Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Riziki Silas Shemdoe (4 total)

MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. AISHA M. MDUYAH aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa vyumba viwili vya maabara katika Shule ya Sekondari Msakwalo iliyopo Kata ya Ovada, Wilayani Chemba?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisha Msantu Mduyah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2012, ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara katika Shule ya Sekondari Msakwalo ulianza kwa nguvu za wananchi, ambapo ujenzi huo ulifikia 45%. Aidha, mwaka 2022, Serikali iliunga mkono juhudi za wananchi kwa kupeleka shilingi milioni 35, kwa ajili ya kukamilisha chumba kimoja cha maabara ambacho kilikamilika na kinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2026/2027 Serikali, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, imetenga shilingi milioni 30, kwa ajili ya kukamilisha chumba kimoja cha maabara katika Shule ya Sekondari Msakwalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya shule zilizojengwa kwa nguvu za wananchi, ikiwemo Shule ya Sekondari Msakwalo, kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. REGINA H. MIKENZE K.n.y. MHE. KIJA L. NTEMI aliuliza:-

Je, hatua gani zinahitajika ili kupatiwa Halmashauri Jimbo la Katoro na Busanda, ambayo yamekidhi vigezo vya kuwa na halmashauri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa na Mamlaka za Wilaya, Sura 287 na Mamlaka za Miji, Sura 288, pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala katika Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mwaka 2025, ambao umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa, ili kupandisha hadhi na kuanzisha maeneo mapya. Taratibu zinazopaswa kufuatwa ni kuwepo kwa kusudio la kuanzisha halmashauri mpya, ambalo linapaswa kujadiliwa na kupitishwa kuanzia ngazi ya Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kisha maombi hayo kuwasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa na kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la kupatiwa Halmashauri kwa Jimbo la Katoro na Jimbo la Busanda baada ya kutolewa Mwongozo wa Uanzishaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2025, bado halijawasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, hivyo mamlaka zinazohusika ziendelee na taratibu kwa kufuata Sheria na Miongozo iliyoainishwa.
MHE. MARIRTA G. KIVUNGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya cha Mfereji ikizingatiwa kuwa, fedha za ujenzi wake zilitengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali alilolileta Mheshimiwa Marirta Gido Kivunge, Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mfereji ina jumla ya wakazi 8,068 na ina vijiji vinne vya Komesha, Emurua, Idonyonado na Mfereji. Vijiji vya Mfereji na Idonyonado vina zahanati zinazotoa huduma. Aidha, Kijiji cha Emurua, ujenzi wa zahanati upo hatua ya ukamilishaji na Kijiji cha Komesha ujenzi upo hatua ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2024/2025 Serikali imetoa shilingi milioni 250, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, Kata ya Sepeko, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Ujenzi umehusisha jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, choo cha nje na kichomea taka. Aidha, ujenzi umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma kuanzia mwezi Julai, 2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wakazi wa Kata ya Mfereji wanapata huduma za rufaa na dharura katika hospitali ya wilaya wakati Serikali ikiendelea kutenga fedha na kujenga vituo vya afya kwenye kata za kimkakati zitakazokidhi vigezo kote nchini, ikiwemo Kata ya Mfereji katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Kata ya Didia, ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, Kata ya Didia ina jumla ya wakazi 19,093. Kata hii inakidhi kigezo cha kuwa na kituo cha afya. Kwa sasa wakazi wa Kata ya Didia wanapata huduma za dharura na upasuaji katika Kituo cha Afya cha Kanisa cha Bugisi. Tunafahamu kwamba, kituo hiki ni cha taasisi binafsi kwa hiyo, wananchi wakienda pale inabidi walipe, hili tunalitambua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata za kimkakati zitakazokidhi vigezo, ikiwemo Kata ya Didia katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida.