Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Leonard Douglas Akwilapo (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kudra zake na tumesimama hapa leo kuongea mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Vilevile, ninaomba nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kutoa hoja yoyote na kuchangia, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa nafasi zake mbili, kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na pili kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiwa kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi alijipa heshima kubwa ya kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kinyang’anyiro hicho ninapenda kuwashukuru sana sana wananchi wa Jimbo langu la Masasi Mjini, ambao walikipa Chama Cha Mapinduzi ushindi mkubwa sana wa kiti cha urais, kiti cha Mbunge na vilevile viti vyote vya Madiwani katika Jimbo letu la Masasi Mjini.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine vilevile, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa kwangu kwa kunipa jukumu la kuiongoza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ambayo inagusa hisia za kila Mtanzania kwa wakati huu. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba nitajitahidi kufanya kazi hizi kwa juhudi zote, kwa weledi wote na kumwomba Mwenyezi Mungu anisaidie ili niweze kutekeleza majukumu yale ambayo yanalengwa kwa Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, ninapenda sasa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri, ambayo imegusa maeneo mengi ya utekelezaji wa Serikali. Kwa upande wa Wizara yetu ya Ardhi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza masuala ambayo ni muhimu katika usimamizi wa sekta ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni usimamizi wa upangaji na upimaji wa ardhi. Wote wanaelewa kwamba hili ndilo suluhu katika kuweka mipango ya ardhi iwe sawia ili kusiwe na migongano wala migogoro. Kwa hiyo, tumeshalichukua hilo na pia lipo katika mipango yetu ya kiwizara. Vilevile amezungumzia kuhusu uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA. Suala lingine aliongelea maboresho ya huduma za uthamini na ulipaji wa fidia, kuna utatuzi wa migogoro ya ardhi, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na uboreshaji wa miundombinu ya upimaji na ramani.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge lako hili ninaahidi kwamba, Wizara itazingatia maelekezo haya yote yaliyotolewa katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuongeza tija, uwazi na kasi ya utoaji wa huduma za ardhi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na masuala ya ardhi yaliyoainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, zipo hoja mbalimbali ambazo ziliibuliwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakiwa wanachangia hotuba hii ya mjadala. Takribani ya Waheshimiwa Wabunge 10 tumewasikia wakiwa wanatoa hoja mbalimbali ambazo zinahusiana na mambo ya ardhi. Wametoa maoni na ushauri kuhusu hoja mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, moja kati ya mambo ambayo wameyazungumza Waheshimiwa Wabunge ni kuweka utaratibu madhubuti wa kutatua na kudhibiti migogoro na hususan ile inayohusu wakulima na wafugaji. Suala lingine walilolizungumzia ni kuhusu kuongeza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi za vijiji, kwa kuamini kwamba mambo mengi sasa hivi yanatendeka huko vijijini kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kurahisisha taratibu za upatikanaji wa hati miliki za ardhi. Jambo la nne ambalo wamelizungumza Waheshimiwa Wabunge wengi ni kuwezesha upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi hii ya ardhi ambayo inazungumzwa pande zote za nchi; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba alitoa maelekezo kwa Wizara nne, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI; na Wizara ya Maliasili na Utalii; tukishirikiana pia na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa kwako kwamba tumeshaanza vikao vya maafisa ambao watajadili na kuchakata na kutoa maoni juu ya namna bora ya kusimamia ardhi ili kuondoa migogoro. Baada ya hapo watafika katika ngazi ya Waheshimiwa Mawaziri