Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Riziki Silas Shemdoe (16 total)
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nina swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo langu la Ukonga, hasa Halmashauri yetu Jiji la Dar es Salaam moja ya mambo yaliyopelekea halmashauri ikahamisha utaratibu wa kukopesha moja kwa moja ni baadhi ya watumishi wa halmashauri na baadhi ya Madiwani walisemwa kwamba wamekuwa wakitumia mlango wa nyuma kujikopesha, lakini pia kuwepo na vikundi ambavyo sasa vimekopeshwa zaidi ya mamilioni na vimetajwa kuwa havionekani.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni kuwa; je, kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa na kodi zetu, ni kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuyataja hadharani hayo makundi ama hivyo vikundi vilivyokopa ambavyo sasa havionekani, sambamba na baadhi ya watumishi wa halmashauri ambao siyo waaminifu waolijingiza katika mtego huu ambao leo unapelekea halmashauri zetu kuhamisha Mfuko huo kupeleka kwenye benki, benki ambazo zinasababisha tushindwe kupata mikopo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Naibu wangu ameyatoa, kama alivyosema, tulikuwa na kikao na benki hizi. Kilichotokea ni kwamba, kweli kwenye majiji kuna fedha nyingi ambazo hazijakopeshwa uki-compare na kwenye halmashauri za wilaya na miji. Shida iliyopo, kutokana na maelezo waliyotupa benki; la kwanza, ni kweli kwamba walikuwa na masharti magumu, lakini kwa sasa sharti linalotakiwa kwa mtu kwa kikundi kukopa ni wale wanakikundi kuwa na NIDA.
Mheshimiwa Spika, nini kimesababisha sasa majiji yawe na fedha nyingi; wamesema, ni kwa sababu wale wanaounda vikundi walioko Dar es Salaam kwa mfano wanakutana kimjini mjini, kwa hiyo hawawezi na inakuwa ngumu sana kupata kikundi kimoja cha watu ambao wanaweza kukopeshwa kwa wakati huo. Hii ni kwa sababu, huyu ametoka Segerea, mwingine ametoka Ubungo, mwingine tena ametoka Kawe na wanakutana Kariakoo kwenye biashara. Wakiwa pale kila mtu hajui huyo mwenzake ametokea wapi.
Mheshimiwa Spika, proposal ya benki ni kwamba, ikiwezekana tuwape mikopo individuals kama tunavyofanya kwa walemavu; lakini tuwe na condition moja kwamba huyu individual tunayempa mkopo atuhakikishie kwamba kwanza ana biashara, ana leseni ya biashara; lakini pili, ataweza ku-employ angalau watu watatu kwenye ile biashara kutokana na mkopo tunaowapa.
Mheshimiwa Spika, kama hii itafanyika, kitu cha kwanza zile bilioni zilizolala kule benki zitatoka. Kitu cha pili, tutaona kwamba tume-create ajira kwa vijana ambao ni moja ya vitu ambavyo tunaviangalia sana kwenye fedha hii. Kwa hiyo Bunge lako hili ninaomba lielewe kwamba, tutakwenda kuona namna ya kubadilisha ule mwongozo na kukubali kwamba tuwe na pilot ya majiji ya kutoa mikopo kwa individuals ambao watatuhakikishia kwamba wata-create ajira kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, nimeomba nisimame nitoe ufafanuzi huu na kushukuru sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri kwanza ninaipongeza Wizara yako kwa kazi kubwa mnayoifanya na jitihada za Serikali yetu, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hata hivyo, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza; kwenye jibu lako la msingi umezungumzia halmashauri kutenga shilingi milioni 30, kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya maabara na utakubaliana na mimi kwamba, halmashauri nyingi bado vipato vyao ni vidogo. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo wananchi wameanza ujenzi kwa maabara wanaweza kukamilishiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mbali na changamoto za maabara, kwenye shule nyingi za sekondari kumekuwa na upungufu wa mabweni, hasa katika Jimbo la Bunda Mjini. Ukienda pale Shule ya Bunda Sekondari, ambayo inafanya vizuri, tena imekuwa namba moja kwenye Mkoa wa Mara, kuna upungufu wa mabweni na maeneo mengine katika Jimbo la Bunda Mjini. Ni lini sasa Serikali itahakikisha inajenga mabweni, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wetu na ufaulu unaongezeka?