Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lulu Guyo Mwacha (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. LULU G. MWACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninachukua fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia Wizara hii muhimu, mahususi ya Nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jemedari wetu kwa kazi kubwa anayoifanya katika kusukuma maendeleo katika sekta nzima ya nishati. Pia ninawapongeza wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kukimbiza gurudumu la maendeleo katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii pia kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Deo Ndejembi, Waziri wa Nishati pamoja na dada yangu Mheshimiwa Salome Makamba pamoja na watendaji wote wa Wizara hii ya Nishati kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya hasa katika kipindi hiki cha mpito katika Taifa letu. Ninampongeza sana kaka yangu ninaona hata amepungua kidogo baada ya Strait of Hormuz kufungwa lakini ninawatia moyo sana, kazi siyo rahisi, lakini nina hakika tutapita salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea suala la nishati tunaongelea uhai wa uchumi wetu, tunaongelea fursa za ajira kwa vijana wetu, tunaongelea matumaini ya kila mwanamke wa Taifa hili kujikwamua kiuchumi kupitia Sekta ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaongelea kila mfanyabiashara mdogo mdogo ambaye ana nia ya kupanua biashara yake na kuongeza kipato chake. Tunapojadili hotuba hii, tunapojadili bajeti hii tuna nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wetu wanaendelea kujikwamua kiuchumi kupitia Wizara yetu ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana kuipongeza Serikali yangu, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa waliyofanya katika Sekta hii ya Nishati. Kumetekelezwa mradi mkubwa wa umeme wa jua ambao ni megawatts 150 ambao mpaka kufikia sasa megawatts 50 zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mradi mkubwa wa kupokea na kupoza umeme ambao ni wa kilowatts 400 kwenda 220 mpaka 33. Mradi huu umetekelezwa kwa fedha za ndani ambazo ni shilingi bilioni 2.7 ambazo ni fedha zetu wenyewe za ndani. Hii yote ni katika kuimarisha Sekta hii ya Nishati ambayo inaendelea kuwaletea matokeo chanya Watanzania wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuipongeza Serikali kupitia TANESCO kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya nishati ambayo imeweza kufikisha umeme mpaka vijiji vyote. Mpaka saa hizi tumeendelea kwenye vitongoji ambapo miezi kadhaa iliyopita mradi mkubwa wa shilingi trilioni 1.2 umesainiwa kufikisha umeme kwenye vitongoji 9,009 kwenye nchi yetu yote. Kwa hivyo, ninaipongeza sana Serikali kupitia Wakala wake wa REA. Ninaipongeza pia Serikali kwa ajili ya nishati hii safi ya kupikia ambayo katika hili Mheshimiwa Rais amekuwa champion wetu Barani Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio ya Serikali katika Sekta hii ya Nishati, lakini kumekuwa na changamoto kubwa katika fees ya connectivity ya umeme kwenye vijiji vyetu. Umeme wa REA ilisemekana kuunganishwa ni shilingi 27,000, lakini kuna baadhi ya vijiji ambavyo wanaunganishiwa ule umeme kwa shilingi 370,000. Tunakuwa hatuwatendei haki wale wanavijiji ambao wanatakiwa waunganishiwe kwa shilingi 370,000. Hivyo ninaiomba sana Serikali yangu, ninaomba sana sana tuwe na fair price kwa watu wote wa vijijini. Tuangalie namna ambavyo kwa hao watu wa vijijini tunaweza tukapunguza price ikawa kote fair kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo limejitokeza wananchi wengi wa vijijini wanalalamika, kuna suala la ulipaji wa units. Mwanakijiji akilipa umeme zaidi ya shilingi 9,000 anatolewa kwenye ule mfumo wa chini kupelekwa mfumo wa kati. Let's say kuna mtu mjini kamnunulia umeme wa shilingi 100,000, kesho wanamtoa kutoka kwenye ule mfumo wa chini wanampeleka kwenye mfumo wa kati ambao baada ya hapo anakuwa analipa gharama zaidi. Kwa mwananchi wa kijijini anashindwa anakuwa anakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kila mwananchi wa Kitanzania aweze kuunganishiwa umeme na aweze kutumia kwa gharama nafuu. Kwa hivyo, ninaiomba sana Serikali waangalie pia na suala la bei hiyo kwamba akiwa ni shilingi 9,000 akizidisha anatakiwa awe analipa zaidi. Tunaomba sana Serikali waangalie suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye suala la nishati safi ya kupikia, kwenye hili suala ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara nzima ya Nishati. Wananchi wa kijijini wakishanunua gesi wanashindwa kuendelea kununua kwa wakati mwingine kwa sababu ya bei zake zinakuwa kubwa. Mwananchi wa kijijini anashindwa kununua kwa shilingi 25,000 ama shilingi 56,000. Kwa hivyo, ninaomba Serikali yangu iangalie namna ambavyo hawa wanakijiji waweze kununua gesi kulingana na kipato chao.

Mheshimiwa Naibu Spika, isiwe lazima iwe kwamba lazima anunue kilo sita ule mtungi mdogo ama ule mtungi mkubwa kilo 15, basi kuwe kuna ujazo hata wa kilo moja kwamba leo ana shilingi 3,000 anaweza kununua gesi ya shilingi 3,000, leo ana shilingi 6,000 ama shilingi 5,000 wanaweza kununua gesi ya shilingi 5,000 ama shilingi 6,000. Kwa sababu mwananchi wa kijijini leo anaona bora akanunue mkaa wa shilingi 5,000 ama shilingi 2,000 aendelee kupikia mkaa au kuni kutokana na gharama kubwa za gesi. Kwa hivyo ninaiomba Serikali yangu sana iendelee kupunguza gharama za gesi ambapo tutakwenda kuwasaidia wananchi hususan vijana na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yangu kuhusu suala la mafuta, hapa tunapopitia kipindi cha mpito Serikali imehakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kubaki salama. Lakini niishauri Serikali yangu iendelee kuhakikisha inakuwepo na reserve kubwa ya mafuta, ili wakati mwingine jambo kama hili linavyotokea tunakuwa hatuna wasiwasi kwamba wananchi wetu watakosa mafuta. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu iendelee kuwaangalia wananchi wake kwa namna ya jicho la tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)