Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Neema Peter Majule (5 total)

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuongea tena mara ya pili katika siku ya leo. Nimefurahi sana kuongea leo ili nami pia niweze kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Siyo hivyo tu, kumpongeza kwa birthday yake leo na kweli hata kama hatupo huko, lakini tumemtakia birthday njema siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninampongeza sana Mheshimiwa Spika na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitoe shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuingia Bungeni, nafasi ambayo niliipambania kwa miaka 10 bila kupata, lakini sasa nimefanikiwa kuingia Bungeni. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru wanawake wa Dodoma kwa kuweza kuniamini na kunipa kura nyingi sana. Kati ya kura 1,581 niliweza kupata kura 1,524. Kwa hiyo, ninawashukuru sana wanawake wa Dodoma, wameniamini sana na mimi nitawawakilisha vyema Bungeni. Siyo hivyo tu, nitafanya utumishi uliotukuka kuweza kuwatumikia wanawake wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani sana kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, niliiona ni hotuba ya kiongozi tena iliyo thabiti kabisa, kiongozi mwenye madaraka, lakini upande wa pili ili-sound kama hotuba ya mama tena mama mlezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongee maeneo machache ambayo ninamsikia Rais wangu akiongea kama mama. Pale alipoingia tu na kuanza hotuba yake kwa kuonyesha masikitiko yake kwa matukio yaliyotokea Oktoba 29, hiyo ilikuwa ni sauti ya mama. Pia, alipoendelea kuwasamehe wale vijana ambao waliingia kwenye mkumbo hiyo pia ilikuwa ni sauti ya mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, aliongea sasa kama mama, akasema, nikimaliza nafasi yangu sipendi kusemwa kwa majengo, miundombinu, barabara, maghorofa, lakini niache tabasamu kwa Watanzania. Hiyo niliona ni sauti ya mama ndani ya hotuba ya Rais wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ilikuwa ni dira yetu ya miaka mitano ambayo tutaifuata na inaenda sambamba kabisa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Niliona Rais ame-summarize Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye hotuba fupi aliyoitoa kwenye Bunge lako Tukufu hiyo tarehe 14, Novemba, 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite kwenye hotuba hiyo na mawazo yangu niyatoe kwenye uchumi na uwekezaji wa wananchi. Amesema: “malengo yetu ya kiuchumi ni kupandisha kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka 5.6% hadi zaidi ya 7%.” Kwa hiyo, alikuwa na maana kwamba economic growth yetu itaenda zaidi ya 7%. Pia, akasema kwamba itaongeza ukuaji wa huduma za kijamii ambazo ni muhimu sana, hata tuzo nyingi amepata kwa ajili ya huduma za kijamii, kujenga hospitali, kujenga zahanati mpaka vijijini, kujenga vituo vya afya na kujenga hospitali za rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu hahitaji kutoka mkoa kwenda mkoa mwingine tayari hospitali za rufaa zimejengwa kwenye kila mkoa na hapo moja kwa moja ameokoa maisha ya mwanamke na mtoto. Hivyo, wanawake tumerefushiwa maisha yetu, hatufi mara nyingi kwa kujifungua au kwa njia ya uzazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu mwanamke amejipambanua kwa kutujengea vituo vya afya na zahanati kuanzia chini vijijini, kwenye tarafa zetu, kwenye wilaya zetu na hospitali za rufaa zipo kwenye kila mikoa yetu. Hivyo, kongole nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, amejikita katika kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi. Hapo ndiyo tunaona barabara, madaraja yanajengwa, anafanya uwekezaji rafiki ili tuweze kufanya maendeleo ya kiuchumi. Nami ninampongeza tena Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. Pia, anasema ataimarisha masoko na mitaji na kuhamasisha uwekezaji wa ndani, anatia moyo Watanzania kuwa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa tunafikiri wawekezaji ni wazungu. Mzungu akija ndio anatetemekewa kuwekeza, lakini sasa hivi tunatiwa moyo wawekezaji