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza pia, Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuuliza swali la nyongeza, kwa niaba ya Mheshimiwa Aisha Msantu Mduyah, ambaye anajitahidi sana kuwasemea wananchi wa Mkoa wa Dodoma, ikiwemo pia Wilaya ya Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli halmashauri zetu nyingi zina vipato vidogo, lakini utakubaliana na mimi kwamba, hizi halmashauri tumezigawa kwenye makundi kwa namna ya kupeleka fedha za maendeleo. Kuna ambazo zinatakiwa kupeleka 70%, kuna ambazo zinatakiwa kupeleka 40%, pia, kuna ambazo zinatakiwa kupeleka 20%. Kwa mantiki hiyo, tulivyokuwa tunapitisha bajeti tuliangalia Halmashauri ya Chemba inatakiwa kupeleka asilimia ngapi, ili kufanya miradi ya maendeleo ionekane. Ndipo hapo sasa ambapo pamesababisha Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kupeleka fedha hizo, shilingi milioni 30, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea tu kusema kwamba, Serikali inaendelea kutafuta fedha, ili kuweza kukamilisha maabara na miundombinu mingine yote, ambayo imeanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili la nyongeza, Mheshimiwa Ester Bulaya umeuliza suala la mabweni na umezungumzia sana kwenye Halmashauri yako ya Bunda. Hapo, umechukua advantage ya Chemba, lakini umeenda Bunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, Waheshimiwa Wabunge wote hapa wakisimama wanaulizia suala la mabweni kwa sababu, ni ukweli usiopingika kwamba, tunahitaji kuwaweka wanafunzi karibu, ili waweze kupata elimu yao kwa ukaribu na usalama zaidi. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kutafuta fedha, ili tuone namna ya kujenga mabweni, hasa kwenye zile shule ambazo ziko mbali na makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita iko tayari na inafanya kazi hii ya kutafuta fedha, ili tuweze kujenga mabweni kwenye shule zetu hizi. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Shule ya Sekondari Mswakalo ni shule pekee inayofanya vizuri ndani ya Wilaya ya Chemba na Mheshimiwa Waziri hilo unalijua, lakini watoto wetu wanashindwa kukamilisha ndoto zao. Kwa mfano, matokeo ya safari hii tuna division one na two peke yake, hatuna three wala zero, lakini watoto hawa wanashindwa kutimiza ndoto kwa kutokuwepo tu kwa hizo maabara mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mapato yetu unayajua, mnatakiwa kutuletea 70%. Hatuna uwezo wa kutenga fedha za ndani, kwa ajili ya ujenzi wa maabara au kukamilisha nguvu za wananchi. Wananchi wetu wameendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba, wanatimiza ndoto za watoto wetu, kwa ajili ya kuja kuwa viongozi wa kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Mheshimiwa Waziri, kwa ajili ya kutupatia hiyo shilingi milioni 30 nyingine ya pili, ili twende tukakamilishe majengo haya, watoto wetu waendelee kufanya vizuri na hatimaye tuweze kuandaa Taifa la kesho lenye weledi, utu, ubinadamu na uungwana wa Taifa lao, kwa ajili ya kuja kulitumikia? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Kunti Majala, Mbunge wa Chemba, kwa kuwasemea sana Wananchi wake wa Chemba. Siyo hili la Shule ya Sekondari Msakwalo tu, lakini huwa anafanya mambo mengi kuhusu maendeleo ya Wananchi wa Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la shilingi milioni 30, namhakikishia Mheshimiwa Kunti kwamba, bajeti iliyopita tuliielekeza halmashauri ile kutokana na fedha ambazo wametenga, kwa ajili ya miradi ya maendeleo kupeleka fedha ile na tumepitisha hapa Bungeni kwamba, Halmashauri ya Chemba ipeleke shilingi milioni 30. Suala la kuongeza shilingi milioni 30 nyingine, Mheshimiwa Kunti Majala nakuhakikishia kwamba, tutakapopata fedha mara moja tutaona namna ya kuzipeleka fedha hizo kwenye Shule hii ya Msakwalo, ili kukamilisha zile maabara zote mbili zilizobaki na wanafunzi wale waendelee kusoma kwa juhudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapa pongezi sana Shule ya Msakwalo kwa namna wanavyofanya vizuri kwenye masomo yao. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Shule ya Sekondari Matombo kuna mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula, bweni la wasichana, pamoja na uzio. Sasa ni mwaka wa pili mradi huo umesimama. Je, ni lini Serikali itakwenda kuendelea na mradi huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mfaume, kwa swali hili la nyongeza ambalo ameuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ni kweli tunafahamu ujenzi huo umesimama, lakini nitapeleka timu mara moja iende ikaangalie shida ya pale ilikuwa ni nini na tuone namna ya kuweza kukwamua jambo hili. Ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, ninaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kubwa ya kujenga shule katika Jimbo la Kalenga. Bahati mbaya shule zile za zamani kwa kweli, kutokana na uwezo wetu hazina maabara; zipo ambazo zina maabara moja, nyingine mbili, wakati tunahitaji maabara angalau tatu, ili kutimiza ile haja ya wanafunzi kuweza kusoma masomo yote ya sayansi. Je, ni lini Serikali itatupa bajeti, ili tuweze kujenga hizo maabara?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Kiswaga kwa kuuliza swali la nyongeza. Swali hili hakuulizia, kwa ajili ya halmashauri yake pekee ama jimbo lake pekeyake, lakini ameliuliza kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya tathmini kuona ni maabara ngapi ambazo zinatakiwa kujengwa kwenye shule zetu za sekondari nchi nzima, ili kuwawezesha wanafunzi wetu kusoma masomo ya sayansi. Tutakapopata fedha tutahakikisha kwamba, tunapeleka angalau kwa kila jimbo na kwa kila halmashauri fedha hizo, ili tuweze kujenga maabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hapa wote watakuwa mashahidi kwamba, kuanzia mwezi wa tano hadi mwezi huu wa nane tumepeleka fedha, kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hasa kwenye masuala ya madarasa na shule. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo, ili tutakapopata fedha tuweze kuzipeleka huko, kwa ajili ya ujenzi wa maabara kwenye shule zetu hizi. Ahsante.
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini bado ninapenda kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na adha kubwa wanayopitia wananchi wa Majimbo mawili ya Katoro na Busanda. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kufanya haraka sana kuwapelekea halmashauri, ili kuweza kuwanusuru na adha hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, katika Jimbo la Katoro tunalo jengo ambalo lipo tayari, kwa ajili ya halmashauri. Je, hatuoni kama linaweza kusaidia kuharakisha harakati hizo za kulipatia Jimbo la Katoro na Busanda halmashauri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, ambayo yameletwa kwa niaba ya Mheshimiwa Engineer Kija Limbu Ntemi, juu ya jambo hili. Wizara iko tayari kupokea, kujadili na kupeleka kwa uharaka maombi haya kwa mamlaka, kwa ajili ya kuridhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, kutokana na mwongozo uliotolewa mwaka 2025, Halmashauri hii ilipelekewa mwongozo ule, ili waweze kuleta kwa kuzingatia vigezo vilivyotolewa. Vigezo hivi ni idadi ya watu, ili tuweze kuanzisha halmashauri mpya ni lazima tuwe na watu wasiopungua laki tano. Kwa Katoro kwa sasa ni kweli idadi ile imezidi, tuna watu zaidi ya milioni moja, kwa hiyo kigezo hiki wamekitimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vigezo viwili vingine ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatakiwa ivitimize; cha kwanza ni ukubwa wa eneo na cha pili ni kujitegemea. Kwamba, ili halmashauri iweze kupewa kuwa halmashauri ni lazima iwe na uwezo wa kifedha wa kujitegemea usiopungua asilimia 50. Kwa leo hii Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 26 tu. Tumewapelekea mwongozo ule waweze pia kuleta, ili jambo hili tuweze kulifanyia kazi kwa uharaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza ni kuhusu uwepo wa utayari kwa kuwa na jengo ambalo lingeweza kutumika, kwa ajili ya kuanzisha halmashauri hii. Pindi watakapotimiza vigezo hivi tuna uhakika kwamba, Wizara yetu italichukua jambo hili na kulifanyia kazi kwa haraka, ili na jengo lile baadaye liweze kutumika. Ninakushukuru sana.
