MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya TARURA Wilaya ya kaliua ili kufungua barabara katika vijiji vipya 22 vilivyopo Jimbo la ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhael Masanja Lufungija, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini katika Wilaya ya Kaliua unasimamia mtandao wa barabara wenye jumla kilometa 1,370.41. Kati ya hizo, kilometa 9.23 ni barabara za lami, kilometa 329.73 ni barabara za changarawe na kilometa 1,031.45 ni barabara za udongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2020/2021 bajeti ya matengenezo ya barabara katika Wilaya ya Kaliua ilikuwa shilingi milioni 987. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 na kuendelea bajeti hiyo imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 4.3, sawa na ongezeko la 335.66%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufungua vijiji vipya 22 vilivyopo Jimbo la Ulyankulu kupitia bajeti ya miaka ya fedha 2021/2022 hadi 2024/2025 Serikali ilitekeleza jukumu la kufungua barabara mpya za vijijini. Vijiji vilivyonufaika na utekelezaji huo ni pamoja na Twigu, Nhw’ande katika barabara ya Twigu – Nhw’ande (kilometa sita); Vijiji vya Taba, Imara, Ibapa, Keza katika barabara ya Taba – Imara – Keza (kilometa nane); na Vijiji vya Usonga, Ikonongo katika barabara ya Usonga – King’wangoko (kilometa 18).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2026/2027 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 785 kwa ajili ya kufungua na kuboresha barabara zinazoelekea katika vijiji vipya. Vijiji vitakavyonufaika na mpango huo ni pamoja na Nyasa, Itumbo katika barabara ya Nyasa – Itumbo (kilometa 6.5), vijiji vya Mwahalaja, Upele na Miti Mitano katika barabara ya Mwaharaja – Mpandamlowoka (kilometa 38.5).
MHE. JAPHAEL M. LUFUNGIJA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga maghala ya kuhifadhia mazao Kata ya Uyowa katika kitovu cha biashara Mwamnange ambapo tayari eneo lipo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Wizara imepanga kufanya tathmini ya maeneo mapya ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa ghala. Tathmini hiyo itasaidia kubaini mahitaji ya uwezo wa kuhifadhi mazao katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuiwezesha Serikali kutenga bajeti ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa ghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Japhael Masanja Lufungija kuwa suala lake limechukuliwa na litafanyiwa kazi na Serikali baada ya kufanya tathmini kwenye kata ya Uyowa katika center ya kibiashara Mwamnange.