wa ndani kuwekeza kwenye viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Ana kitengo maalumu cha kuwatia moyo wawekezaji wa ndani, lakini akigusa moja kwa moja, ni kutia moyo shughuli zetu za madini, na pia kuwawezesha au kuwadhamini mikopo hao wawekezaji wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme tu ukweli tumaini hili ni kubwa sana kwa wanawake na vijana pamoja na watu wa makundi maalum kwa sababu zile 10% za kila halmashauri bado zinaendelea. Alipotamka hivi tu, nafikiri wanawake na vijana wote tulifurahi. Hilo ni tumaini kubwa sana kwa wanawake wa Kitanzania kwamba tutaendelea kupata hizo 10% za mikopo, na bado ataendelea pia kufanya mifuko yote ya uwekezaji iliyo chini ya ofisi yake ya kiuchumi, yapata mifuko 74, nayo pia itaendelea kuwasaidia wanawake, vijana na makundi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Dodoma sisi tumenufaika sana na hizi 10%. Kwa miaka minne tu wanawake wamepokea shilingi bilioni 1.6, kwa Dodoma Mjini peke yake. Siyo hivyo tu, tumeendelea kunufaika na mifuko kama TASAF na tumeenda kunufaika na mifumo mingine kama Women Development Funds. Kwa hiyo, sisi tunaendelea kunufaika na mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutuwazia vizuri wanawake, vijana pamoja na makundi maalum kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ni hilo tumaini sasa la shilingi bilioni 200 ambazo nazo pia zinaenda kwa wajasiriamali wote, lakini wanufaika wakubwa watakuwa ni hao hao wanawake, vijana na makundi maalum pamoja na wazee wameongezwa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza sana hotuba hii, ina mashiko. Tunawaomba tu watendaji kwenye Wizara mbalimbali na sekta mbalimbali watumie vizuri maneno haya yaliyowekwa kwenye hii hotuba ili wanufaika wawe watu wote ikiwepo wanawake wote hasa wa vijijini. Tukiwa kwenye kampeni, tulipokwenda vijijini, wanawake wengine hawajawahi kusikia na kupata hii mikopo. Hivyo basi, yatengenezwe mazingira rafiki ambayo mikopo hii itaweza kuwafikia wanawake waliopo vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, elimu hiyo ya fedha ambayo tuliongea hata asubuhi iendelee kutolewa mpaka kule vijijini ili wanawake, vijana na makundi haya maalum yaweze kupata elimu ya fedha ili sasa waweze kurasimiwa biashara zao na waweze kukopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono sana hotuba ya Rais wangu mpendwa kabisa. Mungu ambariki, ampe maisha mema na leo ni birthday yake, tunamhitaji akiwa na afya njema aendelee kufanya majukumu yake, ahsante sana. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi na nimefurahi sana kumfuata kijana kuongea, maana kijana amejikita kwenye mambo ya vijana mpaka wote tumefurahi na hii ndiyo sura ya Bunge lako lina wawakilishi wa kila sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya kutusaidia na kutuwezesha kutupa Mawaziri pamoja na Manaibu Waziri ambao wamekaa kwenye Wizara hizi na hata kuweza sasa kutoka na Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka 25. Moja kwa moja niipongeze Wizara ya Mipango na niipongeze Wizara ya Fedha: Mpango uliopita wa miaka mitano ulikuwa mzuri umetusogeza mpaka tulipo na kweli maendeleo makubwa yamefanyika nchi za Kiafrika zinashangaa, dunia pia nayo inashangaa kwa maendeleo makubwa ambayo Tanzania imeweza kupiga kwa miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumepata Mpango mwingine ambao kama wanavyosema wenzangu na walivyounga mkono ya kwamba Mpango huu ni wa Kisayansi na Kiteknolojia: Mpango ambao unaweza kutupaisha tukaenda mahali pazuri zaidi, lakini tuna Mpango huu wa muda mrefu sasa wa miaka 25 na huu Mpango wa miaka mitano, halafu tumepewa Mpango wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchambuzi wangu mimi nataka kuchangia nafasi sasa ya mwanamke katika Mpango huu. Nimeupitia Mpango na kuweza kuona nafasi ya mwanamke, Wabunge wengi wamechangia mambo mbalimbali na wamegusa kwa namna moja au nyingine mambo ya wanawake katika Mpango huu. Hata hivyo, ninataka niseme kwamba, wanawake tumepaishwa zaidi kipindi hiki cha kuwa na