na baadaye tutatoa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ametoa maelekezo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaendelea na mikakati yetu ya ndani ya kila siku ya kusimamia mambo yote yanayohusu ardhi. Kama tunavyofahamu, wizara inafanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuendesha kliniki za ardhi ambazo ya mwisho kabisa tutaikumbuka kabisa ilikuwa inaitwa Samia Ardhi Kliniki ambayo ilikutana na watu takribani 13,000 wenye matatizo mbalimbali ya ardhi. Takribani 8,000 walisikilizwa na kutatuliwa matatizo yao. Tutaendelea na kliniki hizi kwa sababu ni moja kati ya mikakati ambayo imeonesha ufanisi mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi. Kwanza kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Kuna mambo mengine ni kuhusu tu sheria, watu wanajua kwamba ardhi hii inamilikiwa na mtu Fulani, lakini wanaingia. Hiyo ni kutengeneza migogoro. Kwa hiyo, tutazidi kutoa elimu kwa wananchi wajue kwamba si vizuri kuingia katika eneo ambalo si lako na kuanza kuliendeleza.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna migogoro mingi ambayo inatokana na vitendo hivyo vya wananchi wetu; wanaingia mpaka katika ardhi ambazo ni mali ya taasisi, tena za Serikali. Kule Mtwara nilifika mpaka nikasikia kwamba wameingia katika maeneo ya jeshi. Sasa mpaka mimi nikashangaa, mpaka eneo la jeshi linavamiwa na wananchi, lakini yote hayo ni kwa sababu ya kutozingatia sheria, taratibu na kanuni.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tunaliangalia ni kuongeza kasi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi; tukijua kwamba hiyo nayo ni njia mojawapo ya kutatua migogoro. Vilevile, tutaendelea kutambua na kusajili nyanda za malisho kwa ajili ya kukabidhiana na changamoto ya mwingiliano baina ya watumiaji, hasa katika maeneo ya wakulima na wafugaji. Vilevile, kuna wawekezaji na kuna Hifadhi za Taifa. Tutaongeza kasi ya upangaji wa miji hii, maeneo haya ili kuondoa migogoro.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kusimamia kwa ukaribu taratibu za utwaaji wa ardhi kwa kuhakikisha kwamba wamiliki wa ardhi iliyotwaliwa wanalipwa fidia yao kwa haki, kwa ukamilifu na kwa wakati. Hapa niombe, taasisi zote ambazo zitaomba kutwaa ardhi mahali popote pale zijiandae, ziwe na fedha za malipo kwa wale wafidiwa. Kwa sababu, tutakapokuwa tumefanya upimaji na kufanya tathmini, wananchi wasichukue muda mrefu kabla ya kufanyiwa malipo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vijiji, Serikali inaendelea kutenga bajeti ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji ili kuondoa migongano ambayo nimeieleza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka huu wa Fedha 2025/2026 ambao tunaumaliza tumeandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 253 na hivyo kuwa na jumla ya vijiji 4,925 ambavyo vimeandaliwa mipango yao ya matumizi ya ardhi. Mwaka huu wa fedha unaokuja, tumejipanga kuweka mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 426; na kwa hii tutakuwa tunaongeza idadi ile ambayo tunayo mpaka sasa hivi 4,925.

Mheshimiwa Spika, upimaji na uandaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ndilo suluhisho la migogoro yote ya wakulima na wafugaji, kwa sababu huwa inawahusisha wadau wote wa hilo eneo na kukubaliana nini kifanyike katika eneo lao na maeneo gani yawe ya mifugo, maeneo gani yawe ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, katika kurahisiha upatikanaji wa hati miliki Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inajiingiza katika mifumo ya TEHAMA; na tunavyoongea mpaka sasa hivi, majiji yote nchini yanatumia mifumo ya TEHAMA katika mambo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Tuna jumla ya halmashauri 48 ambazo nazo zimekwishaingizwa katika mfumo. Hapa niwaondolee wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, masuala ya kupata eneo moja kuwa na hati mbili hayatatokea tena kwa sababu mfumo utakataa kuweka jina la mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyajadili tutayatolea ufafanuzi wakati wizara yangu itakapokuwa inawasilisha bajeti yake mwezi Mei tarehe 28; lakini yote tumeyachukua na tunayazingatia.

