Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Chief Thomas Mgonto Kitima (2 total)

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Ikungi Mashariki, kuna visima vingi vilichimbwa, lakini maji hayajaweza kusambazwa katika maeneo mbalimbali. Mfano mzuri ni Kijiji cha Misule, Kata ya Misughaa. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Kata ya Misughaa, Kijiji cha Misule wanaweza kusambaziwa maji na wanaweza kupata hayo maji ili waweze kuwa na imani ya Serikali yao kwa maana ya kumtua mama ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa maeneo ya Misughaa, kwanza kabisa Serikali itachimba visima na baada ya kuchimba visima tunafanya pump test na baadaye tunajiridhisha na que ya maji. Tukishajiridhisha na que ya maji, maana yake sasa ndiyo tunafanya usanifu wa kutengeneza mtandao unaoendana na maji ambayo yanazalishwa pale. Kwa hiyo, tukishajiridhisha, baadaye sasa tunayafikisha kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bajeti ya kwanza ilikuwa kuchimba visima, bajeti ya pili ni kusambaza baada ya kujiridhisha na uwingi wa maji yaliyopatikana katika visima. Ninamtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwa vile tumekamilisha uchimbaji wa visima na pump testing imeishafanyika. Sasa tuko kwenye mchakato wa kuingiza katika bajeti ya kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kujenga mtandao wa maji ili maji yawafikie watumiaji na wananchi wa Misughaa. Ninakushukuru sana.
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunavyozungumza ni takribani wiki ya nne wananchi wa Kata ya Mang’onyi katika Jimbo la Ikungi Mashariki hawana maji kabisa, na sababu kubwa ni kwamba motor imeungua na pa kubadilishwa mpaka iende Dar es Salaam. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu hawa wa Mang’onyi ili waweze kupata huduma ya maji kwa haraka? Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Mbunge hujasikika vizuri, naomba utaje hilo eneo ambalo maji yamekatika kwa muda ili Mheshimiwa Naibu Waziri asikie.

MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunavyoongea ni takribani wiki ya nne wananchi wa Kata ya Mang’onyi katika Jimbo la Ikungi Mashariki hawana huduma ya maji, na sababu ambayo inazungumzwa ni ile motor kwamba imeungua na ili ibadilishwe lazima ipelekwe Dar es Salaam.

Je, Serikali inatoa kauli gani ili hawa watu wa Mang’onyi waweze kupata maji ukizingatia ni kwamba ni kata ambayo ina wawekezaji wakubwa ambao wanasaidia maendeleo katika Jimbo zima la Ikungi Mahariki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru sana kaka Mheshimiwa Thomas, Mbunge kutoka Ikungi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa changamoto hii na kwa Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tatizo dogo la motor haliwezi kuwafanya Watanzania wakose huduma ya maji safi na salama. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kutumia fursa hii kumwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, hili suala alifuatilie haraka sana ili wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara ya Maji hatuwezi kushindwa kutekeleza jambo dogo kama hilo. Nimtoe hofu, hili jambo tumelipokea na tutalifanyia kazi na uhesabu kwamba hili tatizo limeisha. Ahsante sana. (Makofi)