, hazijulikani zilipo; kuna shilingi milioni mbili nilitoa katika Kata ya Nyamihoro kutoka katika mfuko wangu wa Jimbo, hazijulikani zilipo; kuna Shilingi milioni moja ilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa choo katika Shule ya Msingi ya Msambara, VEO kakimbia nazo hazijarudi; na vilevile nilitoa shilingi 500,000 kwa ajili ya Nyamihoro na zenyewe hazijulikani zilipo. Naomba sasa wakati wa majumuisho nipate majibu ya nini kinafanyika au tutapataje hizi pesa ziweze kufanya maendeleo katika jimbo langu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuanzishwa kwa kidato cha tano katika Shule za Sekondari za Nansimo na Buramba. Katika Shule ya Nansimo miundombinu imetosha, yaani kuna mabweni na madarasa, yanatosha; lakini katika Shule ya Buramba kuna madarasa lakini hakuna bweni. Nilipoongea na Afisa Elimu, akasema kwamba haiwezekani kuanzisha Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari ya Buramba kwa sababu hamna bweni. Mimi naona hilo siyo tatizo, haya mambo tumeambiwa kuanzia miaka mitano iliyopita mpaka leo na shule haijaanzishwa. Naomba tuanzishe Kidato cha Tano, bweni litatufata baadaye. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWNEYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Charles Kajege.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Vile vile kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba kazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ndio ameianza, Watanzania tutegemee makubwa huko mbeleni tutakapokwenda. Pia, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wa Wizara hii kwa utendaji wao wa kazi nzuri ambazo wanafanya mpaka muda huu. Wameweza sasa hivi kuifanya Tanzania ipitike kwa urahisi angani, ardhini na majini, nawapongeza sana. Lakini vile vile nampongeza Engineer Mativila Mtendaji Mkuu wa TANROADS na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara Engineer Maribhe kwa kazi nzuri sana ambayo wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza tena Wizara hii kwa kuweza kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Nyamuswa – Bunda - Bulamba – Kisole kwa kiwango cha lami. Kwa sasa tunasafiri na kusafirisha mizigo yetu kwa raha mustarehe, nawashukuru sana. Vilevile naishukuru Wizara kwa kupanga kukamilisha vipande vya barabara kati ya Kibara na Kasaunga na pia Kisole na Kisole Kivukoni kwa kiwango cha lami. Ukamilishaji wa vipande hivi utasaidia kuunganisha barabara nzima kutokea Kisorya mpaka Nyamuswa kwa kiwango cha lami, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nitumie fursa hii kuiomba Wizara sasa kuipandisha hadhi Barabara ya Kisambala…

MHE. BONIPHANCE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: … Mugala na Musoma Vijijini. Barabara hii ina traffic kubwa sana ya watu pamoja na mizigo, na vile vile barabara hii ni shortcut ya watu waendao Musoma na vile vile watokao Musoma kwenda sehemu za Ukerewe naomba sana Wizara ifike kupandisha barabara hii.