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi. Ninataka nipate majibu kwa Waziri. Jimbo la Ulyankulu liliahidiwa kuwa na Halmashauri yake ya Ulyankulu na ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wetu Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2010. Wananchi hawa kwa mahitaji makubwa, ikumbukwe mwaka 2010 hata uchaguzi waligoma, lakini Serikali iliahidi kuwapa halmashauri na mpaka sasa 2015 pia, iliahidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kupata majibu. Je, ni lini Halmashauri ya Ulyankulu itakubaliwa kuanza kwa sababu, tayari vigezo vyote ambavyo Waziri amevieleza na kutimiza vikao tulikwishafanya; ninataka nipate majibu ya Serikali, ni lini sasa Halmashauri ya Ulyankulu itaanzishwa, ili kujibu hoja ya wananchi hawa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mbunge wa Ulyankulu kwa kuuliza swali lake la nyongeza kuhusu ni lini Serikali itaanzisha halmashauri kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, kuna mwongozo ambao umekwishatolewa, wa mwaka 2025. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tukitoka hapa nimpatie mwongozo ule, ili aurejeshe kwenye halmashauri mama na waweze kuanza mchakato huo, ambapo unaanzia kwenye halmashauri mama, unakwenda kwenye wilaya, kwenye vikao vya DCC, unakwenda kwenye mkoa kwenye vikao vya RCC na hatimaye ile taarifa inaletwa Wizarani kwetu, ili tuweze kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge tutakapotoka hapa tuonane, ili nimpatie mwongozo ule. Nitamwambia Katibu Mkuu na timu yake wapeleke mwongozo ule kwa Mkurugenzi, ili kazi yao iweze kuanza. Ninakushukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Halmashauri ya Bunda imeanzishwa mwaka 1980, ikatoka hapo mwaka 1995 ikagawanyika kuunda Jimbo la Mwibara, ambalo tayari lina halmashauri mpya. 2015 likapatikana Jimbo la Bunda Mjini, tayari lina Halmashauri imejengwa. Majengo yaliyokuwa ni ya Halmashauri ya Bunda yako wazi na sisi leo tunatembea tunaenda Kibara, kilometa 140. Je, ni lini wataturudisha kwenye majengo yetu na kuteua Mkurugenzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Getere kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye jimbo lake. Mheshimiwa Getere jambo hili tumelijadili sana, mimi na yeye. Tuko kwenye mpango wa kuona ni namna gani sasa tunaweza kutumia majengo yale yaliyo wazi, ili wananchi wanaozunguka kutoka Bunda wapite Bunda Mjini ndipo waende kwenye jimbo la Mheshimiwa Getere waweze kupata huduma kwa ukaribu. Kwa hiyo, tutaendelea kulijadili suala hili, mimi na yeye Mheshimiwa Getere, pamoja na wataalam wetu, ili tuone ni namna gani tunaweza kutatua jambo hili. Ninakushukuru sana.
MHE. MARIRTA G. KIVUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umbali mrefu kutoka Kata ya Mfereji mpaka Hospitali ya Wilaya ya Monduli, ambapo wananchi wetu ndipo wanapopata huduma kwa sasa. Je, Serikali ina dhamira gani mahususi ya kuhakikisha fedha zinatengwa, kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Mfereji na kukamilika kwa wakati?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Marirta Gido Kivunge kwa kuwasemea Wana-Monduli.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba, Kata ya Mfereji ni moja ya kata za kimkakati. Sisi, kama Wizara, tumekaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha tukiwaomba shilingi bilioni 23, ili tuweze kujenga vituo vya afya 94 kwenye halmashauri zetu zenye kata hizi ambazo ni za kimkakati, ikiwemo Kata ya Mfereji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambapo fedha hizi zitatoka, tunawahakikishia Wana-Kata ya Mfereji kwamba, tutapeleka fedha hiyo, ili waanze kujenga kituo cha afya kwenye Kata ya Mfereji. Ninawasilisha.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni takribani mwaka mzima amezungumzia suala la kutoa fedha, kwa ajili ya kujenga vituo vya afya. Ndani ya Bunge hili kuna Wabunge waliopata fedha na kuna Wabunge hatujapata fedha hadi leo kiasi kwamba, wananchi hawatuelewi, nikiwemo mimi Kata ya Matamba, ndani ya Jimbo la Wilaya ya Makete.