Rais, Mwanamke Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mpango huu ambao tumeletewa wa miaka 25, pia wanawake wamepewa nafasi kubwa sana. Lakini niseme tu kwa nini nimekuwa na interest hiyo, kwanza, kwa sababu mimi zaidi ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, mimi pia ni Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake idadi yetu sisi ni 51% population ambayo tumehesabiwa mwaka jana 2025, lakini pia ndiyo wazalishaji wakubwa na ndio wanaoweza kuupeleka uchumi huu kutoka hatua hii kwenda hatua nyingine. Kwa sababu wanawake wamejikita zaidi kwenye kilimo, asilimia kubwa ya wakulima ni wanawake na pato la Taifa ambalo linachangia ni 54%, ambao watendaji wakubwa kwenye field ni wanawake. Hivyo basi, hatuwezi kutenga maendeleo makubwa ambayo tunayatarajia pasipo kuwahusisha na kuwaongelea wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wanawake wamejikita kwenye biashara ndogondogo ikiwepo biashara za kati (SME), kwa hiyo ni wanawake ndiyo waliofanya. Wanawake pia wamejikita kwenye kazi za huduma za jamii, hivyo basi niseme kwamba, Mpango huu ambao tunao, tutaenda vizuri tukiwa kwenye usawa wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipendekeze moja kwa moja nisije baadaye mwishoni nikashindwa vitu vya kupendekeza. Niseme basi Mpango huu kama tutaweza kuenenda ukiwa na mlengo wa usawa wa kijinsia viwekwe moja kwa moja viashiria mahususi vya kijinsia katika Mpango mzima, lakini pia kwenye bajeti, yaani kuwe na indicators ambazo ni mahususi kabisa za kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, ushiriki mzima wa wanawake kuanzia kwenye Mpango, lakini pia kwenye ufuatiliaji kwa maana ya monitoring, lakini pia kwenye tathmini. Kuwepo na ushiriki wa wanawake kwenye stage zote hizo kuanzia kwenye mipango; kwenye utekelezaji mpaka kwenye tathmini. Tukienda kwa pamoja hivyo, ninaamini kwamba tunaenda kufikia haya malengo vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niseme kwamba, uchumi jumuishi ambao tumeamua kwenda nao kwa sasa hivi utaenda kuinua mapato yetu ya Taifa mpaka dola za Kimarekani trilioni moja, lakini pia pato la mtu mmoja mmoja linaenda kwenye dola za Kimarekani 7,000 ifikapo 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yatatokea tu kama tutaongeza fursa za ajira kwa wanawake: wanawake ndiyo ambao ni wazalishaji, lakini siyo hivyo, tutaweza kujikwamua tu kwa kupunguza umaskini kuanzia ngazi ya kaya au kuanzia ngazi ya familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini ukiuongea kati ya mwanamke na mwanaume aliye masikini zaidi ni mwanamke kwa sababu ya mila zetu na desturi ya kwamba kwenye ngazi ya kaya mmiliki wa mali ni mwanaume na utaweza kuona haya mara mwanaume anapoondoka duniani yule mwanamke hawezi kuruhusiwa kumiliki ardhi aliyonayo pale inachukuliwa na familia ya mwanaume. Kule alipotoka kwenye familia yake hajapewa ardhi, huku alipoolewa nako hapewi ardhi, hivyo umaskini wa mwanamke ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kwenda kwa pamoja basi tulenge kuzikwamua kaya ambazo mara nyingi zinakuwa headed au zinakuwa zinaongozwa na wanawake, huko ndiko ulipo umaskini. Kama tutakuwa na Mpango mzuri wa kuwakwamua wanawake kwenye ngazi ya familia, moja kwa moja tutakuwa tumefanikiwa kulikwamua Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mambo ya elimu; kama tutaweza kutoa elimu kwa wasichana vizuri kabisa, tunawapanua wasichana uwezo kama unavyoona Mheshimiwa Magreth ame-present pale, uwezo wake umepanuka, msichana huyu amepewa elimu. Hivyo basi tunaweza kumkwamua, tunaweza kuwakwamua wanawake kuanzia kuwapa elimu ya kutosha kuanzia wakiwa wadogo. Mpango huu umeonesha tunaongeza idadi ya shule za sekondari na ushiriki wa wasichana kwenye elimu ya sekondari na tunaongeza pia hata teacher-student ratio kutoka 105 kwa Mwalimu kwenda wanafunzi 40 kwa Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo itasaidia kuongeza fursa ya elimu kwa wasichana na tutawaongezea wasichana sasa uwezo wa kushiriki kwenye biashara za ushindani. Siyo hivyo tu, tunapoenda kuangalia mambo haya moja kwa moja tunapoongelea mwanamke tunaongea juu ya mwanamke na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumefanikiwa sana kupunguza vifo vya wanawake na Watoto wachanga. Mpaka sasa hivi ni vizazi 104 tu katika 1,000 wanawake wanaopoteza maisha. Mpango huu unaenda kupunguza vifo hivi mpaka vizazi 85 tu kati ya vizazi 1,000, lakini inapunguza vifo vya watoto kuanzia 33 hadi 27. