Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Juma Zuberi Homera (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninaomba kutumia nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu pamoja na kuniwezesha kufanya kazi zangu vizuri katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Tanzania naishukuru sana na taasisi zote zilizoko chini ya hii Wizara ya Katiba na Sheria. Pia, ninawashukuru viongozi wangu wengine akiwemo Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Naibu Spika; na Viongozi wengine wote wa Bunge pamoja na wewe mwenyewe Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kwa namna anavyonisaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niishukuru Menejimenti ya Wizara, Mahakama ya Tanzania pamoja na kiongozi kinara kabisa Eliakim Maswi, Katibu Mkuu tukisaidiana vyema na Naibu Katibu Mkuu na Viongozi wote walioko chini ya Wizara hii ambao niliwataja hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Namtumbo kuendelea kuniombea wakiungana na wazazi wangu ambao niliwataja hapo awali pamoja na familia yangu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nishukuru Waheshimiwa takribani wa Bunge zaidi ya 19 wamechangia katika hoja yangu ambayo nimeitoa hapo asubuhi. Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mheshimiwa Mariam Mungula, Mheshimiwa Asha Saleh, Mheshimiwa Nyamizi Simon Mhoja, Mheshimiwa Happiness Daniel Ngwando, Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mheshimiwa Neema Peter Majule, Mheshimiwa Yohana Stephen Msita, Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, usiwataje kwa sababu ya muda…

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, sawa. Nitambue tu kwamba wako 19 ambao wamechangia kwenye hoja yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme machache ambayo hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Moja kuna suala ambalo lilitajwa hapa na Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Serikali ichukue hatua makusudi za haraka kuhakikisha Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Taasisi ya Kisheria Ilemela, Mwanza ukamilike kwa wakati, ikibidi kumnyang’anya mkandarasi kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mkakati umewekwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo imeunda timu ya usimamizi wa mradi huu na tuna uhakika utakamilika kwa wakati. Hatua stahiki za haraka zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvunja mkataba kwa mujibu wa sheria kama mkandarasi huyu ataendelea kusuasua kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilibuni mikakati kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati pasipo kuathiri ubora wa maamuzi. Ushauri umepokelewa Serikalini kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeweka mikakati ifuatayo ili kumaliza mashauri kwa muda mrefu na kupunguza mashauri. Imeendelea kuweka mkakati wa kufanya majadiliano nje ya Mahakama kwa lengo la kupunguza mlundikano wa mashauri dhidi ya Serikali ambayo yameweza kuyamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, vilevile kwa kushirikiana na Mahakama kama mdau mkuu inaendelea na mkakati wa kumaliza masharti ya muda kwa muda mrefu kwa kusikiliza mashauri hayo kupitia vikao maalum (Special Session [BRN]) ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa kupunguza na kumaliza mlundikano wa mashauri Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo lilizungumzwa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge, Serikali iharakishe utatuzi wa mgogoro wa ardhi ikiwemo mgogoro wa wakulima wa chai katika Mkoa wa Tanga. Serikali imepokea shauri hili na itahakikisha migogoro ya ardhi ikiwemo migogoro ya wakulima wa chai hususan katika Mikoa ya Tanga itatatuliwa kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ianzishe Mahakama ya Mkoa itakayokuwa na mamlaka ya rufaa kwa Mahakama za Wilaya ili kupunguza idadi ya kesi zinazowasilishwa Mahakamani. Ili kupunguza mzigo wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Serikali imepokea ushauri huu wa Wabunge wa kuanzisha Mahakama ya Mkoa itakayokuwa na Mamlaka ya Rufaa kwa Mahakama za Wilaya. Kwa kushirikiana na Mahakama tutafanya uchambuzi wa mapendekezo hayo na mara baada ya uchambuzi kukamilika, Serikali itatoa taarifa ya hatua zilizochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo alizungumzia kuhusiana na kwamba kumekuwepo na changamoto za uwasilishwaji wa fedha za retention katika Ofisi za Wilaya na Halmashauri, vitendea kazi na watumishi ili kuwezesha utoaji wa huduma za RITA ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vifo, vilevile takwimu za vizazi na vifo na ni muhimu katika mipango ya nchi na vyema zitatuliwe hizo changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya