Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa mbele yako hapa na kutoa mawazo yangu kwa hoja hii, ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie katika maeneo kadhaa; moja, ni eneo la Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano. Eneo hili kwanza ninachukua nafasi kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta hii. Na-declare interest, mimi kwa miaka 10 nimekuwa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania, kwa hiyo, nimeona namna anavyowashika mkono wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia taarifa hii, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais katika eneo la kuendelea kujenga maisha ya wafanyakazi baada ya kustaafu kwa maana eneo la hifadhi ya jamii, Mheshimiwa Rais ametatua tatizo ambalo lilikuwa linafanya wafanyakazi wakose amani baada ya kumaliza kazi. Hapa nasema suala la Serikali hii ya Awamu ya Sita kuamua kulipa deni lile la pre-99 la michango ya watumishi ambao hawakuchangia huko mwanzo kabla ya kuanzisha Mfuko wa PSPF, ambao ilifika shilingi trilioni 4.7. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alivyopewa tu kijiti hiki kwa mara ya kwanza alilipa shilingi trilioni 2.15 kwa non cash bond, lakini sasa hivi ukiangalia thamani ya Mfuko huu wa Utumishi wa Umma umefika shilingi trilioni 13.9 baada ya kumaliza deni hili la pre-99. Hili tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tena kumpongeza Waziri Mkuu, ambaye Wizara hii ipo chini yake na Waziri wa Kazi, ndugu yangu Mheshimiwa Sangu, nimeona ameanza vizuri. Nimekaa kwenye sekta hii kwa miaka 10, kwa mara ya kwanza wakati bajeti hii inaandaliwa Waziri aliwaalika viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi na kubadilishana nao mawazo na baadaye kushiriki katika kushuhudia bajeti hii wakati inasomwa. Hili ni jambo kubwa sana kwa maana limewaweka karibu wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya wafanyakazi ni sehemu ya kuandaa mazingira bora ya wafanyakazi sehemu ya kazi na sisi kwa sababu, tumejishirikisha kwenye shirika la kazi duniani na mikataba tukaikubali, basi suala la kuhakikisha kwamba, tunakuwa karibu na tunasimamia vizuri vyama vya wafanyakazi ni suala ambalo ni la muhimu sana. Ninataka nishauri jambo kidogo hapa, kule kwenye vyama vya wafanyakazi yapo masuala hayaendi vizuri; huko mwanzo tunakumbuka tulikuwa na JUWATA, baadaye tukawa na OTTU, tukawa na TFTU, baadaye tukaenda vyama vya kisekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaenda kwenye vyama vya kisekta, mfumo ulikuwa mzuri sana kwamba, kila chama kilipewa sekta maalum, lakini katikati hapa toka 1995 mpaka sasa Katiba za vyama zikabadilishwabadilishwa katika hatua ambayo sekta moja, chama kimoja, kikaenda kwenye sekta zingine. Kwa hiyo, kuna migogoro ambayo haitoi taswira nzuri ya hivi vyama kwenye kutenda kazi na kuwatumikia wanachama wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kuwatumikia wanachama wao, basi wao wanagombana, kwa maana ya kugombania wanachama na hasa chama kinachoshughulikia Serikali za Mitaa na kile ambacho kinashughulikia Wafanyakazi wa Serikali kuu, wanagombania sana wafanyakazi wa sekta ya afya. Kwa hiyo, katika eneo hili ninashauri kwamba, ofisi hii au Wizara ione kwa namna gani inaweza ikaweka mipaka, ili vyama hivi vi-concentrate kwenye kuwahudumia wanachama badala ya kugombania wanachama. Huo ndio ulikuwa ushauri wangu kwenye sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Hapa ninataka nioanishe ni kwa namna gani tunaendana na mipango yetu kwenda kule kwa wananchi. Kama tunakumbuka, tumechangia hapa Mpango wa Miaka mitano, tumepata taarifa au Hotuba ya Mheshimiwa Rais; hotuba yake ukiangalia kama kuna kitu cha mwisho cha