Mheshimiwa Spika, kwa kufika hapo ninaomba niunge mkono hoja na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imetupa mwelekeo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadiro ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninaomba kutumia fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia wote sisi hapa afya njema na pia kuniwezesha mimi kusimama tena hapa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hotuba yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Kaspar Kaspar Mmuya, Mbunge wa Ruangwa ambaye ameongea hivi punde na ni kweli anafanya kazi kubwa sana katika maeneo aliyoyaongea hapo ikiwa ni pamoja na kusimamia mambo ya hati na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya kipekee nikupongeze wewe na Mwenyekiti kwa namna ambavyo mmeendelea kuendesha shughuli za Bunge kwa kipindi chote ambacho Waheshimiwa Wabunge walipokuwa wanajadili hotuba ya Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, niishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri ambayo imetoa ushauri na maoni ambayo yanalenga kuboresha utendaji na utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Niwahakikishie kwamba Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Kamati kwa ukaribu mkubwa sana ili kufikia malengo ambayo tumeyaainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Wabunge waliochangia hotuba yangu ya bajeti ni 29 ambapo wamechangia kwa kuzungumza na kwa maandishi. Nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wabunge wote kwa michango yao ambayo ni mizuri na itatusaidia sana katika kuboresha utendaji wa sekta ya ardhi. Aidha, itatuwezesha kufikia malengo ya Wizara na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa lengo pana la kuwapa wananchi wetu furaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuwashukuru Wabunge wote waliotoa pongezi na ushauri kwa Wizara. Aidha, hoja zote zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ni muhimu sana na tutazizingatia mpaka kwenye nukta. Hata hivyo kwa sababu ya muda nitatolea ufafanuzi baadhi ya hoja kwa ujumla wake na tutahakikisha kila hoja inajibiwa kwa maandishi na kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi vijijini imepata uchangiaji mzuri sana kutoka kwa Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mbunge wa Korogwe vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Vilevile, Mheshimiwa Jafari Chege wa Rorya, Mheshimiwa Taska Mbogo wa Viti Maalum, Mheshimiwa Masanja Kadogosa wa Bariadi Vijijini, Mheshimiwa Ali Khalil Mirza wa Kiembe Samaki na leo Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kutoka Tabora.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri hamna haja ya kutaja majina na yote hayo, endelea tu.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tunakubaliana na maoni yao kwamba waandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni nyenzo muhimu sana katika kuongeza tija katika uzalishaji mali, kuzuia migogoro hasa ya wakulima na wafugaji, vilevile kuboresha makazi na hatimaye kufikia malengo tuliyojiwekea kwenye Dira 2050.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye hotuba yangu, azma ya Mheshimiwa Rais ipo wazi kabisa kwenye hili ambapo inalenga kuhakikisha kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi inaongezeka. Kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 48.11 na kati ya shilingi hizo bilioni 9.71 ni matumizi ya kawaida, lakini sehemu kubwa ambayo ni shilingi bilioni 38.4 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hii ni ongezeko kwa 378% ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zitawezesha kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 1,492 pamoja na kuandaa hati za hatimiliki za kimila 87,000. Vilevile, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau ili kuongeza uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji zaidi. Ninapenda kutumia fursa hii kuzielekeza halmashauri ambazo zimekasimiwa mamlaka za upangaji kutenga fedha kwa ajili ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa pia na masuala ya mipango miji na uendelezaji wa maeneo chakavu nchini ambayo imechangiwa pia na Waheshimiwa kadhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme kwamba usimamizi na uendelezaji wa miji unaongozwa na mipango ya jumla na mipango ya kina. Mipango hiyo inatoa mwongozo wa mgawanyo wa matumizi mbalimbali, kiwango cha uendelezaji, aina ya miundombinu na huduma zinazotarajiwa kutolewa kulingana na idadi ya watu inayotarajiwa kuishi katika eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa mamlaka za upangaji nchini kusimamia kwa ukamilifu mipango iliyopo ili kuleta tija na kuboresha mandhari ya miji na kiwango cha huduma zinazopaswa kutolewa katika miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja iliyotolewa na Kamati ambayo pia imechangiwa na baadhi ya Waheshimiwa kuhusu kurejeshewa 20% ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ili kuipa nguvu Wizara kutekeleza majukumu ya kukusanya, kupanga, kupima na kusambaza mifumo ambayo hoja hii tumeipokea kwa furaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru Serikali kutuwezesha katika ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi kwa mwaka huu hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 191 mpaka ilipofika tarehe 15 Mei, 2026 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 50 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka uliotangulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo haya hadi tunavyozungumza sasa hivi hapa yamefikia shilingi bilioni 203. Sina budi kuishukuru sana Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuweza kuona umuhimu wa urejeshaji wa 20% ya fedha za makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ili ziweze kusaidia kazi ya ukusanyaji, upangaji, upimaji na usambazaji wa mifumo. Ninatambua kuwa suala hili linafanyiwa kazi na Serikali kupitia kikosi kazi cha maboresho ya sera za kikodi. Bila shaka katika muda mfupi ujao itakamilika na kufanyiwa maamuzi katika ngazi zinazohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa kadhaa walizungumza vilevile kuhusu changamoto zilizopo katika ulipaji wa fidia kwa wakati na kuzingatia bei ya soko. Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanalipwa fidia stahiki maeneo yao yanapotwaliwa kwa manufaa ya umma, Wizara imetoa Waraka Na. 2 wa Uthamini na Ulipaji Fidia wa mwaka 2024 ambao umeelekeza kwamba Wizara, mamlaka za mikoa, wilaya, taasisi za umma, taasisi binafsi, mashirika ya umma, mamlaka za halmashauri za miji na wale wote wanaohusika kulipa fidia wanapaswa kwanza kuthibitisha uwepo wa fedha kwa ajili ya malipo ya fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nitumie fursa hii kuzielekeza hizo mamlaka zote zinazotwaa ardhi kuzingatia taratibu hizi za utoaji wa ardhi na kulipa fidia stahiki na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi (KKK) ambayo imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Ninapenda kuwataarifu kuwa Wizara imejipanga kuongeza kasi ya kupanga ardhi katika maeneo ya miji na vijiji kwa kushirikiana na sekta binafsi. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Wizara ya Fedha kuchukua hatua madhubuti kwa halmashauri zote zilizokopeshwa fedha kurejesha fedha hizo kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliarifu Bunge lako kuwa kwa sasa Wizara imeboresha utaratibu wa urejeshaji wa fedha za mikopo kwa kuwa na namba ya kumbukumbu ya malipo yaani control number inayotolewa wakati wa mauzo ya viwanja; hatua ambayo itawezesha fedha za mikopo kulipwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Wizara, tofauti na ilivyokuwa utaratibu hapo awali. Aidha, nitumie fursa hii kuzipongeza zile halmashauri ambazo zimekamilisha marejesho ya fedha walizozikopa na vilevile kuzitaka halmashauri ambazo hazijakamilisha kufanya hivyo mara moja, ni vizuri kutii sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa matumizi ya mfumo katika kuboresha utoaji wa huduma bora ambayo pia itapunguza gharama na muda wa ufuatiliaji kwa wananchi. Hoja hii imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kukufahamisha kuwa Wizara inaendelea na zoezi hili, kuhakikisha mfumo wa e-Ardhi unasambazwa katika halmashauri zote hapa nchini na tutaongeza kasi kwa mwaka huu 2026/2027. Miongoni mwa kazi tutakazozifanya ni kubadilisha kumbukumbu za ardhi kutoka nakala ngumu kwenda nakala tepe na kuboresha mifumo kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, imechangiwa pia na wachangiaji wengi. Ninapenda kukufahamisha kuwa Wizara imepokea ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge na niseme kuwa tutaendelea na kazi ya kuandaa mwongozo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na tutashirikisha wadau mbalimbali wanaohusika katika mnyororo mzima wa upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu. Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha andiko maalum kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Nyumba. Mfuko huu utakapoanzishwa utawezesha Serikali kuwa na fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ambayo ilitolewa na Mbunge wa Monduli na nimuombe tu Mheshimiwa Isack Copriano aridhie tukutane naye pamoja na wataalamu ili kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ambayo aliyaainisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nimhakikishie kwamba nipo tayari kufanya ziara jimboni kwake ili tusikilize malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi kwa pamoja. Nachelea kutoa maamuzi hapa kabla sijapata taarifa za kina, nisije nikaleta mgogoro mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kinondoni pia tuliambiwa kwamba Halmashauri ya Kinondoni ni miongoni mwa halmashauri 169 nchini zinazohusika katika utekelezaji wa programu ya urasimishaji makazi nchini. Aidha, mwenendo wa utekelezaji wa shughuli hizo haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Tarimba Abbas, tutakwenda pamoja katika jimbo lake na Wilaya nzima ya Kinondoni, kwa sababu nimeshangaa kuambiwa kwamba hata Magomeni watu wanakaa kwenye nyumba ambazo hazina hati, ambapo nilikuwa naamini ni mji wa zamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Aprili, 2026 jumla ya makazi 66,175 yametambuliwa katika eneo lake na kurasimishwa, lakini kama bado mengine, tutaendelea kuyafanyia kazi ili maeneo yote yaweze kurasimishwa. Bila shaka yoyote, kuna haja ya kuongeza kasi, naahadi kwamba tutakuja katika suala hilo tukiwa na kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la usimamizi wa watumishi waliopo halmashauri limeongelewa na Waheshimiwa wengi. Ninapenda kusema kwamba Serikali ilifanya uamuzi huo kuhamisha mamlaka ya nidhamu kule, lakini kutokana na hoja sasa zinazoendelea kutolewa, Wizara itakaa chini na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi ili kuangalia namna bora ambayo watumishi wale watatoa tija kubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha Kamisheni ya Ardhi kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza ambayo itashughulikia sekta nzima ya ardhi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya. Kamisheni hiyo itakuwa na jukumu la kusimamia watumishi wake kama zilivyo taasisi nyingine za Serikali, mfano RUWASA, TARURA na nyinginezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 Toleo la mwaka 2023 hii ilikuwa ni ahadi ambayo iliyotolewa na Mheshimiwa Rais na yeye alitolea maelekezo. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba yote hayo yatazingatiwa na mamlaka hiyo ikianzishwa tutakua hatuna hoja ya kuuliza watumishi wako wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kunti pia aliulizia suala la Chemba, nimhakikishie kwamba tutakwenda kama tulivyomuahidi ili tuweze kutatua matatizo yaliyopo kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Kiteto, ndugu yangu Mheshimiwa Olelekaita, analifahamu, tulizungumza na nilimuahidi kufika kule na mpaka sasa hivi ile taarifa ya wataalamu imeshakamilika na tutapanga tu ni lini twende naye tukaiseme kwa pamoja kule ili wananchi wa Kiteto wapate furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi kutopewa milki za ardhi katika maeneo ya hifadhi za bahari na madai ya fidia katika Jimbo la Mtwara Vijijini, nimhakikishie Mheshimiwa Premji kwamba wawekezaji wa nje huwa hawapewi hati zile ambazo wanapewa wananchi wa Tanzania, wao wanapewa derivative, hawapewi zile zile zenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tutaliangalia vilevile kama ambavyo ameliongea ili tukifika kwake na huyu yuko njiani ninapoenda nyumbani kwetu Masasi napitia kwake. Kwa hiyo, tutakutana pale, tutalizungumza tuone tunalikamilisha namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya maeneo ya wazi imechangiwa sana nayo, tunatoa rai kwa halmashauri zote kulinda maeneo yaliyowazi. Maeneo yaliyowazi siyo kwa ajili ya kazi nyingine yoyote, bali ni kuufanya mji upumue na wananchi wapate sehemu za kupata burudani, waweke bustani kule, wananchi wakaondoe frustration. Tunaambiwa kwamba unavyopita kwenye bustani akili zinapumzika kidogo. Kwa hiyo, niwatake wote wa halmashauri, maeneo ya wazi wajenge bustani ili wananchi wetu wapate sehemu za kupumzika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kutokana na ufinyu wa muda, Waheshimiwa Wabunge wengi hawakupata nafasi ya kuchangia hotuba zao, naomba niwahakikishie kuwa tutakuwa tayari kwa wakati wowote kupokea ushauri, maoni na changamoto kutoka kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa leo tulipata vilevile michango ya Waheshimiwa Wabunge kadhaa, upimaji wa mashamba hoja iliibuliwa na Mheshimiwa Nawanda, tumeipokea kwa ari kubwa, tutajipanga kwa kushirikiana na halmashauri na vyama vya msingi ili tutekeleze jambo hili ambalo tunaamini kwamba ni muhimu mashamba yetu nayo yawe yamepimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea pia ushauri wa kupima miji, tunatambua umuhimu wa kufanya hivyo. Mheshimiwa Mariam Mungula, pia alizungumzia upungufu wa nyumba nchini tunautambua na sisi tunasema tutakuwa na sera ya nyumba na makazi, itaunganisha mambo ya nyumba na mambo ya makazi, uboreshaji wa nyumba na makazi na hii sera imeshaanza kufanyiwa kazi na zoezi linaendelea. Itakapokamilika tutaiwasilisha katika mamlaka husika ili iweze kurasimishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kutoka Tabora