MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru, wananchi wa Kilimarondo na Kiegei wanatembea umbali wa kilometa 126 kufuata huduma ya kifedha inayotokana na mitandao ya simu. Je, Serikali ina mkakati gani kuwajengea minara ya uhakika ili kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa Fadhili Liwaka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo aliyoyataja kama nilivyoeleza awali yote yako katika mpango mkakati wa Serikali wa Miaka Mitano wa Ujenzi wa Minara katika maeneo yote yenye changamoto hapa nchini.
Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Fadhili kwamba maeneo yote aliyoyataja hayo tutayafikia katika kipindi hiki cha mkakati huu kwa sababu tunakwenda hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, kadri fedha inavyopatikana, tutakuwa tunatekeleza mkakati wetu na tunategemea kwamba ifikapo mwaka 2030 changamoto ya mawasiliano nchini itakuwa tumeitatua au tumeimaliza kabisa.
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na majibu mazuri na ya kutia moyo ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa maeneo ya Kiegei na Kilimarondo yamekuwa na mwamko mkubwa wa uzalishaji wa madini, hususan madini ya dhahabu na kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na uhitaji wa huduma za kifedha na kufanya miamala mbalimbali ya simu. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kushawishi na kusukuma kampuni mbalimbali za simu za mkononi ili ziweze kwenda kujenga minara na kuwezesha huduma hizi muhimu za upatikanaji wa fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa majibu na jitihada hizi za kuhakikisha kwamba tunapata mawasiliano yenye huduma za kifedha ni za muda mrefu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana utayari wa kuongozana na mimi japo kwenda kutembelea kwa siku nzima ili ajionee mazingira ya mawasiliano na masuala ya miamala katika maeneo ya Kilimarondo na Kiegei? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaanza kwa kumpongeza, Mheshimiwa Liwaka amekuwa mfuatiliaji mzuri wa huduma hizi za kidijitali katika Jimbo lake na ni msumbufu kwelikweli. Amekuja Wizarani zaidi ya mara kumi, kwenye simu yangu nina meseji zake zaidi ya 30 na watu wasiomfahamu kama ni Mheshimiwa Mbunge wanaweza kudhani kwamba ni mtumishi wa Wizara yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninampongeza sana kwa kuwapigania wananchi wake. Hakika wananchi wa Nachingwea wamepata Mbunge jembe, jembe ulaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kujibu swali la pili kuhusu kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Liwaka. Ninamhakikishia Mheshimiwa Liwaka kwamba niko tayari, baada ya Bunge hili, tutapanga mimi na yeye ni lini nitakwenda kutembelea ili nikajionee hali halisi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, Wizara yetu inaendelea na mazungumzo na watoa huduma mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanafikisha huduma katika eneo hilo kwa sababu amesema ni eneo la uzalishaji na lina mwingiliano mkubwa wa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hili, ninamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano kupitia taasisi zake kuratibu haya mashauriano yanayoendelea na watoa huduma ili kuhakikisha kwamba wanapeleka huduma za minara katika eneo alilolitaja Mheshimiwa Liwaka la Kiegei mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba Dira yetu ya 2050 inaitaka sekta binafsi iwe mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya nchi yetu na sisi hilo tumelizingatia, tunawasiliana na watoa huduma wetu ili kutekeleza pia dira yetu hii. Ninakushukuru. (Makofi)