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa nini sasa? Ni kuzidi kuwekeza zaidi katika sekta ya afya ili tuendelee kuboresha maisha ya wanawake na Watoto, lakini siyo hivyo huduma za dispensary zinapoanzishwa na vituo vya afya zilenge kuwapa ajira nyingi zaidi wanawake kwa maana ndiyo watoa huduma za kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutaweza kufaulu sana kuwanufaisha wanawake kwenye huu Mpango wetu wa miaka 25, lakini Mpango wetu wa miaka mitano ambao moja kwa moja umejikita kupunguza umaskini. Pia tutaweza kufanikiwa kwa huu Mpango wetu wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe mapendekezo yangu, zaidi ya kuongeza indicators kwenye kila Mpango na pia na bajeti, lakini pia fedha za mikopo za wanawake ziongezwe kwenye bajeti, ambayo itatengwa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Tunashukuru sana kwa mchango mzuri. Muda umekwisha malizia sentensi ya mwisho.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii ya kuchangia jioni. Nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu ambaye amefanya mambo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka kwa issue hii ya maji ni ajenda kabisa ya Rais wetu. Toka alipokuwa Makamu wa Rais, ajenda ya kila mwanamke ni ajenda ya Rais. Akiwa Makamu wa Rais amehakikisha alipambana na kupunguza vifo vya mwanamke na mtoto, akijipambanua kabisa kwamba yeye ni mwanamke. Pia amebeba ajenda hii ya maji kumtua ndoo mwanamke kichwani, lakini amebeba ajenda nyingine sasa hivi ya kumtua mwanamke kuni kichwani. Moja kwa moja ajenda yote ya mwanamke inakuwa ajenda ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kongole nyingi sana ninampatia Rais wetu kwa kazi kubwa na kutuangalia sisi wanawake kwa jicho la tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana pia Mheshimiwa Jumaa Aweso. Nami ninasema ni Waziri wangu, akiwa Waziri hivi hivi aliniteua kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA. Kwa hiyo, nimefanya naye kazi kwa karibu sana. Ninafahamu uwezo wake mkubwa wa kuchapa kazi. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, ninampongeza Naibu Waziri, ninampongeza Katibu Mkuu, sasa hivi mwanamke Mwajuma, anafanya kazi nzuri sana katika Wizara hii ya Maji. Tuna imani kubwa sisi wanawake wa Tanzania nzima ambao ndiyo tunatuliwa huu mzigo wa maji kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo niseme tu kwamba, Jiji letu la Dodoma linakuwa kwa kasi sana. Asilimia tano ya ukuaji wa miji hii mikubwa ambayo ndiyo inafanya hata kama production inaongezeka, hatuwezi kuona kwa kasi hivyo kutokana na ukuaji wa miji hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamtia moyo mwanangu Mheshimiwa Jumaa Aweso. Aendelee kukazana tu kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji. Dodoma water table ipo karibu sana. Hivyo wataalam waendelee kufanya geological survey waone kila maji yalipo yaweze kutoka kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme kwamba, Hayati Julius Kambarage Nyerere toka mwanzo alikuwa na nia ya kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Dodoma. Alisema atachimba mfereji mrefu kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma. Azma hiyo amekuja kuitimiza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kutimiza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wetu, maji ya Ziwa Victoria Dodoma tunayatarajia kwa matarajio yote na ambaye utatekeleza haya ni wewe. Kwa hiyo, sisi tunaona kwamba uandike historia kwenye uongozi wako wa Uwaziri; sasa maji haya yasiwepo kwenye makaratasi tena, yaje Dodoma. Kwa hiyo, kwenye kipindi hiki bajeti hii itakayopitishwa, anza moja kwa moja mkakati wa kuyaleta