uwasilishaji wa fedha za retention katika Ofisi za Wilaya na Halmashauri imetatuliwa ambapo asilimia tano ya mapato yanayokusanywa kwa kila Wilaya na Halmashauri huwasilishwa katika Ofisi hizo. Kuhusu vitendea kazi ni kweli changamoto hiyo ipo na kwa kutambua hilo katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, imetenga bajeti ya shilingi 850,000,000 kwa ajili ya kununua vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watumishi katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, RITA ilipokea watumishi 63 na kufanya jumla ya watumishi kufikia 405 ikilinganishwa na hapo awali kulikuwa na watumishi 342. Aidha, RITA imepata kibali cha kuajiri watumishi 73. Ni kweli utoaji wa takwimu za vizazi na vifo ni muhimu kwa kutambua RITA ndiyo chanzo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini RITA tumeanzisha programu ya masaa 48 ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo. Kwa kushirikiana na Taasisi ya Ufilisi na Udhamini (RITA) tulifanya uzinduzi wa vyeti vya kuzaliwa kwa masaa 48 mwezi Desemba, 2025. Tangu uzinduzi uliofanyika Machi, 2026 Wakala umepokea jumla ya maombi 445,512. Kati ya maombi yaliyopokelewa 420,863 yalifanyiwa kazi na vyeti vilitolewa ndani ya masaa 48 hivyo tulifanikiwa kwa zaidi ya 94%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Serikali ikamilishe mchakato wa kuhamisha mashauri ya ardhi kwenda kwenye mfumo wa Mahakama na pia Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria naye alizungumzia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeshaanza utaratibu wa kuhamisha mashauri yaliyokuwa yanashughulikiwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda katika mfumo wa Mahakama ya Tanzania. Hatua hii ilifikiwa baada ya majadiliano na Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote kwa pamoja kupitia maelekezo ambayo aliyatoa Mheshimiwa Rais tarehe 13 Januari, 2026, katika Mkutano Maalum Judicial Square; mojawapo ya maelekezo aliyoyatoa aliyatoa kwamba, kuhamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mahakama. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge jambo hili limefanyiwa kazi kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwa Waheshimiwa Wabunge, bajeti yetu mwaka huu inakwenda kumaliza kabisa changamoto ambazo zingeweza pia kwenda kuleta changamoto kubwa kwenye Dira ya 2050. Kwa hiyo, tunakwenda kurekebisha sheria kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Kurekebisha Sheria Nchini pamoja na Tume ya Kuandika Sheria Nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumzia masuala mbalimbali, ningependa nijibu pia machache. Mheshimiwa Happiness Ngwando ambaye ametupongeza, lakini pia tunashukuru sana kwa mchango wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya siku 120 pia tunakwenda kuzindua Mfumo wa E-Legal Aid ambao tutakuwa tuna uwezo wa kupeleka changamoto zetu kwenye mfumo na tukapatiwa majibu kwa haraka ili kuweza kuboresha zaidi mfumo wa msaada wa kisheria nchini. Ndani ya siku 120 tunakwenda kulifanya jambo hilo. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kama vile Mheshimiwa Kenneth Ndingo ambaye ametupongeza, lakini amezungumzia masuala ya Mabaraza ya Ardhi na kusema kwamba masuala ya Dira ya 2050 tungetamani yasikwame kwa changamoto ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba sisi kama Wizara mojawapo ya kitu ambacho tunakwenda kukifanya ni ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi, kitengo ambacho hakikuwepo mwanzo. Sasa hivi kimewekwa kwenye bajeti hii na kitengo hiki kimeanzishwa baada ya Mheshimiwa Rais kutupa kibali cha kuanzisha kitengo hiki muhimu katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mageuzi ya sheria kwa ajili ya uwekezaji na uchumi nchini ambayo tunakwenda kufanya kazi kubwa ya mabadiliko ya sheria ili kuwavutia wawekezaji, lakini pia kuwafanya wawekezaji wawe na unafuu ili tuweze kujenga nchi yetu iende kwenye uchumi wa juu zaidi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda pia kusimamia utatuzi wa masuala ya ajira, uteuzi, nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama na Taasisi zingine zote zilizoko chini ya hii Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, nikushukuru sana wewe binafsi kwa namna ambavyo ulivyotuongoza vyema hapa kwenye kikao chetu cha leo cha Bunge. Hakika unastahili pongezi za dhati sana Mheshimiwa Mwenyekiti wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, waweze kuiunga mkono bajeti hii ili tuweze tukafanye mabadiliko makubwa na mageuzi makubwa ya upatikanaji wa haki na maendeleo makubwa ya kasi kuelekea Dira ya 2050 pamoja na bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaafiki.

(Hoja ilitolewa iamuliwe)