Je, ni lini fedha zitatoka ili sisi Wabunge ambao hatujapata, tupate fedha hizi, ili siasa yetu majimboni iweze kutulia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru na namshukuru sana Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete, kwa kuuliza swali hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika kwamba, hizi microphones zote unazoona zimewaka sasahivi ni wale 94 ambao hawajapata fedha ile ya awamu ya kwanza tuliyopeleka kwenye Halmashauri zingine na kwenye majimbo mengine. Nakuhakikishia kwamba, mimi na Waziri wa Fedha tumekaa na tumekubaliana kwamba, flow ya fedha itakapokuwa nzuri tutapata fedha hizo, shilingi bilioni 23, ambazo tutazipeleka kwenye vituo hivi 94 mara moja, kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimuondoe shaka Mheshimiwa Festo Sanga kwamba, fedha ile itapatikana kwa sababu, ndiyo tumeanza tu mwaka; fedha hii ikipatikana tutaipeleka kwenye vituo hivyo 94, kikiwemo kituo alichokitaja. Ahsante.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali langu la nyongeza; kwa kuwa, kwenye Mkutano wa Bunge uliopita niliomba Mwongozo wa Kiti cha Spika juu ya hatma ya vituo vya kimkakati. Na kwa sababu, sasa Mheshimiwa Waziri amesema msimamo wa Serikali ni kwamba, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha wanafanya kazi kwa Pamoja, kuhakikisha fedha zinapatikana, ili kuwezesha kumalizika kwa vituo vile vyote vya kimkakati. Ninaomba kwanza niondoe sasa lile ombi langu la mwongozo kwa sababu, nimeupata vizuri kupitia kauli ya Waziri. Nawashukuru kwamba, kwenye kituo chetu nilichokiombea wakati ule, cha Nampungu, kimepelekewa fedha zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu. Mwaka 2010 Mheshimiwa Rais Magufuli, wakati wa kampeni, alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kata ya Namiungo, ambayo ina vijiji saba na ni kata kubwa sana yenye wakazi wengi...
NAIBU SPIKA: Ngoja kwanza Mheshimiwa. Mheshimiwa Ado.
MHE. ADO S. ADO: ...ninauliza swali sasa. Ni lini ahadi hii itatekelezwa?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge samahani. Umesema mwaka gani?
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Naibu Spika, 2015.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ado Shaibu, kwanza kwa kuondoa mwongozo ule ambao alikuwa ameuleta Bungeni. Hii inaonesha ni namna gani Mheshimiwa Ado amekuwa mwenye busara sana kuona kwamba, hakuna haja ya kuendelea kujadili jambo hili kwa sababu, limepata ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kata hii anayoitaja Mheshimiwa Ado ni moja ya kata ambazo zinatakiwa kupelekewa fedha, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pale. Ni kweli tunafahamu kwamba, kata ile ina vijiji saba ambavyo vinategemea kupata huduma, kama tutajenga kituo cha afya pale. Kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Ado, na ninafahamu anafahamu uchapakazi tulionao kwenye Wizara yetu, tutahakikisha tunampelekea kituo hicho cha afya pindi tutakapopata fedha. Ninakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Swali langu linahusu kituo cha afya; mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilituletea Bungeni mapendekezo ya kuchagua vipaumbele kujenga vituo vya afya vya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, ni lini vituo hivi vya afya vya kimkakati vitaanza kujengwa, ikiwa ni pamoja na kituo cha afya cha kimkakati kwenye Kata ya Ivuna, ndani ya Jimbo la Momba?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Condester Sichalwe kwa kurejea Bungeni na sote tunapaswa kumpa pongezi kwa kutuongezea kijana ndani ya Tanzania yetu, hongera sana. Hongera sana Mheshimiwa Sichalwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati kwenye kata aliyoisema nitahakikisha kwamba, wakati wowote ule tutakapopata fedha tutapeleka kwenye Jimbo la Momba, ili kituo kile kiweze kujengwa na kuhudumia wananchi wa kata ile na pia, wananchi wa Jimbo la Momba. Ninakushukuru sana.