maji Dodoma. Nina imani kubwa ya kwamba utafanya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie mambo machache tu kwa ajili ya Wizara yetu ya Maji. Kwanza kabisa tufanye huo utafiti. Kitengo cha utafiti kiwe kikubwa kwa ajili ya kutafiti tunatafiti miamba yetu tunaangalia maji yalipo. Katika utafiti huu wataalam wetu waangalie pia mabadiliko ya tabianchi. Tunasema tunatoa maji kwenye maziwa yetu na mito yetu, lakini wafanye ulinganifu na mabadiliko ya tabianchi. Tusijekuwa tunachukua maji, tunapata maji, lakini tunaharibu pia mazingira yetu ambayo sisi wanadamu tunapaswa kuishi hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ambalo ushauri wangu uelekee kwenye maintenance, yaani kwa ajili ya kutengeneza miundombinu iliyochakaa. Upotevu wa maji bado upo 30% mpaka 35%, lakini tukijitahidi tukafika kile kiwango cha Kimataifa cha 25% kwa kufanya ukarabati wa miundombinu. Ninataka niseme pia kwamba, siyo ukarabati peke yake. Sisi hapa Dodoma tuna SAWA Group. Hawa ni vijana ambao kila siku wanaangalia maji yanavuja wapi na kutoa taarifa na tunafanya maintenance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninampongeza sana Mkurugenzi wangu pia Aron Joseph, anafanya kazi nzuri ya kuzuia upotevu wa maji. Ninaiomba Wizara itenge emergence funds na pia itenge maintenance funds. Huku tunaongeza production huku tunafanya maintenance, lakini pia tunazuia upotevu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ambalo ninapenda kushauri Mheshimiwa Waziri, ninaomba kushauri kuhusu prepaid meters; kwa kweli prepaid meters peke yake ndiyo suluhisho la jambo hili. Samahani ninamalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, prepaid meters tungekuwa kama TANESCO, kwa hiyo hatutapata mambo ya ubambikizaji wa bills na vilevile the same time tutaweza ku-maximize profit ya mauzo yetu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami ya kuchangia hotuba, mpango, na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu sana kunifikisha siku ya leo na hata kunipa ujasiri na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia mchango kwenye mpango huu na bajeti hii mahususi ambayo ni kama jumuishi tu ya wizara nyingi ambazo zinafanya chini ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kabisa ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana ambayo Rais amefanya. Kwa kweli tunasema kutoka kwenye dhati ya mioyo yetu ya kwamba amefanya kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka kabisa alipoanza tu Urais, alihutubia wanawake wa Tanzania nzima kupitia wanawake wa Dodoma, akasema; “Jukumu hili ambalo nimepewa, tumepewa sisi wanawake wote. Hivyo basi twendeni tukafanye kazi kwa bidii, tuthibitishe uwezo wetu kwamba wanawake tunaweza.” Kweli kabisa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kabisa na chenji imebaki. Shukrani nyingi nampa na kumpongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine za pili, basi ziende kwa Waziri Mkuu. Waziri wetu Mkuu toka alipoteuliwa amefanya kazi nzuri na hasa hapa juzi juzi ambavyo amepita kwenye ziara zake za kila halmashauri akisikiliza kero, na kubaini kero kwenye halmashauri mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona watu wengi, makundi ya watu yakijitokeza wenye matatizo, kweli ametoa msimamo sasa kwa watendaji wote wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa haki. Yeye kama Msimamizi Mkuu wa Serikali, ametoa dira kwa wafanyakazi wengine wa Serikali kuendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani nyingine nazipeleka kwa Mawaziri wote na Naibu Mawaziri, wamefanya kazi kubwa kwa siku hizi 100 za utendaji wa Rais kwa awamu hii ya pili ambayo amefanya. Tumewaona, mimi Kamati yangu ya Utawala, Katiba na Sheria, tumezunguka na Mheshimiwa Ridhiwani kwenye ziara tulikuwa pamoja kila mahali. Kongole nyingi sana kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize shukrani kwa Mwenyekiti wangu wa UWT wa Taifa, Mheshimiwa Mama Mary Pius Chatanda, ni Mbunge mwenzetu, lakini kwa kweli imetufurahisha sana Mbunge huyu kuwa miongoni mwetu sisi