SPIKA: Mheshimiwa Kajege, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba wakati anazungumza barabara ya ile ya kuunganisha Kisorya, amesahau kusema barabara ya kutoka Balili kwenda Mugeta nayo inapaswa kuunganisha.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Kajege, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, huyo ni Comrade, naipokea taarifa yake. Kuna changamoto ambazo bado Wizara inatakiwa kuzitatua ili kuweza kufanikisha malengo ya Serikali yetu. Kwa mfano, kuna Shirika la Air Tanzania Limited, shirika hili limekodisha ndege kutoka Shirika la TGFA, lakini nikiangalia kwa sababu nimepata bahati kwamba nipo katika Kamati ya PIC, na Viongozi Wakuu wa ATCL wamekuwa wanakuja katika Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika kuangalia tumekuta kwamba tatizo kubwa katika ATCL ni mkataba kati yake na TGFA, mkataba huu kwa kweli si rafiki. Ninaiomba sana Serikali iuangalie tena mkataba huu ili uweze kufanywa kuwa rafiki. Lakini tatizo lingine katika ATCL ni madeni iliyorithishwa, madeni hayo hayalipiki. Ningeomba Serikali iangalie namna nyingine ya kuweza kuchukua madeni haya. Vilevile kuna mwingiliano mkubwa wa Serikali kuipatia ATCL namna ya kufanya kazi, yaani waliache sasa Shirika la ATCL lifanye kazi kibiashara, lihudumie njia zenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano siku moja nilikuwa Mwanza, ndege ya ATCL ilikuwa inatoka Chato. Ndani ya ile ndege nilipoingia niliikuta ina abiria watatu lakini utakuta abiria wengi wapo hapa Dodoma wanasubiri ndege za ATCL kuweza kuwasafirisha. Ningeomba sana Serikali iliache Shirika hili liweze kufanya kazi yake ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni utitiri wa vituo bubu vya ukaguzi wa malori na mizigo katika barabara zetu. Ukitoka Dar es Salaam mpaka kufika Tunduma kuna vituo bubu zaidi ya 100. Haya malori yenye mizigo yakitoka Bandarini yanasimamishwa kila sehemu, yanakaguliwa kila sehemu na wakati mwingine yanchukua muda mrefu. Mfano mmoja siku moja nilikutana na dereva mmoja ambaye alikuwa anatoka Dar es Salaam kwenda Tunduma saa mbili nikamkuta akiwa amesimamishwa pale Kibaha lakini wakati narudi saa 12 jioni kutoka Morogoro nilimkuta bado amesimama pale. Wahusika walikuwa wanadai kwamba kuna cheti ambacho kilikuwa kimesainiwa lakini aliyekuwa amekisaini yuko kwenye mkutano. Kwa hiyo hakumruhusu huyo dereva aendelee na safari mpaka tena wapate aliyesaini kile cheti (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi vituo ni mojawapo ya vikwazo vikubwa sana vya biashara kati ya Tanzania na nchi zingine, lakini vile vile ni chanzo vile vile cha kuwafanya watumiaji wengine wa bandari zetu washindwe kutumia bandari yetu. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie sana hivi vituo bubu, ikiwezekana viondoke vyote vinafanya nini? Kama mizigo ikishakaguliwa bandarini kwa nini iendelee tu kukaguliwa tena njiani? Itakaguliwa kule mwishoni. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu kuna Kivuko cha Mugala - Musoma Vijijini ni kibovu, hiki kivuko kimekuwa ni kibovu kwa muda mrefu. Wananchi wanaotaka kusafiri kwenda Musoma Vijijini na wanaotoka Musoma Vijijini kuja Jimboni kwangu Mwibara wanapata tabu sana. Naomba sana Serikali sasa ikamilishe ukarabati wa hicho kivuko.