ku-conclude, katika hotuba yake alisema ni tabasamu kwa Watanzania kwa miaka mitano hii, lakini ukisema miaka mitano hiyo, tutaenda kutoa tabasamu kwa nyenzo ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaenda kutoa tabasamu kwa nyenzo ya Mpango wa Miaka Mitano, huu ambao nao tumeuzungumzia hapa. Tunapoelekea kwenye Mpango wa Miaka Mitano maana yake ni tunatekeleza kwa mpango wa mwaka mmoja hadi mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ndiyo landing ground ya mipango yetu inayokuja, nikajiuliza nikisema tabasamu kwa Mtanzania ni maeneo yapi ambayo ukiweza ukifanya utawagusa, nikasema kama kuna maeneo ya msingi ya kwanza ni pale ambapo tunaenda kum-assure Mtanzania eneo lake la kujishughulisha katika maisha yake, huyu Mtanzania anafanya nini? Kama tutaenda kugusa pale tutamtengenezea tabasamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ni eneo la huduma, ustawi. Je, akitaka kumpeleka mtoto shuleni anapokelewaje? Anapata mazingira ya namna gani? Anapougua anapata mazingira yapi? Maeneo haya mawili tuki-capitalize tukaweka juhudi kubwa ndipo tutatengeneza tabasamu kwa Watanzania. Tabasamu hii tutaitengeneza kwa miaka mitano, huu ni mwaka wa kwanza tunataka tuanze, ninadhani ni eneo la kwanza ambalo tunatakiwa tuweke mazingira mazuri ya kwenda huko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikaangalia kwenye bajeti ya TAMISEMI nimeona maeneo mengi ambayo yamezungumza mafunzo katika level ya Mkoa na nini, lakini nikasema hapa na nishauri kidogo. Ushauri wangu ni kutengeneza eneo zuri la kuanzia kwenda kutengeneza tabasamu na tabasamu hili kule tukisema eneo la uzalishaji na eneo la ustawi wa jamii, walioko maeneo haya ni wafanyakazi wa Serikali za Mitaa, ni watu ambao wananchi wanafanya nao kazi moja kwa moja, sasa je, katika bajeti hii tumeliwekaje hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunapelekaje kule kwenye Halmashauri namna ya kutekeleza mazingira mazuri kwa mwaka huu wa kwanza ili baada ya miaka mitano tuone tabasamu. Nilitamani kuona namna ya kwenda kuwajengea uwezo kule kwenye Serikali za Mitaa ili watafsiri haya mawazo ya mpango wa miaka mitano wa kuleta tabasamu kwa wananchi. Kwa hiyo, nilitamani kwenye bajeti hii tuone ni mikoa inaandaliwaje kwenda kuwawezesha Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifika kwenye Serikali za Mitaa je, tunaandaje kutoka kwenye halmashauri yenyewe kwenda kwenye kata? Leo tuna Afisa Kilimo kule Mcholi chini kabisa Jimbo la Newala Mjini...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kidogo. Ninatamani twende tukamwekee malengo ambayo yataenda kumgusa mwananchi ili aweze kupata tabasamu kwa kuzalisha korosho vizuri na akaona faida ya yeye kuwa na akampenda huyu mtumishi kuwa sehemu ya maisha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu. Kwa sababu ni mara ya kwanza ninachangia, ninaomba kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuniwezesha kuwa sehemu ya Bunge hili la Kumi na Tatu. Nishukuru tena chama changu kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kupeperusha bendera katika Jimbo la Newala Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua ni maamuzi ya viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama chetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninawashukuru sana. Vilevile, ninawashukuru pia viongozi wa mkoa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa Mheshimiwa Saidi Nyengedi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana pia wananchi wa Jimbo la Newala Mjini wakiongozwa na Kamisa wa Chama chetu aliyeko pale Alhaji Mwangi Rajab Kundya na Mwenyekiti wangu wa CCM Mheshimiwa Jabir Mtanda. Vilevile ninawashukuru sana wananchi hawa kwa kutoa kura nyingi sana 98% kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Urais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie tu wakati Mheshimiwa Rais akiwa mgombea, alivyokuja Mtwara nilimwambia kwamba Wana-Newala Mjini watakupa kura nyingi ambazo kwa Kimakonde ni kura za kumbambandija. Kwa hiyo, kwa 98% alizopewa ni kura za kubambandija kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuaminiwa na Watanzania wote na kupewa kura za kutosha. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuteuliwa na kupewa nafasi hiyo kubwa kabisa inayosimamia utendaji wa nchi yetu. Katika hotuba yake ya kwanza ameonesha dira kabisa kwamba nini anakitaka Watanzania na watendaji wote waweze kutumikia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuweza kupeperusha utendaji katika Wizara zao. Pia, niwapongeze tena Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na wewe binafsi kwa kuchanguliwa katika nafasi zenu hizo. Vilevile, niwapongeze Wenyeviti wa Bunge, Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati ambazo zinasimamia utendaji wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hizo pongezi niombe sasa kuanza kuchangia mipango yote mitatu na Mwongozo wa Bajeti ya mwaka 2026/2027. Ninaomba nijikite eneo moja tu, eneo la kwanza, kigezo cha maendeleo ambayo sisi wenyewe tumejiwekea katika mpango kwamba kwa miaka 25 tunataka Mtanzania awe na kipato cha dola 7,000. Eneo hili ukiangalia kwa miaka mitano ya kwanza tumesema afike dola 1,638. Ukiangalia kwa kipato alichokuwa nacho sasa Mtanzania ni tofauti ya dola 361, sasa ukichukua hiyo dola 361 kwa awamu tano za miaka mitano hatufiki hiyo dola 7,000 kwa Mtanzania tutakapofika mwaka 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamaanisha nini hapa? Ninamaanisha kigezo tulichojiwekea ni kikubwa ambacho tunatakiwa sisi kama Watanzania tuweze kuhakikisha kwamba tunaamua kwa dhati kuleta maendeleo kwa wananchi. Maendeleo katika mpango yanabebwa na nini? Yanabebwa na sekta ya uzalishaji, lakini ukisoma mipango hii hata ile ya nyuma inasema changamoto kubwa ambayo imewahi kutokea katika mipango ya nyuma ni uhafifu wa kuchangia sekta ya uzalishaji, ndiyo imefanya mipango mingi isiende kama tulivyotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa nchi yetu sekta ya uzalishaji kubwa ni ipi? Ambayo inabeba Watanzania wengi zaidi ya 54% inabeba hiyo, ni sekta ya kilimo. Kwa hiyo, ni lazima tuone kwa namna sekta ya kilimo tunaweza kuleta maendeleo makubwa ambayo yanawagusa Watanzania wengi ili wakifika mwaka 2050, basi waweze kuwa na kipato cha dola 7,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kwa nchi yetu kina maeneo tofauti tofauti na mazao ambayo yanategemea maeneo tofauti tofauti. Nikizingatia eneo ambalo mimi ninatoka eneo la Newala, zao kubwa kule ni korosho. Tunaweza tukasema kwa namna gani tunajipanga kuhakikisha uzalishaji wa zao la korosho ambao umekuwa ukiongezeka basi uongezeke maradufu ili wananchi wa Newala Mjini inapofika mwaka 2050 waweze kupata kipata hicho cha dola 7,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilitaka nione, tuwe na dhamira ya dhati ya kuona je, kama wakulima wa korosho na mashamba yao waliyokuwa nayo kwa namna gani tunaboresha yale mashamba ili upatikanaji au mvunaji wa korosho atoke kwenye tani anazopata leo, basi aweze kupata tani zaidi, ili aweze kupata kipato cha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tulenge katika mazao yote si tu wakulima wa kubwa hata hawa wakulima wadogo, kwa nini? Kwa sababu tukileta nguvu kwa wakulima wadogo tukiwasaidia wakaweza kuongeza kipato chao tutaweza kuweka mazingira mazuri ya utofauti wa kipato kwa Watanzania. Kwa sababu hawa watakuwa wana kipato ambacho