wanawake. Tumejisikia faraja kuwa na mwenyekiti wetu mahali hapa. Hivyo, inaonekana tuna nafasi kubwa wanawake kufanya maendeleo kwa niaba ya wanawake wenzetu Tanzania nzima kwa kuwa na mwenyekiti wetu hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, ninaomba sasa nitoe hoja zangu kupitia hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tumefurahishwa sana, kama nilivyosema, na utendaji kwa miaka hii minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, madarasa mengi yamejengwa, na shule zimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka takwimu zimetolewa hapa karibu madarasa 78,000 yamejengwa, lakini shule nyingi sana. Watoto wetu walisoma kwenye shule mbovu sana, lakini sasa tuna shule za kisasa mpaka vijijini. Hii ni fahari kubwa sana kwa nchi yetu ya Tanzania hasa kwenye sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo na kwenye sekta ya afya, Rais amefanya na Serikali imefanya vizuri sana. Zahanati mpaka vijijini kabisa, lakini vituo vya afya, siyo hivyo tu, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa, hospitali za rufaa, vifaa kwenye mahospitali yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi kwa Serikali yangu kwa kazi kubwa sana ambayo imefanyika. Mpango huu ambao umewakilishwa mahali hapa, tunaenda kufikia level nyingine Watanzania wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye uchumi wa kati, sasa tunaenda kwenye uchumi wa kati lakini wa juu. Kwa maana tunaenda kupanda kwa kutoa mipango mikubwa ambayo imepangwa kama itatekelezwa na kufuata kama tulivyopanga. Niseme tu kwamba, tunaweza kwenda kwa pamoja hivyo, sambamba na maendeleo yote pamoja na miundombinu, pamoja na huduma za kijamii ikiwemo hizo huduma za elimu, huduma za afya na miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaenda vizuri zaidi tukienda na huu uchumi shirikishi ambao tunashirikisha wanaume na wanawake kwenye maendeleo twende pamoja. Siyo hivyo tu, lakini tunaposema kwamba uchumi jumuishi, ni sekta zote zishirikiane kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni maji, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni elimu, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni afya, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni kilimo ambacho ndiyo tunategemea Tanzania nzima, uchumi wetu utakuzwa na kilimo kwa 85%. Hata hivyo, sekta binafsi hatuwezi kuisahau ambako tunategemea katika Dira yetu ya 2025 mpaka 2050, private sector wana-contribute 75%. Huo ndio utakuwa uchumi shirikishi maana tunaenda wote kwa pamoja bila kuachana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema hivyo, ninamlenga mwanamke. Sasa mwanamke lazima ashirikishwe kuanzia ngazi ya kupanga, kwenye utekelezaji, na pia ashirikishwe kwenye tathmini. Tukimwacha nyuma mwanamke, maendeleo hayataenda. Kwa hiyo, twende pamoja na wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, contribution ya mwanamke katika maendeleo haya ni 80%, na ukimwendeleza mwanamke, moja kwa moja umeendeleza familia na moja kwa moja umeendeleza jamii. Hivyo basi, mipango yetu na bajeti yetu imhusishe mwanamke moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite katika kile kipengele cha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Kuna mipango mingi imepangwa na ikiwemo hizi 10% za halmashauri. Ndugu zangu ni kitu ambacho kimekuwa faraja sana kwa wanawake, kama ukisikia michango mingi ya Wabunge, kila mtu amegusia kuhusu 10%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu hiki ni mtaji, wanawake wanahitaji mitaji kwa ajili ya biashara zao, kwa ajili ya miradi. Hivyo basi, Serikali i-pay attention na kitu hiki, na kukiangalia, na kukifuatilia kwa karibu sana ili kuona kama kweli kuna ugawaji sawa wa hizi 10%, na kuna ufuatiliaji wa karibu ili wale watendaji wanaokiuka kitu hiki, basi waweze kuchukuliwa hatua ili hao wanawake wapokee hiyo faraja yao ya 10%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna hizo shilingi bilioni 200 ambazo zimetengwa kwa ajili ya wajasiriamali ambazo zimewekwa benki. Hata hii pia ni faraja kubwa