Mheshimiwa Spika, kingine ni tunahitaji kivuko kwenda katika Kisiwa cha Nafuba. Kisiwa hiki kina watu wengi sana na ni kikubwa sana, watu wengi mahitaji yao wanachukua katika nchi kavu huku. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali sasa iweze kutafuta kivuko kwa ajili ya kusafirisha wananchi kwenda Nafuba na kuja sehemu zingine za Jimbo la Mwibara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo jingine liliopo ni vibali vya kusafirisha mitambo ya ujenzi, kwa mfano inapotokea mkandarasi anataka kusafirisha mtambo mmoja kwenda katika mkoa mwingine kibali lazima akipate kutoka Dodoma. Hiyo inachukua muda mrefu sana kuweza kupata hivi vibali, inapoteza muda wa biashara na inakuwa kabisa ni usumbufu mkubwa, naomba kuwa na decentralization ya kutoa hivi vibali vya kusafirisha mitambo ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni malipo ya waliopisha Mradi wa Barabara ya Bulamba – Kibara – Kisorya. Barabara hii imeshakamilika muda mrefu lakini wahusika bado hawajalipwa. Jana wakati natoa taarifa kwa mzungumzaji mmoja niliomba Serikali iingilie kati kuweza kuwalipa wahusika fidia zao ili na wao waweze kuendesha maisha yao vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema haya machache naomba niunge mkono hoja hii na nawapongeza sana Wizara na Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi niweze kuchangia hoja yetu hasa ya Kamati ya PIC. Awali ya yote nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi njema ambayo anaifanya kuijenga nchi yetu, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ripoti yetu inavyosema kwa kweli hali ya Taasisi zetu ni mbaya sana bado zinakabiliwa na changamoto kibao. Kwa mfano taasisi zetu karibu zote bado zinapokea ruzuku kutoka Serikali lakini licha ya kupokea hizi ruzuku bado mapato yake ya ndani hayajakuwa kwa kiasi, kwa zaidi ya asilimia kumi kwa mwaka na hii inafanya utegemezi wa hayo mashirika iendelee kuwa makubwa katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwekezaji wa Serikali katika kipindi kirefu kwa mfano mpaka kufikia mwaka 2021/2022 Serikali ilikuwa imewekeza zaidi ya trilioni 73.36 katika Mashirika ya Umma, lakini vilevile katika kipindi hicho imepata gawio la bilioni 850 tu, sasa tukiangalia dhana nzima ya privatization kwa mfano Serikali ilikuwa inataka iache isiwe tena na mzigo wa kuyabeba mashirika ambayo hayawezi yakajiendesha yenyewe lakini pamoja na nia nzuri ya Serikali naona bado haya mashirika hayajafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni uanzishwaji wa kampuni tanzu na baadhi ya taasisi. Kwa mfano, Shirika la TANESCO limeanzisha Kampuni ya TCPM ambayo madhumuni yake ilikuwa ni kujenga nguzo za zege. Kampuni hii ilianzishwa Mwaka 2014 lakini mpaka mwaka huu kampuni haijazalisha hata nguzo moja ya zege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wafanyakazi wa hii kampuni wapo wanapata mishahara na wanapata posho; huu ni mzigo mkubwa sana kwa TANESCO. Sasa kama haiwezi kufanya shughuli ambazo imeanzishiwa hii kampuni haipaswi kuendelea kuwepo. Naishauri Serikali kama itaona umuhimu, vyema ikalifuta hili Shirika la TCPM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambazo wanazo bado ni madeni makubwa ambayo mashirika yetu yanakabiliwa nayo. Kwa mfano, TANESCO pamoja na TRC bado wana madeni makubwa. Haya madeni yanafanya makampuni yashindwe kujiendesha vizuri na hivyo kutokuweza kutoa huduma ambazo yanapaswa yatoe. Mimi naishauri Serikali yangu iangalie namna ya kuyasaidia haya mashirika ili yaweze kujiendesha na kutuletea tija katika uendeshaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo naliona katika haya mashirika ni matumizi mabaya ya ofisi au upigaji mkubwa ambao tunauona. Kwa mfano, TPDC ilianzisha Kampuni Tanzu ya TANOIL. Madhumuni yake ilikuwa ni iweze ku-stabilize mafuta, yaani uweze kununua mafuta in back na kuweza ku-stabilize upatikanaji wa mafuta nchini na bei yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kampuni kwa muda wote imekuwa ikipata hasara, nitataja hapa. Kwa mfano, mwaka 2019/2020 ilipata faida kidogo ya shilingi 31,644,000. Kuanzia mwaka wa 2020/2021 ikaanza kupata hasara na ilipata hasara ya shilingi 666,264,000. Katika msimu uliofuatia 2021/2022 ilipata hasara kubwa zaidi ya shilingi zaidi ya bilioni 7.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ilipata hasara hii? Hii kampuni iliamua kuuza mafuta chini ya bei elekezi ya EWURA, sasa ikapata hasara ya bilioni 7.8. Sisi na Kamati tunajiuliza, je, hii kampuni kwanza ina Bodi na Menejimenti na bado ni Kampuni Tanzu ya TPDC. Sasa tukashindwa kujua, je, wakati inachukua haya maamuzi ya kuuza mafuta yake chini ya bei elekezi kulikuwa na incentives gani? Ni nani alitoa approval? Ilikuwa ni bodi yake, nani au Wizara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpaka muda huo pamoja na kwamba menejimenti ilivunjwa lakini hatuwasikii wakifikishwa mahakamani hawa watu. (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtemvu.