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninaomba kurekebisha kidogo, ni Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, siyo Halmashauri ya Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira kuu ya Serikali ya kugawa jimbo na kupata Jimbo jipya la Itwangi ni pamoja na kuhakikisha inasogeza huduma kwa wananchi wake. Kata ya Didia ni miongoni mwa kata kumi zilizomo Tarafa ya Itwangi, ambapo kuna kituo cha afya kimoja tu. Je, Serikali ipo tayari sasa kutuletea fedha kuanza ujenzi kwa mwaka huu wa fedha 2026/2027?
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi mara baada ya Bunge hili, aje Jimbo la Itwangi na Kata ya Didia, ili ajionee shida kubwa tuliyonayo ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Jimbo jipya la Itwangi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunafahamu kwamba, jimbo hili lenye kata kumi lina kituo kimoja tu cha afya. Kwenye orodha ile ya vituo 94 ambavyo tunatakiwa kupeleka fedha pindi tutakapopokea kutoka Hazina, Kata ya Didia ni moja ya kata hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Azza Hillal Hamad kwamba pindi fedha hizi zitakapotoka mara moja tutahakikisha kwamba tunapeleka fedha kwenye Kata hii ya Didia ili kituo kile ambacho kinategemewa na wananchi wengi kiweze kuanza kujengwa na kutoa huduma kwa wananchi wa Kata ya Didia na wananchi wa Jimbo la Itwangi kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari baada ya Mkutano huu wa Bunge kuongozana na Mheshimiwa Azza ili niweze kwenda kuona adha iliyoko kwenye eneo lile na tuone namna ya kuongea na wananchi na kuwahakikishia kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata yetu ya Didia. Ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2008 kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru aliweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Mchichira.
Je, lini Serikali itapeleka fedha ikizingatiwa wananchi wale tayari wameanza kujenga wenyewe kituo kile cha afya? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Kaka yangu Katani kwa namna anavyofanya kazi vizuri. Ni mara nyingi tumekuwa tukijadili mambo kadha wa kadha ambayo tumeyatafutia suluhisho na yeye ni shahidi kwamba kwenye Jimbo lake tumepeleka suluhisho mara zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kituo hiki cha afya anachokisema Mheshimiwa Katani, kwa kuwa kimeanza kwa nguvu za wananchi tutapeleka timu yetu kutoka TAMISEMI ili iende ikaangalie pale ambapo wananchi wameshaweka nguvu zao imefika asilimia ngapi ili na sisi kama Serikali Kuu tuweze kutafuta fedha na kwenda kuwasaidia wananchi wa Kata ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Waziri, miaka mitatu iliyopita tulileta majina ya vituo vya mkakati, Kata ya Matui wananchi zaidi ya 30,000 na Kata ya Dongo zaidi ya 28,000. Ni lini tutapata pesa kwa ajili ya kujenga vituo vya afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Kaka yangu, Mheshimiwa Olelekaita kwa namna anavyowasemea wananchi wa Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba baada ya kikao hiki leo nikae na Kaka yangu, Mheshimiwa Mbunge, tuweze kuona wapi tumefikia na kama vituo vile vipo kwenye orodha ya vile vituo 94 na kama havipo kwenye orodha tuone namna ambavyo tutalishughulikia jambo hili ili wananchi waweze kupata huduma. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ng'ambo iliyopo katika Jimbo la Tabora Mjini ina wakazi 17,826, haina kituo cha afya wala zahanati. Wakazi hawa wanakimbilia Hospitali ya Mkoa ya Kitete kwenda kupata huduma za afya na eneo tunalo. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanatupelekea fedha ili wananchi wangu waweze kupata huduma za afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza sana Dada yangu Mheshimiwa Hawa, kwa namna anavyofanya kazi, yeye ni shahidi kwamba mimi nilifika jimboni kwake na tulifanya kazi kubwa kwenye Hospitali ya Kitete lakini vilevile kwenye kituo kimojawapo cha afya ambacho kinaendelea kumaliziwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitahakikisha kwamba tunawapeleka timu tukaangalie eneo lile na kuona namna tutakavyolitafutia fedha kama halipo kwenye vituo hivi 94 basi tuone ni namna gani tunavyoweza kuongea na wafadhili tuweze kupata fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kwenye eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.