sana kwa wanawake. Uwekwe utaratibu mzuri wa kuhakikisha walengwa wanafikiwa na hii hela ili wanawake waweze kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ukweli, mchango mkubwa ambao sisi wanawake tunataka katika Serikali yetu, la kwanza kabisa, wanawake wanahitaji hiyo mitaji. Hili ni hitaji la kwanza la wanawake. Pili, wanawake wanahitaji masoko. Wauze wapi biashara zao? Wanawake wafundishwe tu, wanaweza. Ukimfundisha mwanamke jinsi masoko yanavyopatikana au namna hata ya kusafirisha bidhaa nchi za nje, wanawake wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kuwe na link ya utengenezaji wa bidhaa na usafirishaji wa bidhaa, au kuwe na link ya utengenezaji bidhaa na masoko ili wanawake wakitengeneza bidhaa zao ziwe na ubora, lakini pia zipate masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ambalo wanawake wanahitaji, ni elimu. Elimu inayotakiwa ni elimu ya fedha, elimu ya ujasiriamali. Pia wanawake wapewe skills ndogo ndogo tu, jinsi ya kuwa na wazo la biashara na namna ya ku-develop wazo la biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wafundishwe hata skills ndogo za kuandika business plan. Mwanamke ajifunze vitu hivyo ili ajue ya kwamba mradi wake ambao anaenda kuufanya utakuwa na faida au hauna faida? Hapo ndipo mwanamke apewe mkopo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Ninaomba nimalizie kwa kusema kwamba wanawake watapata faraja kubwa sana wakipata hii mikopo na kama shida ni dhamana, ufunguliwe mfuko wa dhamana ambao utawasaidia wanawake na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi hii ya kufika mahali hapa na pia ninaomba niweze kuipongeza sana Wizara hii ya Katiba na Sheria kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. Ni chombo ambacho tunakitegema Watanzania wote cha kutunza haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Juma na pia nimpongeze Naibu Waziri mwanangu Zainab kwa kazi kubwa anazofanya. Ninampongeza Katibu Mkuu; ninawapongeza watendaji wote wa vitengo vyote vya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, tulifanikiwa kutembelea hata miradi ambayo wanaifanya, ni kazi nzuri sana ambayo imefanyika. Hivyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea sana, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli ameongoza nchi hii kwa kufuata Katiba na sheria, ndiyo maana tuna hii amani na utulivu. Si hivyo tu, ameiwezesha Wizara hii kufanya kazi yake kwa kuruhusu hela za kutosha kwenda kwenye Wizara hii. Kongole nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ya kwamba chombo hiki sasa ni chombo ambacho sisi Watanzania wote tunakitegemea kwa ajili ya haki hasa tunapoongelea habari ya Mahakama. Hivyo, tuna matarajio makubwa, Watanzania wana matarajio makubwa ndiyo maana Wabunge hapo wakisimama wanasema juu ya sheria mbalimbali ambazo zinabidi zibadilike ili ziweze kwenda sawa na wakati huu tulionao. Ninaamini kwamba Waziri Juma atakuwa anasikia jambo hili na atakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Wizara hii ya Katiba na Sheria imefanya jambo zuri sana hasa ile Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ambayo imesaidia Watanzania wengi. Tumeona wamewafikia karibu Watanzania milioni 7.4, lakini wanaume wakiwa milioni 3.6 na wanawake wakiwa milioni 3.8. Ina maana Watanzania wengi wamenufaika na hii kampeni. Niombe tu kwamba iendelee, imekuwa faraja kubwa. Watu walikuwa na matatizo, lakini hawana fedha za kulipia mambo ya sheria. Sasa tuna huduma ya Miswada ya Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu na sisi UWT tuna Kamati ambayo pia ina wanasheria wabobezi ambao pia wanasaidia wanawake katika mambo haya ya msaada wa kisheria. Tume-copy na ku-paste, lakini inasaidia. Kwa hiyo, moja kwa moja tunaunga mkono jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo labda inabidi sasa tuweze kuona ambayo yanaweza yakakinzana kidogo na huu msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, mambo ya rushwa bado yapo ambayo yanaweza yakawa yanasumbua katika suala hili nayo tuyaangalie tuweze kudhibiti jinsi tunavyoweza.


Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu kuna gharama zingine ambazo mtu ambaye amepewa msaada wa kisheria, gharama kama za usafiri na accommodation. Yaani gharama nyingine ambazo zinaweza zikawa mzigo kwa mtu japokuwa amepewa msaada wa kisheria, lakini bado gharama zingine ambata zikawa kikwazo kwake. Wizara pia ipanue, inaweza kuwa hata na Mfuko tu maalum kwa ajili ya kuwasaidia hao watu ambao wanawapatia msaada wa kisheria, lakini pia wapate na misaada mingine ya kujikimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ucheleweshwaji wa kesi. Kesi zikiwa za muda mrefu sana, mtu anahangaika hata kama ana msaada, anahangaika hizo gharama, anasubiri kesi ni ya muda mrefu, inamaliza mwaka na inaanza mwaka mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema watu wanakata tamaa njiani kabla hawajapata hiyo haki yao, hata kama wana msaada wa kisheria. Hivyo, kesi ziwe zina muda mfupi, ziweze kumaliza kwa wakati ili huyu sasa aweze kufaidi huo msaada wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mambo ya ubambikizwaji wa kesi. Kuna kesi zingine zinabambikizwa, watu wanalalamikia mambo kama haya. Hivyo basi, Wizara au Mahakama pia iweze kuona vitu kama hivyo. Yaani kweli unasikiliza, unasema kweli hivi huyu mtu anaweza akafanya hivi? Unatumia na vyanzo vingine, hata vyanzo vya kisaikolojia kwamba kitu hiki ninafikiri huyu mtu…; kwa hiyo, yapo mazingira ambayo yanaweza kuonesha kuwa huyu mtu amebambikizwa kesi ili pia tuweze kuwa sasa na huduma nzuri ya msaada wa kisheria, lakini haya mambo mengine manne ni muhimu pia kuyaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninaomba kuchangia ni mambo ya RITA. Kwa kweli RITA ni chombo muhimu ambacho kinatupa sisi vyeti vya kuzaliwa na vifo, lakini kuna shida kwenye RITA. RITA inabidi sasa hivi nayo ijirekebishe ili iweze kuwasaidia watu. Wanafunzi, mtu amefiwa na wazazi wote anaambiwa ukalete cheti cha kifo.


Mheshimiwa Mwenyekiti, muda mrefu anapokwenda kutumia kutafuta cheti cha kifo cha wazazi wake, kwanza ana machungu yeye kuwa yatima, RITA iwe na kitu angalu kirafiki angalau cha kuweza kutoa huduma haraka kwa watu ambao wana maumivu. Pamoja na wajane, amefiwa na mume huku anaenda kutafuta mambo ya cheti, pia ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu RITA inabidi pia ibadilishe mambo. Zaidi ya kutumia zile kanuni walizonazo RITA iwaangalie...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako. Muda wako umekwisha.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaomba kuunga hoja mkono. (Makofi)