TAARIFA

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Mzungumzaji anaendelea kuzungumza vizuri juu ya changamoto za Kampuni Tanzu. Unapozungumzia Menejimenti hiyo ambayo ilikuwa imesimamishwa na kujiuliza whether wamepelekwa Mahakamani au la? Nakupatia tu taarifa kwamba wamesharudishwa ofisini mpaka sasa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Charles Kajege, unaipokea hiyo taarifa ya Mheshimiwa Issa Mtemvu?

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru sana. Naipokea taarifa yake nzuri sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo mojawapo ya puzzle ambazo Kamati yetu imekutana nazo, kwamba upigaji wa namna hii au matumizi mabaya ya ofisi lakini wahusika wanafikishwa tu mahakamani, au tuseme wanafikiswhwa TAKUKURU lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nafikiria kwamba ni muda umefika muafaka sasa wa Serikali yetu ianze kuwa hard kwa vitu na watu kama hawa. Iwafikishe Mahakamani na kusimamia kabisa kwamba wanatendewa haki zao kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na hayo kwa sababu wenzangu wengi wamechagia vizuri huko nyuma, mimi nilitaka kuchangia tu hayo machache na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kukuza Sekta yetu ya Utalii Nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala machache; la kwanza ni kuhusu vizimba. Katika hotuba ya wizara inaonesha katika mwaka ujao wa fedha watajenga vizimba vitatu tu katika Wilaya ya Bunda; hivi vizimba ni vichache sana. Kwa mfano nikiangalia ukubwa wa Jimbo langu, urefu wa ufukwe peke yake katika Ziwa Viktoria ni zaidi ya kilometa 100, lakini vilevile tuna zaidi ya mialo 40. Sasa, hivi vizimba vitatu vitajengwa wapi? Nilikuwa ninaomba Serikali ifikirie kujenga zaidi ya vizimba 40 katika jimbo langu (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu fidia au kifuta jasho, ninasema ni fidia. Kwanza haitoki mapema, lakini vilevile ni kidogo sana kama walivyozungumza wenzangu. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake atueleze kwamba ni hatua gani sasa Serikali inachukua ili kuhakikisha kwamba wale wananchi ambao wanapata madhara na wao wanapata kifuta jasho kwanza mapema, lakini vilevile kiwe ambacho kinawasaidia katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusu vituo vya askari. Kutokana na mashambulizi ya wanyamapori katika jimbo langu nilikuwa ninaomba sasa tupate vituo vya askari wanyamapori katika maeneo yafuatayo: Kwa mfano, Buzigwe, kila mara kumekuwa na tatizo la mamba, ninaomba kuwe na kituo kingine Buzigwe; kingine katika Vijiji vya Mayolo; Kasaunga; Kisolya; Nampindi; Bulomba; Nchigondo; Mugala; Isikilo; na Namuhula. Hivi vyote ni vijiji ambavyo kila wakati kila mwaka kunakuwa na matukio ya mamba au matukio ya tembo kukanyaga watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie muda wangu kuunga mkono hoja, lakini nitapenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufunga hoja yake aje na majibu yatakayotosheleza ili nisiweze kukamata shilingi. Ahsante sana. (Makofi)