alitoa pongezi nyingi kwa watendaji wa Wizara na mimi kwa niaba yao nazipokea; pongezi kwa Kamishna, pongezi kwa DG National Housing, pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi alizungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda nimfamishe Mheshimiwa Mbunge kuwa mwaka huu tutapanga vijiji 1,492 na tutaendelea na hiyo kasi hadi tumalize vijiji vyote 12,333. Tulipata vilevile hoja ya kupanga matumizi bora ya ardhi nchi nzima, Mheshimiwa Mbunge akirejea kwenye hotuba yangu atagundua kwamba tunao huo mpango na nilitoa taarifa kuwa tunanunua ndege ambayo itatusaidia kwenye zoezi hili na mambo yatakuwa mazuri, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Paresso alizungumzia Mabaraza ya Ardhi na nimshukuru sana, kwa sababu alitoa historia ndefu kuhusu kuanzishwa kwa mabaraza haya na sababu zilizosababisha yaanzishwe. Akasema hali ilivyo sasa ni kweli siyo Wilaya zote zina mabaraza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe wasiwasi, katika hotuba yangu nimesema kupitia kwa mwaka huu unaokuja, tutaanzisha Mabaraza ya Ardhi kwa wilaya zote zilizobaki na vilevile tutateua Wenyeviti wa Mabaraza ambayo hayana Wenyeviti. Aidha, nimwelekeze Katibu Mkuu sasa aanze mchakato wa kujaza nafasi zilizowazi kwa Wenyeviti wa Mabaraza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwita Waitara, huyu ni mkali sana, Mheshimiwa Mwita Waitara tulipanga kwenda Tarime kweli tukatatue tatizo lililopo kule. Ahadi yangu nimhakikishie kwamba ipo palepale na nimwombe Mheshimiwa Waitara, kwa sababu huyu ni mwanafunzi wangu wa kemia na alikuwa mwanafunzi bora kabisa wa kemia pale University of Dar es Salaam na alipata marks nzuri; sasa asimnyang'anye shilingi mwalimu wake, najua hawezi kushika shilingi. Sasa utashikaje shilingi ya mwalimu wako?

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge amekiri mwenyewe kuwa Wizara ina mambo mengi. Kwa hiyo, najua kwamba anajua tutakuwa tunafanya mambo mengine kabla hatujaenda kwake, lakini kwake tutafika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja pia ilitolewa ya wanawake kupewa nafasi ya kumiliki ardhi. Ninaomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba mwezi Machi mwaka huu tulikuwa na Kliniki ya Samia Ardhi. Hii ilikuwa mahususi kwa akina mama, lakini kama mnavyojua, walikuwa akina mama na akina baba tu. Na akina baba pia walikuja na tuliwahudumia akina mama zaidi ya 12,000. Hoja ilikuwa ni kuwapa elimu kuhusu umiliki wa ardhi, lakini vilevile kama kuna matatizo ya umiliki tuyashughulikie na walifurahi sana baada ya ile kliniki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nisisitize kwamba kliniki hizi zimekuwa na manufaa sana. Tumepata pongezi nyingi sana kwa kuendesha hizi kliniki, ni leo tu hapa ndiyo nimesikia kwamba kliniki zina matatizo kidogo, lakini mara zote tumekuwa tunaambiwa kwamba kliniki zimesaidia sana. Kama kuna mapungufu tutayaboresha ili kliniki ziwe na manufaa zaidi ya pale ambapo tumefikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ambayo nataka niichangie ni ya Mheshimiwa Rashid Mtima, nafikiri yeye alizungumzia ukuaji wa miji ambapo akasema Tanzania inaongoza kwa asilimia tano. Nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba hoja ya ukuaji wa miji imekuwa ni hoja nzito sana katika mikutano ya Bara la Afrika hata ya kidunia. Nakumbuka tulivyokuwa Nairobi kwenye Mkutano wa African Urban Forum lilizungumziwa sana na ilikuwa ni lengo mahsusi la mkutano huo na mapendekezo yalitolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tulivyokuwa tena kwenye World Urban Forum kule Azerbaijan limezugumzwa pia. Siyo Tanzania tu peke yake ni karibu dunia nzima kwa sababu kuna sababu zinazofanya watu waje mijini. Lakini nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Tanzania tumepunguza push factors zinazowaondoa wananchi kijijini, zinazowakimbiza ikiwa ni pamoja na mambo ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika sasa hivi REA imetapakaa karibia nchi nzima, ni vijiji vichache sana ambavyo bado havijapata huduma hii, lakini mambo ya maji, shule, barabara na mitandao ya simu za mkononi ni vitu ambavyo vitapunguza kasi ya wananchi kwenda mijini kwa sababu tutapunguza hiyo wanaita push factor. Lakini pull factor bado ipo, miji inakuwa vizuri, inapendezeshwa vilevile, kwa hiyo watu pia wanaitamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kufikia hapo, niseme tu Wizara yangu itafanyia kazi mapendekezo yote ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa siku ya leo na jana, vilevile na niwapongeze sana kwa kwa maoni yenu na tunasema kwamba yale ambayo sijayaongelea hapa tutayaleta rasmi kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sema unatoa hoja.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.