kitakuwa na uhakika tunavyoelekea mwaka 2050, kwa sababu tofauti kubwa ya kipato inaleta risk kwenye usalama wa nchi. Kwa hiyo, lazima wakulima wadogo wadogo tuwape nafasi, tuwasaidie na wenyewe tuwainue kwenye uchumi kuelekea hiyo dola 7,000 kwa mwaka 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninatamani mpango huu twende tukaushushe kwa wakulima wadogo wadogo na namna gani tunaweza tukashusha mpango huu kwa wakulima wadogo wadogo? Ni kupitia katika halmashauri zetu kwa sababu kule ndiko wako Maafisa Ugani ambao wataweza kuwashauri wataweka record za wakulima wao kwenye maeneo yao na kuona je, wanajipanga vipi kumwezesha mkulima anayepata tani moja leo ili ikifika mwaka 2050 apate tani mbili, tatu kutoka katika shamba lao, hili linawezekana. Kwa hiyo, lazima Mpango huu tukashirikishe halmashauri, tushirikishe watendaji wa halmashauri kutokea Mkurugenzi, Madiwani, Wakuu wa Idara na kule chini kwa watu ambao wanaenda kusimamia kilimo chetu cha kila siku. Ninaomba sana Mpango huu uweze kuzingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tunapowasaidia wakulima wadogo wadogo wakaweza kuzalisha kwa mfano kwenye korosho baada ya mavuno tuwekeze kwenye kubangua. Korosho inayobanguliwa nchini kwetu ni ndogo sana ni tofauti na nchi nyingine za Afrika. Ivory Coast wanabangua zaidi yetu sisi, sisi tunabangua asilimia isiyovuka 20. Ivory Coast wanatafuta 80% kwenye ubanguaji. Kwa sababu korosho ghafi ukiuza unapata fedha ni kama robo ya bei ambayo ungeipata ungebangua. Kwa hiyo, hili litatu-assure wakulima wetu kuweza kupata fedha nyingi, lakini hata tutakapouza nje kuweza kupata fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubanguaji huu ukienda Newala leo unaanza kwenye kaya, mtu mmoja mmoja ana mashine ya kubangua na watu wanakuja kununua korosho iliyobanguliwa lakini vikundi vya akinamama. Tuwekeze na viwanda vikubwa viweze kubangua tuweze kuuza korosho ambayo imekuwa processed ambayo inatoa fedha nyingi kutafuta hiyo 7,000 ya mwaka 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili tuliwekee nguvu kweli na si tu kwenye korosho, niseme mazao mengine maeneo mbalimbali tuweke kwenye large scale lakini vilevile, tuweke kwa mkulima mmoja mmoja ili kuwainua Watanzania wote kwa umoja wao. Tusije tukawaacha watu wenye uchumi mdogo chini huko vijijini ambao baadaye wanaweza wakahatarisha afya ya nchi hii kiusalama. Hilo nilikuwa ninataka nilichangie vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kwenye korosho kusini, nani anasimamia korosho? Ni vyama vya msingi. Ukienda kwenye Mpango tumezungumzia kuongeza idadi ya wanachama. Nilikuwa ninaomba mpango uangalie vilevile nani anaongoza ushirika? Tuweke mifumo ambayo tutapata viongozi waadilifu ambao watalinda fedha za wanachama wao na kuwapatia fedha zao ili tuweze kufika hiyo dola 7,000. Tukiwa na viongozi ambao wao wakikaa pale wanafanya wakulima wasipate haki yao ya msingi ya kilimo walichokifanya kwa mwaka mzima itakuwa tunawanyonya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima Mpango nao uone na uweke mifumo ambayo tutapata viongozi kwa ajili ya ushirika, kwa sababu wao ndiyo wanaosimimia hili zao kule chini. Nilikuwa ninataka nishauri hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukimzungumzia Mtanzania kwenye sekta hiyo ya kilimo aweze kupata hizo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, muda umekwisha.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba tuwekeze kwenye umwagiliaji, huko nako tufanye Mtanzania awe anafanya kazi muda wote na kuweza kupata kipato muda wote. Pia, wanaosimamia Madiwani na viongozi wa Serikali za Mitaa, tuone namna ya kusimamia haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)