Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Fadhili Ally Liwaka (1 total)

MHE. FADHILI A. LIWAKA aliuliza:-

Je, lini huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zitapelekwa kwa wananchi Kilimarondo na Kiegei ambao hufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 120?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Fadhili Ally Liwaka, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa simu za mkononi ni muhimu kupatikana kabla ya kupata huduma za pesa mtandao ili kuwezesha mawasiliano kati ya simu ya mtumiaji na mfumo wa huduma za kifedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia miradi ya UCSAF tayari imejenga minara miwili ya TTCL inayotoa huduma za mawasiliano. Mnara mmoja unatoa huduma katika Kijiji cha Nanjihi, Kata ya Kilimarondo na mwingine upo katika Kijiji cha Kiegei, Kata ya Kiegei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa TTCL inayo huduma ya pesa mtandao kupitia T-PESA, nimemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL kuhakikisha mawakala wa pesa mtandao wa T-PESA wanakuwepo katika vijiji vya Kilimarondo na Kiegei ili waweze kutoa huduma za kifedha kupitia mtandao wa simu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika maeneo hayo ili kuona changamoto zilizopo ikiwemo upatikanaji wa kampuni nyingine za watoa huduma za mawasiliano katika maeneo hayo. Hii itawezesha kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuhamasisha kampuni nyingine za mawasiliano ya simu kutumia minara iliyowekwa kusimika mitambo yao ili kuwezesha wananchi kupata mawasiliano ya simu na huduma za fedha kutoka mitandao hiyo pia.